MUNGU WA BETHELI

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atkuzwe ndugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU lililo hai.
Utajisikiaje kwamba unafanya jambo jema mbele za MUNGU na miaka mingi inapita kisha MUNGU anakuja kusema na wewe kwamba yeye ni MUNGU wa siku ile ulipofanya jambo jema mahali pale ulipofanya  mbele zake hivyo amekuja kukubariki.
Utajisikiaje unatoa sadaka zako njema kwa MUNGU aliye hai kisha siku nyingi zinapita lakini kwa sababu MUNGU huwa hasahau anakuja kukumbusha kwamba yeye ni MUNGU uliyetoa matoleo mbele zake kwa uaminifu na sasa amekuja kukubariki na kuwaabisha watesi wako.
Utasijikiaje ikiwa siku moja uliweka agano na MUNGU  na siku nyingi zikapita kisha MUNGU anakuja kukuambia kwamba yeye ni MUNGU wa siku ile ulipofanya agano na yeye na sasa amekuja kukubariki na hakuna atakayezuia.
Utajisikiaje kwamba uliweka nadhiri mbele za MUNGU na ukaitimiza nadhiri hiyo kwa uaminifu na ikapita miaka kadhaa MUNGU anakutokea na kukuambia yeye ni MUNGU wa siku ile ulipoweka nadhiri na sasa amekuja kukufuta machoni na kukubariki.
Hakika ni furaha ya ajabu sana.
Jifunze ujumbe huu ambao nilipousoma kwa mara ya kwanza nilifarijika sana na nikagundua hakika MUNGU huwa hasahau hivyo kama ulitenda mbele zake kwa upendo na furaha hakika ipo siku anaweza kukupa shangwe ya kudumu.
Uliweka nadhiri au agano na ukaona MUNGU nachelewa lakini kumbe MUNGU hajawahi kusahau hata siku moja hivyo siku moja anakuja kukujulisha kwamba yeye ni MUNGU wa siku ile ulipofanya tendo jema na sasa anakubariki kwa tendo lako jema.
Habari za Yakobo huwa zinanipa nguvu sana ninapozisoma.
Iko hivi Yakobo baada ya kubarikiwa na Isaka Baba yake aliogopa kuuawa na ndugu yake aitwaye Esau. 
Mwanzo 27:41 '' Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo.''
 Wazazi wao wakajua kabisa kwamba Esau atamuua Yakobo hivyo wakamwambia Yakobo aende nchi ya mbali ambako  ndio chimbuko la Rebeka mama yake na Yakobo. Yakobo hakuondoka na kitu bali alitembea kwa mguu, hana kitu wala mali yeyote, hakuwa na vitu vingi na inawezekana kabisa alijua hata chakula kidogo alichokuwa nacho kingeisha, alikuwa anamkimbia ndugu yake.
Biblia inasema Mwanzo 28:10-12 '' Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa MUNGU wanapanda, na kushuka juu yake.''
 Biblia inasema Yakobo akachukua jiwe na kulifanya mto wa kulalia porini peke yake, akalala na kuota ndoto. Ni mazingira magumu sana sana na inawezekana wewe wala hujawahi kupitia mazingira hayo magumu. Kutoka familia nzuri na kujikuta unalala porini peke yako na mawe ndio mto wako wa kulalia, sio jambo jepesi sana. Asubuhi kulipokucha Biblia linasema hivi.
'' Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake. Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu. Yakobo akaweka nadhiri akisema, MUNGU akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa MUNGU wangu. Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.-Mwanzo 28:18-22''
 Yakobo akamua kuita mahali pale jina jipya yaani Betheli.
Yakobo kisha akaamua kuweka nadhiri kwa MUNGU 
Yakobo akala na kiapo kwamba kama akienda salama na kurudi salama na MUNGU akimbariki hakika atamtolea MUNGU fungu la kumi.
Yakobo  baada ya hapo akaenda nchi nyingine nchi nyingine iitwayo wana wa mashariki(Mwanzo 29:1)
Tunafahamu baada ya hapo Yakobo akamuona Raheli kisimani na ndio ikwa chanzo cha kufika kwa ndugu wa mama yake ambako ni taifa la kwamba na kwao.
Yakabo akaanza maisha mapya huku agane lake na MUNGU likisimama imara, na nadhiri yake ikiwa hai mbele za MUNGU.
MUNGU akamfanya Yakobo kuwa baraka hata kwa wenyezji wake, Yakobo akafanya kazi mbalimbali kama mfanyakazi huko alikokuwa. Yakobo akadanganywa na kuonewa, yakobo akajikuta kwa sababu hana wazazi huko na hana mali huko basi alitakiwa kuajiriwa kwa miaka 7 ndipo hiyo miaka saba ya kuwatumikia wenyeji iwe ndio mahari ya kumpata mke, Baada ya miaka hiyo saba Yakobo akaukuta amedanganywa hivyo akapewa miaka mingine 7 ya kutumika ili kumpata Raheli kipenzi cha moyo wake.
Yaani kwa sababu huna mali na huna wazazi wa kukupa pesa ya mahari ili kupata mke basi unatumika miaka 14 ndipo mahari inatimia na unakabidhiwa mke.
Inawezekana Yakobo alichoka na alisahau agano lake na MUNGU.
Inawezekana Yakobo hakujua kama nadhiri yake na MUNGU inaishi.
 Inawezekana Yakobo hakujua kwamba mji wa Luzu aliubadili jina na kuuita Betheli na kisha akafanya ahadi njema kadhaa hapo Betheli mbele za MUNGU.
Baadae MUNGU asiweza kusahau akajifunua kwa Yakobo akisema maneno muhimu sana.
Biblia inasema hivi '' Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda wanyama wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutendea Labani. MIMI NI MUNGU WA BETHELI, HUKO ULIKOTIA MAFUTA NGUVU, NA KUNIWEKEA NADHIRI. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa.-Mwanzo 31:12-13''
 Yaani Yakobo alifanya agano la  nadhiri miaka 21 nyuma lakini MUNGU anamwambia ''.Mimi ni MUNGU wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri ''
Mfano wako ni wewe ndugu,
Inawezekana ulikuwa unaomba sana na kuweka nadhiri na ukaona kama MUNGU hatatenda lakini MUNGU aliyeweza kukumbuka nadhiri ya Yakobo ya miaka 21 kabla atashindwa nini kukutimizia wewe ambaye labda ni mwaka tu umepita?
Inawezekana ulipoona miezi 7 imepita tangu uweke nadhiri ulianza kulalamika na kunung'unika, ndugu mngoja BWANA tena baki ukimwamini maana yeye ni mwaminifu na wa haki, hivyo atatenda.
Inawezekana uliweka agano na MUNGU, inawezekana ulitoa sadaka nzuri sana lakini baadae ukaona kama ulikuwa hasara, ndugu kama ni katika KRISTO YESU hakika hukula hasara hata moja, MUNGU ni mwaminifu sana sana hivyo baki kwenye kusudi lake maana yeye atatimiza yote aliyokuahidi.
Inawezekana umetoka kijijini una ndala lakini MUNGU anaweza akakubariki mjini ulikoenda na siku moja utarudi kusalimia kijijini ukiwa na gani.
Inawezekana uliondoa kwenu ukiwa peke yako na unaenda mjini ambako huna ndugu hata mmoja lakini MUNGU anaweza kukulinda na kukubariki kama uko katika kusudi lake kama ilivyokuwa kwa Yakobo.
Nampenda MUNGU wa Betheli maana alimkumbuka mtumishi wake kama ambavyo atakukumbuka wewe.
Mimi Peter Mabula kuna wakati nilikuwa katika wakati mgumu sana sana. Nilikuwa sina kitu na wakati huo nilikuwa mpaka navizia wanafunzi wa Bweni Sekondari wakimaliza kula na mimi navamia mesi yao na kuokota vipande vya ugali na mchuzi wa maharage uliogandiana kwenye mesi ya kulia chakula, nachukua na kula ndio mlo wa usiku unakuwa umeisha. Niliwahi kuteswa na wachawi sana na nilikuwa naisha maisha ya woga na hofu kubwa. Ilifika siku nikaingia agano mbele za MUNGU juu ya mambo matatu. Nilimwambia MUNGU kwamba kama akinipa kazi itakayonipa pesa nzuri, kama akinipa mke mzuri na uzao, Kama akinipa Nyumba ya kujenga mimi mwenyewe hakika ningemtumikia hadi watu wangenishangaa sana au kuniona kama kichaa maana nisingechoka kumtumikia Bwana YESU Mwokozi. MUNGU alinifanyia muujiza wa ajabu mno ambao hata kueleza hapa hautoshi, hakika MUNGU anatimiza ahadi yake, MUNGU Baba ni mwaminifu na wa haki hakika. Mimi kwa mazingira yale sikudhani wala kutarajia kama siku moja nitakuwa na mke na watoto, nyumba yangu au kazi. Kwangu mimi niljua vitu hivyo haviwezekani kabisa, lakini Bwana YESU ni mwaminifu sana.
Ndugu ukiweka nadhiri kwa MUNGU, au ukafanya agano na MUNGU, au ukafanya agano kupitia matoleo hakika ukibaki katika kusudi utamuona MUNGU.
Ngoja nikuambie mambo ya baraka kadhaa kuhusu Yakobo aliyekumbukwa na MUNGU tangu kule Betheli.
1.  Yakobo akaja kukutana na Raheli ambaye akaja kuwa mke wange mpenzi.
Mwanzo 29:9-11 ''Hata alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo za baba yake, maana aliwachunga. Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo za Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulifingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo za Labani, ndugu wa mamaye. Yakobo akambusu Raheli, akainua sauti yake akalia.''

2. Yakobo akaoa.
Mwanzo 29:28 ''  Yakobo akafanya hivi, akatimiza siku zake saba. Naye akampa Raheli binti yake kuwa mkewe.''

3. Yakobo akapa uzao.
Mwanzo 30:22-24 '' MUNGU akamkumbuka Raheli; MUNGU akamsikia, akamfungua tumbo. Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, MUNGU ameondoa aibu yangu. Akamwita jina lake Yusufu, akisema, BWANA aniongeze mwana mwingine.''

4. Walioishi na Yakobo waligundua kwamba MUNGU amewabariki kwa sababu ya Yakobo.
Mwanzo 30:27 ''  Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba BWANA amenibariki kwa ajili yako. ''

5. Yakobo alibarikiwa sana hata watu wakaanza kumuonea wivu.
Mwanzo 31:1 ''Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote.''

6. MUNGU wa Betheli alikuwa pamoja na Yakobo.
Mwanzo 31:5 '' Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini MUNGU wa baba yangu amekuwa pamoja nami.''

7. MUNGU aliwaonya watu ndotoni ili wasimchukize Yakobo mtumishi wake.
Mwanzo 31:24 ''MUNGU akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.''

Ndugu hakika MUNGU Baba  ni mwaminifu mno.
YESU KRISTO akikuambia kitu hakika kitakuwa.
ROHO MTAKATIFU akikuongoza kufanya jambo la ki MUNGU hakika ni kwa faida yako njema.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments