MUOMBAJI OMBEA NCHI YAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu kokote uliko.
Inawezekana kabisa nchi yako ina amani sana sasa hivyo huna msukumo wa kuiombea nchi yako, jifunze kwa mataifa mengine ambayo na wao kuna muda walikuwa na amani sana lakini wakati huu wako katika vita.

Inawezekana kuna mambo katika taifa lako hayaendi sawa mbele za MUNGU, wewe muombaji ndio mwenye kumkumbusha MUNGU hivyo simama katika zamu yako kuiombea inchi yako.

Isaya 62:6-7 ''Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani. ''

 
Watu waliokombolewa na Bwana YESU ndio walinzi wa kiroho, hivyo wewe uliye mlinzi wa kiroho hakikisha kwa maombi yako nchi yako inakuwa salama.


Kuna mambo mengi sana kibiblia na kiroho ya kuliombea taifa lako.
Baadhi ni haya.


1. Omba toba kwa ajili ya nchi yako ili MUNGU ainusuru nchi yako kuingia katika uharibifu ambao uko tayari kuja kwa sababu ya maovu kuongezeka na watu kukosa hofu ya MUNGU.
 
1 Nyakati 7:14 '' ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.''


2. Katika maombi ya kuhusika na taifa lako usisahau kuhusika zaidi na malango ya taifa.
 
Mfano Kampala na Entebe ni lango la kuikamata Uganda Yote, hivyo hakikisha lango la nchi yako liko salama.
Nairobi na Mombasa ni lango la kuikamata Kenya yote, hivyo ombea lango la nchi yako.
Dar es salama, Mwanza, Dodoma, Zanzibar au Arusha ni Malango ya kuikamata Tanzani kiroho, hivyo ombea malango ya taifa lako.
Lusaka ni lango la Zambia, Kinshasa ni lango la Kongo, Kigali ni lango la Rwanda, Bujumbura ni lango la Burundi na mataifa mengine yote yana malango ya nchi hivyo hata kama sijalitaja taifa lako tambua kwamba kuna malango katika taifa hilo, hivyo ombea malango katika nchi yako ili shetani asipitishe uharibifu kwa taifa unaotokea katika lango la Taifa.
Kumbuka Mfano Ninawi walifanya maovu mengi kiasi kwamba MUNGU akataka kuwaangamiza kama Sodoma na Gomora, MUNGU akamtuma Yona Nabii akisema ''Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.-Yona 1:2 ''
Yona alifika katika Lango la nchi ile na watu wale kuanzia na mfalme walitubub kwa MUNGU na MUNGU akaifuta adhabu ambayo ingewapata, kilichosababisha wasiangamizwe ni toba tu, hivyo muombaji hakikisha unatubu kwa ajili ya nchi yako.
Tubu kwa ajili ya maovu, tubu kwa ajili ya watu kumsahau MUNGU, tubu kwa ajili ya kila hila ambazo ni pando la shetani ili kuleta uharibifu.
Kumbuka japokuwa kila mamlaka huwepo kwa kibali cha MUNGU(Warumi 13:1) lakini kuna watawala pia MUNGU anaweza kujuta kwa sababu ya jinsi wanavyotawala, Hivyo MUNGU akijuta na kughairi kinachofuata ni adhabu.
Mfano ni huu 1 Samweli 15:10-11 '' Ndipo neno la BWANA likamjia Samweli, kusema, Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia BWANA usiku kucha.''

Siku moja Musa aliambiwa na MUNGU kwamba MUNGU ataufuta ukumbusho wa Amaleki na hata leo hakuna Taifa duniani linaitwa Amaleki.
Kutoka 17:14 '' BWANA akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu. ''
Je kama taifa lako liko katika hali kama ya Amaleki utafanyaje?
Hata sodoma na Gomora hawakujua kama kuna kufa wote, walidhani wana uwezo wa kujilinda, lakini walisahau kwamba huwezi kujilinda mbele za MUNGU, Ndio maana hakuna hata mmoja aliyeizuia adhabu ya MUNGU kwao.


3. Ombea amani katika taifa lako.
 
Zaburi 133:1 ''Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. ''
Kuna mataifa wa ukabila, kuna mataifa kuna chuki kati ya jamii fulani na jamii fulani, ndugu usishabikie tu kundi mojawapo ila omba kwa ajili ya amnai ya nchi yako.
Mataifa mengine wenye mamlaka wamewataabisha watumishi wa KRISTO, ni hatari sana, maana MUNGU anaweza kuharibu ufalme huo.
Mathayo 23:37-38 ''Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka! Angalieni, nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa. ''
YESU alisema siku moja kwamba ''bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. -Luka 23:28 ''
Ndugu lia kwa ajili ya nchi yako, tubu kwa ajili ya taifa lako, ita neema ya MUNGU kwa ajili ya taifa lako.


4. Omba mapenzi ya MUNGU yatimizwe katika taifa lako na ufalme wa MUNGU utawale kwa watu wote wa taifa lako.
 
Mathayo 6:9 '' Basi ninyi salini hivi; BABA yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, ''


Ndugu usomapo ujumbe huu naomba uombe kwa ajili ya nchi yako, ukiwa katika maombi yako ya kufunga omba kwa ajili ya nchi yako.
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments