WOKOVU NA UBATIZO

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Siku moja miaka michache imepita kuna mtu aliniuliza swali hili ''WOKOVU Na UBATIZO Kipi Bora?'' niliwaza sana kwanini ndugu huyo aulize swali hilo?
Nikamjibu  Kwamba ''WOKOVU Ni Bora Na UBATIZO Ni Muhimu Maana Vyote Vyatokana Na MUNGU.''

Ngoja leo  nizungumzie kidogo kuhusu wokovu na kwa sehemu kuhusu ubatizo.

Wokovu ni nini?

=Wokovu Ni Mpango Wa MUNGU Kumwokoa Mwanadamu Kupitia YESU KRISTO.
 Wokovu Ndio Kuokoka.
Waefeso 2:8-10 ''Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika KRISTO YESU, tutende matendo mema, ambayo tokea awali MUNGU aliyatengeneza ili tuenende nayo.''
Unapompokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako unakuwa umelipokea kusudi la MUNGU la wewe kuishi milele katika yeye.
Baada ya kumpokea YESU unasajiliwa mbinguni kama mwanachama hai wa ufalme wa MUNGU. Ufalme wa MUNGU una kanuni zake za maisha na hizo ndizo wanatakiwa kuishi waliookolewa na Bwana YESU. 
Kumpokea YESU kama Mwokozi ndio kuzaliwa upya na MUNGU na wakati huo ndio unaanza kuishi maisha ayatakayo MUNGU, na Biblia hapo juu  inasema kwamba '' tu kazi yake, tuliumbwa katika KRISTO YESU, tutende matendo mema, ambayo tokea awali MUNGU aliyatengeneza ili tuenende nayo.''
Kwahiyo unapookoka hakika unatakiwa uanze kuyaishi matendo mema ambayo MUNGU aliyatengeneza tangu zamani, matendo hayo mema yanaagizwa vyema sana katika Neno la MUNGU ambalo ni Biblia kwa njia ya Injili ya YESU KRISTO Mwokozi.
Ndio maana ni muhimu ukajua kwamba imani ya kweli inayoweza kukupeleka uzima wa milele ukitii ni imani ya Wokovu wa YESU KRISTO pekee, imani hiyo ya kweli chanzo chake ni kulisikia Neno la KRISTO.
Warumi 10:17 ''Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO.''
Ndio maana Biblia inatoa uhakika kwa waliookoka na wanaishi maisha mema aliyoyatengeneza MUNGU kwamba ''Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika KRISTO YESU.   -Warumi 8:1''
 Kuokoka Ni Kuishi Maisha Ya Ushindi Dhidi Ya Dhambi.
 Kuishi Maisha Ya Ushindi Dhidi Ya Dhambi Ndio Mpango Halisi Wa Wokovu Wa KRISTO. 
1 Petro 1:15 '' bali kama yeye(MUNGU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''
 Huwezi Kuokoka Nje Na KRISTO.
Yohana 14:6 '' YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi.''
Najaribu kukupitisha katika maandiko ili uelewe vyema.
Kumbuka jambo hili kwamba hakuna Wokovu Nje Na KRISTO
 Matendo 4:12 ''Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. '' 

 Ngoja niseme machache pia kuhusu ubatizo.
Nakumbuka nimeshafundisha mara kadhaa kuhusu ubatizo wa maji na kuhusu ubatizo wa ROHO MTAKATIFU au ubatizo wa moto.
Ngoja nikujulishe machache muhimu kuhusu ubatizo.

Ubatizo ni nini?

Na Ubatizo Ni Kuuzika Utu Wa Zamani Na Kuanza Kuishi Katika Utu Mpya Uitwao Utakatifu.
Ubatizo Wa Maji Ni Ishara Ya Nje Ya Badiliko La Ndani Ya Mtu La Kuacha Mabaya Na Kuanza Mema.
Wakolosai 2:12 '' Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za MUNGU aliyemfufua katika wafu.''

 Ubatizo Wenye Uzima Ni Ubatizo Katika Bwana YESU Tu. 
Bwana YESU Ana Uzima Sasa Kisha Uzima Wa Milele.
Lakini pia ngoja nikujilishe jambo muhimu sana.
Kuna Tofauti Kati Ya Ubatizo Wa ROHO MTAKATIFU Na Kujazwa ROHO MTAKATIFU, Lakini Naomba Tujue Kwamba Kujazwa ROHO MTAKATIFU Kwa Mara Ya Kwanza Ndio Kubatizwa ROHO MTAKATIFU. 
Matendo 2:4 ''Wote wakajazwa ROHO MTAKATIFU, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama ROHO alivyowajalia kutamka.'

Kubatizwa ROHO MTAKATIFU Ni Jambo Linalofanyika Mara Moja Lakini Kujazwa ROHO MTAKATIFU Ni Jambo Linalotakiwa Kufanyika Siku Zote Katika Maisha Ya Mwamini. 
Waefeso  5:18b ''bali mjazwe ROHO; '' 
 
ROHO MTAKATIFU Atakuwa Na Wateule Wa KRISTO Milele.
 Yohana 14:16-17 ''Nami nitamwomba BABA, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye ROHO wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.   ''
 Hivyo Hakuna Wa Muhimu Katika Maisha Ya Mteule Kama ROHO MTAKATIFU. 
Hakuna muhimu kuliko ROHO MTAKATIFU na Neno la MUNGU baada ya mtu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi.
Kama Hujajazwa ROHO MTAKATIFU Tamani Jambo Hilo Huku Ukiomba Na Kudumisha Utakatifu. 
Kumbuka jambo hili muhimu sana kwamba kama usipozaliwa mara ya pili huwezi kuurithi ufalme wa MUNGU.
 Yohana 3:5 ''YESU akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa ROHO, hawezi kuuingia ufalme wa MUNGU. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwaROHO ni roho. ''
Kuzaliwa mara ya pili ni kuokoka na kuanza kuishi maisha matakatifu ya kuongozwa na ROHO MTAKATIFU. 
Ndio maana wanaoongozwa na ROHO MTAKATIFU tu ndio wana wa MUNGU walio tayari kwa ajili ya uzima wa milele.
Warumi 8:14 ''Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''
Hivyo ulipompokea YESU ulimpokea pia na ROHO MTAKATIFU hivyo tembea sasa kwenye Neno la MUNGU la injili ya KRISTO huku ukimtii ROHO MTAKATIFU.
Kuna viwango vya aina tatu vya ujazo wa nguvu za ROHO MTAKATIFU kwa wateule.
 Kuna ubatizo wa ROHO MTAKATIFU, ukiendelea vyema ujue utaingia hatua ya pili ambayo ni kufurika ROHO MTAKATIFU na kama ukivuka kiwango hicho huku ukijifunza sana Neno la MUNGU na kuliishi kusudi la MUNGU basi utafikia kiwango cha juu sana ambacho ni kupakwa  mafuta na ROHO MTAKATIFU, Ndugu tamani kufikia hatua hii kubwa sana ambayo ukiifikia itakufanya umtumikie vyema sana Bwana YESU.
Isaya 61:1-2 '' ROHO ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha MUNGU wetu; kuwafariji wote waliao;''
Hata baadhi ya wachungaji na maaskofu au viongozi wakubwa kabisa kanisani wapo ambao hawajawahi kufikia kiwango hiki cha kupakwa mafuta na ROHO MTAKATIFU mwenyewe.
Mafuta hayo sio yale ambayo baadhi ya watumishi huwapaka watu mafuta bali, mafuta haya ni nguvu kubwa za ROHO MTAKATIFU mwenyewe ndani ya mteule wa KRISTO anayeishi maisha matakatifu na anamtumikia KRISTO kwa moyo na uaminifu sana.
 
  Baada ya kukufafanulia naamini sasa umeelewa.
Kama huwa unajiuliza Wokovu na ubatizo kipi bora naamini umepata majibu muhimu sana.
Je Wokovu Na Ubatizo Kipi Hutangulia?
 Jibu Ni Kwamba Wokovu Hutangulia.
Wokovu Ni Kumpokea YESU Na Kubatizwa Ni Kumvaa KRISTO. Wokovu Na Ubatizo Ni Muhimu Sana. Waenda Mbinguni Huokoka Na Kubatizwa Na Kuishi Maisha Matakatifu.  
 Marko 16:16 '' Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.   ''

  Sisi wateule wa MUNGU si tu Tutashinda Bali Tunashinda Kwa Jina La YESU KRISTO.

Labda ngoja nikuulize pia mambo haya muhimu ili na wewe ujijue uko kundi gani.
Mkristo shujaa ni yupi?
1. Ni jasiri katika Imani yake bila kuteteleshwa na elimu nyingine iliyo kinyume na Biblia.
2. Analisoma Neno la MUNGU, analitafakari, analitii na kulitendea kazi.
3. Ana maono katika kazi ya MUNGU ili kuzaa matunda mema kwa utumishi wake unaotokana na maono mazuri katika injili ya KRISTO.
4. Anaenenda kwa ROHO MTAKATIFU na kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.
5. Ameacha na dhambi zote na sasa anaishi maisha matakatifu.
6. Ni mvumilivu, hodari na anayeichuchumilia taji ya uzima.
7. Humpendeza KRISTO.
 
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments