HUDUMA NA KARAMA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
MUNGU alitoa karama mbalimbali katika Kanisa lake kwa kusudi maalumu.
Maana mojawapo ya Neno ''karama kibiblia'' ni Zawadi za neema ambazo mtu anayempokea YESU KRISTO kama Mwokozi anapewa na ROHO MTAKATIFU ili amtumikie MUNGU.
Karama kwa Kanisa  ni kipawa au uwezo fulani ambao mtu anapewa na MUNGU ili amtumikie YESU KRISTO Mwokozi.
Maana ya Neno ''huduma'' ni shughuli au kazi anafanyazo mtu kwa manufaa ya wengi.
Unapofanya huduma mfano ya kuhubiri injili ni kwa manufaa ya wale unaowapelekea injili hiyo ya Wokovu wa KRISTO, lakini pia ni kwa manufaa yako kiroho maana MUNGU ameahidi mambo mengi mazuri kwa wanaomtumikia, mojawapo ya mambo hayo ni kwamba MUNGU atawaheshimu wanaomtumikia. 
 ‘’ Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, BABA atamheshimu. –Yohana 12:26 ‘’
Kwa  maana hizo tunagundua ya kwamba karama ni muhimu na huduma ni muhimu sana. Lakini wapo wenye karama lakini hawafanyii kazi karama zao hivyo huduma yao kutokuonekana.
Ni muhimu sana kuifanyia kazi karama yako njema uliyopewa na MUNGU ili umtumikie katika Kanisa.
Ni vyema sana uwemo siku zote katika huduma uliyopewa na Bwana YESU.
1 Wakorintho 12:4-11 " Basi pana tofauti za karama; bali ROHO ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana(YESU) ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule; mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye(ROHO MTAKATIFU).''

Ndugu yangu uliyepewa karama na MUNGU inakupasa kujua kwamba.

1. Karama yako ni zawadi uliyopewa na MUNGU baada ya kumpokea YESU KRISTO Kama Mwokozi.

 1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."

2. Ukiitumia vibaya karama yako ujue utapata hasara kubwa, hivyo itumie karama yako kwa KRISTO, tena itumie vizuri karama hiyo kwa kusudi la MUNGU.
 1 Wakorintho 4:1-2" Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu."

3. Hujapewa karama ili uwe na kiburi, tena hujapewa karama ili ujiinue, Bali umepewa karama ili umtumikie KRISTO, umepewa karama ili uwafanye watu kumtukuza MUNGU na kuokoka.
  ''Haleluya. Mshukuruni BWANA, liitieni jina , WAJULISHENI WATU MATENDO YAKE-Zaburi 105:1''


4. Itumie vyema karama yako.
Lengo la wewe kupewa karama ni ili mwili wa KRISTO ujengwe

Waefeso 4:12 '' Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa KRISTO ujengwe; ''
Je ni kweli wewe unaujenga mwili wa KRISTO.
Mwili wa KRISTO ni jumuiko la waliompokea YESU KRISTO kama Bwana na Mwokozi wao.
Je unaujenga mwili wa KRISTO?
wengine kupitia karama zao na huduma zao wala hawaujengi mwili wa KRISTO Bali wanaubomoa.
Wewe hakikisha huwi katika kundi la wanaoubomoa mwili wa KRISTO.


Jukumu lako Kama mtumishi wa MUNGU ni kuwafanya watu wampokee YESU KRISTO kama Mwokozi wao na ili kuwafanya pia wafunguliwe vifungo vya Giza vyote.
Kumbuka YESU alikuja kufanya kazi hizi mbili.

1. Kuokoa wanadamu.
Luka 19:10 "Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea."

2. Kuwafungua watu vifungo vya giza .
1 Yohana 3:8b " Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi."


Wewe kama Wakili au balozi wa YESU KRISTO basi inakupasa kuzingatia kazi za YESU kwa wanadamu.
Kazi hizo zote lazima zifanye kazi pamoja.

YESU akikuokoa na akakuwekea huduma ndani yako inakupasa huduma uitimize.
Jilinde, jitunze na jifunze ili kutimiza huduma yako.
Huduma yeyote katika Injili ya KRISTO huwa ina CHANZO na CHANGAMOTO.
Chanzo cha huduma yako ni Wokovu wa KRISTO uliomfanya ROHO wa MUNGU kuingia katika maisha yako na kukupa huduma.
Usitishwe na challenges (Changamoto) bali endelea mbele ili kutimiza huduma yako.
Uwe mwangalifu kujifunza na kujitunza wewe mwenyewe kwanza ndipo upate kuwatunza kwa Neno la MUNGU hao ambao MUNGU amekupa kuwahudumia.

 Kama huna wito wa MUNGU huwezi kuwa na maono ya mbele ya kazi ya MUNGU.
Wito aliokupa MUNGU katika KRISTO ni wa muhimu sana kwako katika kufikia maono na malengo yako ya mbele.

Wengi sana pia wanajiita watumishi wa MUNGU, Nasema wanajiita kwa sababu hawamtumikii KRISTO hivyo hao ni watumishi feki au watumishi hewa.
Mtumishi wa MUNGU ni yule ambaye anamtumikia MUNGU katika  KRISTO YESU huku yeye mwenyewe akiwa ameokolewa na YESU KRISTO.
Ndugu, kumbuka sana jambo hili kwamba wateule wa Bwana YESU ndio watumishi pekee wa MUNGU, Warumi 1:5-6 Biblia inasema ‘’ ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa YESU KRISTO; ‘’


Labda sasa ngoja nikushauri mambo yafuatayo;
Pambana katika haya kuhusu huduma au karama yako ambayo YESU KRISTO au ROHO MTAKATIFU amekupa.

1. Pambana ili kuilinda huduma au karama yako.

2. Pambana ili kuiboresha huduma au karama yako.

3. Pambana ili kuikuza huduma au karama yako.

4. Pambana katika utumishi ili umpendeze MUNGU.

Njia za kupambana ziko nyingi baadhi ni hizi.

1. Maombi.

1 Thesalonike 5:17 ''ombeni bila kukoma;''
 
2. Kujifunza Neno la MUNGU.


1 Timotheo 4:15-16 ''Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote. Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.'' 

  3. Kumsikiliza ROHO MTAKATIFU.
Warumi 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''
 
4. Kujifunza kwa watumishi wenzako wa YESU KRISTO.


2 Timotheo 3:14-17  ''Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika KRISTO YESU. Kila andiko, lenye pumzi ya MUNGU, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa MUNGU awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.''

Kumbuka pia kwamba huduma inayoanza ni ngumu kuliko huduma unayotakiwa kuiendeleza ambayo ilianzishwa na wengine.
Kwa mtumishi wa MUNGU ni muhimu kujua kwamba;
1. Umeitwa kuanzisha huduma?

2. Umeitwa kuendeleza huduma?
3. Umeitwa kuitegemeza huduma?
4. Umeitwa kuibeba huduma katika mambo kadhaa ya ki MUNGU?
Wewe umeitwa kufanya nini katika huduma unayosukumwa kuifanya rohoni mwako?
Kila mteule wa MUNGU katika Kanisa ameitwa kufanya huduma katika kazi ya Injili.
Ngoja nikupe mfano;
Ndugu mmoja aliokoka na kujiunga na kanisa changa ambalo Mchungaji ndiye aliyekuwa anafanya kila kitu.
Mchungaji ndiye alikuwa anaset vyombo, anaimba sifa na kuabudu na kuhubiri. Kanisa hilo hakukuwa na kwaya ya Kanisa japokuwa kulikuwa na wana kanisa wengi kiasi. Ndugu huyo baada ya kuokoka alipata msukumo wa kuanzisha kwaya ya Kanisa na kundi la kusifu na kubudu kanisani ili mambo yaende vizuri na ili kumpunguzia mzigo Mchungaji.
Alipomwambia Mchungaji alikubaliwa na kwa sababu alikuwa na mzigo ndani basi alianzisha huduma hiyo ya kwaya kanisani. Baada ya miezi kadhaa kwaya ilikuwa vizuri na hadi watu wakawa wanaulizana "Mbona haya hatukuyafanya mapema hadi huyu ndugu alipookoka na kisha alipoanzisha". Baada ya muda kadhaa kwaya ile ilikuwa maarufu nchini kwa uimbaji mahiri. Huyo ndugu aliitwa na MUNGU kuanzisha huduma ile kanisani.
Wewe unasikia wito gani?
Inawezekana kanisani kwenu huwa hamna mkesha wa maombi,inawezekana huwa hamshuhudii, inawezekana huwa hamtembelei wagonjwa n. k.

Ziko huduma nyingi mno ambazo watu wa MUNGU hupewa na MUNGU kama wito ili kuzianzisha.
Inawezekana zamani huduma hizo zilikuwepo ila kwa sasa hazipo hivyo unaweza ukasikia msukumo wa kuifufua huduma hiyo.
Zingatia tu wajibu wako.
kama umeitwa kuanzisha , kuendelea, kutegemeza n.k
Timiza tu wito wako.
Wengine wito wao ni kutoa pesa ili injili iende, timiza wito wako.
Wengine wito wao watoe maeneo yao ili kanisa lijengwe, ndugu timiza wito wako.
Kuna huduma nyingi mno ndugu lakini jitahidi kutimiza wito wako uliopewa na MUNGU katika mwili wa KRISTO.

Je umeitwa kufanya huduma gani?
Ikiwa MUNGU amekuita na ameweka maono ndani yako hakikisha unatimiza maono hayo kwa utukufu wa MUNGU.
Fanya kazi ya MUNGU katika injili ya KRISTO YESU Mwokozi.

Mfano ni huu ambapo MUNGU anataka Waisraeli aliowaokoa kutoka Misri, Wamtumikie kwa mioyo yao yote.
Kumb 10:12 '' Na sasa, Israeli, BWANA, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche BWANA, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; ''

Jambo lingine napenda kukujulisha ni kwamba kama unahudumu katika kazi ya MUNGU unahitaji sana kuwa makini.
Uwe makini na mwangalifu kwanza wewe mwenyewe ili usitoke katika kweli ya injili ya KRISTO.
Uwe mwangalifu katika matendo yako, katika maneno ya kinywa chako na katika fundisho lako. Mtume Paulo kama mmoja wa wanaohudumu katika kazi ya MUNGU Siku moja alisema Maneno haya kwa kila anayemtumikia MUNGU katika Kanisa, iwe kwa cheo, karama au utumishi wa aina nyingine yeyote,
Alisema " Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo ROHO MTAKATIFU amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake MUNGU, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.-Matendo 20:28-30

Mteule wa MUNGU unahitaji kuwa makini Sana katika kazi ya MUNGU uifanyayo.
Umelazimishwa na nani kumtumikia MUNGU?
Kama hukulazimishwa basi umeitikia wito wa MUNGU wa kumtumikia, na kwa sababu ni wito kutoka ndani basi tumika kwa KRISTO kwa moyo wa upendo.
Kumbuka;
Ukimtumikia MUNGU yeye atakuheshimu na ukianza kuwatumikia wanadamu MUNGU atakuacha.

Unahitaji kuwa makini ili huduma yako katika Bwana YESU itimize kusudi la MUNGU.
 Usinyamaze pale ambapo unatakiwa kuwaambia watu waokoke.
  '' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22   ''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.

Comments