JIPONYE NAFSI YAKO LEO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Jiponye nafsi yako, usiangalie nyuma.
Mwanzo 19:15-17 '' Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu. Akakawia-kawia; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, kwa jinsi BWANA alivyomhurumia, wakamtoa wakamweka nje ya mji. Ikawa walipomtoa nje, mmoja(Malaika) alisema, JIPONYE NAFSI YAKO USITAZAME NYUMA, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea.''
 Lutu na familia yake walikuwa wanaishi katika duniani ya maovu kama ambavyo wewe leo unaishi katika duniani ya maovu mengi.
MUNGU akaamua kuwateketeza watu wote huko Sodoma na Gomora alikokuwa Lutu lakini ni Lutu  akapata neema mbele za MUNGU. Malaika wa MUNGU waliotumwa kutekeleza adhabu kwa Sodoma na Gomora walimwambia Lutu na mkewe na binti zake wawili kwamba wajiponye nafsi zao wasiangalie nyuma.
Ukweli ni kwamba watenda dhambi wa sodoma na gomora waliangamizwa kwa moto, Lutu na familia yake walipona kwa sababu waliokoka, japokuwa mke wa Lutu aliokoka na kurudi nyuma hivyo naye akaangamia.
Ndugu yangu unayesoma ujumbe huu, ROHO wa MUNGU amenijulisha nikuambie kwamba wewe ambaye hujaokoka jiponye nafsi yako leo na wewe uliyeokoka jiponye nafsi yako na usiangalie nyuma.
Unajiponyaje nafsi yako?
Ni YESU KRISTO pokee anayeweza kukuponya nafsi yako.
Kabla hajaja duniani unabii kumhusu ulisema hivi '' Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake YESU, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.-Mathayo 1:21''
YESU pekee atakayewaokoa watu wenye dhambi, huko ndipo kuwaponya wasiende jehanamu ya milele.
Ndugu, unatakiwa kuokoka leo kwa kumpokea YESU KRISTO kuwa Mwokozi wako, tubu katika KRISTO  dhambi zako zote na kisha usizifanye tena, huko ndiko kujiokoa nafsi yako.
YESU Mwenyewe anapokuja duniani anathibitisha unabii uliosema kwamba atawaokoa watu wenye dhambi, na sasa anasema mwenyewe kwamba  '' mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Yohana 10:10-11''
 Ndugu unatakiwa kumpokea YESU leo,  unatakiwa kujiponya nafsi yako leo.
Wokovu sio kifamilia bali wokovu ni wa mtu binafsi.
Usiseme kwamba baba yako au mama yako wakiokoka ndipo na wewe utaokoka. Ndugu, wokovu sio kifamilia bali wokovu ni wa mtu binafsi katika familia. Inawezekana kabisa familia nzima mkawa mmeokolewa na Bwana YESU lakini kila mmoja atasimama mbele za MUNGU kivyake maana wokovu sio wa kifamilia bali ni wa mtu binafsi.
Ni vyema sana kila mtu katika familia yako au ukoo wako akawa ameokolewa na Bwana YESU.
Wewe ambaye umeshaokolewa na Bwana YESU KRISTO nisikilize kwa makini sana.
YESU KRISTO siku unampokea kama Mwokozi wako alikutoa Misri na sasa uko safarini  kwenda mbinguni, kazi yako iliyobaki ni kujiponya nafsi yako kwa kutokuangalia nyuma.
Lutu na mkewe na binti zake walipata neema kwa MUNGU.
Mwanzo  19:12-13 '' Basi wale watu(Malaika) wakamwambia Lutu, Je! Unaye mtu hapa zaidi? Mkwe, wanao, na binti zako, na wo wote ulio nao katika mji, uwatoe katika mahali hapa; maana tutapaharibu sisi mahali hapa, kwa kuwa kilio chake kimezidi mbele za BWANA; naye BWANA ametupeleka tupaharibu.''
 Hawa walipata neema kwa MUNGU lakini wakwe za Lutu walikataa neema ya wokovu waliyopewa.
Mwanzo 19:14 '' Lutu akatoka akasema na wakweze, waliowaposa binti zake, akasema, Ondokeni mtoke katika mahali hapa kwa sababu BWANA atauharibu mji huu. Lakini akawa kama achezaye machoni pa wakweze.''
 Baada ya wakwe zake kukataa neema ya wokovu, Lutu aliambiwa awachukue mkewe na binti zake wawili na kuanza safari ya kuondoka pale.
Wakiwa safarini mke wa Lutu naye akaamua kuangalia nyuma na kuidharau neema ya MUNGU na baada tu ya kugeuka nyuma akawa nguzo ya chumvi.
Mwanzo 19:26 '' Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi.''
 Hivyo ni watu watatu tu waliokoka katika ile hatari mbaya sana.
Katika maisha ya leo kuna hatari kubwa moja ambayo kila mwanadamu anatakiwa kuiepuka, hatari hiyo inaitwa jehanamu.
Ndugu jiponye nafsi yako leo.
Lutu aliambiwa  na Malaika '' hima jiponye'' yaani fanya haraka sana ujiponye.
Mwanzo 19:22 ''  Hima, ujiponye huko, maana siwezi kufanya neno lo lote, hata uingiapo humo. ........ ''
 Ndugu yangu unayesoma somo hili, nakuomba fanya hima sana ujiponye, Mkimbilie YESU KRISTO Mwokozi uli usalimike.
Warumi 8:1 '' Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika KRISTO YESU.''
 Ndugu, jiponye nafsi yako leo kwa kuokoka.
Mama na Baba jiponyeni nafsi zenu leo kwa kumpokea YESU KRISTO Mwokozi.
Kaka au Dada jiponye nafsi yako leo kwa kuokoka, Kumbuka kwamba Bwana YESU alikuja kukutafuta wewe ili akuokoe.
  '' Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.-Luka 19:10 ''
YESU alikuja ili wewe usiende ziwa la moto, hivyo ndugu jiponye nafsi yako leo, jiponye roho yako leo.
Tuko nyakati za mwisho na maovu ni mengi sana.
Ndugu usiendelee kuwa mzinzi na mwasherati tena, bali okoka na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Ndugu usiendelee kuiba na kusema uongo tena,  bali okoka na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Ndugu usindelee kunywa pombe tena na kuvuta sigara na bangi, bali okoka na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Ndugu usiendelee na uchawi tena wala ushirikina,  bali okoka na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Ndugu usiendelee kwenda kwa waganga wa kienyeji tena wala usiendelee kuhusika na mizimu ya ukoo wenu tena,  bali okoka na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Ndugu usiendelee kutumainia wanajimu tena wala usikubali uwe na nyota yako iliyotokana na unajimu,  bali okoka na kuanza kuishi maisha matakatifu.
Ni saa ya wokovu ndugu, ni saa ya kujiponya nafsi yako.
Tito 2:11-14 '' Maana neema ya MUNGU iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa KRISTO YESU, MUNGU mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.''

Wewe pia uliyeokoka hakikisha huangalii nyuma tena kama mke wa Lutu alivyoangalia nyuma akageuka nguzo ya chumvi.
Kama kabla hujaokoka ulikuwa kahaba, hakikisha baada ya kuokoka huendelei na ukahaba.
Kama ulikuwa mwizi au tapeli hakikisha baada ya kuokoka huendelei na dhambi zako za kwanza.
Kila dhambi yako ya zamani ambayo uliitumikia sana kipindi hujamjua YESU Mwokozi basi sasa baada ya kumpokea YESU kama Mwokozi usikubali kuzitumikia tena dhambi.
Kuirudia dhambi baada ya kuokoka huko ni kuangalia nyuma wakati Neno la MUNGU linakuambia ''Jiponye nafsi yako usiangalie nyuma''
1 Yohana 1:7-9 '' bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.''
 Ndugu, Damu ya YESU KRISTO haifuniki dhambi.
Damu ya YESU KRISTO haipunguzi tu dhambi.
 Damu ya YESU KRISTO hufanya kazi mbili kwako unayetubu na kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.
Damu ya YESU KRISTO huwa inafuta dhambi zako zote unapotubu kwa KRISTO na pia damu ya YESU KRISTO hukutakasa hivyo baada ya kumpokea YESU na kutubu wewe unakuwa sio mchafu tena maana damu ya YESU KRISTO ya agano inakuwa imekutakasa, hivyo sasa unakuwa safi mbele za MUNGU Muumbaji.
Ndugu, hakikisha unajiponya nafsi yako leo.
Kama umeshampokea YESU hakikisha huangalii nyuma tena.
Kwa shetani ulishatoka zamani hivyo usifanyie kazi tena mambo yote ya shetani.
Misri ulishatoka zamani hivyo usienende tena Kimisri.
Wewe sasa uko njiani kwenda mbinguni hivyo hakikisha unafuata ya mbinguni.
Jiponye nafsi yako tena usiangalie nyuma.
Kumbuka mbingu tunayoiendea ni mbingu ambayo hatakuwepo mwovu, ndio maana nasema mpokee YESU leo na kutubu na kuacha dhambi zako zote.
Ufunuo 21:27 '' Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.''
 Bwana YESU anakungoja umtambue kama Mwokozi kisha umpokee kama Mwokozi wako binafsi na kuanza kulitii Neno lake, YESU anakungoja ili aiponye roho yako.
YESU KRISTO anasema '' Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.-Yohana 14:21''

 Ndugu nakuomba jiponye nafsi yako leo kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.
Yohana 1:12-13 '' Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''
Ndugu, asije mtu wa namna yeyote akakudanganya hata kukutoa kwa YESU Mwokozi.
Jiponye nafsi yako leo kwa kuokoka na kuacha dhambi zote.
1 Petro 1;14-15 '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''
 Ndugu, jiponye nafsi yako kwa kuacha uzinzi, uongo, utoaji mimba, uchawi na kila dhambi uzitendazo.
Wagalatia 5:19-21 ''Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa MUNGU.''
Jiponye leo ndugu kwa kuacha dhambi dhambi zote za siri uzitendazo.
Jiponye nafsi yako leo kwa kuacha kuabudu shetani, majini, sanamu au miungu mingine ya namna yeyote.
Ndugu jiponye nafsi yako leo kwa kuacha usaliti wa ndoa.
Jiponye nafsi yako leo kwa kuachana na mahawara wako wote.
Ndugu, niponye nafsi yako leo kwa kumkataa shetani na kazi zake zote.
Ndugu jiponye nafsi yako kwa kumkimbilia Bwana YESU aliye hai.
Mithali 18:10 '' Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.''
 Ndugu jiponye nafsi yako leo, jiokoe nafsi yako leo kwa kumkimbilia YESU KRISTO Mwokozi.
Jiponye nafsi yako leo, nasema tena ni leo ndugu ndio unayo nafasi ya kujiponya nafsi yako, ni leo leo leo leo leoooooooooo.
  '' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22   ''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.

Comments