MAISHA YA MATAKATIFU YA WOKOVU NDIO FUNDISHO LA INJILI YA KRISTO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Maisha ya Wokovu ni maisha ya kumwishia MUNGU katika KRISTO YESU.
Wafilipi 1:21" Kwa maana kwangu mimi kuishi ni KRISTO, na kufa ni faida."

Kama umeokoka na unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO basi tambua kwamba inakupasa kumwishia KRISTO.

Hakikisha unamjua vyema YESU KRISTO na unamfahamu sana ili utende yanayompendeza yeye.
Kuna baadhi ya watu wa MUNGU kazi yao ni kumpinga MUNGU huyo huyo kisha wanadai wako upande wake na wanamtumikia.
Ndugu, Mimi nakushauri kwamba jifunze zaidi kumjua Mwokozi YESU na jifunze kufahamu ni nini kinachompendeza MUNGU ili wewe sasa utende tu yayompendeza yeye.

Waefeso 5:10 " mkihakiki ni nini impendezayo BWANA."
Unaweza ukawa mpinga Kristo harafu huku unajiita uko katika KRISTO huyo huyo, ni hatari sana.
Ndio maana Bwana YESU alisema kwamba sio wote wamwitao Bwana Bwana watakaourithi ufalme wa MUNGU.

Ndugu hakikisha uko upande wa YESU KRISTO Mwokozi na unatenda yanayompendeza.
Mtu asiyedumu katika fundisho la KRISTO huyo mtu hana MUNGU ila ana majini tu na majoka.
2 Yohana 1:9 " Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya KRISTO, yeye hana MUNGU. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba(MUNGU) na Mwana(YESU) pia."
Asiyedumu katika fundisho la KRISTO huyo hana MUNGU.
Asiyedumu katika fundisho la KRISTO hujitenga na KRISTO.
Ukiwa huna YESU KRISTO ujue huna MUNGU.
Usipokuwa na MUNGU ujue una shetani tu.
Asiye na YESU KRISTO huyo hana MUNGU ila ana miungu tu, ni jambo la hatari sana.
Watu wengine wana fundisho la dini tu ila sio fundisho la KRISTO, ni hatari sana.
Watu wengine wana fundisho la dhehebu lao tu ila hawana fundisho la KRISTO, ni hatari sana.
Watu wengine wana fundisho la Nabii wao tu au mtume wao ila hawana fundisho la KRISTO, ni hatari sana.
Ndugu unalihitaji fundisho la KRISTO kuliko chochote.


Hakikisha unazaa matunda mema.
Wanaosikia Neno na wasizae matunda ni kwa sababu
1. Hawafanyii kazi hilo Neno la MUNGU walilolisikia
Yakobo 1:22 " Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu."

2. Wanamruhusu shetani kuliondoa Neno mioyoni mwao .
Mathayo 13:19 "Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia."

YESU KRISTO ni kiunganishi kati ya sisi wanadamu na MUNGU Muumba wetu.
Ukitaka uhusike na MUNGU basi husika na YESU KRISTO.
Ukitaka uhusike n uzima wa milele aliouandaa MUNGU basi husika na Wokovu wa YESU KRISTO.
1 Yohana 5:11-12 " Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima."

Kama ni dini tu na madhehebu vilikuwepo tangu zamani sana lakini viliwafanya wanadamu wasiwe waenda mbinguni.
Mfano hai ni dhehebu la mafalisayo au dhehebu la masadukayo. Hawa walikuwa ni dini na dhehebu zenye mafundisho ya kiroho lakini hazikuwa katika kweli ndio maana MUNGU alimleta YESU KRISTO ili kwa mara moja ya milele watu wanaotaka kwenda uzima wa milele basi wamfuate YESU KRISTO na injili yake.
Yuda 1:3 "Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu."

Waenda uzima wa milele tulikabidhiwa imani ya uzima Mara moja tu kwa YESU KRISTO kufa msalabani ili kutuokoa. Dini za kabla ya hapo na baada ya hapo zilizo kinyume na Bwana YESU hayo ni mapando ya shetani ili kuwapeleka watu jehanamu.
Ndugu unamhitaji YESU KRISTO kuliko unavyohitaji kitu kingine chochote.
Unamhitaji YESU kuliko hata dini na dhehebu.
YESU hakuja kuleta dini(Maana zilikuwepo) Bali habari njema za Ufalme wa MUNGU ili mwanadamu kwa kupitia YESU KRISTO aungane na MUNGU na aungane na ahadi za MUNGU, ahadi juu zaidi ni ya uzima wa milele.
Ndugu nakuomba uelewe kwamba ukiamua kuhusika na YESU KRISTO ndio umechagua kuhusika na MUNGU aliyeziumba mbingu na dunia.
Kumpokea YESU KRISTO na kumtii kama Mwokozi ndio kumpendeza MUNGU.
YESU alikuja kwa faida yako Mwanadamu.
Mpokee kama Mwokozi wako ili uhusike na uzima wa milele.
Yohana 3:16-18 " Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."



Watu wengi misingi ya maisha yao ya kiroho imejengwa juu ya dini na dhehebu na sio juu ya fundisho la KRISTO YESU na Wokovu.
Aliyejengwa juu ya dini huiona dini ni ya thamani kuliko YESU KRISTO Mwokozi.
Mtu aliyejengwa juu ya dhehebu huliona dhehebu lake ni thamani kuliko hata Wokovu.
Mtu aliyejengwa juu ya dini anaweza akamuona Mchungaji/Askofu wake au Mwanzilishi wa dhehebu lake ni wa muhimu kuliko hata Biblia.

Waliojengwa msingi wao wa kiroho katika dini au dhehebu Huwaogopa wanadamu kuliko MUNGU. Anaweza akafanya dhambi huku akijificha Mchungaji au kiongozi wake asimuone. Mtu huyo hamwogopi MUNGU Bali hujaribu kujificha kwa wana Kanisa, huyo hajui kama MUNGU alishamuona kabla ya wote kumuona.
Ndugu zangu, ni muhimu kujua kwamba Bwana YESU hakuleta dini ila alileta Wokovu.
Bwana YESU alileta mfumo wa maisha matakatifu yanayompendeza MUNGU ili tuwe tayari kwa ajili ya uzima wa milele
Matendo 4:12 "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo."

Usipoishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO, hata kama unazingatia sheria za dini na dhehebu hutaweza kuingia uzima wa milele.
Dini na dhehebu vinaweza kujaa misimamo na misimamo mingine ni kinyume na Neno la MUNGU kwa wakati huu.
Dhehebu linaweza kukupa sheria na kujifunza tu kwa mwanzilishi wa dhehebu na kumnyenyekea sana na kumtii sana hata ukawa kama mwabudu sanamu tu.
Dhehebu linaweza kuleta msimamo lakini Wokovu unaekekeza utakatifu katika KRISTO na kisha uzima wa milele.
1 Petro 1:14-15" Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye(YESU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"

Kama dhehebu halifundishi kweli ya KRISTO ni heri kuondoka na kujiunga Kanisa lingine ambako wanahubiri Wokovu na utakatifu bila woga.
Kumbuka ukifanya yaliyo ya KRISTO wewe uko ndani ya KRISTO, na hakuna anyeweza kukutoa kwa KRISTO kama unaishi maisha matakatifu katika yeye.

Bwana YESU anasema  '' Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.-Yohana 10:29 ''  
Ukifanya yanayomchukiza KRISTO wewe uko nje ya KRISTO.
Ukimkosa YESU KRISTO umekosa vyote.
Dhehebu na dini usiviweke sana rohoni hata ukamsahau Bwana YESU.
Kuna watu wakristo wakisikia mtu anaisema vibaya Biblia na yeye anaweza kuwasapoti lakini akisikia mtu anakosoa kitu kidogo kuhusu dhehebu lake anaweza hata akachukua jiwe kumpiga aliyekosoa dhehebu.
Kwa haraka haraka unagundua Kabisa kwamba moyo wa huyo ndugu umejengwa juu ya dhehebu na sio juu ya Neno la MUNGU.


Kila mtu anatamani mabadiliko mazuri ya kiroho.
Jambo muhimu ni unabadilishwa na nani?
Unabadilishwa na nini?
Unabadilikaje.
Kwa wateule wa KRISTO ni muhimu sana kuzingatia mambo haya chini katika mabadiliko ya kiroho mazuri unayotaka.
1. Hakikisha unabadilishwa na YESU KRISTO kwa kumtii.

2. Hakikisha unabadilishwa na Neno la MUNGU.
3. Hakikisha ROHO MTAKATIFU ndio kiongozi wako katika mabadiliko.
 Ndugu Zangu, Hukumu Ya MUNGU I Karibu. 
Ninaumia Moyo Ninapowaona Wababa Na Wamama Wanatenda Dhambi Bila Hofu. 
Ninaumia Moyo Ninapowaona Wakaka Na Wadada Wakifanya Dhambi Kila Saa Na Dakika. 
Bwana YESU anawashangaa akisema  '' Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima.-Yohana 5:40 ''
Ndugu Yangu Unayetenda Dhambi, Je Una Mpango Gani Na Maisha Baada Ya Kufa? 
 Watu Uzinzi Na Uasherati Wamegeuza Kuwa Kama Maji Ambapo Kila Siku Lazima Wanywe Maji. 
Uongo,utapeli Na Wizi Imekuwa Kama Jambo La Kawaida Kwa Walio Wengi, Kwenda Kwa Waganga Wa Kienyeji Imekuwa Fashion. 
Dhambi Za Kila Namna Zinawatesa Wengi. 
Hawa Wote Wakifa Bila Kumpokea YESU Hawawezi Kwenda Uzimani. 
Ndugu Yangu, Hasira Ya MUNGU BABA Itakaposhuka Juu Ya Wanadamu Duniani Utakuwa Wapi Mtenda Dhambi? 
Ndugu Yangu Kimbilia Kwa YESU Leo. Mwanadamu Unayemkataa YESU Leo Elewa Jambo Hili Kwamba Siku Inakuja Ya Hukumu, Wengi Siku Hiyo Watasema "Ni Heri Nisingelizaliwa". Ndugu Hakuna Ujanja Wala Ujuaji Utakaokusaidia Siku Hiyo Ila Mpokee YESU KRISTO Leo, Maana Hakuna Uzima Nje Na YESU, ni wakati wa kujikana 
  Luka 14:26-27 ''Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.''
Ndugu, sio wakati wa kufuata mambo ya kidunia, huu ni wakati wa kuokoka na kuanza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu.

 '' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22   ''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.

Comments