MAOMBI YA KUHARIBU ROHO ZA NYOKA ULIZOZIONA KWENYE ULIMWENGU WA ROHO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi.
Namshukuru sana MUNGU Baba maana shuhuda zinazotokana na masomo haya ni nyingi sana, sifa na utukufu wote ni kwake Muumbaji wetu.
Leo  tunaharibu na kuangamiza roho za nyoka tulizoziona ndotoni au kwenye maono.
Kwa maana nyepesi sana kujua kuhusu nyoka uliyemuona kwenye ulimwengu wa roho ni kwamba nyoka ni adui.
Nyoka huwakilisha adui, hiyo ndio maana nyepesi ya nyoka katika ulimwengu wa roho.
Tangu Mwanzo kabisa tunaona MUNGU akitangaza kwamba kutakuwa na uadui katika ya uzao wa Mwanamke na uzao wa nyoka
Mwanzo 3:15 '' nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.''

Kwa hiyo kwenye ulimwengu wa roho haijalishi umemuona nyoka katika mazingira gani lakini hiyo ina maana ya kwamba ni adui.
Leo tunaomba maombi ya kuangamiza maadui wanaokuja kwa umbo la nyoka ndotoni au kwenye maono, leo kwa maombi yako kupitia jina la YESU KRISTO, malaika wa MUNGU watawaangamiza maadui wote unaowaona kwa umbo la nyoka.
Isaya 27:1 ''Katika siku hiyo BWANA, kwa upanga wake ulio mkali, ulio mkubwa, ulio na nguvu, atamwadhibu lewiathani, nyoka yule mwepesi, na lewiathani, nyoka yule mwenye kuzonga-zonga; naye atamwua yule joka aliye baharini.''
Ukisoma andiko hilo unakutana na maadui wanne walio katika umbo la nyoka ambao MUNGU anaahidi atawaua, roho hizo za nyoka ni nyoka  aina ya Lewiathani wengine huita Leviathan, nyoka mwepesi, nyoka wa kuzongazonga na joka.
Inawezekana wewe unapambana na adui anayezongazonga kila baraka yako, yaani majini wanaharibu kila baraka yako kuanzia afya, ndoa, uzao, uchumi na kibali, na wewe kwenye ndoto au maono huwa unaona tu nyoka mara anakimbia, mara anapanda mti, mara anakula n.k.
Kwa ndoto unakuwa unajulishwa ni adui wa aina gani unapambana naye.
Kumbuka kwamba nyoka humbeba adui, yaani nyoka ndotoni ni nyumba ya kukaa adui. Ndio maana nyoka alimbeba shetani kwenda kumdanganya Eva.
Wewe unaweza ukaona nyoka na usijue unapambana na adui gani maana nyoka ni nyumba tu ya kumbeba adui.
Unaweza ukamuona mchawi akikuroga, wewe huoni mchawi husika kwa sura bali unamuona tu nyoka ndotoni.
Kwa ufupi baadhi tu ya mambo makubwa ambayo unaweza kuona nyoka ndotoni akiwakilisha ni haya.
1. Nyoka huwakilisha majini na majeshi yote ya pepo wabaya.
2. Nyoka huwakilisha mizimu na wakuu wa giza.
3. Nyoka huwakilisha uchawi au mchawi, uganga wa kienyeji au mganga wa kienyeji au unajimu.
4. Nyoka huwakilisha mikataba ya kishetani, mamlaka za kishetani na falme za giza.
5. Nyoka huwakilisha roho ya uongo yaani wewe umevamiwa na roho ya uongo au kuna watu watakuzushia uongo sana utakaoharibu eneo fulani la maisha yako.
Roho za nyoka ni roho za mashetani na hizo hazitakiwi kuhusika na maisha yako mteule wa KRISTO.
MUNGU hukufunulia kwa ndoto ili ujue fikra za shetani na mawakala zake na sasa uharibu mipango hiyo ya giza., hakikisha unazijua fikra za shetani na baada ya kuzijua ziharibu kwa damu ya YESU KRISTO.
2 Kor 2:11 '' Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.''
 Unaweza ukaona nyoka ndotoni na hivyo kujua kusudi la maadui zako kupitia roho ya nyoka uliyoiona.

Makundi mawili ya roho za nyoka.
a. Maajenti wa kuzimu, hawa wametajwa vyema katika Waefeso 6:12 kwamba '' Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.''

b. Wanadamu walio uzao wa nyoka.
Mathayo 23:33 '' Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum?'

 Mwanadamu anapokuwa uzao wa nyoka ina maana hii.

1. Mtu huyo ameingia agano la kishetani, hivyo siku zote hufanya mambo ya kishetani kwa ajili ya kuukuza ufalme wa shetani.
Mathayo 12:34 ''Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake.''

 2. Dini za uongo zote ni uzao wa nyoka.
Dini za uongo ni dini au madhehebu yote yanayopingana na YESU KRISTO na wokovu wake kwa wanadamu wote.
Luka 3:7 ''Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?''
Kwanini dini za uongo ni uzao wa nyoka? Ni kwa wamefundishwa mafundisho yaliyotoka kwa shetani ambaye ndiye joka kuu.
 Ndugu, je wewe ni uzao wa nyoka? au
Je umekataa kuokolewa na YESU KRISTO ?
Kama umekataa kuokolewa na YESU KRISTO hakika umejiwrka katika uzao wa nyoka.
Kama umemkataa YESU hakika unajiweka katika kundi baya yaani uzao wa nyoka.

3. Mtu anayeutumikia ufalme wa shetani.

4. Mtu aliyeingia mikataba ya kishetani.
Katika maombi kama unapambana na mtu aliye uzao wa nyoka  inakupasa kuipiga roho ya nyoka ndani yake ili imwache, kama mtu huyo akishupaza shingo, MUNGU anaweza akampiga kwa maombi yako na anaweza hata akaangamia.
Kwa ufupi wachawi wote, waganga wa kienyeji, wanajimu na kila anayemtumikia shetani, hao ni uzao wa nyoka.
Mfano wa wanadamu walio uzao wa nyoka ni hapa ambapo MUNGU anamwita farao kuwa joka yaani nyoka mkubwa.
Ezekieli 29:3 ''nena, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa aoteaye kati ya mito yake, aliyesema, Mto wangu ni wangu mwenyewe, nami nimeufanya kwa ajili ya nafsi yangu.''

Ngoja nikupe ndoto kadhaa ambazo watu walinishirikisha kuhusu nyoka ndotoni walivyoona.
Mtu wa kwanza aliota akiona jengo  kubwa la ibada(Sio Kanisa) likiwa ni joka kubwa sana jeupe limejikunja katika mfumo wa jengo huku kichwa likiwa juu kabisa na watu wengi wanaingia humo na kuabudu kisha wanaondoka, joka lile lilikuwa limejivilingisha kiustadi  na kuwa jumba zuri la ibada, kichwa chake kilikuwa juu na kichwa hicho ndicho kilikuwa nembo ya dini hiyo.
Hiyo maana yake ni kwamba kuna dini ni uzao wa nyoka maana hawamwabudu MUNGU wa mbinguni anayepatikana katika KRISTO YESU pekee.
Yohana 8:44-45 ''Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo. Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki.''

Mtu wa pili aliota ndoto akimuona mtu mwingine  akimlisha nyoka chakula, hiyo maana yake kuna mtu anatoa kafara au sadaka kwa mashetani na kusababisha vifungo vya kipepo kwa watu fulani.
Pia ni hatari sana kutoa sadaka sehemu ambako YESU KRISTO Mwokozi hayupo. Unaweza ukaongeza vifungo  vya giza na sio kuviondoa.
Kama unampa Mtumishi sadaka hakikisha mtumishi huyo ni mtumishi wa kweli wa YESU KRISTO.
Sadaka zina nguvu sana kiroho lakini ukitoa sehemu ambapo YESU KRISTO hayuko ni hatari kwako.

Siku moja mimi Mwenyewe P Mabula niliota ndoto nikiona kundi kubwa la watu wa kanisa fulani wakiwa katika safari, kwenye hilo kundi alikuwepo na nyoka mmoja mrefu anaenda pamoja na kundi lile.
maana yake katika kundi la watu wa MUNGU wale yuko wakala wa shetani. Hata Kanisani kwenu mnaweza mkaabudu na mchawi, anaweza hata mtumishi akawa ni wakala wa shetani, hakikisha unafanyia kazi kimaombi kile unachoona ndotoni.
Jambo lingine muhimu kuhusu ndoto za nyoka ni kwamba, usifanyie kazi maelekezo ya namna yeyote uliyopewa na nyoka au huyo adui aliye katika umbo la nyoka uliyemuona ndotoni.
Kumbuka nyoka ana vita na wateule wa MUNGU
Ufunuo 12:17 ''Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari. ''  hivyo nyoka ndotoni anaweza hata kukudanganya na kujikuta unafungwa zaidi vifungo vya giza.
Wapo watu leo ni waganga wa kienyeji kwa maelekezo waliyoambiwa na nyoka ndotoni.

 Ngoja nikuambie maana kadhaa za nyoka ndotoni.
1. Kuota nyoka anazunguka nyumba yenu maana yake ndoa yako au familia yenu ina maadui hivyo usipopambana na hiyo roho ya nyoka unaweza kushangaa ndoa inakufa au familia yenu au ukoo unasambaratika.. 
2. Kuota nyoka   nyoka anaingia ndani ya nyumba maana yake ndoa yako, au familia au kundi lenu limeshavamiwa na wakala wa shetani, hivyo mambo yote yanaweza kuharibika usipopambana na roho hiyo ya nyoka.
3. Kuota nyoka anaingia katika chumba chako maana yake mapepo wako katika harakati za kuvamia moyo wako, hivyo okoka, acha dhambi na anza kumcha MUNGU kwa usahihi.
4. Kumuona nyoka kisimani maana yake kuna adui kwenye chanzo chako cha kipato anayekuzuia kufanikiwa.
Wakuu wa giza, wachawi au hata wanadamu wanaotumika kipepo unaweza ukawaona wakiwa nyoka kwenye ndoto au unawaona wakibadilika kuwa nyoka 
Unaweza ukaota ndoto ukimuona nyoka kazini kwako au ukamuona mtu akibadilika nyoka, maana yake  kuna mtu anayetumika kipepo katika kundi la wafanya kazi wenzako.
Nyoka pia ni roho ya uongo hivyo hivyo unaweza ukaona nyoka na usipoomba  maombi ya kuangamiza roho za nyoka utashangaa baada ya muda unazushiwa uongo mbaya ambayo unaweza kupelekea kufukuzwa kazi, kuhamishwa eneo zuri au kusimamaishwa kazi.
Unaweza ukaona nyoka na baada ya siku kadhaa utashangaa familia inagombana, kukufukwa kazi, kukataliwa na mchumba au mwenzi wako wa ndoa n.k
Kuna maana nyingi sana hivyo unamhitaji ROHO MATAKATIFU ili akujulishe nyoka uliyemuona ndotoni awakilisha nini na amebeba nini, nyoka hata anaweza kubeba hata mambo zaidi ya moja hivyo ukijua ndipo utajua aina ya maombi unayotakiwa kuomba ili kuharibu hila hizo za kishetani.
ROHO MTAKATIFU ni wa muhimu sana katika maisha ya kila mwenda mbinguni.
1 Kor 2:10 ''Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.''

Aina ya maombi Kibiblia ya jinsi ya kuziharibu na kuziangamiza roho za nyoka ulizoziona.

1. Kanyaka na kuziangamiza roho za nyoka ulizoziona kwenye ulimwengu wa roho.
Luka 10:19 '' Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.''

Maana yake ni kwamba usiwaruhusu mawakala wa shetani kukushambulia, hivyo washambulie wewe.
Maana take  unyamazishe mipango ya shetani iliyokusudiwa juu yako.

2. Jitenge na roho za nyoka yaani usimbe nafasi shetani katika maisha yako, kumbuka shetani ndio nyoka mkuu.
Waefeso 4:27 '' wala msimpe Ibilisi nafasi.''

3. Mpige kila adui anayekuja kwako kwa umbo la nyoka.
Zaburi 91:13 ''Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu. ''

4. Watoe nyoka watoke katika maisha yako na katika baraka yako.
Marko 16:18a ''watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa  ''

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni MAOMBI YA KUHARIBU ROHO ZA NYOKA ULIZOZIONA KWENYE ULIMWENGU WA ROHO.   Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. 


  MAOMBI YA KUHARIBU ROHO ZA NYOKA ULIZOZIONA KWENYE ULIMWENGU WA ROHO.


 Nakutukuza MUNGU Baba Mwenyezi maana hakuna aliye kama wewe. Nakushukuru Bwana YESU KRISTO Mwokozi wangu maana ulinipenda upeo hata ukanipa thamani mimi niliyekuwa sina thamani.
Nakushukuru ROHO MTAKATIFU maana wewe ndiye Mwalimu wa kweli na wewe ndiye unayeliongoza Kanisa hai la MUNGU duniani.
Eee MUNGU Baba naomba unisamehe dhambi zangu zote, makosa yangu yote na maovu yangu yote, Eee Bwana YESU Mwokozi naomba unipe neema katika wokovu wako, naomba nami unikumbuke katika ufalme wako BWANA, nipe neema niishi maisha matakatifu siku zote za maisha yangu.
Niko hapa leo nikitumia Mamlaka ya jina la YESU KRISTO kuharibu na kuangamiza roho zote za nyoka nilizoziona kwenye ulimwengu wa roho.
Kila adui aliyevaa umbo la nyoka niliyemuona kwenye ulimwengu wa roho, adui huyo nampiga kwa moto wa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
Kila jini na mzimu anayefuatilia maisha yangu au baraka zangu,  nampiga kwa moto wa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
 Kila mkuu wa giza anayefuatilia baraka zangu au maisha yangu nampiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO, mkuu huyo wa giza awe angani au ardhini au habarini au porini au popote, nampiga kwa moto wa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
 Kila nguvu za giza zilizotumwa kichawi ili zije kuniharibia ndfoa yangu, uchumba wangu, familia yangu au kaxzi yangu, hizo nguvu za giza naziharibu kwa moto wa jina la YESU KRISTO.
Kila adui wanamke au mwanaume anayekuja kwangu kwa umbo la nyoka, nampiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO.
MUNGU wangu wa mbinguni amenipa mamlaka nne za kiroho ambazo kwa hizo nawashinda maadui wote kwenye ulimwengu wa roho. Mamlaka hizo ni jina la YESU KRISTO, Damu ya YESU KRISTO, nguvu za ROHO MTAKATIFU na Neno la MUNGU la ufunuo.
Sasa kwa jina la YESU KRISTO nawapiga maadui wote wanaojibadilisha kuwa wanyama au wadudu ninaowaona ndotoni, hao maadui nawapiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO.
kila wakala wa shetani na kazi zake zote naziharibu kwa damu ya YESU KRISTO ya agano.
Kila kifungo nilichofungwa na maadui ambao walikuja kwa umbo la nyoka, hicho kifungo nakinyunyuzia damu ya YESU KRISTO na sasa kwa jina la YESU KRISTO naamuru kifungo hicho kifutike, tena kuanzia sasa kifungo hicho hakitafanya kazi kamwe.
Leo nawashinda maajenti wa kuzimu wote wanaowinda baraka zangu au maisha yangu, nawashinda kwa neno la MUNGU katika jina la YESU KRISTO aliye hai.
Imeandikwa katika Yeremia 5:14 kwamba '' Kwa sababu hiyo BWANA, MUNGU wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala.''
Ni leo maneno yangu yamefanywa kuwa moto na mawakala wa kuzimu kuwa kama kuni na kwa jina la YESU KRISTO moto unawala leo.
Enyi watendakazi wa madhabahu za kuzimu mnaofuatilia ndoa yangu, mnaofutailia kazi yangu, mnaofutailia uchumba, mnaofutailia biashara yangu, kwa mamlaka ya jina la YESU nawapiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO.
Imeandikwa katika Luka 10:19 kwamba Bwana YESU amenipa mamlaka ya kukanyaka nyoka, hivyo kila adui niliyemuona ndotoni kwa umbo la nyoka nampiga adui huyo kwa damu ya YESU KRISTO.
 Katika jina la YESU KRISTO najitenga mbali na kila roho za nyoka.
roho za nyoka za kuleta ajali na mikosi, naziharibu kwa damu ya YESU KRISTO na najitenga nazo mbali kwa jina la YESU KRISTO.
roho za nyoka za kuleta ugomvi katika ndoa, katika uchumba, katika kazi yangu, katika familia yangu na katika kundi langu, hizo roho za nyoka naziharibu kwa damu ya YESU KRISTO na najitenga nazo mbali kwa jina la YESU KRISTO.
 roho za nyoka za kuleta vifungo, balaa, maagano ya giza, ndoa za kipepo au kuleta uzushi,  hizo roho za nyoka naziharibu kwa damu ya YESU KRISTO na najitenga nazo mbali kwa jina la YESU KRISTO.
roho za nyoka za kukaba watu usiku, kunitisha au kuharibu uchumi wangu, hizo roho za nyoka naziharibu kwa damu ya YESU KRISTO na najitenga nazo mbali kwa jina la YESU KRISTO.
Kila roho za nyoka kokote ziliko zinazofuatilia maisha yangu, baraka zangu, afya yangu, ndoa yangu uzao wangu au kibali changu, hizo roho za nyoka naziharibu kwa damu ya YESU KRISTO na najitenga nazo mbali kwa jina la YESU KRISTO.
 Eee MUNGU Baba naomba BWANA kwa ROHO wako mtakatifu kamfunue kila wakala wa shetani aliyejificha kanisani ili nikae mbali naye, kamfunue rafiki yangu anayetumika kipepo dhidi yangu.
Kila mwanadamu anayemtumikia shetani nipe kumjua Eee MUNGU wangu  ili kuanzia sasa nisifanyie kazi ushauri wake wa aina yeyote.
Eee Bwana YESU nakuomba safisha kanisa lako leo, kanisa linahitaji kusafishwa na wewe.
Katika jina la YESU KRISTO kila ndugu yangu, rafiki yangu au mtu wangu wa karibu  aliyevamiwa na mapepo ambao ni roho za nyoka, naziamuru hizo roho za nyoka kumwacha sasa, katika jina la YESU KRISTO aliye hai.
Naharibu kila mipango ya kipepo inayopangwa usiku au mchana kuhusu maisha yangu, nafuta mipango hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila roho ya nyoka haijalishi niliiona miaka mingi iliyopita, haijalishi niliiona ndotoni mwaka uliopita au mwaka huu, hiyo roho ya nyoka naiharibu kwa damu ya YESU KRISTO. kile ambacho roho ya nyoka niliyoiona imekibeba nakiteketeza kwa moto wa damu ya YESU KRISTO.
Kila maadui kwenye ulimwengu wa roho kokote walipo naharibu kazi zao zote na kila ratiba yao na kalenda yao naifuta kwa damu ya YESU KRISTO.
kuanzia sasa mimi nalindwa na damu ya YESU KRISTO.
Kuanzia sasa malaika wa MUNGU Baba watafanya kituo katika maisha yangu.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na na kupokea ushindi.
 Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 4 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi  juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU?  Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsap).

mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments