SADAKA,DHABIHU NA ZAKA KWA UJUMLA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Moja ya masomo ambayo watumishi wengi wa MUNGU hawapendi kufundisha ni pamoja na somo la kuwaagiza watu kuwa watoaji wa zaka, dhabihu na sadaka. Maana mtumishi anaweza hata kukimbiwa na watu kwa sababu tu anawafundisha watu utoaji na kumbe utoaji ni agizo la MUNGU mwenyewe.
Makanisa mengine Mchungaji anaweza kumwita rafiki yake aje afundishe Kanisani kuhusu utoaji maana akifundisha mwenyewe watu watamuona kama anawalazimisha kutoa hela zao ili wampe yeye. Hata mimi kukuletea ujumbe huu leo haikuwa kirahisi sana, ila ROHO wa MUNGU akuhudumie wewe vilevile alivyokusudia.
Tuanze na sadaka ni nini.
Sadaka ni matoleo ya hiari ambayo mtu anamtolea MUNGU ibadani au kwa kwa kuwapa wanaostahili.
Sadaka Ni zawadi inayotolewa kwa MUNGU kwa kusudi la
kuonyesha upendo, heshima na utii Kwa yeye ambaye ingawa tunamtolea yeye lakini nikuonyesha vyote ni vyake na anavimiliki japokua tunavyo sisi.

 Wateule wengi wameshindwa kuwa watoaji wazuri kwa sababu wanadhani walivyonavyo, MUNGU hana mamlaka navyo.
Zaburi 24:1 "Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA, Dunia na wote wakaao ndani yake."

Ndugu mtu wa MUNGU kumbuka hili;
Ulivyonavyo, wewe mwenyewe na utakavyovipata vyote ukiwemo wewe ni Mali ya MUNGU.
Wewe ni wakili tu kwa vitu ulivyonavyo ila mmiliki wa vitu hivyo ni MUNGU.
Utajiri, mshahara mzuri, na mafanikio ya biashara, MUNGU ana mamlaka navyo.
MUNGU anaweza kuvitaka muda wowote kwa faida yako.
Utoaji ni njia mojawapo ya kumtambulisha mtu kwamba ni mnyenyekevu kwa MUNGU.
Ukisikia Sauti ya ROHO MTAKATIFU ndani yako ikikuambia kumtolea MUNGU basi mtolee MUNGU.
Unaweza ukakataa kumtolea MUNGU na ulinzi wa MUNGU ukiondoka katika chanzo chako cha kipato, hakika utamuendea MUNGU baadae ukilia na kutubu, kwa sababu ulidhani kwamba mshahara wako mzuri ni Mali yako na MUNGU hahusiki navyo.
Ni MUNGU mwenyewe ndio anayeagiza wateule wake kuwa watoaji, na utoaji huo utaifanya kazi ya MUNGU kusonga mbele.

2 Kor 9:10-12 ''Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu; mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao MUNGU shukrani kwa kazi yetu. Maana utumishi wa huduma hii hauwatimizii watakatifu riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo MUNGU; ''
Hivyo utoaji ni jambo la muhimu sana pia.
Unaweza ukaving'ng'ania unavyodhani ni vyako na kisha vikaja kukukimbia, lakini ukijua kwamba vyote ulivyonavyo ni Mali ya MUNGU hakika utamweshimu MUNGU hata kwa Mali zako.
1 Nyakati 29:11-13" Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote.
Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote.
Basi sasa, MUNGU wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu."

Kwenye sadaka MUNGU huangalia utii wetu tu kwake.
MUNGU akitaka auone Upendo wetu halisi basi hutujaribu kupitia matoleo.

Matoleo ambayo Biblia inasisitiza ni sadaka, dhabihu na zaka.
Sadaka ziko za aina kama 7 hivyo unavyotoa sadaka ni muhimu uijue sadaka hiyo ni ya nini na ili mtumishi wa MUNGU aombe kama sadaka inavyodai, ndivyo majibu sahihi ya utoaji yatatokea kama ahadi ya MUNGU ilivyo katika Neno lake.
Badhi ya aina za sadaka ambazo Biblia inataja ni
1. Sadaka ya amani(Kutoka 32:6, Yoshua 8:31, 1 Wafalme 8:63)
2. Sadaka ya dhambi(Walawi 4:3, Hesabu 6:14, Ezekieli 43:21)
3  Sadaka ya hatia(Walawi 5:6,Hesabu 18:9,Ezekieli 42:13)
4.  Sadaka ya kuinuliwa(Walawi 7:14,Kumb 12:6, Nehemia 10:37)
5. Sadaka ya shukrani(Yeremia 17:26, Walawi 7:12)
 Ziko nyingi sana zikiwemo sadaka ya malimbuko, sadaka ya mbegu, sadaka ya kawaida, sadaka ya nadhiri n.k

Dhabihu ni nini?
Dhabihu ni matoleo anayotoa mtu  baada ya kutoa sehemu ya kumi ya pato lake.
Dhabihu ni sadaka anayoitoa mtu juu ya fungu kamili la kumi la kipato chake.
Mfano wewe mshahara wako ni lako moja, fungu la kumi au zaka ni 10,000 na unachoongeza juu ya zaka ni dhabihu. Mfano kama Mshahara wako kwa mwezi ni laki tano na wewe unatoa zaka elfu 70 basi zaka ni Elfu 50 na elfu 20  inayobaki ni dhabihu.
Kama wewe unafanya biashara na labda kwa mwezi unapiga hesabu na kukuta faida ni milioni moja basi fungu la kumi ni laki moja na kama utatoa laki na 50 basi hiyo 50 elfu ni dhabihu,
Dhabihu nayo ni kitu cha muhimu sana sana kwa watoaji wanaotaka kumbariki MUNGU na kupokea  ahadi za MUNGU kwa watoaji.
MUNGU Baba anasema  ''Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu. -Zaburi 50:5 '' 
Sadaka za dhabihu wala haziwasumbui watu kutoa ila changamoto kubwa ya utoaji ni zaka au fungu la kumi, na wapi pa kutoa
Nimewahi kuulizwa mara nyingi sana juu ni wapi pa kupeleka fungu la kumi.
Ngoja nijibu hapa.
Sehemu nyingi  za Biblia na sehemu nyingi ambazo MUNGU aliagiza juu ya utoaji zaka ni kupeleka katika nyumba yake yaani Kanisani kwa sasa, na pia MUNGU aliagiza kutoa kwa makuhani au walawi ambao ni watumishi wake, labda ni kwa ajili ya kuiendeleza kazi ya MUNGU na matumizi ya watenda kazi katika nyumba ya MUNGU, Mfano hai wa kupeleka zaka Kanisani ni  Malaki 3:10 '' Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.'' 
Lakini pia nje na Kanisani na nje na kwa watumishi wa MUNGU inaweza ikatolewa kwa yatima na wajane japokuwa watu wengi zaidi wanaotaka kutoa zaka kwa yatima na wajane ni watu wale ambao hutaka  kutoa kiwango kisicho sahihi na fungu la kumi halisi, hapo wanakuwa wanajifurahisa na sio kumtolea MUNGU.
Ndugu mmoja aliniuliza ''Mtumishi kwani ni lazima kutoa zaka kanisani tu?'' Nikamjibu ''Kwani wewe unajisikia kutoa wapi?'' akasema ana miezi miwili sasa huwa anatoa zaka yake kwa yatima, Nikamuuliza ulitoa Shilingi ngapi na mshahara wako ni kiasi gani? nilibaki nacheka maana badala ya kutoa laki moja kama fungu la kumi yeye hupeleka kwa yatima elfu kumi na kusema ametoa fungu la kumi. Nilichogundua ni kwamba asilimia kubwa zaidi ya wanaotaka kutoa zaka nje na Kanisani au nje na Watumishi wa MUNGU, watu hao hawatoi zaka bali hutoa zawadi na huku wao wakiita zaka. Katika kumtolea MUNGU haitakiwi kuwa hivyo, ndio maana siku zote mimi ushauri wangu ni kwamba watu watoe zaka kanisani au mahali ambako wanajifunza Neno la kweli la MUNGU la kuwaimalisha na kuwakuza kiroho.
Na makanisa mengi yana utaratibu wa kutembelea yatima na kusaidia wajane hata kama ni mara moja moja basi pesa yako mtoaji itahusika pia.
Biblia inasema usitoe kila mahali zaka yako au sadaka au dhabihu bali toa kule ambako MUNGU Baba atapachagua.
Kumb 12:11 '' wakati huo itakuwa kwamba mahali pale atakapopachagua BWANA, Mungu wenu, alikalishe jina lake, hapo ndipo mtakapoleta kila kitu ninachowaamuru; sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu zote teule mtakazoweka kwa BWANA.'' 
Anayejua eneo sahihi la kutoa zaka yako, sadaka yako na dhabihu yako ni ROHO MTAKATIFU hivyo mtii sana na kumsikiliza maana yeye ndiye kiongozi wa Kanisa la KRISTO duniani. Enenda kiroho itakusaidia.
Zaka na fungu la kumi ni kitu kimoja yaani ni moja ya kumi ya kipato chako unamtolea MUNGU.
 Kama unafanya biashara na kupata faida, basi moja ya kumi ya faida unatoa zaka.
Jinsi ya kutoa zaka ni pale mtu anapopata kipato.
Jambo kubwa ni kutoa kwa upendo kwa MUNGU 

Kutoka 25:1-2 '' BWANA akanena na Musa, akamwambia, Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. ''
MUNGU hukumbuka matoleo yako na kukutendea mema
Zaburi 20:3-4 ''Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.''
Kumtolea MUNGU matoleo hutengeneza agano na MUNGU, soma Zaburi 50:5
Unaweza ukasoma pia Mwanzo 22 ukaona jinsi Ibrahimu alipomtii MUNGU kutoa sadaka inayomgusa MUNGU alimbariki Ibrahimu na uzao wake wote hata Leo.
Utoaji wako kwa MUNGU unaweza ukatengeneza agano na MUNGU kwa ajili hadi ya uzao wako baada yako.

Unaweza ukatoa sadaka au zaka bila kupenda, lakini huwezi kumpenda MUNGU bila kutoa sadaka na zaka.

Utoaji wakati mwingine huonyesha kiwango chako cha kumpenda MUNGU. Zaka na fungu la kumi ni kitu kimoja yaani ni moja ya kumi ya kipato chako, unamtolea MUNGU. Kuna mtu aliacha ibada baada ya kufundishwa kwamba awe anatoa fungu la kumi la mshahara wake.
Akaamua kuhama Kanisa na kwenda Kanisa lingine akidhani huko hawatoi fungu la kumi. Huko nako baada ya kukuta utaratibu ni ule ule akaamua kuacha kusali na baadae mambo yake yakamzonga akaamua kwenda kwa waganga wa kienyeji na kujikuta ameingia maagano mabaya sana.
Watu wengi sana wamejikuta wakiacha kusali na kugeuka wapagani kwa sababu tu ya fungu la kumi, wengine wamekosa mbingu kwa sababu ya kumwacha YESU na chanzo chao cha kumwacha YESU ni fungu la kumi.

Ndugu yangu, vitu vyote ni Mali ya MUNGU, hata Mali au kipato unachokipata kutokana na kazi yako nzuri serikalini au kwenye makampuni au mashirika, vyote ni Mali ya MUNGU.
Zaburi 24:1" Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA, Dunia na wote wakaao ndani yake."

Hata wewe mwenyewe ni Mali ya MUNGU na hata mshahara wako ni Mali ya MUNGU, MUNGU akiutaka siku yeyote anaweza kuuchukua au kukuondolea hiyo kazi.
Kwa MUNGU tunatakiwa tu kumtii na sii kujaribu kushindana.
Serikali yenyewe ina kukata zaidi ya fungu la kumi na mbili, je kutoa fungu la kumi ndiko kukufanye uwe mpagani na mwenda Jehanamu?


Malimbuko ni sadaka ambazo zinahusisha mazao ya kwanza kwa mkulima kumtolea MUNGU kama shukrani kwa MUNGU kwa kumfanikisha.
Sadaka ni matoleo ya hiari ambayo mtu anamtolea MUNGU.
Katika utoaji zingatia kutoa kwa Imani na sio mazoea.
Zingatia kuambatanisha utoaji wako na maombi.
Mtolee MUNGU kwa moyo na sio kwa kujilazimisha au kwa sababu kuna sheria ya kutoa kwa lazima.

Wengi pia badala ya kutoa matolea sahihi kwa MUNGU wao hutoa zawadi na sio sadaka wala zaka.
Ukitoa zaka isiyotimia unakuwa hujatoa zaka Bali umetoa zawadi.
Ukitoa sadaka ili watu wakuone umetoa, hapo unakuwa umetoa zawadi.
Ukitoa sadaka ili uonekane kwa watu hapo unakuwa umetoa zawadi.
Ukitoa Mali au pesa ya wizi hapo ujue hujatoa kwa MUNGU kwa usahihi Bali umejifurahisha kwa udhalimu wako.
Kibiblia matolea ya kumtolea MUNGU yanaitwa matakatifu na yanatakiwa kuwa hivyo.

Sadaka takatifu ndio inayotakuwa kutolewa ili kupata matokeo sahihi.
Zaka sahihi na timilifu ndio inapaswa kutolewa.

Toa kwa sababu unampenda MUNGU na sio kutoa kwa sababu unavyo.  Kumbuka pia kwamba MUNGU hataki matoleo ya ubatili.
Matoleo ya ubatili ni sadaka isiyo sahihi mfano huwezi kuiba pesa harafu ukasema ''ngoja niipeleke kanisani ili MUNGU anibariki zaidi''. hapo utakuwa unajidanganya wewe mwenyewe na huo ni ubatili mkubwa. matoleo ya ubatili ni pamoja na kupeleka sadaka isiyo sahihi mfano una laki 1 mfukoni lakini unamtoleaMUNGU Tsh. 100. hii sio haki na kumbuka kwamba hata hiyo laki moja uliyonayo ni MUNGU kakupa. na MUNGU hapa anaangalia tu utii wetu sio kwamba ana shida na pesa.
Kumbuka sana hii Kumbu 12:13 ''Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo; '' Hivyo hakikisha unatoa kule ambako ROHO wa MUNGU amekupa amani.
Sadaka inayotoka katika moyo wa mtu aliyeisikia sauti ya MUNGU juu ya kutoa sadaka huwa ina kazi kubwa ila haifuti dhambi.
Ibrahimu alipoambiwa kutoa sadaka nzuri alitoa na MUNGU akasema atabariki hadi watoto wake lakini sio kufuta dhambi, dhambi inafutwa kwa toba na sio kwa sadaka.
Sadaka ina kazi nyingi kiroho lakini haifuti dhambi.

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments