USILIGEUZE KANISA LA MUNGU KUWA PANGO LA WANYNG'ANYI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
Ujumbe huu ni ufunuo kwa kila mwana kanisa popote aliko duniani, naomba somo mpaka mwisho na watumie na wana kanisa wengine popote waliko.
Kwanini nyumba ya MUNGU igeuzwe pango?
Ni nani anaigeuza pango? kwa jinsi gani anaigeuza kuwa pango?
Labda ngoja nianze na maana ya neno pango.
 Pango ni mahali wanapokaa nyoka, mbweha na kila wanyama na wadudu wabaya.
Kanisa la MUNGU halitakiwi kuwa pango maana yake Kanisani hakutakiwi kukaa watu walio na roho za kishetani na walio na ajenda za siri za giza na hakutakiwi kukaa watenda maovu.
Lakini leo kuna baadhi ya makanisa ni mapango ya wanyang'anyi kabisa, wala sio mimi   nasema lakini ni MUNGU Mwenyezi mwenyewe anasema.
Yeremia 7:11 '' Je! Nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, imekuwa pango la wanyang'anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema BWANA.''
 Kanisa la KRISTO halitakiwi kuwa pango la wanyang'anyi.
Kanisani ni mahali wanapotakiwa kuwa watakatifu waliokombolewa kwa damu ya YESU KRISTO, ikiwa tofauti na hivyo ujue mahali hapo ni sawa na pango la wanyang'anyi.
 Kanisani pia mahali ambapo anakuja mwenye dhambi, mchafu lakini kwa lengo kutubu na kukubaliwa na MUNGU, na tangu hapo mtu huyo anakuwa sio mchafu tena.
Marko 11:17-18 '' Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake. ''
 Bwana YESU alipokuwa anayasema haya wala hakuwa anaongea na walio nje ya Kanisani bali walio ndani.
Bwana YESU aliwaambia watu kwamba kwanini wamegeuza nyumba ya MUNGU kuwa pango la wanyang'anyi, wala hakuwa anasema na watu waliokuja kuokoka siku hiyo bali alikuwa anazungumza na viongozi wa hekalu  na washirika wa muda mrefu pale.
Hata leo kuna watu wamegeuza Kanisa la MUNGU kuwa pamgo la wezi maana wanyang'anyi ni wezi.
Kuna watu wako kanisani muda mrefu sana lakini hawajafisha matendo yao ya kale.
Mtu aliokoka akitokea kwenye uzinzi na uasherati lakini hata baada ya kuwa mshirika wa Kanisa anaendelea na uzinzi na uasherati, huyo ameligeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Mtu alikuwa mwizi kabla ya kumpokea YESU, lakini hata baada ya kumpokea YESU ameendelea kuiba, huyo ameligeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Mtu alikuwa changudoa kabla ya kumpokea YESU lakini hata baada ya kumpokea YESU ameendelea kuwa changudoa, huyo ameligeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Mtu alikuwa tapeli kabla ya kumpokea YESU lakini hata baada ya kumpokea YESU hajaacha mtu huyo utapeli, huyo ameligeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Hata wewe ndugu unayesoma ujumbe huu kama unahusika na dhambi fulani kwa siri huku na kanisani ukienda tambua kwamba wewe umeligeuza kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Maovu ya namna yeyote ufanyayo, iwe ni uzinifu, uchawi, kuvaa kikahaba, umbea, usengenyaji n.k hivyo vyote kama hutaviacha hakika wewe umeligeuza Kanisa la MUNGU kuwa pango la wanyang'anyi.
Kuna mtu alikuwa anajichua na mwingine alikuwa anapiga punyeto kabla ya kuokoka, lakini watu hao hata baada ya kuokoka wameendelea na dhambi hizo mbaya, huko ni kuligeuza Kanisa la MUNGU kuwa pango la wanyang'anyi.
Ndugu, ukimpokea YESU KRISTO kama Bwana na Mwokozi wako hakikisha unayafisha yaani kujitenga mbali na  matendo ya dhambi uliyokuwa unayafanya kabla ya kumpokea YESU. 
Wakolosai 3:5-10 '' Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;  kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya MUNGU.  Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo.  Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba.''

Ndugu kumbuka ya kwamba tuko katika nyakati za mwisho, na nyakati hizi ROHO wa MUNGU analionya Kanisa  '' Basi ROHO  anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;-1 Timotheo 4:1''
 Watu wengi sana wamejitenga na imani, yaani wamejitenga na YESU KRISTO na wokovu wake.
Wako pia watumishi ambao wanamtumikia shetani na sio kumtumikia YESU KRISTO Mwokozi, hao wamejifanya kuwa pango la wanyang'anyi maana wao wenyewe ndio wanyang'anyi.
Mathayo 21:13 '' akawaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.''
 Ndugu isiwe ni wewe umeingia kanisani na ajenda yako ya siri ya uchawi na hutaki kuuacha huo uchawi.
Isiwe ni wewe umeingia Kanisani ili uwapate mabinti wasiojitambua au uwapate vijana wasiojitambua ili ushiriki nao uzinzi au uasherati.
Wako watu wametumwa na shetani ili kwenda kuwaangusha watu wa Kanisani.
Wako watu wana mikataba na shetani ili wahakikishe wanawaondoa watu kwa YESU.
Wako watu walitumwa na kuzimu ili kuanzisha makanisa au huduma, hao wameligeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Wako watu wanaimba bongo fleva kanisani,  hao wameligeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Wako watu wanaimba rap au hip hop Kanisani, hao wameligeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Wengine kiujanja ujanja wanawashirikisha wimbo watu waliosimama vyema kiroho hivyo yeye anarap na mwimbaji mzuri anaimba ndani ya wimbo huo, huko ni kukoseshana na ni kuligeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Ulikuwa mwimbaji wa kidunia na ukaokoka, hakikisha sasa unaimba nyimbo za injili halisi.
  Kama wewe ni mwimbaji wa nyimbo za injili usikubali kushirikishwa katika rapa au hip hop na hizo wengine wanaita nyimbo za injili wakati ni rap.
Nakushauri ndugu imba Biblia na sio kuimba mambo mengine, imba YESU KRISTO anayeokoa na sio kuimba mambo mengine.
Wengine wanajiita waimbaji wa nyimbo za injili lakini hata huyo mwenye injili yaani YESU KRISTO hawajawahi kumtaja, haifai kuwa hivyo.
Wako watu wala hawajaokoka ila wanajifanya tu kuwa wameokoka,hao wameligeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Ndugu, usiwe wewe mtu wa namna hiyo.

Ninazo shuhuda nyingi za watu wa Kanisa katika maeneo yao lakini waliponisimulia wenyewe nilibaki nashangaa sana sana, baadhi ya shuhuda hizo ni hizi;
Dada mmoja siku moja alinipigia simu nimuongoze sala ya toba. Nilipokuwa namuongoza sala ya toba ghafla rohoni nikasikia sauti inasema ''Acha'' nilishangaa sana na ndio mara ya kwanza kusikia sauti ya ROHO wa MUNGU ikinikataza kuacha kumuongoza sala ya toba mtu. Niliacha na kumuuliza dada yule kama kuna siri ameficha ambayo anatakiwa aniambie kama mtumishi wa MUNGU ili nimsaidie. Dada yule huku akilia aliniambia maneno magumu  mengi sana, baadhi ya hayo Akaniambia kwamba utaratibu wa dhehebu lao huwa wachungaji wanapata uhamisho mara kwa mara, sasa Kanisani kwao wameshahamia wachungaji watatu tofauti tofauti na wote ameshatembea nao, yeye ni kiongozi Kanisani  lakini hadi mmoja kati ya wachungaji hao alimbebesha mimba   na wakaitoa mimba hiyo, pia alisema ameshawahi kutoa mimba zaidi ya kumi, hakika kanisa kuna mahali limegeuzwa kuwa pango la wanyang'anyi. Ilibidi nimshauri kwa kina sana na kumfundisha na kumuombea maana hasira ya MUNGU ilikuwa kali juu yake, Namshukuru MUNGU huyo mtu aliokoka upya na sasa anamtumikia Bwana YESU katika kweli.
Mama mmoja aliniambia kwamba alienda kuombewa kwa nabii fulani  na alipofika huko nabii alitaka kumbaka kwenye ofisi ya kanisa, hakika Kanisa la MUNGU kuna mahali limegeuka pango la wanyang'anyi.
Rafiki yangu mmoja alihama kikazi, huko alikohamia alikuta zaidi ya nusu ya washirika Kanisani pale ni wachawi, hadi mchungaji na wazee wa Kanisa ni wachawi, hilo ni pango la wanyang'anyi.
Leo hata kutoa mimba kwa baadhi ya watu hata walio Kanisani limekuwa jambo la kawaida sana, huko ni kugeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Leo watoa rushwa na wapokea rushwa hata makanisani wapo, huko ni kugeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
MUNGU hataki Kanisa lake kuwa pango la wanyang'anyi.
MUNGU anataka Kanisani kuwepo waenda mbinguni na sio waenda jehanamu.
Mtu aliyeligeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi anaweza kukosa mbingu.
Ndugu usikubali kuligeuza Kanisa kuwa pango la wanyang'anyi.
Luka 19:45-46 ''Akaingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.''
Ndugu usigeuze Kanisa kuwa kichako chako cha kuficha uovu.
Usivae uchi uchi Kanisani, ukifanya hivyo utakuwa umeligeuza Kanisa kuwa pango la wezi, na wezi hao ni wewe.
  '' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22   ''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.

Comments