USILIVUNJE AGANO LAKO NA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU, nasema na mtu hapa sasa na ni kusudi la MUNGU kabisa.
 Ujumbe wa leo unasema usilivunje agano lako na MUNGU.
Agano ni nini?
Kwa maana nyepesi Agano ni patano au makubaliano.
Hivyo agano lako na MUNGU ni makubaliano baina yako  na MUNGU.
Ni wewe ndio unajua ulikubaliana nini na MUNGU Muumbaji wako.
Je ulikubaliana nini na MUNGU Baba wa mbinguni?
Je ulikubaliana nini  na Bwana YESU juu ya maisha yako?
Ndugu usilivunje agano lako na MUNGU.
Zaburi 111:5 '' Amewapa wamchao chakula; Atalikumbuka agano lake milele.''
 Biblia inasema kwamba MUNGU atalikumbuka agano lake milele.
Wako watu wengi wameweka agano na MUNGU, ndugu usikubali kulivunja agano lako na MUNGU Muumbaji wako.
Wako watu siku moja walikuwa katika nguvu za ROHO MTAKATIFU na katika uwepo wa ROHO MTAKATIFU wakatoa ahadi njema au nadhiri, kwa jinsi hiyo waliingia agano na MUNGU.
Wako watu kwa sababu ya kupitia mazingira magumu sana waliamua kuingia agano na MUNGU au waliweka nadhiri kwa MUNGU, ndugu timiza agano lako na MUNGU, timiza yote yanayohusiana na agano ambalo umeingia na MUNGU.
Kipindi fulani mimi P Mabula nilikuwa katika mazingira magumu sana, vitisho vya wachawi na adha mbaya nyingi, ni zamani, ni zaidi ya miaka ya miaka 15 iliyopita, nilikuwa sijampokea YESU lakini kutokana na mazingira ya hatari niliyokuwepo niliamua kuweka nadhiri mbele za MUNGU kwamba akinipa mambo matatu muhimu sana ninayoyahitaji maishani mwangu basi nitamtumikia hadi watu watanishangaa sana. MUNGU ni mwaminifu sana maana haikutokea wakati huo maana nilikuwa bado kiumri sijayahitaji hayo matatu lakini kwa sababu MUNGU ni mwaminifu na hajawahi kusahau basi muda ulipofika wa kuyapokea nilipokea kimiujiza sana. Ndugu usilivunje agano lako na MUNGU bali litimize.

FAIDA ZA KUWEKA AGANO NA MUNGU.

1. Utazidishiwa baraka zinazohusiana na agano husika.
Mfano ni huu, Hana aliweka nadhiri mbele za MUNGU kuhusu uzao
 1 Samweli 1:10-11 '' Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.''
 Kwa sababu MUNGU ni mwaminifu sana na hukumbuka maagano basi alimtimizia Hana hitaji lake la kupata mtoto wa kiume. Hana alikuwa amefungwa tumbo asizae(1 Samweli 1:5) lakini MUNGU anashika maagano hivyo agano aliloingia Hana mbele za MUNGU lilileta majibu sahihi sana.
 1 Samweli 1:20-22 ''Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA. Kisha yule mtu, Elkana, na watu wote wa nyumbani mwake, wakakwea kwenda kumtolea BWANA dhabihu ya mwaka, na nadhiri yake. Bali Hana hakukwea; maana alimwambia mumewe, Sitakwea mimi hata mtoto wangu atakapoachishwa maziwa, hapo ndipo nitakapomleta, ili ahudhurie mbele za BWANA, akae huko daima.   '' na kwa sababu Hana alitimiza yote yaliyokuwa ndani ya nadhiri yake basi  MUNGU alimwongezea watoto wengine kwa sababu amezingatia agano lake, hata wewe ukizingatia agano lako na MUNGU hakika MUNGU anaweza kukuongezea baraka zinazohusiana na agano husika. Hana aliweka agano kuhusu uzao lakini wewe unaweza ukaweka nadhiri au ukaingia agano na MUNGU kuhusu kitu chochote, ndugu ukitembea kwenye agano hilo na kutimiza hakika MUNGU anaweza kukuongezea baraka nyingi zinazohusiana na agano hilo uliloweka mbele zake.
Hana aliyekuwa tasa alipata watoto sita kwa sababu ya yeye kutimiza yote yaliyo katika agano lake na MUNGU.
1 Samweli 2:21 ''Naye BWANA akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za BWANA.''
 inawezekana wewe ni tasa katika mambo mengi, inawezekana ni tasa katika biashara, kila ukijaribu unafeli. Ndugu nadhiri unayoiweka mbele za MUNGU hakikisha unaitimiza.

2. Uzao wako utakombolewa na MUNGU kama uzao huo uko katika agano lako na MUNGU.
Kutoka 2:24-25 ''MUNGU akasikia kuugua kwao, MUNGU akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo. MUNGU akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.''
 Ukisoma maneno haya ya MUNGU unaiona nguvu ya agano ilivyo ya ajabu sana.
MUNGU alikwenda kuwaokoa waisraeli Misri si kwa sababu walikuwa wanaomba sana bali MUNGU alikwenda kuwatoa Waisraeli Misri kwa sababu ya agalo aliloliweka Ibrahimu miaka mingi kabla. Ndugu, kazi yako au watoto wako au afya yako au biashara yako inaweza kukumbolewa na MUNGU baadae kwa sababu tu wewe uliweka agano mbele za MUNGU na kulitimiza agano hilo.

 3. MUNGU atafanya kama agano lilivyo.
Mwanzo 28:20-22 '' Yakobo akaweka nadhiri akisema, MUNGU akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa MUNGU wangu. Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya MUNGU; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.''
 Yakobo alikuwa mpakani mwa nchi yake na nchi nyingine, akaamua kuweka nadhiri ya agano mbele za MUNGU.
Wakati huo Yakobo alikuwa ana fimbo tu, hana Mali wala vitu vya thamani. MUNGU ni mwaminifu sana maana alitenda kama agano linavyotaka.
Mwanzo 30:27-28 '' Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba BWANA amenibariki kwa ajili yako. Akasema, Sema mshahara wako utakao, nami nitatoa. Akamwambia, Umejua jinsi nilivyokutumikia, na jinsi wanyama wako walivyokuwa kwangu. Maana mali yako ilikuwa haba kabla sijaja, nayo imezidi kuwa nyingi, BWANA akakubariki kila nilikokwenda. Basi sasa, nitaangalia lini mambo ya nyumba yangu mwenyewe? ''

 Ndugu yangu, japokuwa kuweka agano au nadhiri mbele ya MUNGU ni jambo jema sana   na linalowahisha baraka zako kuja kwako lakini pia kumbuka sana kwamba kuna madhara makubwa kama wewe ukienda kinyume na agano uliloweka, kuna madhara kama usipotimiza nadhiri yako.
Ukiweka nadhiri hakikisha unaitimiza, ukiweka agano hakikisha unatimiza.
Binafsi mimi kama Mtumishi wa MUNGU nimeshiriki kuombea watu wengi sana na baadhi ya watu hao waliahidi mbele za MUNGU mambo makubwa sana, lakini baada ya kutendewa muujiza na MUNGU hawakutekeleza nadhiri zao na ahadi zao, hiyo ni hatari. Siku watu hao wanaahidi wala hawakusema ''Mtumishi nikijisikia nitafanya hivi'' bali walisema ''Naahidi mbele za MUNGU kwamba nitafanya hivi, naweka nadhiri leo maana nitatimiza''
Ndugu, ukiweka nadhiri hakikisha unaitimiza.
Kuweka nadhiri sio mpaka uwe mbele za watu, hata moyoni mwako tu unaweza kupanga na asijue mtu yeyote lakini nadhiri hiyo njema kwenye kazi ya MUNGU hakikisha unaitimiza.

MADHARA YA KULIVUNJA AGANO LAKO NA MUNGU.

1.  Utapata laana au adhabu ya kiroho katika kila eneo la maisha yako.
Mfano ni huu, kwa watu walioingia agano la kumtumikia MUNGU  kisha wasitimize kumtumikia MUNGU katika KRISTO, wakaamua kwenda kinyume na agano linavyotaka, Biblia inasema maneno haya kuhusu wao.
Malaki 2:2-4 '' Kama hamtaki kusikia, na kama hamtaki kuitia moyoni, ili kulitukuza jina langu, asema BWANA wa majeshi, basi nitawapelekeeni laana, nami nitazilaani baraka zenu; naam, nimekwisha kuzilaani, kwa sababu hamyatii haya moyoni. Angalieni, nitaikemea mbegu kwa ajili yenu, nami nitapaka nyuso zenu mavi, naam, mavi ya sadaka zenu; nanyi mtaondolewa pamoja nayo Nanyi mtajua ya kuwa mimi nimewapelekeeni amri hii, ili agano langu liwe na Lawi, asema BWANA wa majeshi.''
 Wanaoambiwa hapa ni Walawi yaani watumishi wa MUNGU.
Hata wewe uliyemwahidi Bwana YESU kwamba utamtumikia inakupasa sana kumtumikia ili laana isikufuate.
inawezekana uliingia agano la kumtumikia MUNGU baada ya Bwana YESU kukutendea makuu, ndugu usivunje agano lako na MUNGU. Hebu jiulize mfano, Hana aliingia agano na MUNGU kwamba kama MUNGU atampa Hana mtoto wa kiume basi mtoto huyo Hana angempeleka Hekaluni ili mtoto amtumikie MUNGU daima. Hana baada ya kumpata Samweli angeamua kukaa naye, kumpa majukumu mengine ya maisha na sio kazi ya MUNGU, angesema mfano kwamba anataka mtoto wake asome aje awe Polisi  au daktari na sio Mchungaji, hakika angepata madhara makubwa yeye Hana na Mtoto wake Samweli pia, ndugu jitahidi sana usilivunje agano lako na MUNGU bali litimize.
Watoto wako wanaweza kupata shida kubwa kwa sababu tu wewe ulivunja agano lako na MUNGU.
Wako watu waliahidi kujenga makanisa, kununua viwanja vya kujuenga makanisa, kununua vyombo vya mziki Kanisani lakini MUNGU alipowabariki walivunja agano lao na MUNGU na kuendelea na mipango yao wakidhani ni salama tu. Ndugu unaweza ukakataliwa na MUNGU kwa sababu umeshindwa kumtumikia Bwana YESU.

2.  Hasira ya MUNGU itawaka juu yako na MUNGU atawaacha maadui zako wakutese.
Mfano hai ni huu, Waamuzi 2:20-21 '' Basi hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu; mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa;   ''
 Baada ya Waisraeli kulivunja agano lao na MUNGU kuna mabaya yaliwakuta.
Biblia inasema kwamba hasira ya MUNGU ikawaka juu ya Israeli, inawezekana na kwako hasira ya MUNGU inawaka juu yako kwa sababu umeliharifu agano uliloweka na MUNGU.
Biblia inasema ya kwamba MUNGU hatawafukuza maadui za Israeli kwa sababu Israeli wamelivunja agano lao na yeye.
Hata wewe inawezekana japokuwa unaomba sana lakini wachawi na majini wameruhusiwa waendelee kukutesa kwa sababu tu umevunja agano lako na MUNGU, kwa sababu tu hujatimiza nadhiri ulizoahidi mbele za MUNGU.
MUNGU anaweza asiwafukuzwe wakuu wa giza wanaoshambulia kazi yako, kwa sababu tu umevunja agano lako na MUNGU.
MUNGU anaweza asiwakemee wezi wanaokuibia, anaweza asiwafukuzwe maroho ya magonjwa kwako, hivyo kujikuta kila mara unaibiwa na kila mara unaumwam, kwa sababu tu umelivunja agano lako na MUNGU.
Ndugu, nakuomba sana usilivunje agano lako na MUNGU.
Kama uliapa kwamba utamtumikia Bwana YESU siku zote basi anza sasa kumtumikia kwa kuwafanya watu waokoke. Fanya kazi ya MUNGU kwa uaminifu na juhudi.
Kama uliweka nadhiri ya agano mbele za MUNGU kwamba utamtolea sadaka nzuri basi hakikisha unatimiza.
Ndugu mmoja alisumbuka sana kupata kazi, baadae akaweka nadhiri ya agano kwa MUNGU  kwamba kama MUNGU atampa kazi nzuri atafanya kazi kubwa kanisani kwa pesa zake. MUNGU akambariki kweli kazi nzuri sana. Baada ya kupata kazi yule ndugu akahama kanisa, akabadili line za simu ili wachungaji wasimsumbue, lakini kwa sababu alivunja agano lake kwa MUNGU baada ya muda alifunkuzwa kazi bila kosa, ndipo alianza kwenda kwa watumishi mbalimbali kuombewa bila mafanikio kwa muda mrefu hadi alipolikumbuka agano lake na MUNGU ndipo alirudi kule kule alikoahidi.
Ndugu usikubali kwenda kinyume na agano lako na MUNGU.
MUNGU anasema hataliharifu agano lake wala kulibadili Neno alilosema.
Zaburi 89:34 ''Mimi sitalihalifu agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.''
 Timiza nadhiri yako mbele za MUNGU, timiza agano uliloingia kwa MUNGU.
Kama umesahau anza kukumbuka leo.
 '' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22   ''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.


Comments