JINSI KINYWA CHAKO KINAVYOWEZA KUAMBATANA NA MAMLAKA YA JINA LA YESU KRISTO KATIKA MAOMBI YAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la ushindi katika vita.
Wakristo tumeamuriwa na MUNGU kuomba kupitia jina la YESU KRISTO, ili tupokee kwa MUNGU na ili  tushinde vita vya kiroho dhidi ya maadui zetu wote.
Bwana YESU mwenyewe alilisemea jina lake kuhusu sisi kulitumia katika maombi yetu akisema ''Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.   -Yohana 14:13''
Tena katika Biblia kuna mifano hai mingi tu ya watumishi waaminifu wa MUNGU jinsi walivyoomba kupitia jina la YESU KRISTO  na majibu yakawa sawasawa na walivyoomba kupitia jina hilo kuu kuliko yote.
Mfano mmoja wapo ni huu ambapo kiwete alipona baada ya watumishi wa MUNGU kuomba kupitia jina la YESU KRISTO, kiwete ni mtu ambaye ni mlemavu wa miguu yote miwili, yaani hana uwezo wa kutembea  na kiwete huyu wa kwenye Biblia alikuwa zaidi ya kiwete wa kawaida maana tangu amewazaliwa hadi amekuwa mtu mzima alikuwa hawajawi kutembea, lakini jina la YESU KRISTO likitumiwa kwa usahihi lina mamlaka kuu sana hivyo akapona , Matendo 3:1-10'' Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa.  Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu.  Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka.  Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao.  Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. KWA JINA LA YESU KRISTO WA NAZARETI, SIMAMA UENDE.  Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.  Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu MUNGU. Watu wote wakamwona akienda, akimsifu MUNGU. Wakamtambua, ya kuwa yeye ndiye aliyekuwa akiketi na kuomba sadaka penye mlango Mzuri wa hekalu; wakajaa ushangao wakastaajabia mambo yale yaliyompata.'

 Siku moja ROHO MTAKATIFU alinifunulia mambo manne ya ajabu sana juu ya maombi na maombezi yanayoleta uponyaji dhidi ya magonjwa na ushindi.
Aliniambia kwamba ili mtu apone ugonjwa au afunguliwe vifungo yanahitajika mambo manne yafanye kazi, au moja kati ya hayo manne lifanye kazi kwa utukufu wa MUNGU, hayo manne:

1. Imani ya muombaji.  
Waebrania 11:6 '' Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye MUNGU lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.''

2. Imani ya anayeombewa.
 Mathayo 9:27-30 '' YESU alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; YESU akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana. Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate. Macho yao yakafumbuka. .................  ''

3. Mapenzi ya MUNGU juu ya jambo hilo.
Mathayo 6:10 ''Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.  ''
Yaani ni lazima kuyatafuta mapenzi/ Matakwa ya MUNGU juu ya jambo husika.
Mfano, mgonjwa unayemuombea alikosea na akatamkiwa na watumishi wa MUNGU kwamba atapatwa na mabaya, sasa kuomba tu anaweza asipone maana mapenzi ya MUNGU ni toba kwanza. 
Inawezekana ulionywa sana juu ya uzinzi na ulilitukanisha hadi Kanisa la MUNGU kwa jamii kisha baadae ukapata ukimwi, maombi ya hapo inahitajika kwanza toba ya kina na sio tu kusema ''Kwa jina la YESU KRISTO upone sasa huo ukimwi''

Mfano hai mwingine ni huu, Miriamu  kwa makosa yake alipigwa ugonjwa wa ukoma na MUNGU mwenyewe.
Hesabu 12:10 '' Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma. ''
 sasa kama yuko mtu leo mfano wa Miriamu ana ugonjwa au tatizo kubwa sana lakini ni adhabu ya MUNGU, kumuombea mtu kama huyo ili apone sio tu kusema ''Kwa jina la YESU pona sasa'' bali tafuta mapenzi ya MUNGU juu ya jambo hilo kwanza. Kuna mambo mengine  mapenzi ya MUNGU kwanza ni toba ndipo mlango wa kuombea tatizo litoke unafunguliwa, kuna mengine mapenzi ya MUNGU ni sadaka, mfano ni Mama wa Sarepta(1 Wafalme 17:10-16) 
Inawezekana mapenzi ya MUNGU ni wewe kuliomba msamaha Kanisa la MUNGU ulilolidhalilisha kwa tabia zako chafu, inawezekana Mapenzi ya MUNGU ni wewe ukawaombe msamaha wazazi wako wa kimwili au wa kiroho maana uliwatukana  na kuwazushia uongo, Mapenzi ya MUNGU yako mengi sana kulingana na tatizo la mtu na ufunuo. Sasa muombaji ukiona umeomba mtu apone au atoke kwenye tatizo lakini hakutoka basi tafuta kujua mapenzi ya MUNGU ni nini ili hadi mtu huyo apone.
Siku moja nilikuwa namuombea mtu ili apone ukimwi, nilimwambia atubu kwanza kwa sababu ya uasherati na nikamuongoza sala ya toba lakini pia nilipoanza kumuombea nikapata ufunuo kwamba kama atajazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU na akafanikiwa kunena kwa lugha basi aende akapime kesho yake maana ugonjwa wake ungekuwa umeondoka. Ni kweli mama yule alienda Kanisani kwao na siku hiyo Mchungaji wao akafundisha kuhusu ujazo wa nguvu za ROHO MTAKATIFU. Dada yule akaenda mbele kuombewa, wenzake wakajazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU na kufanikiwa kunena kwa lugha lakini kwake ilichelewa ila baadae sana karibia na ibada kuisha akajazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU na kunena kwa lugha, na baada ya kunena kwa lugha alinipigia simu akifurahi sana kwamba amenena kwa lugha katika ROHO MTAKATIFU. Kesho yake akanenda kupima amepona Ukimwi ule na hadi sasa ni zaidi ya mwaka na nusu ni mzima wa afya. Mapenzi ya MUNGU kwa ndugu yule ilikuwa ajazwe nguvu za ROHO MTAKATIFU na atapona maana nguvu za ROHO MTAKATIFU zinaposhuka kwa mtu zinatanguliwa na moto wa MUNGU unaoweza kuunguza kila kazi za shetani katika maisha ya mtu husika kama kuna kusudi la MUNGU katika hilo(Matendo 2:1-4).
 
4. Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU wa kimaombi.
1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.'' 
 
Ngoja nikupe mifano hai juu ya hili ambayo mimi Peter Mabula nilihusika katika maombezi na watu wakafunguliwa.
Mfano wa kwanza, Siku moja nyumbani tulikuwa tunamuombea binti mgeni nyumbani kwangu, tuliomba kwa muda mrefu ndugu yule mapepo hayajamwachia na alikuwa hoi mno, nilianza kusikiliza rohoni kama nitapata ujumbe wa ROHO MTAKATIFU unaoweza kuwa msaada kimaombi hata binti yule afunguliwe lakini sikupata. Ghafla tulipokuwa tunaendelea na maombi mke wangu akaagiza maji ya kunywa kutoka kwenye friji yakaletwa na akaniambia kwamba amepata ufunuo tuyaombea maji yale na tuombe kwa MUNGU kwamba damu ya YESU KRISTO ya agano iambatane na maji yale kisha tumnyweshe binti yule aliyekuwa amezidiwa sana, ndipo mimi na mke wangu tukashika ile glasi ya maji na kuyaombea maji yale kisha tukampa yule binti anywe na alipokunywa tu akaanza kukohoa na kutapika na  kisha muda huo huo akaanyayuka akiwa amepona kabisa, tukamshukuru MUNGU na  huku mgonjwa yule amepona kabisa.

Siku moja nilikuwa namuombea pia mtu kwa simu na nilipokuwa naomba ghafla upande wangu wa kulia mgongoni juu nilisikia kama kuna kitu kinatembea, ile nataka kuacha kumuombea ndugu yule ili nishughulikie mgongo wangu ghafla nikasikia sauti ikisema ''Mgongoni kwako hakuna tatizo ila nakuonyesha sehemu ambayo ina tatizo katika mwili wa unayemuombea'' Hapo hapo nikaendelea na maombi kwa hasira kali ya kiroho ili mtu yule afunguliwe, niliomba kwa muda na kisha nikamaliza na mtu yule nilipomuuliza kama mgongoni kwake kulia juu huwa anahisi nini. Kwanza alinishangaa sana na kusema Umejuaje Kaka Mabula? Nikamwambia aniambie akasema kwamba kuna kitu huwa anakihisi kinatembea mwilini mwake eneo hilo la mgongo na kutulia. Tangu siku hiyo nilipomuombea, kila nikimuuliza kuhusu kitu hicho anasema hajawahi kukisikia tena na alipata ushindi katika hitaji lake.
Siku moja pia nilipata ufunuo kuhusu miguu ya mtu mmoja niliyekuwa namuombea, siku nyingine wakati naanza kumuombea mtu kwa simu nikasikia harufu mbaya kali sana na nikaelewa kuna roho ya kukataliwa  na kuchafuliwa kipepo iko naye, nilipomaliza kumuombea na kumuuliza akaniambia hayo hayo niliyosikia kwa harufu. Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU unategemea na tatizo la unayemuombea hivyo hatuwezi kukariri ila yeye anaweza kutujulisha kama itabidi maana katika maombi unatakiwa kulenga shabaha katika tatizo na sio kulenga shabaha za kimaombi pembini ya tatizo harafu unataka tatizo litoke.
Mteule wa MUNGU uliyeokolewa na Bwana YESU wewe umepewa amri/mamlaka  ya kuharibu nguvu za giza zote huku ukitumia jina la YESU KRISTO na damu ya YESU KRISTO na Neno la MUNGU katika maombi yako.
Luka 10:19 '' Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.   '' 
Mamlaka ya jina la YESU KRISTO  hutumia kinywa chako ili kuharibu nguvu za giza.
Mamlaka  yako iliyo katika kinywa chako unapoomba ni lazima mamlaka hiyo iambatane na funguo kuu nne za kiroho  za kukushindia, Funguo hizo ni Jina la YESU KRISTO, Damu ya YESU KRISTO, Nguvu za ROHO MTAKATIFU na Neno la MUNGU la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.
Ndugu, ombea kinywa chako ili kiambatane na Mamlaka ya KRISTO na ombea kinywa chako ili kitamke mamlaka ya jina la YESU inayozishinda nguvu zote za giza.
Wewe unazishinda nguvu za giza kwa kinywa tu, hivyo ombea kinywa chako.
Ayubu 22:28 ''Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako.''

Jinsi kinywa chako kinavyoweza kuambatana na mamlaka iliyo ndani ya jina la YESU KRISTO.

1.  Okoka na ishi maisha ya haki.
Waefeso 2:8 ''Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU; '' 

2. Jifunze jinsi ya kuzitumia silaha za MUNGU katika maombi.
Waefeso 6:11 '' Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.'

3. Hakikisha unakuwa mtu wa maombi.
1 Thesalonike 5:17 ''ombeni bila kukoma;''
 Unapoomba mara kwa mara unakuwa unajinoa mwenyewe ili ufanyike silaha kali  ya kuharibu nguvu za giza.
Yeremia 51:20 '' Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; ''

4. Hakikisha unamtii na kumsikiliza sana ROHO MTAKATIFU katika maombi.
Yuda 1:20 '' Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU, ''

5. Amini Mamlaka iliyo katika  KRISTO YESU  kwamba uko nayo kwa sababu umeokoka.
Marko 9:23 '' YESU akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.''

6.   Jiepushe kutumia kinywa chako kwa mabaya.
Hakikisha maneno ya kinywa chako ni mema na yanapata kibali mbele za MUNGU.
Zaburi  19:14 '' Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu. ''

7. Hakikisha unajua kanuni za kiroho za kujua nini cha kufunga na nini cha kufungua, nini cha kuharibu na nini cha kupomoa na nini cha kuangamiza na nini cha kuvunja.

Kuhusu kufunga na kufungua MUNGU amekupa kibali lakini hakikisha unajua ni nini cha kufunga na nini cha kufungua.
Mathayo 16:19 '' Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.''

Kuhusu kuvunja, kubomoa, kuharibu na kuangamiza vitu vya giza umepewa kibali na MUNGU lakini lazima ujue ni kipi kinastahili kuvunjwa na sio kuharibu? Ni nini kinatakiwa kuangamizwa na sio kubomoa n.k
Yeremia 1:10a ''angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ''

8. Tumia Neno la MUNGU katika maombi yako.
Waebrania 4:12-13 '' Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.''

Makosa ya waombaji wengi hata mamlaka ya jina la YESU haifanyi kazi kwao.

1.  Hawana imani thabiti kwa MUNGU.
2 Nyakati 20:20B''mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.''

2. Wanaishi maisha ya dhambi na uovu.
Isaya 59:1-2 ''Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.''
Dhambi ni kikwazo cha mambo mengi sana, na Biblia iko wazi sana ikisema maana ya dhambi kwamba ni uasi kwa MUNGU, Sasa kama umemuasi MUNGU je mamlaka yake iendelee kufanya kazi kwako? Jibu ni hapana. 
1 Yohana 3:4 ''Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.''

3. Kukitumia kinywa kwa yasiyostahili mbele za MUNGU.
Yako mengi yaliyo machukizo kwa MUNGU ambayo mtu anaweza kutumia kinywa chake, na kujinajisi kupitia hayo.
''Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu.-Kutoka 23:1''

Na dhambi mojawapo inayowatesa wengi sana kwa kupitia vinywa vyao ni uongo, hivyo usikubali kukitumia kinywa chako kwa uongo.

Waefeso 4:25 '' Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.''

4. Kutokumsikiliza ROHO MTAKATIFU.
Wanaoongozwa na ROHO MTAKATIFU na wanamsikiliza na kmtii hao ndio watoto wa MUNGU, Sasa usipomsikiliza ROHO MTAKATIFU na kumtii ujue umepungukiwa zaidi ya nusu mambo ya ki MUNGU ya msaa kwako, ni hatari sana.
Kumbuka ROHO MTAKATIFU ndiye anaujua uwanja wa vita yako ya kiroho, ndiye anayewajua maadui zako vyema, ndiye anayejua udhaifu wao na nini ufanye ili kuwashinda, sasa usipokuwa mtu wa kuongozwa na ROHO MTAKATIFU ni hatari sana kwako katika kupata ushindi wa kiroho.

Warumi 8:14 ''4 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''

Maombi ya kuombea kinywa chako ili kianze kuambatana na mamlaka iliyo ndani ya jina la YESU KRISTO.

1. Tubu kwa kilichosababisha mamlaka ya jina la YESU Isifanye kazi kupitia maombi yako.
 Matendo 3:19 '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''

2. Ombea kinywa chako ili kiambatane na mamlaka ya jina la YESU KRISTO na ili kitamke mamlaka.
Yohana 14:14 '' Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.'' 

3. Omba MUNGU akuwekee mlinzi katika kinywa chako ili usitumie kinywa chako kwa mambo mabaya.
Zaburi 141:3-4 '' Ee BWANA, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.  Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya, Nisiyazoelee matendo yasiyofaa, Pamoja na watu watendao maovu; Wala nisile vyakula vyao vya anasa. '' 
 
4.Omba kwa imani ukitamka mamlaka ya jina la YESU huku ukitumia Neno la MUNGU  ili kuharibu nguvu za giza zote. 
Mifano ni hii,
=Una mamalaka ya jina la YESU KRISTO ya kuwaponda mawakala wa shetani.
Zaburi 2:9 ''Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi.''

=Una mamlaka ya jina la YESU KRISTO ya kimaombi ya kuwaangamiza maajenti wa kuzimu.
Yeremia 51:20-21 '' Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake; ''
=Una mamlaka ya kufungua milango katika ulimwengu wa roho wa nuru kwa kinywa chako.
Mathayo 7:7 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; '
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments