JINSI YA KUOMBA MAOMBI YA MUDA MREFU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu!
Karibu, tena karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Nakumbuka Mwaka uliopita nilikuletea hapa somo kuhusu Namna ya kuomba muda mrefu na hata leo kwa ufunuo mkubwa zaidi nakuletea somo lingine kabisa kuhusu kuomba muda mrefu na naamini litakuwa msaada mkubwa kwako katika maisha yako ya kiroho, maana maombi ni sehemu kuu yako ya ushindi katika vita ya kiroho.
Maombi huuboresha uhusiano wako na BABA yako wa mbinguni.
Maombi hukutambulisha kwenye ulimwengu wa roho wa nuru kwamba unahitaji msaada kutoka huko hivyo na wao hutuma msaada wa ajabu sana kwako, hutuma Malaika ili wapigane vita upande wako dhidi ya maadui zako, hutuma Neno la ufunuo ili kukuhakikishia ushindi wako, na ROHO MTAKATIFU unapokuwa mtu wa maombi unakuwa unampa nafasi ya kukusaidia na kukufunulia yaliyo sirini. Kwa ujumla maombi ni muhimu sana katika maisha ya Mteule wa KRISTO anayependwa na MUNGU Baba.
Wakolosai 4:2 '' Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani;''
Ni jambo rahisi sana yaani unatakiwa uwe mtu wa maombi na uwe mtu wa kutoa shukrani kwa MUNGU.

Ili uweze kuomba muda mrefu unahitaji yafuatayo;

1. Unahitaji kuwa na uhitaji wa mambo ya kiroho na uwe na kiu ya kiroho ya kuomba muda mrefu.
Mathayo 5:6 ''Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.''

2. Unahitaji kuujua ulimwengu ulimwengu wa roho vyema.
 1Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.''
Ulimwengu wa roho una vitu vingi sana ambavyo vimefichika hivyo unapopata neema ya kufunuliwa chochote kutoka ulimwengu wa roho basi unaweza kuomba muda mrefu kwa sababu unaona na unajua unahitaji nini kulingana na ulivyofunuliwa, anayetufunulia vitu kutoka ulimwengu wa roho ni ROHO MTAKATIFU.
ROHO MTAKATIFU hutufunulia yote yaliyo katika ulimwengu wa roho wa giza ili tuyaharibu na tupingane nayo kimaombi, ROHO MTAKATIFU pia hutufunulia yaliyo katika ufalme wa MUNGU ili tuombe kuyapata au tuombe na kujua jinsi ya kushirikiana na hayo yaliyo ya MUNGU.
Kuujua ulimwengu wa roho unahitaji tu kuwa na ROHO MTAKATIFU na Neno la MUNGU.

3.  Unahitaji kumtii na kumsikiliza ROHO MTAKATIFU katika maombi.
Yohana 14:26 '' Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.''
Kuna tofauti ya kuwa na ROHO MTAKATIFU na kumsikiliza ROHO MTAKATIFU.
Watu wengi waliookoka wana ROHO MTAKATIFU lakini hawamtii wala kumsikiliza.
Sasa katika maombi ya muda mrefu unahitaji sana kusikiliza maelekezo ya ROHO MTAKATIFU ndipo utaweza kuomba kwa muda mrefu na kuomba katika kusudi la MUNGU.
Kuna mbinu nyingi sana za maombi na kuna aina nyingi sana za maombi. Ukiwa unaomba ROHO MTAKATIFU hukujulisha nini muhimu wakati huo cha kuombea.
Sitasahau siku moja mimi P Mabula nilipanga kuomba maombi na nikayaandika lakini nilipoanza kuomba wala sikuombea maombi yangu maana nilipoanza tu kuomba nilisikioa rohoni ''muombee fulani'' ''ombea kitu fulani'' ''ita kitu fulani'' n.k  huko ndiko kumsikiliza ROHO MTAKATIFU na hiyo kwa urahisi sana unaweza kuomba muda mrefu.

4.Unahitaji kuomba kwa kutumia Neno la MUNGU.
Zaburi 107:20 '' Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.''
Neno la MUNGU ni silaha kuu sana ya kumshinda shetani na mawakala zake.
Kama kuna kitu shetani anakiogopa ni Neno la MUNGU.
Kumbuka Bwana YESU alipokuwa katika maombi ya siku 40 alimshinda shetani kwa Neno la MUNGU.
Neno la MUNGU lina ushindi kamili wa mteule wa MUNGU, Neno lina mamlaka ambayo hakuna yeyote kutoka ulimwengu wa roho wa giza anayeweza kulishinda, Neno lina kibali cha MUNGU cha kukushindia wewe.
Kumbuka MUNGU huliangalia Neno lake ili alitimize.
''  .............  kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.-Yeremia 1:12''
Sasa kwa Mfano wewe unaumwa sana lakini Unasoma Mathayo 9:35 ''Naye YESU alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. ''  inayoonyesha ya kwamba Bwana YESU anaponya magonjwa yote na madhaifu yote, hata huo ugonjwa wao ni rahisi na akuponywa na MUNGU, hivyo kimaombi unadai uponyaji wako ukiomba kwa kutumia Neno hilo, ukimkumbusha Bwana YESU juu ya uponyaji ambao anaweza kuufanya hakika unaweza kuomba muda mrefu na kupona hakika.
Ndugu, unahitaji kuwa na Neno la ufunuo ili uweze kuomba muda mrefu.
Pia Neno la MUNGU linakusaidia ili uombe maombi sahihi maana utakuwa uko ndani ya Neno la MUNGU. Siku moja nilijisikia vibaya baada ya kumsikia Mtumishi mmoja wa MUNGU akiomba maombi akisema ''Nakutuma Roho Mtakatifu uende ..........'' Kwa urahisi kabisa unagundua kwamba maombi hayo sio sahihi. Hakuna Mwanadamu yeyote duniani anayeweza kumtuma ROHO MATAKATIFU wala kumwagiza ila tunamuomba na kwa neema yake anatenda, kumwagiza ROHO MTAKATIFU ni kumwagiza Bwana YESU na ni kumwagiza MUNGU hivyo ni makosa na haiwezekani mwanadamu kumwagiza MUNGU, Hivyo unapoomba kwa kutumia Neno la MUNGU itakusaidia wewe kubaki katika kuomba maombi sahihi. Ndugu aliyeomba maombi hayo nilimfuata na kumwambia amekosea sana kuomba maombi ya kumwagiza ROHO MTAKATIFU, akanielewa na mambo yakawa mazuri.
Siku moja moja mimi P Mabula nilikuwa naomba lakini katika hali ya uchovu lakini ghafla nikasikia rohoni sauti ikisema ''Haribu mitego ya mwindaji(shetani) tumia Zaburi 91:3 " Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. ''
 Yaani Neno hilo la MUNGU lilikuja na nguvu za ajabu ndani yangu maana uchovu ulifutika na nikawa na nguvu za ajabu za kuomba muda mrefu.
Neno la Ufunuo ni muhimu sana katika maombi.
Unahitaji kuwa na Neno la Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU ili uweze kuomba maombi ya muda mrefu.
Kama huna uelewa sana wa Neno la MUNGU basi fanya juhudi nyingi kuisoma Biblia yote na uwe unasoma Biblia kila mara, pia kama huna uelewa sana wa Neno la MUNGU omba huku umeshika Biblia mkononi.
Mfano Neno la Ufunuo kwako la kukusaidia katika maombi ni Zaburi 35:1-8 inayosema kwamba ''Ee BWANA, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami.  Uishike ngao na kigao, Usimame unisaidie.  Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako. Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha chini.  Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia.  Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu.  Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake.''
Sasa kwenye maombi unaweza ukaomba hata masaa manne(4) ukitumia maandiko hayo tu.
Mfano kutokea maandiko hayo ya Zaburi 35
Mstari wa kwanza 
=omba ukimwambia MUNGU atete nao wanaoteta nawe
= MUNGU awazuie kuleta madhara kwako  
=MUNGU awapige wanaopigana na wewe kwenye ulimwengu wa roho, taja maeneo mfano MUNGU apigane nao wanaopigana na wewe kwenye suala la ndoa, afya, uchumi, kibali au uzao  wako.
MUNGU apigane nao wanaopigana na wewe ili kuua ndoa yako au uchumba wako, MUNGU apigane nao wanaotaka ufukuzwe kazi au ufilisike.
Bwana YESU apigane nao wanaoleta hila kwako, kwenye afya yako au kwenye mwili wako.
Kwa andiko hilo tu la Mstari wa kwanza tu la kumwambia MUNGU apigane nao wanaopigana na wewe basi unaweza kutaja maeneo 20 na kila eneo umeliombea dakika 3 basi kwa andiko hilo unaweza kuomba saa moja nzima, Je hadi mistari 8 ya hiyo Zaburi 35 utakuwa umeomba masaa mangapi?
 Mstari wa 6 wa hiyo Zaburi 35  unasema ''Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia.''
Ukihusika na kila kundi la nguvu za giza na mawakala wa shetani wote kwamba njia zao ziwe giza na utelezi unaweza ukaomba hata saa moja na nusu.
Mfano, '' Kila wakala wa shetani anayefuatilia ukoo wako, Familia yako,ndoa yako ,Uchumi wako,Uzao wako,Afya yako, Kazi yako, Masomo yako, Kibali chako, Fursa yako, Huduma yako, Wazazi wako, Kanisa la MUNGU kwenu,taifa lako n.k
Baada ya hapo unahakikisha njia yao inakuwa giza na utelezi maadui wote wanaofanya kazi mchana, jioni, asubuhi,alfajiri, adhuhuri au usiku.
Unaweza ukaomba muda mrefu sana kwa sababu unaye kiongozi wako ambaye ni Neno la MUNGU na ukiomba katika jina la YESU KRISTO.

Mambo muhimu katika maombi haya.

1.Omba MUNGU akupe nguvu za kuomba muda mrefu.
Isaya 40:29  '' Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.''

2. Epuka na nenda kinyume na kila kinachokuzuilia kuomba muda mrefu.
1 Petro 4:7 '' Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala.'' 
Biblia inatutaka tuwe na akili hivyo kwa kutumia akili yako unaweza kuomba vyema na kuviepuka vizuizi vya maombi yako..

Baadhi ya mambo ya kuyaepuka ukiwa unaomba ni haya.
=Ukiona kuomba umekaa kunakuletea usingizi, simama na omba huku umesimama
=Ukiona eneo moja unachoka  omba huku unatembea tembea au kuzunguka hilo eneo ulipo.
=Ukiona kuomba huku umefumba macho kunakuletea usingizi basi omba huku umefumbua macho, unaweza hata kuomba huku umeishika Biblia na unaisoma huku unaomba.
=Ukiona kuomba kwa utulivu sana kunakufanya uchoke basi omba huku ukifanya vitendo na kulingana na maombi yako, mfano unaomba maombi ya kukanyaga nguvu za giza basi hata kwa mara chache onyesha kitendo cha kukanyaga ili tu akili yako isichukuliwe na mambo mengine yanayokutaka kukuzuia kuendelea na maombi n.k

3. Onanisha hali yako ya sasa na tukio la ndani ya Biblia ili upate msukumo wa kuendelea zaidi na maombi.
Mfano katika 2 Wafalme 6:18 Biblia inasema '' Na walipomtelemkia Elisha akamwomba BWANA, akasema, Uwapige, nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha.''  
Tunajifunza nini? Elisha alimuomba MUNGU awapige upofu majeshi ya maadui waliokuwa wamemzunguka na ikawa hivyo hivyo.
 Kumbe Mtumishi mwaminifu wa MUNGU anaweza kuomba kwa MUNGU ili maadui zake MUNGU awapige upofu, Mtumishi wa MUNGU wa sasa ni wewe Uliyeokolewa na YESU KRISTO hivyo unaweza kuomba maombi ya kuwapiga upofu maadui zako katika ulimwengu wa roho.
Hivyo unaweza kuomba MUNGU awapige upofu wakuu wa giza wote wanaokufuatilia, majeshi ya pepo wabaya, majini wote,wachawi na kila mawanadamu anayetumika kipepo dhidi yako.

4. Usiwe na jambo moja tu la kuombea bali msikilize ROHO MTAKATIFU anavyokupeleka kimaelekezo ndani ya uombaji wako, hilo analoliweka moyoni mwako wakati ukiomba husika nalo.
Yuda 1:20 '' Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU,'

Maombi kulingana na Zaburi 35:1-8 baadhi ni haya.
1. MUNGU azungumze nao na kuwaonya wote wanozungumza mabaya kuhusu wewe.
2. MUNGU awapige wanaopigana na wewe kwenye ulimwengu wa roho.
3.Ita msaada wa MUNGU mahali ambapo maadui waliinuka sana.
4. Silaha za MUNGU ziwapige wote wanaokufuata kipepo.
5. Waabishwe, wafedheheshwe,wafadhaishwe na kurudishwa nyuma wote wanaokuzulia mabaya na wanaoitafuta nafsi yako ili waiangamize.
6.Malaika wa MUNGU awafuatilie maadui zako katika ulimwengu wa roho na kuwapiga na kuwaangusha chini hata wasiinuke tena mawakala wa shetani wote.
7. Amuru njia ya mawakala wa shetani iwe giza na utelezi kiasi kwamba hakuna atakayekufikia wewe, hakuna atakayeifikia kazi yako, biashara yako ndoa yako, uchumba wako au kipato chako.
8.Amuru uharibifu uwapate kwa ghafla wote wanaopigana vita na wewe katika uliumwengu wa roho.
Ndugu Kumbuka hii Marko 9:23'' YESU akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu. Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.

Comments