KUNA UKARIMU MWINGINE NI FAIDA KUBWA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU atukuzwe.
Karibu kujifunza ujumbe huu mfupi kuhusu ukaribu.
Kuna ukarimu mwingine una faida kubwa sana ya ushindi kwa anayehusika na ukarimu huo.
Maana ya neno ukarimu ni kutoa vitu au mali na kuwapa watu au kuwasaidia watu wanaohitaji bila kuhitaji malipo.
Mtu mkarimu ni mtu ambaye anayependa kutoa vitu vyake au mali zake na kuwasaidia wengine bila kuwa na uchoyo na bila kutazamia malipo kutoka kwa watu hao.
Katila Biblia kuna watu wengi ambao ukarimu wao uliwaongezea baraka ambazo hawakuwa nazo.
Kama Ibrahimu asingewakaribisha wale watu watatu(Malaika) na kuwapa chakula kizuri hakika inawezekana asingebarikiwa mtoto.
Baada ya kuwapa chakula Malaika wale ndipo mmoja kati yao akalisema kusudi la MUNGU kwamba ''Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. -Mwanzo 18:10''
Sarah alikuwa na miaka 89 wakati huo na hakukuwa na jinsi hata aweze kuzaa, lakini ukarimu wao ulifanya abarikiwe uzao tena akawekwa wazi kabisa kwamba ''Mwakani utapata mtoto wa kiume, yaani wewe Sarah mwakani ukiwa na miaka 90 utazaa Mtoto wa kiume bila kupasuliwa na mtoto wa wewe Sarah mtakuwa na afya njema''
Hakika ikawa vile vile kama Malaika alivyosema.
Hata wewe kuna watu wanaweza kuwa kama Malaika kwako, kuna watumishi waaminifu wa MUNGU wanaweza kuwa kama Malaika kwako, kwa wewe kuwakarimu unaweza ukashangaa ROHO MTAKATIFU anawajulisha jambo la kukubariki na hilo hakika linakuwa.
Ibrahimu na Sarah walijua kwamba hawawezi kupata baraka yao ya uzao, Lakini wakasau kwamba JEHOVAH ni MUNGU wa yale yasiyowezekana kwa wanadamu, ukarimu wa Ibrahimu ulimletea faida kubwa, hata wewe sadaka yako, mali yako, nguo zako, mazao yako au chochote chako kinaweza kuwa chanzo cha baraka kuu kwako.
Biblia inasema hivyo kwa habari ya Ibarimu.

Mwanzo 18:2-11 ''Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako.
Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake.''


Kuna ukarimu mwingine una faida kubwa sana kwako baade.
Mama mmoja alikuwa kahaba na katika ukahaba wake alitoa mimbi nyingi kiasi kwamba akaona aende kutoa kizazi ili aendeleze vyema umalaye wake. Baadae kwa Neema ya MUNGU akapata fundisho la Neno la KRISTO na kuokoka. Baada ya kuokoka kijana mmoja akataka kumuoa, yule dada akakataa maana alijua hawezi kuzaa kamwe hivyo alikuwa amechagua kuishi bila kuolewa. Yule Kijana akakubali kuishi naye katika hali hiyo hiyo. Hivyo wakafunga ndoa Kanisani na baada ya muda kwa sababu ya uaminifu wao basi kuna mtumishi aliwatamkia Neno kiufunuo kwamba watapata mtoto na ajabu ni kwamba yule ambaye alishaondoa kizazi alikuja kuzaa watoto baada ya kutamkiwa Neno.
Ukarimu wa mtu unaweza kumfanya ROHO MTAKATIFU kuwafunuliwa watumishi waliofanyiwa ukarimu ili wambariki mhusika.
Biblia inasema '' Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na MUNGU aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, Haki yake yakaa milele.-2 Kor 9:6-9 ''

 
Unaweza ukafanya ukarimu na wakati huo usione matokeo lakini MUNGU huwa hasahau hivyo kwa wakati wake atakupa kushangilia.
Unaweza ukafanya ukarimu MUNGU akawatendea mema hadi watoto wako na wajukuu kwa sababu ya ukarimu wako.
Sarah na Ibrahimu walipofanya ukarimu sio kwamba walibarikiwa muda huo huo bali baada ya mwaka ndipo baraka yao wakaipata.
Mwanzo 21:1-3 '' BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. ''

 
Mama mmoja alikuwa ni masikini sana na kilikuwa kipindi cha njaa sana hivyo alijua chakula kidogo kilichokuwa kimebaki basi hicho angekula na mtoto wake na kusubiri kufanya maana hakuwa na njia nyingine yeyote ya kupata chakula hata aendelee kuishi.
1 Wafalme 17:10-16 '' Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama BWANA, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya. ''

 
Inawezekana ni wewe kabisa ndio uko katika wakati mgumu sana, ndugu ukarimu unaweza kukuletea faida kubwa.
Wako watu ukarimu wao ulisababisha watumishi wa MUNGU watamke baraka za kazi na kweli wakapata kazi japokuwa kwa muda mrefu haikuwezekana.
Unaweza ukasema mbona ''ninavyo vichache'' MUNGU anaweza kutumia hivyo hivyo vichache na ukapata vingi.
Yaliyoandikwa katika Biblia ni mifano hai ili kukusaidia wewe kuielewa mojawapo ya kanuni ya MUNGU ya kubariki watu wake.
Bwana YESU alipokuwa anaifafanua hiyo kanuni mojawapo ya baraka alisema hivi '' Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa. -Luka 6:38 ''

 
Ukarimu wakati mwingine unaweza kukufungulia milango ya ajabu sana ya baraka.
Unaweza ukapona ugonjwa kwa sababu ya ukarimu.
Unaweza ukafunguliwa vifungo kwa sababu ya ukarimu.
Nilichojifunza ni kwamba ROHO MTAKATIFU kwa watumishi huwa hanyamazi bali huwafunulia na kuwapa mzigo wa kuowaombea waliofanya ukarimu.
Huwa sipendi sana kushuhudia kuhusu mambo kama haya lakini napata msukumo kukujulisha ushuhuda huu wa kweli kabisa ulionitokea mimi Binafsi.
Kuna siku moja kuna rafiki yangu mmoja ambaye tumejuana mtandaoni, siku moja aliniambia jambo la ajabu sana. Aliniambia kwamba anasikia msukumo kutoa sadaka kwangu ili nimuombee, nikamwambia kwamba maombi sio mpaka sadaka. Akasema kwamba analijua hilo na ameshawahi kuona masomo yangu nikikemea watumishi wanaofanya huduma hadi wapewe pesa. Lakini akasema hivyo anasikia msukumo usio wa kawaida sana kutoa sadaka kwangu, nikamwambia tuma, akatuma na mimi nikamuombea kama alivyohitaji. Ilipita miezi mingi sana na mimi siku moja saa sita kamili usiku nikiwa ndio naomba ili nilale ghafla nikamuona mtu kwenye maono akiwa katika jeneza, sikumjua mtu huyo kwa sura hivyo nikajua kwamba kuna mtu anayenihusu yuko katika wakati mgumu sana na anafuatiliwa na roho ya mauti wakati huo. Nilianza kujiombea mimi nikikataa roho ya mauti, baadae nikaombea familia yangu, baadae ndugu zangu wote na baadae rafiki zangu wote na wote ambao husoma masomo yangu mtandaoni, baadae nikaanza kuwaombea wote waliowahi kunisapoti katika huduma. Nimeomba nikamaliza na nilipotaka kulala nikaona tena lile jeneza na ndipo nikajua ni nani mhusika hivyo nikaanza kuomba nikikataa roho ya mauti na nikipambana na kila wachawi, majini na madhabahu za giza ambazo zinampangia uharibifu, niliomba kuanzia saa 6 hadi saa 9 ndipo lile jeneza likatoweka na muda huo huo nikampigia simu yule rafiki yangu na kumuuliza yuko katika hali gani. Akaniambia anaumwa sana na amekuwa anapambana na wachawi live wanaotaka wamwangamize, nikamwambia yaliyotokea na akasema ni kweli kabisa.


Kupitia tukio hilo niligundua kabisa kwamba wakati mwingine ROHO MTAKATIFU anaweza akakupa mzigo wa kuhakikisha fulani hapatwi na mabaya yaliyokusudiwa.
Niliwaza sana maana kama ni marafiki wa mtandanoni ninao wengi sana na hata idadi kamili sina, lakini nikagundua kwamba ukarimu wa mtu unaweza kuwa ukumbusho mbele za MUNGU na MUNGU akawapa kukusaidia kimaombi wale uliowakarimu. Mimi siamini kama ni Mtumishi mwaminifu wa KRISTO umemkarimu kisha asikuombee.


Mimi nakumbuka mwaka 2010 mwishoni yaani siku 3 kabla ya kuingia mwaka 2011 nilipata ajali mbaya sana na madaktari walisema kwamba sitapona. Miezi michache kabla ya hapo kuna mtumishi wa MUNGU mmoja mke wake alikuwa mimba na kikafika kipindi cha kujifungua huku huyo mtumishi hana hata mia mfukoni, mimi nilikuwa na laki 3 tu na hiyo ndiyo ningetumia miezi mingi baadae maana hakika sikuwa na chochote na hiyo pesa ilikuwa kama muujiza tu kwangu maana ilikuja kwangu kimaajabu na sikuwa nimewahi kakamata pesa kama hiyo katika maisha yangu, basi aliponiambia kwamba mkewe yuko hospitalini na hali ni mbaya na inatakiwa pesa ndipo afanyiwe operation na hawana hata pesa ya chakula, nikaamua kumpa pesa ile yote na kweli MUNGU akajalia yule mama akajifungua salama na pesa hiyo ndio pekee iliyokuwa inahitajika hospital hivyo, tukaziama pesa kidogo ya nauli ili kurudi nyumbani. Mama yule alinishukuru sana huku akilia. Sasa nini kilifanyika wakati wa magumu yangu yaani baada ya kupata ajali na kuzimia masaa 15 bila kujitambua? Yule mtumishi alipata msukumo wa kwenda porini pekeyake ili kufunga na kuomba hadi siku akiambiwa mimi nimepona. Yaani anaamua kufunga na kuomba akiwa porini hadi siku atasikia mimi nimepona.
Ukarimu ni jambo muhimu sana ndugu. hivyo katika maisha yako kuna mahitaji mengine unaweza ukafanikiwa baada tu ya kufanya ukarimu kwa watumishi wa MUNGU.
Mchungaji wako anaweza hata kukesha kila siku kwa wiki nzima akikuombea wewe kwa sababu tu ya ukarimu wako, hata kama hataki lakini ROHO MTAKATIFU anaweza kumpa mzigo wa kukuombea kwa sababu tu ya ukarimu ulioufanya kwa mtumishi huyo.
Hata kama hapendi lakini ROHO MTAKATIFU anaweza kumuondolea usingizi na kumpa agizo ili akuombee wewe kwa sababu ulifanya ukarimu kwa kanisa la MUNGU au kwenye kazi ya MUNGU.
''BWANA akujibu siku ya dhiki, Jina la MUNGU wa Yakobo likuinue. Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni. Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.-Zaburi 20:1-4 ''

 
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu. Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.

Comments