MAFUNDISHO YA AWALI BAADA YA MTU KUOKOKA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo nina somo fupi kuhusu watu waliookoka karibuni au watu waliookoka zamani ila hawajui wafanyeje.
Kuna watu waliwahi kuniomba niandae somo kuhusu mafundisho ya awali baada ya mtu kuokoka.
Hii ni sehemu tu ya Masomo kuhusu kipengele hicho.
Hata mimi Katika utumishi wangu kwa KRISTO YESU Mwokozi wangu kuna watu kadhaa niliwaongoza sala ya toba, na wengine walinipigia simu ili niwaongoze sala ya toba maana ndio walikuwa wameamua kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao. Nilifanya hivyo na MUNGU akajitwalia utukufu.
Hakika YESU KRISTO anaokoa wote wanaoamua kumpokea na kumtii kupitia Neno lake, Bwana YESU anasema ''Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. - Yohana 10:28''
Mimi nilipompokea Bwana YESU ilikuwa ni Mwishoni mwa mwaka 2008, Baada tu ya kuokoka nilianza juhudi ya hali ya juu ili nifahamu mambo mengi ya kiroho kupitia Neno la MUNGU.
Nilikuwa sikosekani Kanisani kwenye ibada, kila mkesha wa maombi nilihudhuria. Nilinunua Biblia na Tenzi za rohoni na kwa sababu sikutaka usumbufu basi nilikariri kichwani tenzi 61 kati ya 138 za kitabu cha tenzi za rohoni, hiyo ilinisaidia sana maana ilifika kipindi kiongozi wa ibada akisema fungua tenzi namba mfano 67 mimi wala sikujisumbua sana kuangalia tenzi yangu ilipo japokuwa nilikuwa nayo siku zote. Niliimba kama wengine wanaotumia vitabu, hiyo yoye ilikuwa ni juhudu ya kufahamu mambo mengi ya kiroho.
Baada ya muda nilikuwa nashuhudia mitaani ili watu waokoke.
Nilimsumbua sana Mchungaji kuhusu Ubatizo hivyo akaanza kutufundisha masomo ya ubatizo na baada ya mwezi kama na nusu nikabatizwa.
Niligundua umuhimu wa sala ya toba kwamba mtu anatakiwa kuyaishi hayo maungamo aliyoungama mbele za MUNGU, hivyo nilifanya kila juhudi kuiishi sala ya toba.
Najua kabisa YESU KRISTO ni lazima tumkiri katika kumpokea kama Bwana Na Mwokozi wetu.
Warumi 10:9-10 ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.'' 

 
Na Biblia inaonyesha tangu zamani kwamba watu walikuwa wanaungama na kuachana na mabaya ya kwanza, hivyo nasi katika awamu yetu hii ni lazima kila mmoja kumpokea YESU kama Bwana na Mwokozi wetu.
Mfano ni huu ambapo watu waliungama
''Matendo 18:19-20 ''Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la BWANA lilivyozidi na kushinda kwa nguvu. ''

 
Mimi Peter Nilikariri vipengele muhimu katika sala ya toba na kuanza kuviishi maana huko ndiko kushika maungamo.
1 Timotheo 6:12 '' Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi.''
Vipengele hivyo ni hivi kwa uchache.
a. ''Naufunga ukurasa wa dhambi na sasa nafungulia ukurasa wa kutenda mema'', nilianza kufanya hivyo kwa kuachana na dhambi na kuanza kutenda mema.


b.'' Kuanzia sasa shetani hanihusu tena'', nilhakikisha sijihusishi tena na shetani.


c. ''Natubu dhambi zangu zote na sitazirudia tena'', nilianza juhudi kubwa ya kuachana na dhambi zilizokuwa zinanitesa kabla sijaokoka, niliacha uasherati n.k


Hivyo kila mmoja anatakiwa kuyaishi maungamo yake yaani sala ya toba aliyoongozwa na watumishi wa MUNGU siku anampokea YESU KRISTO kuwa Bwana na Mwokozi wake.
Sasa nataka nitumie nafasi hii kuwashauri mambo yafuatayo Watu waliolichagua fungu jema yaani kuamua kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao.


Ushauri wangu kwenu uko katika mambo haya 10.


1. Baki katika kusudi la MUNGU siku zote.
Warumi 8:28-30 '' Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote MUNGU hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye(YESU) awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.''


2. Baki katika Wokovu wa KRISTO, ndilo kusudi la MUNGU.
Yohana 14:6 ''YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba(MUNGU), ila kwa njia ya mimi.''


3. Baki katika kuishi maisha matakatifu siku zote, ndilo kusudi la MUNGU.
1 Petro 1:14-15 ''Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''


4. Baki katika kumtumikia Bwana YESU siku zote, ndilo kusudi la MUNGU.
1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.''


5. Baki katika maisha ya maombi siku zote, ndilo kusudi la MUNGU.
1 Thesalonike 5:17 ''ombeni bila kukoma;''


6. Baki katika kumtii ROHO MTAKATIFU siku zote, ndilo kusudi la MUNGU.
Warumi 8:14 ''Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU. ''


7. Baki katika kuhudhuria ibada ya mafundisho ya Neno la MUNGU siku zote Kanisani, uwe na moyo wa ibada, hilo ndilo kusudi la MUNGU.
Waebrania 10:25 '' wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia. ''


8. Baki katika kulifanyia kazi Neno la MUNGU unalojifunza, Neno la MUNGU ni sauti ya MUNGU hivyo ifuate sauti hiyo inachokuelekeza, ndilo kusudi la MUNGU.
Kumb 28:1 ''
Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; ''

9. Kataa dhambi zote, makosa yote na maovu yote, ndilo kusudi la MUNGU.
Zaburi 34:14 ''Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''


10. Mngoje MUNGU na atakutimizia mahitaji yako, tena mngoje Bwana YESU kwa ajili ya uzima wa milele.
Zaburi 27:14 ''Umngoje BWANA, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA. ''


Kumbuka kwamba ROHO MTAKATIFU huwa anasema kupitia watumishi wake waaminfu "Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22 ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu. Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.

Comments