MASWALI YA KI NDOA

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu ujifunze kitu kutokana na maswali ambayo baadhi ya marafiki zangu waliniuliza na mimi nikawajibu kwa sehemu kama nilivyojaaliwa.
 Maswali mengine magumu ila yanahitaji majibu vilevile.
Mtu mmoja aliniandikia hivi inbox.
Bwana asifiwe!
mchungaji Mabula, nina jambo nahitaji unijuze kwa maana bado sijakua kiroho kutokana na kutopatikana kwa huduma bora ya MUNGU mahali ninapoishi,siyo kwamba nadharau ila huduma hainijengi kiroho,na ndio maana naitafuta huduma bora mpaka mitandaoni,na ninajengwa na huduma yako,
sasa iko hivi kabla sijampokea YESU kristo mimi tayari nilisha kuwa "nimeoa" yaani nina mwanamke ananiita mme, kutokana na hali fulani ya mazingira ninayoishi,na sisi wote wawili mpaka sasa tumeokoka,ila mke wangu alitangulia kuokoka kabla yangu na aliokoka kabla ya ndoa yetu ya kimila ila mimi niliokoka baada ya ndoa! sasa naomba unifahamishe kuhusu hii ndoa iko vipi katika KRISTO?


Majibu ya P Mabula:
Ndoa yako ni ndoa halisi na halali kabisa. Unachoweza kufanya siku ukipenda ni kuibariki tu hiyo ndoa.
Hizi zote ni ndoa halali.
1. Ndoa ya Kanisani.

2. Ndoa ya kiserikali.
3. Ndoa ya kimila au kitamaduni.
ila tu isiwe ndoa ya kuoa mke zaidi ya mmoja.

Ila pia kama mtu ameshamjua MUNGU na anahitaji kuoa basi ni sheria ya kiroho kwake kufunga ndoa Kanisani.
 Wakolosai 3:17-19 " Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye. Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika BWANA. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao."
Hivyo kwa mtu ambaye ameshaokoka haimpasi tena kufunga ndoa za kimila Bali afunge ndoa Kanisani.
Wewe uwe na amani maana uko katika ndoa sahihi mbele za MUNGU, Mnaweza tu kubariki ndoa yenu.
Wale wote ambao walioana kipindi hawajamjua YESU sio kwamba ndoa zao ni feki.
MUNGU akubariki na songeni mbele na YESU Mwokozi hadi uzima wa milele.
MUNGU akubariki.



Mtu wa pili:
Shalom Pastor Peter Mabula, natumaini u mzima. Pastor kwa muda nimekuwa na mwenzangu I mean mtarajiwa wangu. Binti huyu nilimpata magotini na hata baada ya Mwenyezi Mungu kunifunulia nilimwambia, hakukubali mapema lakini aliniomba muda kufikiria juu ya hilo na baada ya kama mwezi hivi akawa amekubali na mahusiano yakaanza.
Tumeendelea vizuri katika kipindi cha miezi mitano ya mwanzo lakini baadaye akawa ameanza kusumbua upande wa mawasiliano, nikawa nampigia simu wakati mwingine asipokee, nikimtumia SMS asijibu but tukikutana na kumhoji anaomba msamaha. Lakini kabla yangu aliwahi kuwa na mchumba na baadaye akawa amesalitiwa, hivyo siku zingine anadai kuwa uaminifu wake kwa vijana ni mdogo na anakuwa hana imani ma mimi akihofia kukutwa na yaliyomkuta kabla. Lakini kwa wakati wote najitahidi kuwa karibu naye nikijitahidi kumsihi na kumjenga kwa kumwambia awe karibu na Mungu yeye ndiye atakayempa ukweli.
Nikiwa katika harakati za mwisho za maandalizi nilimhusisha akasema usijali na akaniahidi yuko pamoja na mimi na akaahidi kunisaidia kwa maombi. Nikiwa katika harakati za mwisho kabisa naona tena mawasiliano yanakuwa hafifu but kila nikimuuliza Mungu ananipa roho ya ushujaa, nisikate tamaa na nisikubali kushindwa na badala yake niendelee na zoezi langu kama kawaida, nakumbuka siku moja nilikuwa nawaza sana na ghafla nikawa nawaza kusitisha zoezi lakini usiku wake nilifanya maombi mazito sana lakini nakumbuka niliijiwa na ndoto nikiwa na mama mchungaji akinisihi nisivunjike moyo, akawa ananifundisha vitu vingi vinavyohusu mahusiano na kikubwa akawa ananisihi nisiwe mtu wa kumwazia mabaya mtu nimpendaye, na nisiwe mtu kushindwa kizembe. Siku hivyo nakumbuka mama mchungaji alinifundisha vitu vingi kweli na hata nilipoamka asubuhi moyo wangu ulikuwa na amani na hata nilipomtafuta tuliwasiliana vizuri kweli.
Sasa leo ni siku ya tatu tena Pastor, hapokei simu yangu, nikimtumia text hajibu na lakini bado moyo wangu unanishuhudia ushindi na hata nimejaribu kumhusisha baba angu mlezi kiroho ameniambia nisikate tamaa kwani jambo jema halipatikani kivyepesi hivyo niendelee kubaki magotini nikimsihi Mungu juu ya hili.
Ombi langu kwako Pastor, kwanza umekuwa Rafiki yangu kwa muda sasa huko Facebook na nimekuwa nikifuatilia mafundisho yako yananibariki kweli hivyo naomba ushauri pamoja na maombi yako juu ya hili linalonikabili.

Majibu ya Peter Mabula:
MUNGU akubariki Sana.

Kuhusu mahusiano hayo kama unauhakika ni MUNGU alikufunulia uwe na amani.
Usikubali kumhukumu mtu kwa njia ya simu, kama hapokei simu au hapatikani hiyo sio sababu ya kumuona kwamba amebadilika au hana upendo.
Endelea na maombi na sikiliza rohoni hivyo songa mbele.
Jiamini kwamba hata bila yeye una uwezo wa kusonga mbele.
Jikubali kwamba wewe uko vizuri na huyo kama ni wako basi atakuwa wako tu, soma Ayubu 42:2 au Isaya 14:27.
Wewe husika zaidi na MUNGU na sio kuhusika mno na mchumba.
Inawezekana inakuwa hivyo ili kukusaidia mfikie ndoa takatifu , maana inawezekana angekuwa karibu yako sana mngeanguka dhambini na hivyo kuifuta ramani yote njema ya kusudi la MUNGU.
Mimi nitakuombea na naamini MUNGU atakupa ushuhuda mzuri.
Endelea na maombi na utakatifu sana maana utafanikiwa hakika.
Usiruhusu pia uchumba wa muda mrefu Sana.
Maana ya uchumba ni mahusiano ya awali kabla ya ndoa, hivyo uchumba ukiuingia kinachofuata ni ndoa hivyo baada tu ya kupata mchumba anza taratibu kupata kibali kwa wazazi pande zote, anza taratibu za kuposa, kisha kutoa mahari na baada ya hapo mipango ya ndoa. Mambo hayo yote tu yanaweza kuchukua mwaka au mwaka na miezi kadhaa hivyo inakuwa vyema. Sasa kama mahusiano tu yanachukua mwaka au zaidi ya mwaka ujue process za posa, mahari na ndoa zinaweza kuchukua muda zaidi hivyo kujikuta mko kwenye uchumba tu miaka mingi jambo ambalo sio zuri sana, hivyo anza taratibu za kufunga ndoa maana ndio kusudi la uchumba.
Nb. Hata wewe unayesoma ujumbe wa ndugu huyu aliyeniandikia nakuomba kama uko kwenye uchumba basi Fanya juhudi za kufunga ndoa.
Usimchukulie vibaya mchumba wako kwa sababu tu hapatikani kwenye simu.
Jifunze kwa ndugu huyu ambaye anahusika na MUNGU kwa maombi.
Jifunze kwa ndugu huyu ambaye hata katika uchumba wake Baba yake wa kiroho anajua na anajulishwa, ina maana sana hiyo ili kukusaidia wewe.
Kuna wengine huwafuata Baba zao wa kiroho yaani wachungaji ili tu wawafungishe ndoa. Sasa hata viongozi wa kanisa wanashangaa kwamba "Hawa watu uchumba ukianza lini? Uchumba ulitangazwa lini na wapi? Mahari ilitolewa lini maana wana kuja tu wamejipangia na tarehe ya kufunga ndoa yao." Ndugu unaweza ukakutana na vikwazo ambavyo kumbe kosa ni lako. Naamini umejifunza kitu.
MUNGU akubariki sana.

Comments