MTUMISHI WA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
YESU KRISTO alipoondoka alituachia Neno lake la injili yake.
ROHO MTAKATIFU hutuletea Neno la KRISTO na kulifafanua ndani yetu ili tulielewe vyema.

Wakolosai 1:26-28 '' siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao MUNGU alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni KRISTO ndani yenu, tumaini la utukufu ambaye sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika KRISTO.''
 
Neno la MUNGU ni la muhimu sana kwetu na Neno ndilo hutengeneza ushindi wetu na afya zetu za kiroho.

Ndugu, endelea kujifunza Neno la MUNGU na kulitii na kuliishi.
MUNGU huangalia utendaji na utekelezaji wa Yale aliyokuambia.
Ndugu hakikisha unatimiza majukumu ambayo MUNGU amekupa katika kazi ya injili ya Wokovu.

MUNGU akiwa upande wako hatakuacha upotee.
Hakikisha tu MUNGU yuko upande wako.
Ili MUNGU awe upande wako hakikisha tu unampokea YESU KRISTO kuwa Mwokozi wako kisha anza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu na hakikisha baada ya kuokoka unaongozwa na kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Warumi 8:14 "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU."

Ndugu liishi kusudi la MUNGU la kuitwa kwako katika Wokovu.
Kataa dhambi na kila uovu.
Kwa njia hiyo MUNGU Baba atakuwa upande wako na kamwe hatakuacha milele Bali atakuwa na wewe.

Kwa sababu wewe ni mtumishi wa MUNGU ni vyema kujajua haya kwamba kumtumikia MUNGU ni;
1. Kumpokea YESU kama Mwokozi.
2. Kumwabudu MUNGU katika kweli.
3. Kufanya kazi yake kwa kuhubiri injili au kutoa pesa zako kwa ajili ya kuipeleka injili.
4. Kusaidia wengine kiroho ili waokoke na wamwabudu MUNGU katika roho na kweli.
5. Kuomba na kuombea wengine.
6. Kulitimiza kusudi la MUNGU la kuitwa kwako katika KRISTO.
7. Kumtumikia MUNGU kwa kutumia karama za ROHO MTAKATIFU na vipawa vya ROHO MTAKATIFU ulivyopewa.
8. Kufanya kila anachokuagiza MUNGU.
Mfano, Mimi nimeagizwa kuwafundisha watu Neno la MUNGU ili waokoke na waliookoka wamtii MUNGU kupitia KRISTO YESU.
Nisipofuata agizo la MUNGU hapo simtumikii.
Nisiposhika wito wa kuitwa kwangu hapo simtumikii.
Ndugu hakikisha unamtumikia Bwana YESU katika Kanisa lake na injili yake.

1 Kor 4:1-2 ''Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu. ''

Ndugu, Ni heri uonekane kituko kwa watu lakini jina lako liwe kwenye kitabu cha uzima wa milele.
Ni heri uonekane kituko kwa watu lakini ulitimize kusudi la MUNGU.
Ni heri uonekane kituko kwa watu kwa ajili tu ya kuhubiri injili ya KRISTO lakini wewe unajua unachokifanya na unaichuchumilia taji ya uzima.
Wakati mwingine wateule wa MUNGU hupitia mambo ya kudharauliwa au kupuuzwa kwa sababu tu wameokoka lakini kwa MUNGU wateule hao ni watu muhimu sana na wanaitwa heri maana baada ya kuondoka duniani wataenda mbinguni.
Mimi binafsi niliwahi kuambiwa napoteza muda lakini baadhi ya walioniambia hivyo zamani ndio hao hao walikuja kushukuru kwa mafundisho baada ya kufunguliwa.
Wakati mwingine kazi ya injili ni kama kupandisha maji mlimani. Wakati mwingine kuna kuchoka na kukatishwa tamaa lakini ukimjua YESU aliyekuita hakika utasonga mbele kuifanya kazi ya MUNGU.

Kuna watumishi wa MUNGU huonekana kama vituko mitaani kwa sababu wanashuhudia injili, lakini ukweli ni kwamba watumishi hao ni heri sana.
Ndugu, kama unamtumikia Bwana YESU na unaishi maisha matakatifu endelea mbele maana kuna taji ya uzima.
Kazi kubwa ni kusonga mbele kwa utakatifu, maombi na utumishi.
1 Wakorintho 15:58 " Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."
 MUNGU anabaki kuwa ni MUNGU.
Nguvu za MUNGU ziko ndani ya Neno lake zikitenda kazi katika kusudi lake MUNGU.

 Neno la kweli la MUNGU huwa haliji kwa bahati mbaya Bali kwa kusudi.
1 Kor 15:57 '' Lakini MUNGU na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu YESU KRISTO.'

Wewe ni Mtumishi wa MUNGU.
Mtumishi wa MUNGU huwa ana
1. Ana Neno la MUNGU.

Yeremia 1:9 ''Ndipo BWANA akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; ''
 
2. Anamtumikia KRISTO.

Yohana 15:16 '' Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba(MUNGU) kwa jina langu awapeni ''
 
3. Analipeleka kusudi la MUNGU kwa watu wote.

Wafilipi 2:13 ''Kwa maana ndiye MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. ''

4. Ni muombaji.

Mathayo 7:7 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; ''

5. Ni mwanafunzi wa Biblia na aliye tayari katika wakati unaofaa na hata wakati usiofaa

 2 Timotheo 4:2 '' lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho.''

Mtenda kazi anastahili posho yake.
Mathayo 10:7-15 " Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.
Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.
Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake. Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka.
Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi. Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu.
Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule."

Ni kweli kabisa mtenda kazi yaani mhubiri wa injili au Mtumishi wa MUNGU anayetumika vyema anastahili posho lake kutokana na kazi yake, lakini ni muhimu kukumbuka kwamba Bwana YESU kabla hajasema kwamba MTENDA KAZI ANASTAHILI POSHO LAKE alisema neno kwa mtenda kazi kwamba MMEPEWA BURE HIVYO TOENI BURE. Yaani usiuze upako uliyo juu yako kwa pesa, usitoe huduma ya maombezi au ushauri wa kiroho kwa pesa.
Wewe umepewa Neno la MUNGU bure, umepewa ufunuo wa ROHO MTAKATIFU bure, umepewa nguvu za MUNGU bure hivyo toa huduma ya kiroho bure.
Ni kweli mtenda kazi anastahili posho lake lakini ni vyema kujua pia kwamba mtenda kazi anayestahili posho lake ni yule anayetenda kazi na sio yule ambaye sio mtenda kazi hata kama anajiita mtenda kazi.
Kama mtenda kazi ametenda kazi na anaendelea vyema kutenda kazi yake aliyopewa kumtumikia MUNGU, tena anatenda kazi ya injili kwa uaminifu huyo ndio anastahili posho lake.
Katika kazi ya MUNGU matendo ndiyo yanayomtambulisha mtu na sio maneno tu.
YESU KRISTO siku zote anataka kazi yake isonge mbele.
Moses Kulola siku moja aliambiwa na Bwana YESU kwamba "Hakikisha unaniletea kondoo wangu katika zizi langu" baada ya kulijua hilo jukumu alilopewa alifanya kazi ya MUNGU kwa juhudi na na nguvu nyingi, alihakikisha kunakuwa na kondoo wanaojiunga katika zizi la Bwana YESU.
Kila aliyepewa kuwa mtenda kazi inampasa sana kutenda kazi ya MUNGU katika KRISTO YESU kwa juhudi na nidhamu.
Hata mtenda kazi hajapewa posho lake basi haipasi kuacha kumtumikia MUNGU, ukiacha kumtumikia MUNGU kwa sababu hujapata posho lako wewe hukuitwa na MUNGU katika kuitenda kazi yake katika injili ya KRISTO.

Yohana 10:12-13 ''  Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. ''

Kama MUNGU amekupa kufanya kazi yake hakika inakupasa sana kuifanya kwa moyo na juhudi kubwa ili kuiepuka laana ya MUNGU. Kumbuka Biblia inasema amelaaniwa mtu yule aifanyaye kazi ya MUNGU kwa ulegevu.
kumbuka laana ni kitu kinachokukamata ili usiendelee.
Unaweza ukakataa kufanya kazi ya MUNGU kwa sababu tu wewe unataka kufanya biashara, lakini kila biashara utakayoifanya itakataa kwa sababu tu kuna laana ya kumgomea MUNGU kuifanya kazi yake. Dawa ni kutubu na kurudi kufanya maagizo ya MUNGU.

Ndugu, kama MUNGU amekupa kazi yake nakuomba Fanya kazi ya MUNGU kwa bidii na kwa moyo ili usiwe uliyelaaniwa.

Wito wako kwenye injili ya KRISTO unategemea sana;
1. Sauti ya MUNGU.

Kumb 28:1 '' Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; '' 
 
2. Neno la MUNGU.
Waebrania 4:12 '' Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.'' 
 
3. Maongozo ya ROHO MTAKATIFU.
Yohana 14:26 '' Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU , ambaye Baba(MUNGU) atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.'' 
 
4. Kumtumikia Bwana YESU.
 Yohana 12:26 '' Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, BABA atamheshimu.''

5. Kuendelea kumcha MUNGU.
Mithali 1:7 ''Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu. ''
Naamini naongea na mtumishi wa MUNGU na huyo amenielewa vyema ili kuufanyia kazi wito wake katika Kanisa la MUNGU.

 Jambo lingine nataka kukuambia ni hili ya kwamba Mchungaji akiwa ni mwizi ni rahisi sana kundi zima kuwa wezi.
Kiongozi akiwa mwizi ni rahisi sana waliochini yake kuwa wezi.
Baba wa familia akiwa mzinifu itakuwa rahisi mno kwa watoto wake kuwa wazinifu.
Ndugu, kama unamtumikia KRISTO tambua kwamba huduma ya Neno la MUNGU haihitaji mtu mchafu.
Huduma ya kumtumikia Bwana YESU inahitaji watakatifu na sio wachafu.
1 Petro 1:15 "bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"

 
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments