MUNGU WA IBRAHIMU, ISAKA NA YAKOBO

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la leo linaloitwa MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.
Unajua kwanini MUNGU anaitwa hivyo?
Yaani kwanini MUNGU anaitwa ni MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.
Ziko sababu nyingi lakini mbili kati ya hizo ni hizi.
 = MUNGU anaitwa ni MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo kwa sababu MUNGU ni MUNGU wa walio hai.
Mathayo 22:32 '' Mimi ni MUNGU wa Ibrahimu, na MUNGU wa Isaka, na MUNGU wa Yakobo? MUNGU si Mungu wa wafu, bali wa walio hai.''

=Maana nyingine ni kwamba inahusu vizazi vitatu vya wenye akili watatu walioamua kumpendeza MUNGU aliye hai.


1. Kizazi cha Ibrahimu ni kizazi cha imani kubwa sana.

2. Kizazi cha Isaka ni Kizazi cha Ahadi, Ingoje ahadi ya MUNGU Baba kwako.

3. Kizazi cha Yakobo ni kizazi cha washindi. 
Yakobo alishindana na Malaika usiku kucha hadi akabarikiwa baraka yake.

Sasa kama wewe Umeokoka maana yake wewe ni kizazi cha Ibrahimu, Isaka na Yakobo na MUNGU wako ni MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo maana ndivyo MUNGU alivyojiita mwenyewe jina hilo la MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.
Kutoka 3:6 '' ...............  Mimi ni MUNGU wa baba yako, MUNGU wa Ibrahimu, MUNGU wa Isaka, na MUNGU wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia MUNGU. ''
 
1.  Sasa wewe mteule wa KRISTO ni muhimu sana kuwa na Imani thabiti katika Bwana wetu YESU KRISTO, uwe na imani kwa MUNGU kama Ibrahimu.
Waebrania 11:8-10 ''Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni MUNGU.''
 Ndio maana japokuwa waliokuwa na imani thabiti katika KRISTO ni wengi sana lakini ni Ibrahimu tu anaitwa Baba wa imani.
Warumi 4:3 '' Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini MUNGU, ikahesabiwa kwake kuwa haki.''
Basi ndugu hakikisha unakuwa na imani thabiti katika KRISTO YESU maana walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu mwenye imani.
Wagalatia 3:9 '' Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani. ''
Waliompokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao hao ndio uzao wa kiimani wa kiroho wa Ibrahimu aliyekuwa na imani thabiti kwa MUNGU.
Wagalatia 3:29 '' Na kama ninyi ni wa KRISTO, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi ''

 2.  Pia muhimu sana pia kuingoja ahadi ya BWANA kwa utakatifu na maombi. Kizazi cha Isaka ni Kizazi cha Ahadi na ndio maana MUNGU pia anaitwa MUNGU wa Isaka.
Wagalatia 4:28 '' Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi.''

3.  Ni muhimu sana kuwa mshindi na kuishi maisha ya ushindi ukiwa na KRISTO YESU Mfalme wa uzima.
1 Kor 15:57 '' Lakini MUNGU na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu YESU KRISTO.''

Ndugu, uliyeokolewa na Bwana YESU, wewe sasa tambua kwamba MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo ndio MUNGU wako.
Jina la MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo anaitwa YAHWEH/JEHOVAH na huyo ndiye MUNGU wa Kanisa la KRISTO.
Zaburi 83:18 ''Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote.''
Kama MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Israeli/Yakobo ndio MUNGU wako basi hakikisha unatembea kwenye maagizo yake ndipo utafanikiwa kiroho na kimwili.
Mifano hai ni hii; MUNGU atakulinda kama ukimtegemea na kumpa Heshima ya Stahiki.

Zaburi 91:14 "Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu."
Ukimpenda MUNGU hakika atakuokoa dhidi ya adui wabaya wanaofuatilia maisha yako.

Andiko hilo la Zaburi 91:14 katika BHN linasema hivi "
MUNGU asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua!"


Mambo muhimu katika kuhitaji ulinzi wa MUNGU ni haya.

1. Kumpenda MUNGU na kumtegemea.
 
Kumpenda MUNGU sio tu maneno Bali ni maneno na vitendo. Kumpenda MUNGU ni kuokoka na kutii Neno lake.
Isaya 26:3-4 " Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele."


2. Kumwamini na kumtambua.
 
Kumwamini MUNGU Baba ni jambo muhimu sana kama unataka akulinde dhidi ya adui zako.
2 Nyakati 20:20 " .......... mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa."


Unahitaji kumtambua MUNGU kama pekee anayeweza kukulinda.
Unahitaji kumkimbilia Bwana YESU ili ukae salama.
Wasiojitambua wao hutambua hirizi kama ulinzi wao, wewe unayejitambua mtambue Baba kama mlinzi wako.
Wasiojitambua hutambua chale zao ndio ulinzi, wewe unayejitambue mtambue Bwana YESU kuwa ndiye mlinzi na Mwokozi wako.

 Fanya sehemu yako ili MUNGU akamilishe ahadi zake kwako.
Huyo ndiye MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Israeli/Yakobo .
Fanya sehemu yako kwa kuomba kwa imani, fanya sehemu yako kwa kufunga na kuomba.
Fanya sehemu yako kwa kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.
Fanya sehemu yako kwa kumtolea MUNGU sadaka nzuri na zaka.

Huyo ndiye MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Israeli/Yakobo.
  Fanya sehemu yako kwa kusaidia wengine.
Fanya sehemu yako kwa kumtumikia Bwana YESU.
Fanya sehemu yako ili MUNGU atimize ahadi zake kwako.
2 Kor 1:20 ''Maana ahadi zote za MUNGU zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; MUNGU apate kutukuzwa kwa sisi.''


Huyo ndiye MUNGU wa Ibrahimu, Isaka na Israeli/Yakobo
Inawezekana huoni njia, huoni pa kutokea, umesongwa na magumu na vifungo vya giza.
Inawezekana wewe huna tumaini hata moja la ushindi katika vita ya kiroho unayopitia.
Inawezekana hufanikiwi kama unavyohitaji na haujui sababu ni nini.
Ndugu, sababu mojawapo kubwa sana ni wewe kukaa mbali na MUNGU.
Kuna hasara nyingi zinaweza kukupata kwa sababu tu uko mbali na MUNGU yaani huyafanyi yaliyo ya MUNGU.
2 Nyakati 15:2 " …...... BWANA yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi."

Sio kila matatizo yanayompata mtu ni kwa sababu amemwacha MUNGU lakini pia ziko adha pia zinazoweza kumpata mtu kwa sababu yuko mbali na MUNGU.
Yoshua 24:20 " Kama mkimwacha BWANA na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema."

Changamoto ya watu wengi leo ni kwamba wao hutaka MUNGU afanye kama wanavyotaka wao lakini wao hawataki kufanya kama vile MUNGU atakavyo.
Ndugu mteule wa KRISTO, Ukitaka ufaulu na ufanikiwe na kisha uwe na uzima wa milele baadae basi unatakiwa ufanye kile ambacho MUNGU anataka.
Usipende tu MUNGU afanye unachotaka wewe bali hakikisha unafanya kile ambacho MUNGU katika KRISTO YESU anataka.

  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments