NAZUNGUMZA NA MTU HAPA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu Yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Hagai 1:2-7 '' BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujenga nyumba ya BWANA. Ndipo neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa, BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka. BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. ''
 
1. Kama unawaza kwamba huu sio wakati wa kwenda mbele za MUNGU, Zitafakari njia zako.


2. Kama unadhani kwamba huu sio wakati wa kujenga Kanisa la MUNGU, Zitafakari njia zako.

3. Kuna unadhani kwamba huu ni wakati wa wewe kuitelekeza kazi ya MUNGU, Zitafakari njia zako.

Baada ya kufakari njia zako tambua hasara hii itakayokupa kama uko kinyume na kazi ya MUNGU kama maandiko yasemavyo hapo juu.

Hasara ni hizi;
1. Utafanya kazi kubwa sana ya kukunufaisha na utatumia nguvu nyingi sana katika kazi yako hiyo lakini utapata faida kidogo sana sana.


2. Utakula na kunywa lakini hushibi(Hii ina maana kubwa sana kiroho)

3. Utavaa nguo za kuzuia baridi lakini baridi bado itakutesa sana maana hutapata joto(Hii ina maana kubwa kiroho)

4. Utapata Mshahara mkubwa kazini kwako lakini utauweka mshahara huo katika mifuko iliyotoboka toboka, yaani Mshahara utaisha huku hujafanya chochote cha maana(Hii ina maana kubwa sana kiroho)

MUNGU anasema kwenye Neno lake kwamba zitafakari njia zako
Nimeanza na haya kama sehemu ya utangulizi wa somo langu la leo.
Akaunti yako ya kiroho ina hazina kiasi gani?
Inawezekana una hazina nyingi za kimwili, inawezekana una hazina kubwa sana ya nguo na vyakula.
Inawezekana una hazina kubwa sana ya pesa na Mali lakini pia unahitaji sana kuwa na akaunti ya kiroho yenye hazina kubwa sana.
Hakikisha una akaunti kubwa ya maombi, hakikisha una akaunti kubwa ya kiroho yenye hazina ya utumishi wako kwa KRISTO na matendo mema siku zote.
Usikubali kukaa bila akaunti ya kiroho yenye hazina nyingi.
Utakatifu katika KRISTO hutengeneza hazina njema ya kiroho kwako.
Matoleo yako ya hiari na upendo kwa MUNGU hutengeneza hazina njema sana za kiroho kwako.
Matokeo ya utumishi wako kwa KRISTO YESU hutengeneza hazina njema sana za kiroho kwako.
Ndugu, hakikisha akaunti yako ya kiroho ina hazina kubwa na njema mbele za MUNGU.
Mathayo 6:19-21 " Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako."


 Ndugu, nataka kukueleza jambo lingine kwamba ukiinuliwa na MUNGU hakikisha unashuka, ili Ubaki umeinuliwa siku zote.
Wengi wakiinuliwa na MUNGU na wao hujiinua na ndio maana ghafla hujikuta wameshushwa chini.
Ndugu ukiinuliwa katika maisha hakikisha unashuka, ili ubaki kuwa juu.
Ukiinuliwa kihuduma hakikisha unashuka ili ubaki juu.
Ukiinuliwa kwa vyovyote hakikisha unashuka ili kwa njia hiyo ubaki juu.
Najua nisemalo ndio maana nimesema.
Ndugu, Ukiinuliwa na MUNGU hakikisha unashuka.
Yakaobo 4:6 '' Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, MUNGU huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.''
Sio kupata kwako kazi ndio udharau hata watumishi wa MUNGU waliokuwa wanalia usiku na mchana ili kukuombea upate kazi.
Sio kuolewa tu au kuoa ndio kukufanye hata kusalimia watu uache.
Sio kunua gari tu au pikipiki ndio udharau hata wazazi wako waliokuzaa.
Sio huduma yako kupata kibali tu kidogo na mahubiri yako umegeuza, badala ya kumhubiri YESU KRISTO anayeokoa, wewe sasa kazi yako imekuwa kuwasema tu vibaya watumishi wengine wa KRISTO.

Kwanini MUNGU akubariki kisha shukrani umpe mwingine na sio MUNGU?
Ulilia sana kwenye maombi kwamba upate mchumba, MUNGU amekupa na shukrani zote unampa mchumba na sio MUNGU.
YESU amekuponya baada ya watumishi kukuombea, wewe shukrani zote unawapa watumishi hadi unawasujudia.
Ulikuwa unateswa sana na vifungo vya Giza, kwa Neema Bwana YESU amekuondolea vifungo, wewe sifa zote na heshima na shukrani umewapa watumishi ambao hata wao hawajui uliponaje hata kama ni wao walikuombea.
Mlikuwa hamna mtoto kwa miaka 10 katika ndoa yenu, kwa Neema ya MUNGU kwa njia ya maombi YESU KRISTO anawabariki uzao. Sasa wewe kila siku asubuhi mchana na jioni unamshukuru Mumeo au mkeo kwa kukupa uzao, unasahau ni MUNGU tu ndio kawabariki uzao. Mbona mkeo au mumeo kwa miaka 10 hakukupa uzao?
Umesahau au?

Umefanikiwa kiuchumi au kikazi baada ya kuombewa, wewe sasa kila siku asubuhi hadi jioni unamtaja mtumishi aliyekuombea wakati aliyekutendea muujiza ni MUNGU wa huyo mtumishi na sio huyo mtumishi.
Biblia inasema Mshukuruni JEHOVAH MUNGU wa uzima kwa maana yeye fadhili zake ni za milele.
Hakuna mwanadamu mwenye fadhili za milele hivyo mshukuru MUNGU na mpe heshima stahiki.
Sina maana mtumishi aliyekuombea usimshukuru Bali mshukuru Mara moja ila shukrani hiyo kwa mwanadamu isiwe ya kumpa heshima na sifa mwanadamu huyo.
Heshima, sifa, utukufu na adhama ni vya MUNGU tu.

Zaburi 136:3-4 " Mshukuruni BWANA wa mabwana; Kwa maana fadhili zake ni za milele.Yeye peke yake afanya maajabu makuu; Kwa maana fadhili zake ni za milele."

Nataka nikukumbushe na jambo hili pia ya kwamba kuna watu walikuwa na maendeleo mazuri sana ya kiroho kabla hawajapata kazi au hawafanikiwa kibiashara lakini baada ya kubarikiwa wameshuka kiroho kwa spidi kali.
Ndugu inawezekana ni wewe ambaye baada ya YESU kukubariki sasa umhitaji tena. Kanisani huwa unaenda Pasaka tu au Mwaka mpya ukisingizia uko busy.
Watu wa MUNGU wengi wasio na mabadiliko ya kiroho mazuri ni wale ambao;
1. Wanatenda dhambi kwa siri.

2. Hawana uwezo wa kushuhudia injili watu wengine wa nje na Kanisa.
3. Ni watu wa kusinzia tu ibadani.
4. Hawawezi kumkiri YESU KRISTO Mwokozi mbele ya watu.
5. Ni rahisi kwao kutekwa na mafundisho ya mashetani.
6. Hawana nguvu za ROHO MTAKATIFU
7. Hawana imani thabiti katika Wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana.
8. Hawalifanyii kazi Neno la MUNGU wanalojifunza.
Ndugu hakikisha unakuwa na mabadiliko mazuri ya kiroho, usiendelee kuwa mchanga kiroho miaka yote.
Liishi Neno la KRISTO na timiza wajibu wako wote kwa MUNGU.

1 Petro 1:15-19 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Na ikiwa mnamwita Baba(MUNGU), yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO.'

 Wanadamu wengi hawampi MUNGU nafasi ya kwanza katika maisha yao.
Kuna ambao wamezipa ndoa zao au biashara zao nafasi ya kwanza katika maisha yao, hawa mambo yakiharibika katika ndoa zao aubiashara zao ndipo huwa wanamkumbuka YESU na sio wakati mambo yakiwa mazuri katika ndoa zao au biashara zao.
Kuna ambao wamezipa kazi zao nafasi ya kwanza katika maisha yao, mambo yakiwaendea vibaya kazini kwao ndipo wanamkumbuka MUNGU.
Ndugu, nimetumwa nikuambie kwamba mpe MUNGU nafasi ya kwanza katika maisha yako yote.
Mpe YESU nafasi moyoni mwako ili akuokoe kwanza kwa ajili ya uzima wa milele, mpe nafasi ROHO MTAKATIFU atawale maisha yako.

Malaki 1:6 '' Mwana humheshimu baba yake, na mtumishi humcha bwana wake; basi, kama mimi ni baba yenu, heshima yangu iko wapi? Na kama mimi ni bwana wenu, kicho changu ki wapi? BWANA wa majeshi awauliza ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau jina langu. Nanyi mwasema, Tumelidharau jina lako kwa jinsi gani? '' 

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments