NDOA NA MASWALI KUHUSU NDOA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU na tujifunze kupitia maswali ya watu ambao waliniuliza maswali hayo, naamini kuna jambo zuri sana utajifunza.
Kwa sababu maswali niliyoulizwa  yalilenga ndoa basi ngoja nianze kufafanua kidogo kuhusu ndoa.
Ndoa ni nini?
Ndoa ni makubaliano kati ya mwanaume asiye na mke na mwanamke asiye na mume kwa ajili ya kuishi pamoja kama mke na mume.
Makubaliano hayo ni lazima yathibitishwe na wazazi wa pande zote mbili na serikali na Kanisa la MUNGU.

Kwanini wazazi wahusike?
Ni kwa sababu ni wazazi.
Kwanini serikali?
Ni kwasababu ni mamlaka inayoweza kumsaidia mwanandoa kupata haki zake hata kipindi mwenzi wake hayupo.
Uhusika wa serikali ni kutoa vyeti vya ndoa.
Mfano mume akifariki kisha ndugu wa mume wanamfukuza mjane na kumnyang'anya Mali, akishitaki serikalini cheti cha ndoa kitahitajika ili kumthibitisha kwamba alikuwa mke halali wa yule mwanaume.
Ndio maana serikali hutoa vyeti viwili yaani anayeolewa anapewa na anaoa anapewa.
Hata hivyo vyeti vya ndoa vina kazi nyingi pia.

Kwanini kanisa la MUNGU?
Ni kwa sababu lazima tuyafanyayo yafanyike katika Bwana YESU.
Kumbuka na sisi tu wa YESU.
Na MUNGU ndio mwanzilishi wa ndoa.
Na ndoa inahitaji ulinzi wa MUNGU na utakatifu.
Kuna mengi sana katika hilo la kwanini ni muhimu kumhusisha MUNGU kwenye ndoa.
Biblia inasema

Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."


Baadhi ya maswali na majibu kuhusu ndoa niliyoulizwa na rafiki yangu mmoja.
Unaweza kujifunza kitu pia.
Karibu.

Swali kutoka kwa mtu wa kwanza:
Kwa kuwa NDOA NI AGENDA YA KIROHO KABISA...
JE, ...
1. maandiko yanasemaje juu ya UKOMAVU WA MTU KIROHO? kabla ya kuingia kwenye ndoa
--ili aweze kuzaa matunda mema ya rohoni!!

2. Mtu atajuaje kuwa kwa sasa amekomaa vya kutosha KUINGIA ndoani ?
3. Vijana wengi wanahudhuria kwenye SEMINA NYINGI ZA NDOA ,,lakini bado wakiingia ndoani ni MGOGORO tu.
Nini SHIDA kuu HAPA?
-------
nawasilisha...


Majibu yangu mimi Peter Mabula..

Swali la kwanza ulilouliza.
Maandiko yanasemaje juu ya ukomavu wa kiroho kabla ya kuingia kwenye ndoa?
Majibu yangu ni haya.

1. Hatukui kiroho ili tuingie kwenye ndoa Bali inatupasa kukua kiroho ili tumpendeze MUNGU na itusaidie kushinda maovu ya dunia na kila kilicho kinyume na MUNGU.
Kwenye ndoa hakuhitaji sana kukua kiroho Bali kunajitaji kukua kiufahamu juu ya Masuala ya ndoa.
Biblia inamtaka kila mwamini kukua kiroho maana ni kwa faida yake katika maisha ya kiroho na sio maisha ya ndoa tu.
Ila kukua kiroho kunaweza kumsaidia mtu kuimudu vyema ndoa yake.
Ila pia kuna watu wamekua sana kiroho lakini ndoa zao zina matatizo makubwa kwa sababu tu kukua tu kiroho hakumfanyi mtu awe na ndoa njema.
Kukua kiroho ni kuukulia Wokovu.
1 Petro2:2 ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;''


Swali la Pili
Mtu atajuaje kuwa sasa amekomaa vya kutosha ili kuingia katika ndoa?
Majibu yangu.
Suala la mtu kujua kwamba amekomaa na anaweza sasa kufunga ndoa ni suala ni mtu binafsi mhusika ila tu asiwe mtoto maana watoto hawaruhusiwi kuoa wala kuolewa.
Kuna wengine hujua wamekomaa na kuanza kutafuta wachumba ili wafunge ndoa wakiwa na miaka 20.
Kuna wengine huwa hawajitambui kama wamekomaa na wanatakuwa kufunga ndoa hata wakiwa na miaka 35 au 49, hao hadi washtuliwe na watu wa karibu yao.
Kuna wengine hujigundua kwamba sasa wamekomaa na wako tayari kufunga ndoa wakiwa na miaka 30 au wengine 45.
Ndio maana nimesema kwamba umri wa mtu kujijua kwamba anatakiwa kuoa au kuolewa ni juu ya ufahamu wa mhusika.

Biblia kwa andiko fupi na lililokamilika inasema.
"Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.-1 Kor 7:9
Mtu ana miaka kuanzia 24 hadi 50 na hajaoa na ni mzima nadhani yampasa kuoa maana atawaka tamaa sana na tamaa hizo asipojua kumcha MUNGU inaweza kuwa hatari kwake.
Tukumbuke pia wanawake wana ukomo wa umri katika kuzaa hivyo kama mwanamke ana miaka 55 na hataki kuolewa huku akitamani siku moja kuolewa na kuzaa watoto nadhani inaweza kumsumbua baadae kama muda wa kuzaa utakoma.


Swali la tatu.
Vijana wengi wanahudhuria semina za ndoa lakini bado wakiingia kwenye ndoa ni migogoro tu.
Tatizo ni nini?

Majibu yangu ni haya.
Migogoro katika ndoa hutokana na mambo mengi na mengine inawezekana hata kwenye semina za ndoa hawakufundishwa.
Ona haya.
1. Kwenye semina za ndoa mtu anaweza kufundishwa jinsi vya kukaa na mwenzi wake lakini asifundishwe kwamba muujiza uliopatikana kwa maombi hutunzwa kwa maombi.
Hivyo wengine wakiingia kwenye ndoa maombi hukoma na kufunga kunafutika na kwa njia hiyo shetani anapanda magugu na kuiathiri ndoa.


2. Kwenye semina za ndoa mnaweza kufundishwa jinsi ya kuandaana na kuambiana maneno matamu, lakini msifundishwe kibiblia jinsi ya kila mwanandoa kukaa kwenye nafasi yake kiroho na kimwili katika ndoa.

3. Semina za ndoa zinaweza kufundisha usafi wa mazingira na miili lakini usifundishwe jinsi ya kuishinda tamaa
Nyongeza A ni hii.
Kuna semina nyingi sana za ndoa lakini Mimi nawashauri watu kuhudhuria semina za ndoa ambazo walimu ni watumishi wa MUNGU waliookoka, maana hao watafundisha Semina Kibiblia na sio kijinsia na kimtazamo.

Ziada B ni hii.
Vyanzo vya ndoa kuwa na migogoro.
1. Kukosa maombi ya kina.
2. Kumruhusu shetani kuwatawala.
3. Kutokukaa kila mtu katika nafasi yake.
4. Kutokumcha MUNGU.
5. Msingi mbovu wa ndoa
6. Kufanyia kazi maneno ya watu wabaya.
7. Kutojua jinsi ya kuufanya upya upendo uliopoa.

Nyongeza C ni hii.
Neno la MUNGU limekamilika hivyo kuhudhuria semina za neno la MUNGU, mikutano ya injili na kuhudhuria ibada na maombi kuna msaada zaidi huko kuliko hata semina za ndoa.
 
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments