UACHE MABAYA NA UFUATE MAAGIZO YA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Somo la leo linasema Uache mabaya ufuate maagizo ya MUNGU..

Zaburi 34:14-16 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa BWANA ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani. ''

Rafiki yangu mmoja aliniuliza umuhimu kwa kuwekwa misalaba kwenye makaburi.
Nilimjibu hivi:
Misalaba kuwekwa kwenye kaburi ni taratibu walizozipanga wanadamu wakiamini kwamba marehemu huyo atafufuliwa kwa ajili ya uzima wa milele. Sio kosa wala dhambi kuwekewa msalaba, ni jambo jema.
Wengine huweka misalaba makaburini ili kuonyesha kwamba mhusika alikuwa mkristo.

Lakini ukweli ni kwamba
Msalaba haumsaidii lolote aliyekufa, Bali matendo yake aliyotenda alipokuwa hai ndiyo yakayomfuata


Obadia 1:15 "Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe."


Hata kama kaburi litapambwa sana na kuwekewa msalaba mkubwa sana, hiyo haimsaidii marehemu chochote.
Bali maisha matakatifu katika KRISTO kama aliyaishi hayo wakati akiwa hai, hapo ndipo atahusika na uzima wa milele.
Mwanadamu huiandaa mbingu yake au jehanamu yake Wakati akiwa hai, akifa kinachofuata ni uzima wa milele kama aliokoka na kuishi maisha matakatifu.
Au kinachofuata ni jehanamu kama akimkataa YESU na hakuishi maisha matakatifu.
Ndugu hakikisha YESU ni Bwana na Mwokozi wako na unaishi maisha matakatifu ya Wokovu katika yeye.


Ndugu zangu, hatuwezi kujiokoa wenyewe sisi wanadamu hata tupate uzima wa milele. MUNGU kwa kulijua hilo alituletea wanadamu Mwokozi mmoja tu wa pekee yaani YESU KRISTO, ambaye alikuja kutoka mbinguni na akapitia tumbo la mwanadamu ili atupate sisi.
Lengo kuu la Mwokozi ni kuwaokoa wanadamu.


Mathayo 1:21 " Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake YESU, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao."

Kumbe ni YESU pekee ndiye anayeweza kuwaokoa wanadamu kutoka dhambini.
Ni YESU KRISTO pekee ndiye anayeokoa wanadamu, nje na YESU hakuna Mwokozi wa wanadamu.
Ndugu mpokee YESU KRISTO kwa imani leo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.
Kama unauhitaji uzima wa milele tambua ya kwamba unamhitaji YESU KRISTO Mwokozi.


Yuda 1:3 " Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu."


Imani kwa ajili ya uzima wa milele ipo moja tu nayo ni kumpokea YESU KRISTO kuwa Mwokozi wako.
Neno la MUNGU ni la muhimu sana kwa watu wote.
Usilipangie Neno la MUNGU watu ambao litawafaa, Usilipangie Neno la MUNGU watu ambao wanalihitaji, bali wewe na wengine wote mnalihitaji Neno la MUNGU.


Yohana 8:47 '' Yeye aliye wa MUNGU huyasikia maneno ya MUNGU; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa MUNGU.''


Katika baadhi ya ibada leo kuna watu wafuatao

1. Watu ambao wakati wa mahubiri wao wanapolisikia Neno la MUNGU huwafikilia watu ambao hawakufika ibadani siku hiyo na kusema moyoni kwamba ''Neno la leo ningemfaa tu fulani''
Ndugu Neno la MUNGU linamfaa huyo fulani lakini pia linakufaa sana na wewe pia unayelisikia, lifanyike kazi Neno hilo na itakusaidia sana.

2. Watu ambao wakati Neno linahubiriwa wao huchagua watu rohoni waliopo ibadani muda huo na kusema moyoni kwamba ''Neno hili ni la fulani kwa sababu yeye anahusika na kitu fulani, Neno la leo linamfaa fulani maana yeye hufanya dhambi fulani''
Ndugu, Neno la MUNGU ni la muhimu sana kwa wote walio ibadani na wasiokuwepo, Neno la MUNGU ni la muhimu kuanzia kwa mhubiri mwenyewe na wanaosikiliza.
Usilipangie Neno la MUNGU watu ambao wanalihitaji.


3. Kuna watu hushangilia ibadani baada ya Neno fulani kufundishwa kwa sababu rohoni mwao wanajua neno hilo haliwahusu wao bali linawagonga vilivyo wahusika, Ndugu Neno la MUNGU lipo kwa ajili ya watu wote.

Yakobo 1:22 '' Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.''

 
Kama Neno linakemea jambo fulani basi wewe usiyehusika na jambo hilo Neno linakufundisha kwamba hata siku moja usithubutu kufanya dhambi hiyo, kwa yule anayetenda dhambi hiyo kwa siri Neno linamuonya ili aache, hivyo hakuna haja ya kuwapangia Neno watu wengine wakati ni wewe upo ibadani.


Mathayo 13:23 '' Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini. ''

 
Kama wewe ni msomaji mzuri wa Biblia utagundua kwamba katika agano jipya maandiko mengi zaidi au karibia yote yanalifundisha Kanisa la MUNGU. Lakini watu wa MUNGU wengi katika Kanisa la Leo hudhani maandiko hayo yalikuwa kwa ajili ya walio nje na YESU kumbe ni maonyo kwa awlio ndani ili waimalike na ili wasirudie makosa ya kwanza.
Ndugu, Neno la MUNGU ni kwa ajili ya watu wote.


Yakobo 1:21 ''Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu. ''


Usikubali kuachwa na MUNGU kwa sababu tu umeacha maagizo yake.
MUNGU anaweza kukuacha kwa sababu tu umeyaacha maagizo yake, uwe makini ndugu, usiyaache maagizo ya MUNGU kwako.


Maagizo mkuu ya MUNGU ambayo unatakiwa kuyazingatia ni haya;

 
1. Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.

Yohana 3:16-18 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. ''
 
2. Kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.
1 Petro 1:15 ''bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''
 
3. Kuenenda na kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.
 Warumi 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''
 
4. Kumtumikia Bwana YESU KRISTO.
1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA. ''
 
5. Kuwa mtu wa maombi.
Wakolosai ''Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; ''
 
6. Kuwa mtoaji wa matoleo sahihi mbele za MUNGU.
 2 Kor 9:6-8 '' Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.  Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.  Na MUNGU aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; ''
 
7. Kujifunza na kulitafakari na kulitendea kazi Neno la MUNGU.
Mathayo 13:23 '' Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini. ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments