HARIBU AGANO LA URITHI LA KIPEPO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

 Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
Ujumbe wetu wa leo unasema kwamba ''haribu agano la urithi la kipepo.''
Maana mojawapo ya neno ''Kurithi'' ni Kumiliki kitu cha mtu aliyekufa ambaye ana uhusiano na wewe wa uzawa, ndoa au alikuteua kabla kwamba uwe mrithi.

Tunajua katika ulimwengu wa roho ya kwamba kuna vitu huwa havifi au havikomi kufanya kazi yake iliyokusudiwa, kama vitu hivyo vilihusika na agano la kudumu.
Mfano hai ni kwamba MUNGU aliingia agano na Ibrahimu na baadae miaka zaidi ya 450 baada ya Ibrahimu kufariki tunaona MUNGU akikikumbuka agano lake na Ibrahimu na kwenda kuwaokoa uzao wa Ibrahimu.

Kutoka 2:24:25 ''MUNGU akasikia kuugua kwao, MUNGU akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo. MUNGU akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.'

Yaani Waisraeli walitolewa Utumwani Misri kwa sababu tu ya agano la Ibrahimu mbele za MUNGU.
Hapo sasa unaona kwamba agano linaweza kuishi hata miaka 400.
Sasa agano hilo la Ibrahimu mbele za MUNGU lilikuwa agano jema sana sana kwa sababu Ibrahimu alikuwa Mcha MUNGU.
 Sasa katika jamii zetu asilimia kubwa ya mababu zetu hawakuwa wacha MUNGU bali walikuwa watu wa kuingia mikataba na mizimu, waganga, wachawi na majini.
Agano ni agano tu na hilo agano linaweza kumfunga mtu na kumtesa hata kama ni wengine waliingia agano kwa niaba yake na sio yeye aliyeingia agano.
Mimi nilipopata neema ya kuokoka mwaka 2008 nilikuwa mgeni katika ndugu zangu maana sikuwahi kusikia mtu aliyeokoka katika ukoo wangu, labda walikuwepo lakini mimi sikuwahi kumuona hata mmoja. Nilijua kazi kubwa niliyokuwa nayo katika ukoo wangu, Hasa siku moja niliposikia sauti ikiniambia ''Omba neema ya wokovu kwa ukoo wako'' Niliona kama mvua na nikaanza kuomba nikisema kwamba ''Neema ya Wokovu wa Bwana YESU imdondokee kila ndugu yangu kama tone la mvua ambavyo linaweza kumdondokea mtu'' 
Nilitamani sana ndugu zangu wafunguliwe fahamu zao ili watambue kwamba bila kuokolewa na Bwana YESU ni kazi bure, nilitamani kila ndugu yangu afahamu kwamba dini tu bila wokovu ni kupoteza muda, dhehebu tu bila kuishi maisha matakatifu ni kupoteza muda tu.
Neno hilo la kuomba neema ya Wokovu kwa ndugu zangu limeendelea kukaa katika kinywa changu karibia kila siku nikiingia katika maombi nakumbuka kuombea na hilo. 
Namshukuru MUNGU Baba maana ndani ya mwaka mmoja tangu mimi nikoke mdogo wangu anayenifuata naye akaokoka, na hata sasa anamtumikia MUNGU aliye hai. 
Kwa miaka hii kumi tangu nimeokoka nimeona ndugu zangu wengi kidogo wakiokoka na wanaishi maisha matakatifu.
Ninachotaka kusema ni nini?
Ni kwamba miaka 250 iliyopita babu za babu za babu zangu walikuwa wanaishije?
 Na mimi ndio natokea ukoo huo huo?
Ndugu ukiwa unatafakari ni muhimu sana kufuta kwa damu ya YESU KRISTO kila agano la kipepo la urithi.

Isaya 28:15 '' Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli; '' 

Wako watu leo wanateswa na nguvu za giza ambazo wala hawakuzitafuta wao ila walizitafuta wazazi wao au babu zao au babu wa babu zao, ndio maana kuna siku nikakufundisha hapa somo linalosema '''MAOMBI YA KUFUTA ADHABU ZA KIPEPO''

Kuna watu leo wanateswa sana na nguvu za giza kwa sababu tu ya hukumu za kipepo zilizopitishwa hata kabla hawajazaliwa, na aliyepitisha alielekezea kwenye kizazi hivyo unaweza kuteswa leo kwa sababu ya hukumu iliyotakiwa aipate babu yako kutokana na yeye kukosana na wachawi wenzake, hivyo kizazi chote kuwa mawindo ya nguvu za giza, ndio maana siku moja nilikufundisha hapa somo linaloitwa''MAOMBI YA KUFUTA HUKUMU ZA KIPEPO''

Inawezekana wewe tangu tumboni mwa mama yako uko katika agano la kipepo ambalo linakutesa sasa, kuna watu ni zao la uzao wa nyoka, ndio maana amerithi kila kitu kibaya kutoka kwa wazazi wake au mababu zake, ndugu unahitaji kufunguliwa na Bwana YESU.
Zaburi 58:3-4 '' Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; Tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo.  Sumu yao, mfano wake ni sumu ya nyoka; Mfano wao ni fira kiziwi azibaye sikio lake.''

Agano la urithi linaweza kumfanya mtoto arithi kwa baba yake au mama yake kila kitu. Miaka ikiendelea na baba au mama akafariki unaweza kukuta wazee wakisema ''kijana huyu kuanzia tabia hadi matendo ni kama baba yake mzazi''
Kwanini iwe hivyo? Wakati mwingine ni agano la urithi.
 Sasa kama amerithi vitu vibaya ujue ni hatari kwake.
Agano la urithi linaweza kuwa ni agano zuri au agano baya, point yangu nataka uharibu kimaombi agano baya ya kurithi linalokutesa sasa.

Haiwezekani ugonjwa uliomuua bibi yako ndio uwe ugonjwa unaokutesa sasa wewe.
Ndugu mmoja siku moja alinipa elimu ya dakika chache ya ajabu sana. Mtu huyo aliniambia kwamba babu yake alikufa na miaka 40 kwa ugonjwa wa kisukari, baba yake naye alikufa akiwa na miaka 40 kwa ugonjwa wa kisukari, na yeye kwa sasa ana miaka 40 na anaumwa sana kisukari, hivyo alikuwa ananiomba nimuombee ili apone. Niligundua kabisa kuna nguvu za kurithi ambayo zilileta uharibifu kuanzia kwa babu yake hadi sasa ni zamu yake. Nilimfundisha jinsi ya kuomba na nikamuombea pia.

Ndugu unateswa na agano gani la urithi?
Kuna watu ukoo mzima ni watu wa kuchelewa sana kuolewa.
Kuna watu bibi alizalia nyumbani bila kufunga ndoa, mama alizalia nyumbani bila kufunga ndoa, Dada wa kwanza hadi wa tano wote walizalia nyumbani bila kufunga ndoa. Ndugu mengine sio tabia ya mtu tu bali kuna  chambo cha shetani. Inawezekana kabisa ukawa huru kuanzia leo hii baada ya wewe kumpokea YESU, kuishi maisha matakatifu na kuombewa juu ya kufuta kila agano la urithi linaloambatana na maisha yako.
 Bwana YESU anasema kwako ndugu kwamba '' Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.-Mathayo 11:28''

Haiwezekani katika ukoo wenu kila anayefikisha miaka kadhaa anafariki, hiyo ilianza kwa babu wa babu, babu wa baba, babu, baba na hata watoto, ni miaka yenyewe wala sio ya kufika uzeeni. Ndugu mpendwa, mengine ni kazi za shetani zikiwemo maagano ya kipepo yanayoshikilia familia tangu kizazi hata kizazi.
Agano linaweza kufanya kazi huku aliyelitengeneza alishakufa.
Kuna kitu kinaitwa damu huwa kinatumika sana katika maagano?
Unajua kwanini?
Ni kwa sababu damu huwa haifi. Likifanyika agano na kisha ikatolewa kafara ya damu ujue damu hata ikiwa ndani ya aridhi kwa miaka 50 itaendelea kunena yaliye yaliyo katika agano. Kama damu inatamka muugue hakika kama hamna YESU na sio waombaji hakika mtaugua tu.
Dawa ya maagano ya kipepo ni moja tu, dawa ni kufuta maagano hayo kwa damu ya YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
1 Yohana 1:7 '' bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.''

 Damu ya YESU inaweza kufuta dhambi zako zote na inaweza kufuta hata maagano waliyoyafanya wazazi wako au mababu zako yanayokufunga sasa.
Tumepewa mamlaka na MUNGU mwenyewe kwamba tumshinde shetani na mawakala zake na madhabahu zake na maagano yake kwa maombi tu huku tukitumia damu ya YESU KRISTO ya agano jipya na kwa Neno la MUNGU la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.
Ufunuo 12:11 ''Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ............. ''

 Kuna watu ni wachawi kuanzia babu wa tatu, babu wa pili, babu, Baba/Mama hadi watoto. Ndugu wengine wanateswa na maagano ya urithi wa kipepo.
Kuna watu wamerithi uongo, ulevi, sigara na machukizo mengine mengi.
Kuna watu wamerithi tabia fulani fulani kiasi kwamba hata kama ni Mkristo asiyesimama imara kwa YESU KRISTO anaweza kuwa katika tabia hizo chafu za kurithi.
Nguvu ya tabia za kurithi ikiwa na nguvu kwa mtu hakika mtu huyo asipokaa sawa anaweza kuacha hata wokovu.

Kuna watu wanateswa na maagano ya kipepo ya kurithi ya dini, maagano hayo yamewazuiliwa watu hao kuokoka na kupata uzima wa milele.
Yohana 3:19-20 ''Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru(Wokovu wa KRISTO) imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa.''

Ndugu, haribu agano la kipepo la kurithi.
Jikague katika maisha yako juu ya agano la kurithi la kipepo.
Hata katika nafasi yako ya kazi ya serikali au ya kuajiriwa unaweza ukateswa na agano la kipepo la kurithi lililofanywa na mtangulizi wako.
Mfano ni huu.
Daudi alipopewa nafasi ya ufalme alirithi na matatizo ya kiti hicho cha ufalme kwa sababu ya makosa ya mtangulizi wake aitwaye Sauli.
2 Samweli 21:1 ''Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni.'' 

Daudi anashangaa njaa kubwa katika nchi  n.k na kumbe ni kosa la mfalme wa zamani na sio kosa lake.
Hata wewe katika ofisi yako unaweza kurithi matatizo yanayotokana na aliyekuwa katika nafasi hiyo kabla yako.
 Watoto wanaweza kurithi adhabu za kipepo zilizotakiwa kuwapata baba zao.
Wajukuu wanaweza kurithi adhabu ambazo zilipaswa kuwapata babu zao.
Maombolezo 5:7-10 '' Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao. Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.  Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu; Kwa sababu ya upanga wa nyikani. Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuu; Kwa sababu ya hari ya njaa ituteketezayo.''

 Ndugu, jitenge leo na maagano ya ukoo ya kurithi yaliyo ya kipepo.
Ndugu mmoja siku moja alisema kwamba kuanzia babu yake, baba yake na yeye mwenyewe  hakuna aliyewahi kufuga hata kuku.
Haiwezekani ninyi ni watu wa kazi, mna juhudi sana katika kufanya kazi, mnaamka mapema sana na kwenda kufanya kazi nzuri kwa juhudu sana  lakini babu maskini, baba hadi mtoto ni maskini yaani hata pesa tu ya nguo ya sikukuu ya pasaka hujawahi kupata.
Mengine ndugu ni kwa sababu ya nguvu za giza.
Kuna watu wao ukoo mzima ni watu wa kuoa mitaala, hilo ni agano la urithi la kipepo.
Ndoa za mitaala ni ndoa za wake wake, yaani babu ana wake 3, baba ana wake wawili na mtoto japokuwa ni mtu wa Kanisa lakini kila siku hamu ya kuoa mke wa pili inamjia, huo ni ushetani unaotokana na magano ya kipepo ya urithi.

Nini ufanye kimaombi?

1. Tubu kwa ajili ya chanzo cha maagano hayo kukufikia wewe.
 Isaya 59:1-2  '' Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. ''
2.  Haribu agano la urithi ulilorithishwa kichawi.
Haribu kwa damu ya YESU KRISTO.

3. Vunja maagano ya giza yote ya uliyorithi kutoka kwa wazazi wako au mababu zako.
Vunja kwa jina la YESU KRISTO.

4. Futa kwa damu ya YESU KRISTO kila maagano ya urithi ya kipepo yale uliyoona ndotoni au kwenye maono na ukajua kwamba unajulishwa juu ya agano la kipepo la urithi.

 5. Bomoa na kuvunja madhabahu za giza zilizotengeneza maagano ya kipepo ya urithi katika ukoo wako.
Kumb 7:5 '' Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. ''

6. Acha tabia mbaya zote zinazotokana na nguvu za giza za kurithi, ziache kwanza kisha omba kwa MUNGU ili tabia hizo zikuachie na zisikufuate tena.
1 Thesalonike 5:22 '' jitengeni na ubaya wa kila namna. ''

7. Omba Bwana YESU amiliki na kutawala roho yako, nafsi yako na mwili wako.


 
'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments