JE NI SAWA MKRISTO KUTUMIA MITISHAMBA KAMA DAWA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU linalotokana na maswali ya rafiki yangu mmoja aliyeniandikia ili nimjibu.
Kupitia majibu ya maswali ya ndugu huyo naamini na wewe utajifunza na kuelewa kitu muhimu sana.
Ndugu huyo aliniandikia hivi "Mchungaji Mabula nakusalimu kwa jina la BWANA wetu YESU KRISTO, shikamoo mimi ni kijana naitwa JEREMIAH niko chuo mwaka wa 3 nianatarajia kuhitimu mwezi July. nimebatizwa nimeokoka katika kanisa la kiroho huku BWANGA CHATO Mkoa wa GEITA. napenda sana huduma zako kiroho tangu nianze kuzifuatilia ukweli zimenijenga kiroho MUNGU aibariki kazi yako.
Nina maswali mawili ambayo yamekuwa yakinipa shida tangu niamini ambayo ni:-
(a) Ili nidumu katika wokovu inahiji kufanya mambo gani kwa sababu nimebatizwa sawa lakini sikupewa mafundisho.......

(b) Je, ni halali mkristo aliyeokoka na kumkiri YESU akiugua aende hospitali? au kutumia majani au miti shamba kwa ajili ya ugonjwa unaomsumbua ilihali ISAYA 53;5 anasema kuwa kwa kupigwa kwake sisi tumepona......
Natanguliza jina la KRISTO aliye hai.......


Majibu ya Mtumishi Peter Mabula:
Ili udumu katika Wokovu inakupasa.


1. Ufundishwe au ujifunze mafundisho ya awali ya Neno la MUNGU.
1 Petro 2:2-3 "Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ikiwa mmeonja ya kwamba BWANA ni mwenye fadhili."


2. Ufundishwe mafundisho ya ubatizo na ubatizwe.
Wakolosai 2:12 "Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za MUNGU aliyemfufua katika wafu."


3. Kuwa mtu wa maombi.
Wakolosai 4:2 "Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani;"


4. Uwe mtu wa ibada.
Waebrania 10:25 "wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia."


5. Linafanyie kazi Neno la MUNGU unalijifunza.
Yakobo 1:22 "Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu."

6. Tamani kujazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU na jifunze masomo kuhusu ROHO MTAKATIFU na utaombewa ujazo wa nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Wagalatia 5:25 "Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO."


7. Weka tumaini lako kwa MUNGU.
Yeremia 17:7 "Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake."


8. Anza kumtumikia Bwana YESU.
1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana."

9. Uwe mtoaji wa Zaka, Sadaka na dhabihu.
  Dhabihu ni sadaka unayoiongeza katika zaka yako.
Mfano kama zaka yako ni Elfu 10 basi ukitoa 13 ujue elfu kumi ni zaka na elfu tatu ni dhabihu.
Zaburi 50:5 "Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu."

Kuna uhusiano mkubwa sana katika kutoa zaka na ukuaji wa kiroho.
Malaki 3:9-11''
Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi. ''

 
Kuhusu swali la pili kwamba Je ni halali Mkristo aliyeokoa kwenda hospitali?
Ndio ni halali maana hospitali zisizohusika na nguvu za giza zimewekwa kwa kusudi la MUNGU ili kuwasaidia watu. Hivyo unapoenda Hospitali hufanyi makosa labda tu Kama utaelekezwa huko vitu ambavyo ni dhambi ndipo hutajihusisha navyo.
Hata hivyo pia hata kama umeenda hospitali tambua kwamba madaktati wanatibu lakini anayeponya ni MUNGU hivyo hata dawa ziombee kwa MUNGU ili MUNGU akuponye kupitia dawa hizo, wapo watu wanaumwa ugonjwa ule ule na wanatumia dawa zile zile lakini mwingine anapona na mwingine anakufa hata kama kanywa dawa za kutibu ugonjwa huo, hivyo mponyaji na MUNGU na sio mwanadamu.

Tunajua wazi kabisa hata akina Luka katika Biblia walikuwa madaktari lakini ni vyema sana kujua kwamba MUNGU ndiye msaada wa thamani katika maisha yako.
MUNGU anasema kwa wateule wake wansomtegemea kwamba ataleta afya, ataleta uponyaji na ataponya.
Yeremia 33:6 "Tazama, nitauletea afya na kupona, nami nitawaponya; nami nitawafunulia wingi wa amani na kweli."


Hatutakiwi kuweka tumaini kwa daktari au kwa dawa Bali tumaini ni kwa MUNGU.
Isaya 26:3-4 " Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele."




 Kutumia miti ili kutibu tatizo lolote sio kosa.
Ufunuo 22:2 inazungumzia MUNGU kuweka mti wa kuwaponya watu.

Maandiko yanasema '' katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa. ''
 
Lakini pia ni muhimu sana kutambua kwamba ninapozungumzia miti shamba sina maana hata moja kwamba uende kwa waganga wa kienyeji.

Ndugu, kwa waganga wa kienyeji usiguse kamwe.
Usiende huko kamwe.
Kwanini usiende?

Ni kwa sababu ufunuo uliotumika kupatikana kwa dawa huko ulitokana na shetani na sio MUNGU.
Zana zote huko zinatokana na shetani na sio MUNGU.
Kiswahili kiko wazi sana kwamba waganga wa kienyeji wanaagua.
Unajua maana ya kuagua au kuaguliwa?
Kuaguliwa ni pale mtu abashiriwapo mambo yatakayompata hapo baadaye au kupigiwa ramli, na kisha kupewa dawa , kama matumizi ya dawa hiyo ya kienyeji umeipata kwa uaguzi basi kwa Mkristo ni kumkosea MUNGU na ni dhambi kubwa sana.
Hata kama kuna mganga wa kienyeji anajitangaza anatibu tambua kwamba huyo ni muaguzi tu na kazi yake ni kuagua, wanaokwenda huko ni wale waliompenda shetani na sio MUNGU Muumbaji wao.

Lakini kama ni mtu anakuambia kwamba tumia mwarobaini au maji ya dafu au juisi ya mapera ili kutibu tatizo lako, hiyo ni sawa.
Dawa za waganga nyingi zina masharti hivyo usitumie hizo.
Waganga wa kienyeji ujihadhari nao sana.
Ufunuo wao wa dawa hautokani na MUNGU.
Ayubu 5: 3-4 "Nimewaona wapumbavu wakishusha mizizi lakini mara niliyalaani maskani yake,Watoto wake wapo mbali na wokovu Nao wamesongwa langoni wala hapana atakayewaponya."

Hivyo utakosana na MUNGU ukijihusisha na waganga wa kienyeji.
Nimesema usiende kwa waganga wa kienyeji maana wao huchanganya dawa na nguvu za Giza, ni hatari mno kwako.
Unaweza ukanywa dawa za mganga wa kienyeji kumbe umemunywa na jini aliyezileta hivyo unakuwa mtu wa kuteswa na nguvu za giza.
waganga wa kienyeji huchanganya mitishamba na mapepo
mfano anakuambia anarudisha nyota huko ni kuwekewa connection na kuzimu, ni hatari usiguse
Umepewa mapepo yakusaidie kukuza biashara zako, wewe unaona dawa kumbe ndani ya dawa kuna majini, utakuwa umepotea sana. Biblia inasema katika Kumb 18:9-12 “Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto , wala asionekane mtu atazamye bao, wala mtu aatazamaye nyakati mabaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo,wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. ”

Pia Biblia katika
2 Nyakati 33:6 inakataza mtu kufanya uganga hivyo hata unayewaendea waganga unakuwa unapishana na kusudi la MUNGU, Biblia inasema ''
Tena akawapitisha wanawe motoni katika bonde la mwana wa Hinomu; akatazama bao, akabashiri, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa BWANA, hata kumkasirisha. ''
Lakini pia wapo watu hutoa dawa za kawaida miti asilia lakini huwa wameziombea kwa miungu yao, hapo hakikisha unafuta kila kamba za kishetani zilizo katika dawa, ndio maana hata kama ni dawa za hospitali au umeelekezwa na mtu juu ya miti fulani inakupasa kuziombea dawa hizo.
Lakini pia wala sio kosa wewe mteule kutumia dawa za miti asilia bali ziombee na sikiliza rohoni mwako kukoje, maana Bwana YESU alituachia amani yake ili itusaidie katika maamuzi.
Ezekiel 47:12 inaonyesha dawa za miti zilizo dawa zinazotokana na ufunuo wa ki MUNGU tunaweza kuzitumia kujitibu, dawa hizo haziko kwa waganga wa kienyeji.
PICHA HII NI MFANO TU NA SIO HALISI

Ezekieli 47:12 "Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe;
utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa."

Vipo vitu vya kawaida kabisa mtu anaweza kuelekezwa na watu wema na akatumia na kupona, mfano
2 Wafalme 20:7 "Naye Isaya akasema, Twaeni mkate wa tini. Wakautwaa, wakauweka juu ya jipu, naye akapona."

soma pia
Isaya 38:21.
Au
Luka 10:34 au pia
2 wafalme 2:20-22.

naamini umenielewa na wengine watakaosoma Ujumbe huu watanielewa vyema.
Ila kwa waganga usiguse kamwe, maana huko ndiko kumejaa dawa za mitishamba lakini zimeunganisha na mapepo na nguvu ya kuzimu, Biblia inakataza kabisa kujihusisha na waganga wa kienyeji.
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments