YAKATAE MASHTAKA YA UONGO MOYONI MWAKO.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

◼️Somo hili lina majibu ya Watu wengi waliowahi kuniuliza maswali.

Baadhi ni hawa;
 ➡️Mtu mmoja aliniambia " Mtumishi siwezi kusamehewa maana nimefanya dhambi kubwa sana hata MUNGU hawezi kunisamehe"

➡️Mtu Mwingine aliniambia "Mtumishi Mabula kuna Sauti naisikia ndani yangu ikiniambia jiue maana hutasamehewa dhambi uliyofanya"

➡️Watu wengine kama wanne waliniambia " Mtumishi nimefanya dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU hivyo siwezi kusamehewa kamwe" nilipowauliza wanitajie dhambi hizo niligundua shetani hataki waende uzima wa milele ndio maana anawadanganya kwamba hawatasamehewa wakati ni dhambi ambazo zinaweza kusamehewa.

Sasa ngoja tuanze hivi ukisoma ◼️Ufunuo  12:10 pale mwishoni unaona Biblia inasema shetani kazi yake Moja ni kuwashitaki Watu mbele za MUNGU usiku na Mchana, Biblia inasema hivi "Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa MUNGU wetu, na mamlaka ya KRISTO wake; KWA MAANA AMETUPWA  CHINI MSHITAKI  WA NDUGU ZETU, YEYE AWASHITAKIYE  MBELE ZA MUNGU WETU, MCHANA NA USIKU."

◼️Na ukisoma Yeremia 31:34 pale mwishoni unaona MUNGU akiisamehe dhambi ya Mtu huwa haikumbuki Tena Biblia inasema hivi "Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue BWANA; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema BWANA; MAANA NITAUSAMEHE UOVU WAO, WALA DHAMBI YAO SITAIKUMBUKA  TENA."

✔️✔️Uovu ni dhambi sugu za muda mrefu mbaya za kujirudia rudia, yaani ni tabia ya kutenda dhambi mbaya lakini hata hizi dhambi MUNGU katika KRISTO YESU anasema atasamehe Wala hatakumbuka.

◼️Lakini pia ukisoma Zaburi 51:3 Biblia inaonyesha kwamba  Kuna dhambi ambayo haijatubiwa inaweza kuwa mbele ya mhusika daima hadi aitubie kwa YESU ndipo inaondoka na kufutika, Biblia inasema "Maana nimejua mimi makosa yangu Na dhambi yangu i mbele yangu daima."

➡️Dhambi itakuwa mbele Yako daima kama hujaitubia kwa Toba ya kweli.

➡️Kuna dhambi zitakuwa mbele Yako daima hadi utubie kwa YESU au umweleze Mtumishi wa MUNGU kama Daudi alivyomweleza Nathani hapo juu ndipo likatoka Tangazo la msamaha.

◼️Faida ya kumweleza Mtumishi wa KRISTO ni kwamba atakuongoza sala ya Toba na Kisha atakufundisha namna nzuri ya kuishinda dhambi hiyo ili isirudi Tena maishani Mwako.

◼️YESU anapokusamehe Ukiona bado unahukumiwa moyoni ujue ni uongo wa shetani, hayo ni mashitaka ya uongo ili kukupunguzia Nguvu za kusonga mbele katika Wokovu, YESU akikusamehe kupitia sala ya Toba huwa haibaki dhambi yeyote.

Wakolosai 2:14 "akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani;"

✔️✔️Hivyo kataa mashtaka ya uongo moyoni Mwako kama umeokoka na bado unahisi Kuna dhambi hujasamehewa.

◼️Lakini kama ulilikosea Kanisa la MUNGU au ulimkosea vibaya sana  Mtumishi wa kweli wa Bwana YESU aliyesimama  katika kusudi la MUNGU na hadi akatamka maneno kama haya ya Nabii Yeremia ambaye aliowasaidia sana kiroho ndio walikuwa wanamuwinda wamuue hadi akaomba maneno magumu, Yeremia 18:23 "Lakini wewe, BWANA, unajua mashauri yao yote juu yangu, ya kuniua; usiwasamehe uovu wao, wala usifute dhambi yao mbele za macho yako; bali wakwazwe mbele zako; uwatende mambo wakati wa hasira yako."

✔️✔️Dhambi ya namna hii ni Muhimu kwenda kutengeneza na Mtumishi wa MUNGU uliyemkosea, kama hayupo Duniani tafuta Mtumishi Mwingine akuombee msamaha kwa MUNGU na kukupatanisha na MUNGU utasamehewa.
Kumbuka Kazi mojawapo ya Watumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU ni kuwapatanisha watu na MUNGU.

2 Wakorintho 5:18 "Lakini vyote pia vyatokana na MUNGU, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa KRISTO, naye alitupa huduma ya upatanisho;"

Sasa msikilize.

◼️Katika ulimwengu wa roho kunaweza kukawa na mashtaka ya aina mbili kumhusu mtu.

1. Kuna mashtaka ya kweli kwa sababu mtu amemkosea MUNGU.

2 Samweli 12:13 "Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa."

2. Kuna mashtaka ya uongo ambapo mawakala wa shetani wanataka kumwathiri mtu wa MUNGU.

Warumi 8:33 "Ni nani atakayewashitaki wateule wa MUNGU? MUNGU ndiye mwenye kuwahesabia haki."

◾Ili kufuta mashtaka ya kiroho unatakiwa ujue ni mashtaka gani.

1. Kama ni mashtaka ya kweli maana ni wewe ulifanya jambo baya na kumkosea MUNGU basi ili kufuta mashtaka hayo inakupasa kutubu kwa MUNGU kwa njia ya  YESU KRISTO na kwa uliowakosea na baada ya kutubu usirudie kosa.

Yeremia 14:20 "Ee BWANA, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi."

2. Kama ni mashtaka ya kipepo dhidi yake au mashtaka ya uongo hayo inakupasa kuyafuta kwa jina la YESU KRISTO kwa njia ya maombi.

2 Wakorintho 2:11 "Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake."

➡️Watu wengi ni wanyonge mioyoni mwao kwa sababu ya kuhukumiwa rohoni mwao.

➡️Kuna watu wengi hushindwa hata kuomba kwa sababu  wanasikia hukumu rohoni.

➡️Kuna watu hujiona ni wakosaji na wanashindwa hata kutulia kwa Bwana YESU.

➡️Mtu mwingine kwa sababu ya dhambi alizofanya zamani, kwa sasa ameshindwa hata kwenda Kanisani akidhani MUNGU hawezi kumsamehe.

➡️Kuna watu hata hutaka kujidhuru kwa sababu tu ya makosa yao ya zamani.

◼️Ndugu zangu naomba niseme yafuatayo.

Isaya 1:16-19 " Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;
"
◼️MUNGU katika KRISTO YESU huwa anasamehe kwa wanaotubu.

◼️Baada ya kutubu na kuacha uovu huo inakupasa sana ujiamini kwamba umeshasamehewa na kinachotakiwa kwako ni kuishi tu maisha matakatifu katika Wokovu wa KRISTO Mwokozi.

 ➡️Ukiruhusu sana kuhukumiwa rohoni wakati umeshatubu na umeokolewa na Bwana YESU ujue ni hila za shetani ili ushindwe kujiamini katika maisha yako ya wokovu wakati ulishasamehewa tangu ulipotubu na kuacha uovu.

Nimewahi kukutana na watu wengi wakihesabu wingi na ukubwa wa dhambi zao.

➡️Mfano hai ambao hutesa watu hadi wengine wanachagua kuendelea na dhambi maana akili yao inajua wamemkufuru ROHO MTAKATIFU na kumbe hata hawakufanya dhambi hiyo.

◼️Ndugu, Mtume Paulo kabla ya utume alikuwa anafanya mabaya sana na hadi dhambi za kuua zilmhusu lakini Uuaji huo wa watu wengi alisamehewa maana hakutenda dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU.

Matendo 9:1 "Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa BWANA, akamwendea Kuhani Mkuu,"

◼️YESU KRISTO anasema hivi dhambi zote na kufuru zote ambazo Mwanadamu anaweza kutenda akitubu kwa MUNGU katika yeye anisamehe dhambi hizo na kufuru hizi isipokuwa dhambi Moja tu ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU.

Marko 3:28-29 " Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru ROHO MTAKATIFU hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele,"

◾Dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU ni ipi?

◼️Dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU ni dhambi ya kuzikana Nguvu zake ambazo ni yeye mwenyewe alikutumia kwa miaka mingi.

➡️Mfano Mtu alikuwa ni Mchungaji au Askofu na Kwa miaka mingi alihubiri Neno la MUNGU na ROHO MTAKATIFU akamtumia kwa Miujiza mingi sana na maelfu ya Watu wakaokoka kupitia Injili yake lakini baadae kwa tamaa au mengine akadanganywa na Watu wa dini nyingine akajiunga nao na kuanza kuhubiri huko kwenye dini mpya kwamba aliyekuwa anamtumia kipindi kile kwa Miujiza Wala sio MUNGU anaanza kusingizia Nguvu za giza ili tu Lengo lake kuudhoofishwa Ukristo au kuwatoa watu kwa YESU, Mtu kama huyo moyoni mwake anajua kabisa ni MUNGU alimtumia lakini kwa kuwafurahisha dini yake mpya au wafadhili wake wake anadanganya ili kuwafurahisha, huyo anamkufuru ROHO MTAKATIFU.

➡️Mfano Leo itokee (Najua haitatokea kwa Jina la YESU KRISTO), itokee Mtumishi wa MUNGU yeyote anayetumiwa sana na MUNGU na mikutano yake ya Injili au huduma yake wanajaa maelfu ya Watu na Miujiza mingi inatendwa na MUNGU harafu miaka 5 baadae Mtumishi huyo ahamie Uislamu na awe anaendesha mihadhara ya dini akipinga kwamba hakuwahi kutumiwa na MUNGU bali zilikuwa Nguvu za giza, huyo anafanya dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU.

➡️Mtu huyo hapo anatenda dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU hawezi kusamehewa na hata kuifikia tu Toba hawezi, akili yake haiwezi kuwa na Toba Tena atafurahia Maisha yake kutenda Maovu.

Waebrania 6:4-6 " Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu, na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo, wakaanguka baada ya hayo, HAIWEZEKANI KUWAFANYA UPYA TENA HATA WAKATUBU; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa MUNGU mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri."

◼️Biblia inapowazungumzia watu hawa inasema Walipewa Nuru ya KRISTO, walikitumia kipawa Cha Mbinguni, ROHO MTAKATIFU aliwatumia akishirikiana nao hao hawawezi Tena kutubu.

◼️Hivyo dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU inawahusu wale ambao wamewahi kutumiwa sana na MUNGU Kwa Miujiza na utumishi mkuu harafu baada wanadharau walivyotumiwa na ROHO MTAKATIFU na kuanza kuzikana kazi zake alizowatumia, hapo wamemkufuru na hawawezi kusamehewa.
Hivyo dhambi hiyo ni ya wachache sana na ni waliokwisha kukionja kipawa Cha Mbinguni.

➡️Hivyo Wewe  uliyewahi kuiba, kuzini, ushoga, ukahaba, kuiba Mume au Mke wa Mtu, kumtukana MUNGU, kudhulumu, kumtukana YESU na dhambi zingine zozote achana na habari ya kusema huwezi kusamehewa, anayekuambia hivyo rohoni mwako ni shetani Wala sio MUNGU hivyo nenda Kanisani ukaokoke na uzima wa milele utaenda ukidumu katika Wokovu kwa utakatifu wa KRISTO.

➡️Wewe unayewaza kujiua kwa sababu unadhani huwezi kusamehewa anayekushawishi ndani Yako ni mapepo hivyo kimbilia Kanisani ukaokoke na uzima wa milele utaenda kama ukidumu katika Wokovu wa KRISTO kwa utakatifu.
Kumbuka ukijiua unajipeleka jehanamu mwenyewe maana Mtu akijiua amefanya dhambi ya kuua na Kwa sababu uhai wako ndio unaishia hapo hakuna nafasi ya kutubu na kutengeneza na MUNGU hivyo unaondoka na dhambi Yako ya kuua yaani umejiua.

➡️Uking'ang'ania kwamba hutasamehewa utabaki katika dhambi na ukifa utaenda jehanamu na kumbe ni mapepo yalikuwa ndani Yako yanakudanganya.

 ◼️Ndugu nakuomba Mpokee YESU KRISTO awe Mwokozi wako na dhambi zako zote utasamehewa kabisa, wako watu walikosea kuliko Wewe wakaamua kutubu na YESU akawasamehe na Sasa Wanamtumikia.

◼️Achana na habari za kujihukumu, nenda Kanisani ukaokoke utasamehewa dhambi zako  zote.

➡️Kuna watu kwa kuhesabu dhambi zao shetani huwashawishi ili wajione hawana sehemu tena katika ufalme wa MUNGU hata wakitubu.

◼️Siku zote MUNGU yuko tayari kumsamehe mtu yeyote anayetubu na kuacha haijalishi ukubwa wa dhambi zake.

◼️Kama kweli umempokea Bwana YESU na umetubu na kuacha dhambi zako zote hakika umesamehewa na mashtaka ya zamani hayakuhusu tena.
Ukiona unasikia hukumu rohoni au mashtaka ujue ni hila za shetani ili kukufanya ujione mkosaji wakati ulishatubu na kusamehewa.

➡️Lakini huwa kuna mashtaka ya wanadamu ambayo ukiyafuata unaweza kuteseka rohoni bure.
Kila shitaka au shutumu wanalikushutumu wanadamu lipime kwa Neno la MUNGU ndipo kama wewe ni mkosaji waombe msamaha na kutubu na kama ni mashtaka ya uongo yafute kwa maombi na tambua kwamba hayo mashtaka hayana madhara kwako kiroho na wasaidie tu watu hao kuelewa kwa usahihi.

➡️Wanadamu wanaweza kukushutumu kwa sababu tu unaomba sana na usipokuwa makini Unaweza kuacha maombi au kupunguza maombi kumbe umefanyia kazi mashtaka ya kipepo yenye lengo la kukuzuia wewe kufanikiwa.

◼️Usipunguze kumwabudu MUNGU na kumtumikia kwa sababu tu ya mashtaka ya maneno ya watu.

◼️Kama ni mashtaka ya kweli basi tubu kwa MUNGU na baada ya hapo tambua kwamba mashtaka yatakayofuata baada ya toba yako hayo hayakuhusu.

Ila kama mashtaka Yako ni ya kweli ni kwamba Mashtaka ya kweli ni mabaya sana maana yanaweza kukuathiri, hivyo chukua hatua kiroho na kivite do ili uwe huru.

1. Mashtaka ya kweli Yanaweza kukuzuia kujibiwa maombi yako.

◼️Hivyo tubu kwanza ili mashtaka husika yafutike.

2. Mashtaka ya kweli yanakuondolea sifa yako njema kiroho.

◼️Tubu katika hilo.

3. Mashtaka ya kweli rohoni mwako ni ishara kwamba wewe ni mchafu rohoni hivyo unahitaji toba.

4. Mashtaka ya kweli yatakuzuia kufanya Huduma njema katika kazi ya MUNGU.

◼️Hivyo tubu kwamba.

5. Mashtaka ya kweli yanakaribisha wewe kusemwa vibaya na watu na yanakaribisha laana za vinywa kwako.

◼️Tubu kama kuna mashtaka ya kweli kukuhusu.

6. Mashtaka ya kweli yanaweza kukuzuia kutoa ulivyonavyo na yanakuzuia kupokea usivyokuwa navyo.

➡️Mfano mtumishi kama anahukumiwa kwa utapeli basi hatasikilizwa vyema maana kibali chake kitakuwa hakina nguvu.
Hivyo toba ya kweli ni muhimu sana.

7. Mashtaka ya kweli yanaweza kukuwekea mipaka katika ulimwengu wa roho.

◼️Hivyo kutubu na kuacha uovu ni muhimu sana.
Kama kuna mashtaka ya kweli kukuhusu basi tubu na kuacha uovu.

◼️Kama ni watu wanakutuhumu bure hayo mashtaka yao yafute kwa kutumia damu ya YESU KRISTO ukiomba katika Jina la YESU KRISTO.

◼️◼️YESU KRISTO alikuja ili kutufutia hati za mashtaka baada ya sisi kumpokea na kutubu.

Wakolosai 2:13-18 "Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.sai Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa KRISTO. Mtu asiwanyang'anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili;"

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments