SILAHA KUU ZA KUFANIKIWA MIPANGO YA KANISA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu mlio kanisa hai la MUNGU aliye hai.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kwa ufupi ili itusaidie katika kuifanya kazi ya MUNGU kwa mafanikio.
Ujumbe huu unaweza kulisaidia Kanisa la mahali yaani tawi la dhehebu, pia ujumbe huu unaweza kulisaidia Kanisa la MUNGU kwa ujumla wake duniani.
Inawezekana Kanisani kwenu nyie na Mchungaji wenu huwa mnapanga mipango mingi lakini huwa haifanikiwi, kuna kitu cha kujifunza katika ujumbe huu. Katika ujumbe huu pale ninaposema Kanisa sina maana ya dhehebu lolote ila nina maana ya mtu binafsi aliye Kanisa hai la KRISTO na nina maana ya watu wanaokutana katika jengo fulani na kumwabudu MUNGU Baba katika KRISTO YESU.
Kuna silaha nyingi za kutufanya tufanikiwe kama Kanisa.
 
Nimekuandalia silaha kuu 3 za kutufanya Kama Kanisa tufanikiwe.
 
1. Maombi.
Mathayo 7:7-8 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.''

2. Umoja.
Zaburi 133:1 '' Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. ''
 
Umoja ni hali ya kuwa pamoja.
Umoja sahihi lazima uambatane na ushirikiano.
Umoja sahihi ni kuwa na nia moja.
Umoja sahihi unahusisha kuungana, kuasaidia, kunia mamoja na kufanya kazi ya MUNGU pamoja.
Umoja hautakiwi kuwa katika maneno tu bali hata katika vitendo.

3. Upendo.
Yahana 13:34-35 '' Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi. ''

Kama Kanisa la KRISTO duniani halina upendo hakika kazi ya MUNGU itayumba sana.
Upendo ni silaha kuu sana kwa Kanisa la MUNGU ili kazi ya MUNGU izae matunda mema.

Kwa sababu Kanisa la MUNGU lazima tuwe na umoja ni muhimu sana kujua jambo hili kwamba Ili umoja wetu uwe na nguvu inatupasa kufanya nini?

Ili umoja wetu kama Kanisa uwe na nguvu inatupasa kufanya yafuatayo.

1. Kila aliye Kanisa ahakikishe anaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.
1 Petro 1:14-16 '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.''

2. Lazima Kanisa tunie mamoja.
1 Kor 1:10 ''0 Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu YESU KRISTO, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. ''
 
= Lazima kukubaliana pamoja na kutekeleza pamoja yale mlioyokubaliana.
=Lazima Kanisa liwe na lengo moja sahihi walilokubaliana Kanisani.

3. Kanisa la MUNGU lazima liwe na tumaini moja la wito.
Waefeso 4:4-6 ''Mwili mmoja, na ROHO mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana(YESU KRISTO) mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. MUNGU mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.''

Ili umoja wetu uwe mzuri tuondoe yafuatayo.

1. Dhambi.
1 Yohana 3:4-10 ''Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake. Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua. Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki; atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. Kila mtu aliyezaliwa na MUNGU hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na MUNGU. Katika hili watoto wa MUNGU ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na MUNGU, wala yeye asiyempenda ndugu yake. ''

2. Unafiki.
Zaburi 12:2-3 '' Husemezana yasiyofaa kila mtu na mwenziwe, Wenye midomo ya kujipendekeza; Husemezana kwa mioyo ya unafiki; BWANA ataikata midomo yote ya kujipendekeza, Nao ulimi unenao maneno ya kiburi;''
 
Mtu mnafiki ni mtu wa aina gani?
Mnafiki ni mtu anayesema kinyume na anavyotenda.
Mnafiki ni mtu anayetoa ahadi kisha asitimize.
Mnafiki ni mtu asiyesema kweli.
Mnafiki ni mtu anayefanya jambo huku anajua sio la kweli.
Mnafiki ni mtu anayetumia hila kujinufaisha.
Katika Kanisa la MUNGU hakutakiwi kuwako wanafiki.

3. Mashindano na matengano.
Wafilipi 2:3 ''Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. ''

4. Tamaa mbaya.
Marko 7:21-23 '' Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi. ''

'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments