USIINGIE KATIKA DHAMBI YA KUTOKUMWAMINI MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

 Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
 Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Wapo watu ambao hawamwamini MUNGU kwa sababu ya mazingira yao wanayopitia.
Wapo watu hawamwamini MUNGU kwa sababu  shetani ameweka uongo katika mioyo yao.
Hakuna asiyejua kwamba MUNGU yuko na ni MUNGU pekee anayepaswa kuabudiwa na kuhimidiwa milele.
Nimewahi kuwasiliana na watu kadhaa wakihitaji msaada wa MUNGU lakini katika maelezo yao ni kama hawamwamini MUNGU, hilo ni kosa kubwa sana.
Ukichunguza Biblia utagundua kwamba makosa ya kutokumwamini MUNGU yalileta adhabu mbaya za ghafla kwa wahusika.
Mfano mmoja wapo ni Musa na Haruni ambao tangu Misri katika safari ya kwenda Kaaanani walijua watafika Kaanani maana wao ndio walikuwa viongozi wa kundi la MUNGU lakini kosa moja la kutokumwamini MUNGU liliwafanya wasifike Kaanani.

Hesabu 20:12 '' BWANA akamwambia Musa na Haruni, KWA KUWA HAMKUNIAMINI MIMI, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa.''

Huo ni mfano wa mtu kushindwa kufikia kusudi fulani katika maisha kwa sababu hajamwamini MUNGU, yaani uliomba kwa MUNGU kwamba upate baraka fulani lakini baadae kwa sababu ya mazingira unayoyapitia kabla baraka haijafika kwako unaacha kumwamini MUNGU, hiyo inaweza kukufanya hata baraka usiipate, ukaishia njiani au baraka hiyo ikaenda kwa mwingine.
Sauli alikuwa Mfalme lakini makosa yake mbele za MUNGU yalimfanya MUNGU ampe Ufalme Daudi wakati akiwa mtoto mdogo.
1 Samweli 15:23-28 '' Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme. Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya BWANA, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao. Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu BWANA. Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la BWANA, BWANA naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli. Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka. Basi Samweli akamwambia, Leo BWANA amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko wewe.''

Ni mbaya sana kutokumwamini MUNGU.
Siku moja kuna ndugu mmoja ambaye huenda Kanisani kwao kila mara lakini baada ya kuomba ili apate Mume kwa muda kidogo na hakupata, akanipigia simu akiniambia kwamba sasa anataka kwenda kwa mganga wa kienyeji maana MUNGU amechelewa kumjibu. Moyoni mwangu nilisikia maumivu makubwa sana baada ya kusikia kauli hiyo kutoka kwa mtu wa Kanisani. Nilimwambia maneno magumu sana kwa sababu ya kutokumwamini kwake MUNGU hata anataka kwenda kwa wakuu wa giza kuomba msaada feki ambao ni wa kishetani.
Yaani ni kama anamlinganisha MUNGU wetu na mganga, yaani MUNGU akishindwa basi mganga yupo, huo ni ushetani ambao hautakiwi kuwa kwa mwanadamu aliyeumbwa na MUNGU.
Biblia inatutaka kumwamini MUNGU na kuwaamini watumishi wake waaminifu katika KRISTO YESU.
2 Nyakati 20:20 ''..................  mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.''

 Kuamini ni nini?
Kuamini ni kukubali kwamba ni kweli.
Kumwamini MUNGU ni kumkubali na kuzikubali kazi zake.
Kumwamini MUNGU ndiko kunakoleta kuthibitika.
Maana ya kuthibitika ni kuonekana wazi kwamba mambo fulani au kitu fulani ni sahihi.
Kumwamini MUNGU ndiko kunakoleta kufanikiwa.
Maana ya kufanikiwa ni kupata unachohitaji au kupata unachotamani.
Kumwamini MUNGU ni jambo la lazima kwa wewe mwanadamu uliyeumba na MUNGU.
Kumwamini Bwana YESU KRISTO ni jambo la lazima sana kwa wewe unayeutaka uzima wa milele.
Mtu akisema kwamba anamwamini YESU ni lazima akamilishe mambo haya mawili.
1 Kumkubali kama Mwokozi.
2. Kumpokea kama Mwokozi.
Kumwamini YESU haiko katika kutamka kwa kinywa tu bali ni kumkiri kama Mwokozi, kumkubali kisha unampokea kama Mwokozi wako.
Hivyo wanaosema kwamba wanamwamini YESU lakini hawahusiki na mambo hayo mawili hapo juu, watu hao Kibiblia wanakuwa hawamwamini YESU.
Kumwamini YESU lazima umkubali kisha umpokee kama Mwokozi.
Pia kumwamini ROHO MTAKATIFU na kumtii ni jambo la lazima sana  kwa wewe unayetaka kuishi maisha ya ushindi duniani kisha ukiondoka uende uzima wa milele.

Kwa jinsi gani unaweza kutenda dhambi ya kutokumwamini MUNGU?

1. Usipoliamini Neno la MUNGU.

Zaburi 107:20 ''Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.''
Usipoliamini Neno la MUNGU hujamwamini MUNGU na ni dhambi.
Usipoliamini Neno la MUNGU alililowapa watumishi wake ili wakujulishe ni dhambi.
MUNGU yuko ndani ya Neno lake akitaka kukusaidia wewe, hivyo usipoliamini Neno la MUNGU na kulidharau unakuwa uko kinyume na MUNGU na ni dhambi.

 2. Usipomwamini Bwana YESU kama Mwokozi wako.

Yohana 3:16 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. ''
Usipomwamini Bwana YESU kama Mwokozi wako unakuwa humwamini MUNGU aliyemleta Bwana YESU.
Hiki ndicho kiini cha wengi kukosa uzima wa milele.
Bwana YESU alikuja kuwatafuta wanadamu watii kwa MUNGU ili waupate uzima wa milele.
Kumkwepa YESU ili asikuokoe ni kumkwepa MUNGU ili asikuokoe na watu wa jinsi hiyo mwisho wao ni jehanamu.
Usipomwamini Bwana YESU na kumpokea kama Mwokozi wako ni dhambi na kwa dhambi hiyo wengi sana wataenda jehanamu.
Biblia iko wazi sana kwamba usipomwamini YESU kama Mwokozi wako utahukumiwa siku ya mwisho, yaani ukifa hujampokea YESU kama Mwokozi wako huwezi kwenda uzima wa milele.
Yohana 3:18 '' Amwaminiye yeye(YESU) hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''
Bwana YESU hata leo hii, hata saa hii, hata dakika hii na hata sekunde hii anakuita ndugu ili umpokee kama Mwokozi wako na ndipo jina lako litaandikwa katika kitabu cha uzima wa milele. Kazi yako itakayobaki ni wewe kuishi maisha matakatifu ya wokovu wake tu.
Luka 19:10 '' Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. ''
 

3. Usipomwamini ROHO MTAKATIFU.

Warumi 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''
Maana yake wale wanaomkataa ROHO MTAKATIFU hawawezi kumpendeza MUNGU hata wakafanyika watoto wake walio tayari kwa ajili ya uzima wa milele.
ROHO MTAKATIFU ndiye aliyeileta Biblia ambayo ni Neno la MUNGU hivyo usipomwamini ROHO MTAKATIFU ni hatari yako ya milele.
ROHO MTAKATIFU yuko katika KRISTO YESU pekee na ROHO MTAKATIFU ndiye kiongozi pekee wa Kanisa la MUNGU duniani akitumia Neno la KRISTO kuwasaidia watu wa MUNGU.
Bila ROHO MTAKATIFU huwezi wewe mwanadamu kamwe kumpendeza MUNGU Muumbaji wako.
Usipomwamini ROHO MTAKATUFU hutaamini na alichokileta hivyo ni dhambi.


 4. Kutokumwamini mtumishi wa kweli wa YESU KRISTO anayekuletea ujumbe wa MUNGU.

1 Kor 11:1 '' Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata KRISTO.''
Kuna aina nyingi ya ujumbe ambao MUNGU anaweza akamletea Mtumishi wake ili akujulishe wewe. Watu wengi sana hufanya dhambi hapo kwa sababu hawamwamini mtumishi wa MUNGU na hata neno lake hawalipokei, kama Neno hilo limetoka kwa MUNGU ni dhambi kama hutaliamini.
Unaweza ukaomba kwa MUNGU na MUNGU akakujibu kupitia mtumishi wake, usipomwamini mtumishi huyo ni hatari kwako.
Biblia inasema kwamba Kanuni ya kufanikiwa kwa watu wa MUNGU ni kumwamini MUNGU na kuwaamini watumishi wake waaminifu katika KRISTO YESU.

2 Nyakati 20:20 ''..................  mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.'
Maana yake unaweza ukakosa mabadiliko kwa sababu humwamini mtumishi wa kweli wa YESU KRISTO anayekufundisha Neno hai la MUNGU.
Usikubali katika maisha yako ukafikia hatua humwamini MUNGU.
 
'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments