MAKUNDI 5 YA WATUMISHI KATIKA KANISA LA LEO.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.

◼️Kuna aina nyingi za Watumishi wa MUNGU katika Kanisa la KRISTO duniani, baadhi ya watumishi ni hawa;

1. Mtumishi anayejijua kwamba yeye ni Mtumishi ila hatumiki au anafanya kazi ya MUNGU Kwa ulegevu.

◼️Biblia inasema kumtumikia Bwana YESU kwa bidii na sio kwa ulegevu, hii ina maana hata Watumishi walegevu wapo.

Warumi 12:11 "kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia BWANA;"

➡️Hili ni Kundi la kwanza la Watumishi yaani ni Watumishi kabisa wa MUNGU ila hawatumiki na hata wakitumika hutumika kwa  ulegevu, wanafanya kazi ya MUNGU Kwa ulegevu, Biblia inasema hilo ni kosa.

Yeremia 48:10 "Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya BWANA kwa ulegevu; na alaaniwe auzuiaye upanga wake usimwage damu."

◼️Ni dhambi Mtumishi wa kweli wa Bwana YESU ila hutumiki au unatumika kwa ulegevu.

Yakobo 4:17 "Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi."

2. Mtumishi asiyejua kama yeye ni Mtumishi wa MUNGU.

 ➡️Mfano hai ni Musa.
MUNGU alimjua Musa kuwa ni Mtumishi wake ila Musa hakuwa anafahamu.

Kutoka 3:11 "Musa akamwambia MUNGU, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri?"

➡️Hapa Musa anapopewa jukumu la utumishi kulingana na huduma yake alikataa maana hakuwa anajua kama ni Mtumishi na alijua hana sifa za utumishi.

Kutoka 4:13 "Akasema, Ee BWANA, nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma."

◼️Lakini Musa huyu huyu ambaye hakujua kama ni Mtumishi Alipokuja kujitambua alifanya makubwa kuliko Watumishi wote Waisraeli waliokuja baadae.

Kumbu 34:10 "Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye BWANA alimjua uso kwa uso;"

◼️Leo Kuna Watumishi wengi wa Bwana YESU lakini hawajifahamu kama ni Watumishi ndio maana wanafanya vitu vya ajabu au hawatumikii MUNGU Kwa sababu hawajui.

3. Mtumishi asiyelitumia Neno la MUNGU kwa halali.

2 Timotheo 2:15 "Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na MUNGU, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli."

➡️Biblia inasema kulitumia Neno la MUNGU Kwa halali, Ukiona hivyo ujue wapo pia Watumishi ambao hawalitumii Neno la MUNGU Kwa halali, Kundi hili la Watumishi ni hatari sana na huleta madhara kwenye Kanisa.

➡️Watu ambao hawalitumii Neno la MUNGU Kwa halali ni wapotoshaji wa Neno la MUNGU.
Wapotoshaji wa Neno la MUNGU Biblia inasema juu yao kwamba ni watu wasio na Elimu ya ki MUNGU na ni watu ambao sio Wakristo imara.

2 Petro 3:16 "vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe."

◼️Ndugu, Usikubali kuwa Mtumishi unayepotosha Neno la MUNGU.

◼️Ndugu Usikubali kuabudu Kanisa ambalo Mchungaji wa hapo anapotosha kweli ya Injili ya KRISTO Kwa tamaa zake au kwa sababu ameshamuacha YESU KRISTO.

4. Mtumishi aliyefungwa na taratibu za dhehebu zilizo kinyume na kusudi la MUNGU.

Matendo 15:10 "Basi sasa mbona mnamjaribu MUNGU na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua."

➡️Ukisoma andiko hapo juu unaona andiko linaita torati kuwa ni kongwa ambalo Waisraeli walishindwa kulichukua ndio maana MUNGU akaleta Agano jipya katika KRISTO YESU Mwokozi.

➡️Huu ni Mfano mmojawapo kati ya mingi  wa watu kufungwa na taratibu za dhehebu, Mfano Leo dhehebu ambalo linafuata torati Mtumishi anayetokea huko hawezi kuhubiri Injili ya KRISTO Kwa usahihi katika baadhi ya Maeneo kwa sababu anafungwa na taratibu za dhehebu.
Mfano taratibu za dhehebu zinazuia Mtu kula nguruwe au kula  ndege aina ya Bata kwa sababu ya torati, Mtu huyo itakuwa mara chache kuwahubiri watu wampokee YESU KRISTO kama Mwokozi ila atahubiri zaidi watu wasile Bata kwa sababu ya kufuata taratibu za dhehebu lake, lakini katika ukweli halisi YESU KRISTO wakati anaondoka agizo lake kuu ni Watumishi wake Wahubiri watu wote kumpokea yeye  YESU KRISTO kama Mwokozi.

Marko 16:15-18 " Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya."

➡️ Mtumishi anayeteswa na taratibu za dhehebu hawezi kuhubiri watu kujazwa ROHO MTAKATIFU na kunena  kwa lugha kwa sababu kwanza yeye mwenyewe hata hajui ROHO MTAKATIFU ni nani wakati andiko hapo juu linasema Watumishi wa MUNGU watanena kwa lugha, na lugha hiyo ni lugha ya ROHO MTAKATIFU.

➡️Leo kwa ajili ya Mtumishi kuteswa na taratibu za dhehebu anaweza hata kuhubiri akikataza watu kuvaa suti, tai au kuhubiri kwamba nguo za langi nyeusi ni za shetani hivyo watu wote wavae nguo nyeusi tu au nyekundu, huyo ni vigumu kuwa na muda wa kuwahubiri watu wampokee YESU KRISTO kama Mwokozi wao.

Watumishi wengi kwa kufuata taratibu za dhehebu zilizo kinyume na KRISTO wamegeuka watumwa hivyo ni Watumishi watumwa wa dhehebu.

Wagalatia 5:1 "Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa."

5. Mtumishi anayejua kwamba yeye ni Mtumishi wa MUNGU na anatumika.

◼️Kwa jina lingine Watumishi wa Kundi hili wanaitwa Watenda kazi katika Shamba la MUNGU.

Luka 10:2 "Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake."

◼️Watumishi hawa ni wachache na YESU KRISTO anasema katika andiko hapo juu kwamba Watumishi wa aina hiyo tunatakiwa tuombe sana kwa MUNGU ili awalete, maana hawa ndio Pekee wanaohitajika.

◼️Hawa ndio wanaotimiza utumishi wao kwa KRISTO maana wanatumika.

Hawa Biblia inasema kwamba ni wachache sana ndio maana Kanisa linasisitizwa liombe kwa MUNGU ili MUNGU apeleke watenda kazi katika ulimwengu .

Mathayo 9:38 "Basi mwombeni BWANA wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake."

➡️Yaani MUNGU asilete tu Watumishi bali alete Watumishi wanaotumika pamoja na yeye.

➡️Mimi sijui wewe ndugu uko kundi gani ki utumishi.

➡️Inawezekana una nafasi ya kumtumikia Bwana YESU lakini hutumiki au haujijui.

➡️Inawezekana wewe una jina la kitumishi kabisa, unaitwa Mchungaji, Askofu, Mwinjilisti, Mtume, Nabii, Mwalimu, Mzee wa Kanisa, Mwenyekiti au Katibu wa wamama au vijana n.k lakini hutumiki au unalitumia vibaya Neno la MUNGU kwa tamaa zako.

➡️Inawezekana wewe ni Mtumishi unayejitambua lakini umetoroka kazi ya MUNGU au hutaki kumtumikia Bwana YESU.

➡️Ndugu, wewe ni Mtumishi gani katika Injili ya KRISTO?

◼️hakikisha unakuwa mtenda kazi unayetumika wakati unaofaa na hata wakati usiofaa.

◼️Hakikisha uko kazini muda wote ukiwaleta watu kwa YESU ili majina yao yaandikwe katika kitabu cha uzima mbinguni na walete kwa YESU ili wafunguliwe vifungo na wawe huru, watoe watu kwenye umateka wa shetani na mawakala zake, watoe watu kwenye mafundisho ya dini na manyonge yasiyiwafanya watu kwenda mbinguni na sasa wafundishe kweli ya MUNGU katika KRISTO YESU.

Naamini umejifunza jambo zuri na utafanyia kazi.
Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments