AINA TANO(5) YA NGUVU ZA MUNGU UNAZOZIHITAJI MTEULE WA KRISTO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU


  Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Siku moja nilikuwa naomba kwamba MUNGU anipe nguvu lakini nikasikia sauti ya ndani ikiniuliza '' Unahitaji MUNGU anipe nguvu za aina ipi?''
Jambo hilo lilinifanya kuwaza siku kadhaa na namshukuru ROHO MTAKATIFU maana alinipa ufunuo kupitia Neno la MUNGU na ufunuo huo ndio somo la leo.
Kama kuna kitu muhimu sana unakihitaji katika maisha yako ni nguvu za MUNGU.
1 Nyakati 16:11 ''Mtakeni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote.''
Nguvu za MUNGU zina faida nyingi sana katika maisha ya wateule wa KRISTO.
Kila mteule wa KRISTO anazihitaji sana nguvu za MUNGU.
Nguvu za MUNGU kila mtu wa kanisa anazihitaji sana.
Nguvu za MUNGU ndizo pia nguvu za ROHO MTAKATIFU, na nguvu hizo zinaweza kuwa ndani tu ya Walio na YESU waliozihitaji kwa maombi.
Zaburi 138:3 ''Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.''

Inawezekana wewe ni muombaji sana na mara kwa mara huwa unamuomba MUNGU kwamba akupe nguvu.
Ni Lugha za kawaida kabisa makanisani wakati wa maombi utasikia ''Eee MUNGU Baba nitie nguvu, nipe nguvu, nijaze nguvu n.k''
Ni vyema kuomba hivyo lakini unatakiwa kujiuliza ni nguvu za aina gani za MUNGU unazozihitaji maana kuna makundi zaidi ya moja ya nguvu za MUNGU ambazo unaweza ukazihitaji kulingana na mazingira yako na uhitaji wako.
Zaburi 119:28 ''  Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, Unitie nguvu sawasawa na neno lako.''

Labda ngoja kwanza nikufundishe maana ya nguvu.

Nguvu ni nini?

a. Maana ya kwanza ya neno ''Nguvu'' ni uwezo wa kufanya jambo.
Nguvu za MUNGU ni uwezo wa kufanya jambo, uwezo huo  anakupa MUNGU katika KRISTO YESU.

b. Maana ya pili ya nguvu ni uvumilivu unaokuwezesha kuendelea mbele.
Nguvu hizi ni muhimu sana na wasio na nguvu hizi hawawezi kuendelea mbele katika safari.

c. Maana ya tatu ya nguvu ni madaraka au uwezo wa kupanga na kufanya mambo yaliyokusudiwa.
Nguvu za MUNGU zinakupa uwezo au mamlaka  na kufanya kitu ulichokusudia.

d.Maana ya nne ya neno Nguvu ni kufanya jambo kwa bidii.
 Nguvu za MUNGU zinakufanya ufanye jambo fulani kwa bidii.

e. Maana ya tano ya neno nguvu ni uwezo wa kujifungua salama kutoka katika vifungo.
Yaani mfano wake ni kama mtu umemfunga kamba mguuni na ana nguvu za kuivuta kamba hiyo kwa sekunde na ikakatika akatoka akiwa huru,nguvu za MUNGU ni za muhimu sana sana.
 Zihitaji sana nguvu za MUNGU katika maisha yako.
Wafilipi 4:13 ''Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.''

Naamini sasa unaanza kuona mwanga halisi kutoka katika ufunuo wa somo hili.
Sasa inawezekana na wewe huwa unaomba sana MUNGU akupe nguvu, unafanya vyema sana lakini mwelezi MUNGU unahitaji nguvu zipi.
Inawezekana unaomba upewe nguvu lakini nguvu unazozihitaji sio nguvu unazoziomba. Ndugu yangu jifunze Somo hili na itakusaidia sana.

Makundi 5 ya nguvu za MUNGU unazoweza kuzihitaji wewe Mteule wa KRISTO.

1. Nguvu za kupata utajiri.

Kumb 8:18 '' Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.'' 
Hili ni kundi mojawapo ya makundi ya nguvub ambazo MUNGU anaweza kuziachilia kwa wateule wake wanaoishi maisha matakatifu.
Inawezekana wewe unatamani nguvu hizo za kupata utajiri lakini hujawahi hata siku moja kumuomba MUNGU akupe nguvu hizi, wewe huwa unasema tu kwamba MUNGU akupe nguvu lakini hupewi kwa sababu husemi unahitaji nguvu zipi.
Lakini pia nguvu za kupata utajiri ni lazima uelewe maana ya utajiri ndipo utajua vyema kuomba ili upewe nguvu za kupata utajiri.
Neno utajiri lina maana ya hali ya kuwa na mali nyingi au vitu vingi.
Katika maombi yako leo omba MUNGU akupe nguvu za kupata utajiri, hizi ni nguvu muhimu sana kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu.

2. Nguvu za Kuendelea mbele.

Isaya 40:29 ''Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.''
Inawezekana wewe kwa sababu ya mazingira uliyopo wala huhitaji nguvu za kupata utajiri ila unahitaji nguvu za kukuwezesha kuendelea mbele.
Inawezekana umevumilia sana kwa sababu ya uzao au mwenzi hadi unaanza kuchoka.
Inawezekana umekwazwa sana, inawezekana unaonewa sana na uko katika wakati mgumu sana, inawezekana unaumwa na hakuna tumaini la kuishi n.k. Ndugu, kama ni hivyo hakika unahitaji nguvu za MUNGU za kukufanya uendelee mbele.
Wako watu walikuwa watumishi wa MUNGU wazuri sana ila baadae ikatokea dhoruba ndogo na katika maombi yao wakawa wanasema kwamba ''MUNGU nipe nguvu'' ni sawa lakini mtu kama anahitaji nguvu za MUNGU za kumfanya aendelee mbele ni muhimu sana akahakikishe anaomba kwamba MUNGU ampe nguvu za kuendelea mbele.
Inawezekana umechoka kwa makwazo ya watu, inawezekana unakatishwa tamaa kila siku.
Ndugu unahitaji MUNGU akupe nguvu na nguvu unazozihitaji wewe ni nguvu za MUNGU za kukufanya uendelee mbele.
Kumbuka kwamba  kwa sababu ya kukosa nguvu za MUNGU za kundi hili, kama unazihitaji, unaweza kujikuta unamkosea MUNGU na usipopata Neema ya kutubu unakosa mbingu, hivyo magumu yako yoyote yasihalalishe dhambi kwako bali Muombe MUNGU akupe nguvu za kuendelea mbele na Wokovu na utakatifu.
Baraka yako ni yako tu hivyo mngoje MUNGU na atatenda, ukiona amechelewa kulingana na wewe basi muombe MUNGU akupe nguvu za kuendelea mbele huku ukingoja baraka zako ambazo hakika zitakuja tu.

Zaburi 27:14 ''Umngoje BWANA, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA. ''
 

Unaweza ukaona umechekewa kuolewa ukaamua kufanya uasherati na hivyo kujikuta unaingia katika vifungo vya giza na madhara mengi sana na baraka zako ndipo zikakimbia zaidi hivyo ukabaki katika dhambi hiyo na  unaweza kukosa mbingu.
Ndugu haijalishi uko katika magumu kiasi gani nakuomba usiombe tu kwamba MUNGU nipe nguvu bali omba kwamba MUNGU nipe nguvu za kuendelea mbele na YESU na utakatifu.
Ndugu unazihitjai sana nguvu za MUNGU za kukufanya uendelee mbele.
Hasa ukiwa katika magumu yeyote yanayotishia wewe kumwasi MUNGU, Ndugu usikubali kumkosa MUNGU bali endelea mbele huku ukimuomba MUNGU akupe nguvu za kuendelea mbele na Wokovu.
Ayubu 4:3-4 ''Tazama, wewe umewafunza watu wengi, Nawe umeitia nguvu mikono iliyokuwa minyonge. Maneno yako yamemtegemeza huyo aliyekuwa anaanguka, Nawe umeyaimarisha magoti manyonge.   ''

 3. Nguvu za kuwashinda mawakala wa shetani.

Zaburi 86:16-17 '' Unielekee na kunifadhili mimi; Mpe mtumishi wako nguvu zako, Umwokoe mwana wa mjakazi wako. Unifanyie ishara ya wema, Wanichukiao waione na kuaibishwa. Kwa kuwa Wewe, BWANA, Umenisaidia na kunifariji.''
 Mpaka adui zako waabishwe basi unahitaji nguvu za MUNGU za kuwashinda maadui hao.
Sasa inawezekana wewe unahitaji nguvu za kundi hili ili uwashinde mawakala wa shetani lakini kosa lako wewe badala ya kuomba MUNGU akupe nguvu za kuwashinda mawakala wa shetani wewe umeomba MUNGU akupe nguvu za kuendelea mbele, sio kwamba ni vibaya kuomba nguvu za kuendelea mbele lakini kabla hujaomba MUNGU akupe nguvu ni vyema ukagundua unahitaji nguvu zipi ndipo utaomba upewe hizo na kufanikiwa sawasawa na uhitaji wako wa Nguvu hizo za MUNGGU kwako.
Mawakala wa shetani utawashinda ukiwa tu na nguvu za MUNGU za kukupa uwezo wa kuwashinda mawakala wa shetani.\
Unahitaji sana kuwa na nguvu hizi na kimaombi tu unaweza kuomba na ukapewa.
 Isaya 41:10-13 ''usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni MUNGU wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia''

4. Nguvu za kustawi.

Isaya 58:11 ''Naye BWANA atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.''

Inawezekana wewe una nguvu za rohoni za kupata utajiri, inawezekana wewe una nguvu za rohoni za kukufanya uendelee mbele hata ukiwa katika magumu, inawezekana wewe una nguvu za roho za kuwashinda mawakala wa shetani, ni sawa kabisa lakini wakati mwingine unahitaji nguvu za MUNGU za kukufanya ustawi.
Kuna watu hata akipewa mtaji wa milioni 50 bado itaisha hiyo pesa kwa sababu hana nguvu za kumfanya kustawi.
Kustawi ni nini?
Kustawi ni ni kuwa na hali njema huku ukiendelea kukua vizuri na kufanikiwa vizuri.
Kumbuka kila jambo huanzia rohoni kabla halitaonekana katika hali ya kimwili hivyo hata rohoni unahitaji sana nguvu za MUNGU za kukuwezesha kustawi ndipo utazipata na kustawi.

5. Nguvu za kulihubiri Neno la MUNGU.

Mika 3:8 ''  Bali mimi, hakika nimejaa nguvu kwa roho ya BWANA; nimejaa hukumu na uwezo; nimhubiri Yakobo kosa lake, na Israeli dhambi yake. ''
Sio kila mtu ana nguvu za kulihubiri Neno la MUNGU.
Inawezekana wewe ni Mtumishi wa MUNGU na huwa unafundisha Neno la MUNGU, Ndugu unafanya vyema sana lakini unahitaji sana kumuomba MUNGU akupe nguvu zake za kukuwezesha kulihubiri Neno la lake.
Kwa walio watumishi tayari naamini wananielewa vizuri zaidi katika kipengele hiki.
Nguvu za MUNGU za kukuwezesha kuhubiri Neno la KRISTO kwa viwango atakavyo MUNGU unaweza kuzipata kama ukimuomba MUNGU akupe.
Nguvu hizi ni muhimu sana maana ndani ya nguvu hizo na kufunguliwa kwa watu kutatokea.
Bwana YESU alipofanya huduma yake alikuwa na nguvu hizi siku zote.
Matendo 10:38 ''habari za YESU wa Nazareti, jinsi MUNGU alivyomtia mafuta kwa ROHO MTAKATIFU na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana MUNGU alikuwa pamoja naye.''
Hata wewe Mtumishi wa MUNGU wa namna yeyote hakikisha unakuwa mtu wa kuomba MUNGU akupe nguvu hizi za kukuwezesha kulihubiri Neno lake kama atakayo yeye MUNGU huku Neno hilo likiambatana na nguvu kubwa za kuwafungua watu na kuwaweka huru siku zote.

 Naamimi sasa umeelewa umuhimu wa nguvu za MUNGU unazozihitaji.
Lakini pia ngoja nikuambie mambo haya muhimu sana.

Mambo yanayoweza kuondoa nguvu za MUNGU kwako.

1. Kumkataa ROHO MTAKATIFU.
Zakaria 4:6 ''................ Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.''
ROHO MTAKATIFU ndiye mwezeshaji wa kila kitu katika maisha ya wateule wa KRISTO.
Hata nguvu za MUNGU kwa jina lingine zinaitwa nguvu za ROHO MTAKATIFU hivyo tambua kwamba sio kwa akili zako bali ni kwa ROHO MTAKATIFU ndipo nguvu za MUNGU zitafanya kazi kwako, hivyo ukimkataa ROHO MTAKATIFU umezikataa nguvu za MUNGU.

2. Kwenda kinyume na kusudi la MUNGU.
Waamuzi 16:19-20 '' Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa BWANA amemwacha.''
Samsoni ni mfano hai kwetu.
Samsoni alikuwa na nguvu za kuwashinda maadui wote na alikuwa ameshawashinda mara nyingi na kwa miaka mingi lakini kitendo cha yeye kwenda kinyume na kusudi la MUNGU kulifanya nguvu za MUNGU kuondoka kwake.
Hata wewe inawezekana umeomba kwa MUNGU kwamba upewe nguvu za MUNGU fulani lakini ukienda kinyume na kusudi la MUNGU hakika nguvu hizo zinaweza kuondoka kwako na hivyo ukapata hasara.
Kumbuka ukimwacha MUNGU na yeye atakuacha hivyo nguvu za MUNGU  hakikisha unazitunza kwa utakatifu na kukaa katika kusudi la MUNGU.
2 Nyakati 15:2 " …...... BWANA yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi."

3. Kutokuwa mtu wa maombi.
Mathayo 11:12 '' Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.''
Tangu zamani za Biblia wenye nguvu za maombi ndio wanaoteka vitu vizuri kutoka ufalme wa MUNGU.
Maombi ndio ufunguo wa kila kitu hivyo ukiacha maombi utakosa vitu vingi ikiwemo nguvu ya MUNGU unayoihitaji.

 4. Kuishi maisha ya dhambi.
Maombolezo 1:14-15 ''Kongwa la makosa yangu limefungwa na mkono wake; Hayo yameshikamana; Yamepanda juu shingoni mwangu; Amezikomesha nguvu zangu; BWANA amenitia mikononi mwao, Ambao siwezi kupingamana nao. BWANA amewafanya mashujaa wangu wote ''
Huu ni mfano hai kwetu kwamba wana wa Israeli walikuwa na nguvu sana lakini dhambi zao ziliwafanya nguvu ya MUNGU kuondoka kwao hivyo wakapigwa na kupelekwa utumwani Babeli.
Dhambi ndio jambo baya ambalo huongoza katika kuondoa nguvu za MUNGU ndani ya mtu.
Kama kuna kitu cha kuepeka sana ukitaka nguvu za kweli za MUNGU ziwe na wewe ni kuepuka  dhambi.
Baadhi ya Watumishi wengi ambao hufanya dhambi wala hawana nguvu za MUNGU ila wameshajiunga na shetani hivyo wanatumia nguvu za shetani na sio za MUNGU.
Kama unazihitaji nguvu za MUNGU hakikisha unatakiwa kuishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU.

5. Kutumia nguvu za giza.
Ufunuo 13:2 '' Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.''
Joka ni shetani na mnyama ni roho ya kuzimu iliyopewa nguvu na shetani, hivyo wapo watu pia wasiompenda YESU hao hutumia nguvu hizo za kishetani.
Nguvu za MUNGU haziwezi kamwe kufanya kazi pamoja na nguvu za shetani.
Hivyo kuna watu wanatumia nguvu za MUNGU na kuna watu wanatumia nguvu za shetani.
Inawezekana wewe unatumia nguvu za shetani lakini unatamani kutumia nguvu za MUNGU, Ndugu kama ni hivyo basi unahitaji kuachana na nguvu za shetani haraka sana, tubu na anza upya na YESU KRISTO kisha utaomba kupata nguvu za MUNGU na utazipata.
Ukianza kutumia tu nguvu za giza ujue nguvu za MUNGU hata kama ulikuwa nazo nyingi ujue zitaondoka muda huo huo maana nguvu za MUNGU haziwezi kufanya kazi pamoja na nguvu za giza.

'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''



Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

+255714252292(Hadi whatsapp).



mabula1986@gmail.com

Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments