HAKIKISHA UMEZALIWA MARA YA PILI

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
Leo tunaangalia habari za Kuzaliwa Mara ya Pili.

➡️Tunapozungumzia kuzaliwa mara ya pili tukumbuke kwamba tulizaliwa mara ya kwanza na Wazazi wetu wa kimwili,  ni pale ulipozaliwa kupitia wazazi wako wa kimwili yaani Baba na Mama, mfano angalia Mwanzo 4:25.
kuzaliwa mara ya pili ni tofauti na kuzaliwa mara ya kwanza, kuzaliwa mara ya pili tunazaliwa na MUNGU Mwenyewe kwa njia ya KRISTO YESU, ndio maana baada ya kuzaliwa mara ya pili tunaitwa Watoto wa MUNGU.

1 Petro 1:3 "Ahimidiwe MUNGU, Baba wa Bwana wetu YESU KRISTO, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake YESU KRISTO katika wafu;"

◾Nini maana ya kuzaliwa Mara ya pili?

1. Kuzaliwa Mara ya pili ni kumwamini YESU KRISTO kama Mwokozi kisha kumpokea kama Mwokozi na baada ya hapo unaanza kuliishi Neno la MUNGU huku ukiongozwa na ROHO MTAKATIFU.

1 Yohana 5:1 "Kila mtu aaminiye kwamba YESU ni KRISTO amezaliwa na MUNGU. Na kila mtu ampendaye mwenye kuzaa, ampenda hata yeye aliyezaliwa na yeye."

◼️ Tunaweza kusema Kuzaliwa Mara ya Pili ni kupokea utu mpya kutoka kwa MUNGU Kwa njia ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi na kukubali kuwa chini ya Mamlaka yake.

2. Kuzaliwa Mara ya pili ni MUNGU kuibadilishwa roho yako kupitia wewe kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi.

Yohana 1:12-13 " Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu."

◼️Yaani ni MUNGU kukuondolea moyo wa jiwe na kukubadilisha kupitia Neno lake.

Ezekieli 36:24-27 " Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi
zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu
wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa
moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi
mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda."

◼️Hivyo MUNGU ndiye Baba mzazi wa roho zetu baada ya sisi kuokolewa na Mwanaye pekee YESU KRISTO Mwokozi wetu.

Yakobo 1:18 "Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake."

3. Kuzaliwa Mara ya Pili ili ni mtu kupokea upya utakatifu kutoka kwa MUNGU, aliye mtakatifu.

Yohana 3:3 "YESU akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa MUNGU."

◼️Utakatifu huu unaupata kwa wewe kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi na baada ya hapo unaanza kuliishi Neno la MUNGU kama linavyoagiza.

◼️Mambo 5 yanayoweza kumthibitisha Mtu kuwa amezaliwa Mara ya Pili.

1. Kuwa na ROHO MTAKATIFU, Kutubu na kufanywa upya na ROHO MTAKATIFU.

Tito 3:5 "si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na ROHO MTAKATIFU;"

◼️Unapookoka jambo hilo huthibitishwa na mambo mawili yaani kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na kutubu dhambi zako zote ili uanze upya na MUNGU, hiyo ni kazi ya ROHO MTAKATIFU na ukifanikiwa katika hayo umezaliwa mara ya Pili.

◼️Jambo la pili ni kuwa na ROHO MTAKATIFU.

Matendo  1:8 "Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu ROHO MTAKATIFU; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi."

◼️Waliozaliwa mara ya pili Wana ROHO MTAKATIFU.

2. Tumezaliwa Mara ya pili kwa kuliamini Neno la KRISTO na kuanza kuliishi.

1 Petro 1:23 "Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la MUNGU lenye uzima, lidumulo hata milele."

◼️Tunapookoka tunaanza kuukulia Wokovu kwa kujifunza sana Neno la MUNGU la Injili ya KRISTO na tunavyoendelea kuliamini hilo Neno la MUNGU linatubadilisha tunaanza kulifuata katika ROHO MTAKATIFU, tukitimia katika hilo tumezaliwa mara ya pili.

◼️Hivyo liamini Neno la KRISTO YESU na liishi daima ili ubaki umezaliwa mara ya pili.

3. Tumezaliwa Mara ya pili katika KRISTO ili tutende haki na tuiishi haki.

1 Yohana 2:29 "Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye."

◼️Kuzaliwa Mara ya Pili huambatano na mabadiliko ya tabia kwa Mtu husika, hivyo ili kukuthibitisha kuwa umezaliwa mara ya pili kweli basi Ishi Maisha Matakatifu ya Wokovu huku ukitenda  haki na kuiishi haki kuu ambayo ni Injili ya KRISTO.

➡️Tenda haki na iishi haki.

4. Kwa sababu kuzaliwa Mara ya pili ni kumwamini YESU KRISTO, kisha kumpokea kama Mwokozi na kisha kuanza kuliishi Neno la MUNGU basi mpende YESU KRISTO na mfuate.

1 Yohana 5:1 "Kila mtu aaminiye kwamba YESU ni KRISTO amezaliwa na MUNGU. Na kila mtu ampendaye mwenye kuzaa, ampenda hata yeye aliyezaliwa na yeye."

◼️Timiza kumpenda Bwana YESU baada kumwamini  kisha kumpokea kama Mwokozi wako.

Mtu aliyezaliwa mara ya pili anayempenda Bwana YESU yukoje?

◼️Mtu huyo kwanza humpokea ROHO MTAKATIFU na Kuenenda katika yeye ROHO MTAKATIFU.

Yohana 14:17 "ndiye ROHO wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu."

◼️Kisha mtu huyo hushika yaliyo na YESU KRISTO.

Yohana 14:15 "Mkinipenda, mtazishika amri zangu.''
Ndugu jichunguze kama kweli umezaliwa mara ya pili na unampenda YESU KRISTO.

5. Aliyezaliwa mara ya pili huushinda ulimwengu, Tumezaliwa mara ya pili ili tuushinde ulimwengu.

1 Yohana 5:4 "Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na MUNGU huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu."

◼️Hakikisha unajifunza jinsi ya kuushinda ulimwengu na anza kuushinda ukiwa nuruni mwa MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.

◼️Ndugu hakikisha umezaliwa Mara ya pili.

Nimesema Hatua za kufikia kuzaliwa Mara ya pili ni hizi;

◼️Kumwamini kisha kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi.

◼️Kutubu dhambi na kuziacha.

◼️ Kukubali kuongozwa na Neno la MUNGU tangu wakati huo.

 ◼️Kumpokea ROHO MTAKATIFU na kuanza kuongozwa na yeye.

◼️ Kuendelea kuishi maisha matakatifu.

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments