IJUE SAUTI YA MUNGU ILI UTENDE KAMA MUNGU ANAVYOKUAGIZA..

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Ni MUNGU ndiye aliyetuumba katika mwili, lakini pia ndiye MUNGU aliyetuumba kiroho baada ya sisi kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wetu.

Yohana 1:12-13 " Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."

Kuna faida kubwa sana kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi.
Baada ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi unafanyika mtoto wa MUNGU na MUNGU anaweza kusema na wewe chochote kiwe kuhusu huduma, familia yako, taifa lako, kazi yako n.k
Lakini pia ni muhimu sana kujifunza sana Biblia ili uijue sauti ya MUNGU inayosema na wewe. 
Kumbuka MUNGU hatafanya jambo lolote bila kuwajulisha watumishi wake.
Amosi 3:7  ''Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.''
Baada ya kuokoka inakupasa sana kujifunza Neno la MUNGU ili ujue kupambanua sauti.Kumbuka kuna sauti aina tatu unaweza kusikia.
1. Sauti ya MUNGU.

2. Sauti ya mwanadamu.
3. Sauti ya shetani.
Ushauri wangu kwako ndugu ni kwamba jifunze sana kuijua sauti ya MUNGU ili ikusaidie kuzipambanua sauti za kibinadamu na zile sauti za kishetani.
Uwe makini pia maana sauti za kishetani ni kwamba zinakufanya ukose tumaini, zinakufanya uwe mwoga na hata zinaweza kukufanya uumwe na kudanganyika.

Na kwa sababu unaihitaji sana sauti ya MUNGU katika maisha yako, napenda kukuambia yafuatayo;

Mambo ya kujua kuhusu sauti ya MUNGU.

1. Sauti ya MUNGU ndio sauti pia ya ROHO MTAKATIFU na ni hiyo hiyo ndio sauti ya Bwana YESU Mwokozi.
Yeye anasema
Yohana 10:27 " Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata."


2. MUNGU hazungumzi na watu ambao hawamtaki, MUNGU anazungumza na watu walio tayari kuisikia sauti yake.

 Kumb 4:35-36 ''Wewe umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa BWANA ndiye MUNGU, hapana mwingine ila yeye. Kutoka mbinguni amekusikizisha sauti yake, ili akufundishe; na juu ya nchi alikuonyesha moto wake mkuu; ukasikia maneno yake toka kati ya moto. '' 


3. Kama unahitaji sana MUNGU aseme na wewe, unahitaji jambo moja tu yaani yaani unamhitaji ROHO MTAKATIFU.
Yohana 14:26 ''Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.''
Kama humhitaji ROHO MTAKATIFU ujue unakaribisha sauti za kishetani na sauti za kibinadamu tu na sio sauti ya MUNGU.


4. Kufaulu au kufanikiwa kiroho kwa Mteule wa KRISTO kunatokana na jinsi anavyosikia sauti ya MUNGU.
Kumb 28:1 ''Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; ''
Hivyo tamani sana kuisikia sauti ya MUNGU.
Iamini sauti ya MUNGU na kuitii.
Omba MUNGU akupe maagizo na yazingatie maagizo hayo.
Unapotii maagizo ya MUNGU inakuletea kufanikiwa sana kiroho.


5. Sauti ya MUNGU inafunua na kujulisha kilichopo.
 1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.''
Katika ROHO MTAKATIFU tunafunuliwa na kujua mambo mengi sana.
ROHO MTAKATIFU hujulisha yanayoendelea katika ulimwengu wa roho wa giza ili tujue jinsi ya kushinda nguvu za giza, ROHO MTAKATIFU pia hutujulisha na kutufunulia yale yanayopangwa na MUNGU juu yetu ili tushirikiane na mpango huo wa MUNGU ambao una faida kubwa kwetu.
Sasa hatuwezi kufananisha sauti ya MUNGU Muumbaji wetu na sauti nyingine.
Ndugu jifunze sana kuielewa sauti ya MUNGU
Baada ya kuisikiliza sauti ya MUNGU na kuitii basi omba kwa MUNGU ili akupe sauti ya kumnyamazisha shetani na mawakala zake.


Baadhi ya faida zinazotokana na kuisikiliza na kuielewa sauti ya MUNGU.
Waefeso 1:17-18 '' MUNGU wa Bwana wetu YESU KRISTO, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; ''
1. Utapata Roho ya hekima/akili.
2. Utapata Roho ya ufunuo.
3. Utapata Roho ya maarifa ya kiroho.
4. Utapata Roho ya kumjua MUNGU na kusudi lake.
5. Macho yako yataangaziwa nuru ya KRISTO.
1 Wakorintho 2:13 "Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na ROHO, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni."

Kazi zote hizo atazifanya ROHO MTAKATIFU kwako kupitia hicho ulichosikia na kuona kilicho katika sauti ya MUNGU kwako.
Jifunze sana kuisikia sauti ya MUNGU, kuielewa na kuifanyia kazi ili uwe heri duniani.


MUNGU anaweza akasema na wewe kwa sauti yake kupitia;
 
1. MUNGU kusema na wewe kwa Ndoto.

Ayubu 33:14-16 ''Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao, ''
Ndoto ni matukio unayoyaona kwa kutumia utu wako wa ndani ukiwa umesinzia.
Note: kuna vyanzo aina 3 vya ndoto. Yaani inawezekana chanzo cha ndoto yako ni MUNGU, inawezekana ni wewe mwanadamu na inawezekana ni shetani.
Nazungumzia tu ndoto ikiwa tu ni MUNGU amekusemesha kwa ndoto.


2. MUNGU kusema na wewe kwa Maono.
Ezekieli 37:1-5 '' Mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya BWANA, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa;  akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana. Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe.  Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la BWANA.  Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi.''
Maono ni matukio unayoyaona kwa kutumia utu wako wa ndani ukiwa hujasinzia.
Maono unaweza kuona hata ukiwa unatembea njiani au ukiwa unaomba.
Lakini hata shetani anaweza kukuonyesha maono hivyo jifunze kuijua sauti ya MUNGU ndipo utagundua maono uliyoona ni ya MUNGU au ya shetani.


3. MUNGU kusema na wewe kwa Mazingira uliyopo.
Mfano unaweza kuwa katika mazingira hatari yanayokuhitaji wewe uombe, hapo huhitaji hadi usikie sauti ikiikuambia kuomba ndipo uanze maombi.
Mfano mwingine kijana umefikia umri wa kuoa mfano una miaka 35 hapo haihitaji hadi uone kwa ndoto au usikie sauti ikikuambia sasa tafuta mchumba ili ufunge ndoa takatifu.
Mfano umeota ndoto au umeona maono ukiona nyoka anakukimbiza, mazingira hayo yanakujulisha kwamba kuna adui katika ulimwengu wa roho anataka kukuangamiza hivyo omba maombi ya Vita ukipigana naye na utamshinda,mazingira tu yamekujulisha.

Ona mfano huu, Hesabu 22:21-23 '' Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.
 Hasira ya MUNGU ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa BWANA akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye.
 Na yule punda akamwona malaika wa BWANA amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani.''

Balaamu alishangaa punda wake amegoma kwenda, mazingira yale yalitakiwa kumjulisha kwamba kuna kitu sio cha kawaida maana ndio ilikuwa mara ya kwanza punda yule kugoma kwenda.
Kuna Mtumishi mmoja aliikimbia kazi ya MUNGU na kwenda kufumgua biashara, biashara ile iligoma na balaa nyingi zilimwandama, mazingira yale tu yalimjulisha juu ya nini kilichopo.
Mimi Peter binafsi wakati naingia facebook mwishoni mwa mwaka 2011 nilikuwa na malengo haya kwa ajili ya facebook; Kupost picha za Yanga siku ikishinda na kuutumia muda huo kuwasimanga simba, kupost vichekesho na siasa, kupost matukio yanayotokea na kubishana na watu mbalimbali ambao nitaona wanaanzisha ligi. Nilifanya vitu hivyo kwa muda huku nimeokoka kabisa lakini nikashangaa nikawa naona maono mengi juu ya kazi ya MUNGU lakini nilishupaza shingi, siku nyingine nikawa nakosa amani moyoni nikiingia mtandaoni, mazingira yale yalitakiwa kunijulisha kitu muhimu cha kufanya kwa utukufu wa MUNGU lakini nilishupaza shingo. Siku moja sitaisahau ambao kuna mtu mmoja kati ya marafiki zaidi ya 2000 niliokuwa nao kwa wakati huo aliniambia maneno magumu sana kwangu wakati hata hanifahamu na hajawahi kuniona, mtu yule alisema ''Wewe umeitwa huku facebook ili uhubiri injili lakiini wewe umekalia tu mipira na siasa'' Neno hilo liliniuma sana sana moyoni mwangu na lilikuwa linajirudia moyoni mwangu, ndipo nikaamua kujiapiza moyoni kwamba kazi yangu mtandaoni itakuwa kuhubiri Neno la MUNGU tu basi. Nilianza kufanya hivyo na hadi leo hii watu ambao nimeshawaongoza sala ya toba ili waokoke ni wengi na hata idadi sikumbuki, watu ambao nimewaombea baada ya wao kujifunza Neno la MUNGU nililopost ni wengi kiasi kwamba hata idadi sikumbuki, kwa miaka sita nimepost masomo ya 800 na ni watu wengi mno wamenipa shuhuda juu ya kile Neno la MUNGU limebadilisha maisha yao kutokana na masomo yangu. Sasa nilijulishwa kwa mazingira lakini nikashupaza shingo ndipo MUNGU akamtuma mtu ambaye alinifungua ufahamu, hata kama mtu huyo yeye wala sikuona amewahi kupost Neno la MUNGU popote, yaani MUNGU alimtumia mtu ambaye hajaokoka ili anifungue fahamu mimi niliyeokoka.
Mazingira ya mtandaoni yalitakiwa kunijulisha sauti ya MUNGU juu ya nini cha kufanya. 
Kuna jinsi nyingi mazingira yanaweza kukusemesha na ukagundua kabisa kuna sauti ya MUNGU ya maelekezo mema kupitia hayo mazingira.
Muhimu jifunze kuijua na kuielewa sauti ya MUNGU ili ugundue ni wapi MUNGU kasema, kumbuka MUNGU ni wa utakatifu tu, hivyo hata kama umesikia sauti au umeona kiroho kwa njia nyingine yeyote kama hakuna utakatifu ndani yake ujue MUNGU hajakusemesha.


4. MUNGU kusema na wewe kwa Neno la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.
 Zaburi 32:8 '' Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.''

5. MUNGU kusema na wewe kwa Malaika.
Mfano ni huu.
Luka 1:13 '' Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana. ''
Malaika unaweza ukamuona au usimuone ila ukasikia tu sauti akikuelekeza jambo la ki MUNGU.


6. MUNGU kusema na wewe mubashara(Live) kwa sauti.
 2 Samweli 2:1 ''Ikawa baada ya hayo, Daudi akauliza kwa BWANA, akasema, Je! Niupandie mji wo wote wa Yuda? BWANA akamwambia, Haya! Panda. Daudi akasema, Niupandie mji upi? Akasema, Hebroni.''

7. MUNGU kusema na wewe kwa Kupitia wewe kuongea na Mtumishi wa KRISTO aliyepewa Neno na MUNGU kwa ajili yako.
Mfano hai ni huu, Isaya 38:4-5 '' Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema,  Enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano.''
Hezekia aliongea na Isaya lakini kumbe Isaya alikuwa amepewa ufunuo na MUNGU kuhusu Hezekia.
Hata wewe unaweza kumshirikisha Mtumishi wa MUNGU jambo na jambo hilo akakujibu kwa kusudi la MUNGU kabisa.
Mtumishi huyo anaweza kuwa anafahamu na akakuambia, lakini pia anaweza kukuambia jambo hata yeye hafahamu kama ni MUNGU anapitisha ujumbe wake.
Mfano ni Mtumishi anahubiri au anafundisha na wewe unasikiliza au unasoma mafundisho yake.
Mfano mwingine Mtumishi anakushauri au anakuelekeza kwa simu au mkiwa mmekaa sehemu.
Hata mzazi wako au ndugu yako anaweza kukuonya au kukusaidia jambo iwe kwa hasira au kwa kawaida na kumbe ndani ya maneno yake kukawa na sauti ya MUNGU ikikuelekeza.


8. MUNGU anaweza kusema na wewe kupitia wewe kusoma Biblia.
Penda sana kusoma Biblia na kulitafakari sana Neno la MUNGU.

Danieli 9:2-3 '' katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la BWANA lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. Nikamwelekezea BWANA Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. ''
Danieli alijikuta siku moja anaanza maombi baada tu ya kusoma maandiko matakatifu.
Hata wewe unaweza kupata maelekezo ya moja kwa moja kupitia Biblia unayoisoma, unaweza ukafungua andiko fulani na pale MUNGU akawa anasema na wewe mambo kukuhusu.

 Mfano siku moja nilisoma  somo kuhusu madhabahu na nikashangaa kupata ufunuo huu;
''Katika Maombi Yako Ya Leo Jiungamanishe Na Madhabahu Ya Mbinguni. 
Madhabahu Ni Daraja Kutoka Ulimwengu Wa Roho Kuja Ulimwengu Wa Mwili. 
 Kila Kitu Unachokiomba Majibu Yake Yatapitia Madhabahuni Kuja Kwako. 
Hata kwenye madhabahu ya mbinguni kuna kitu kitafanyika kuhusu maombi yako yanayofika katika madhabahu ya MUNGU mbinguni.
 Ufunuo 8:3-4 '' Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhabahu, mwenye chetezo cha dhahabu, akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu ya dhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi.
4 Na moshi wa ule uvumba ukapanda mbele za Mungu pamoja na maombi ya watakatifu, kutoka mkononi mwa malaika. ''

Point Ya Leo Uwe Mtakatifu Na Jiungamanishe Na Madhabahu Ya Mbinguni Kwa Maombi Utashinda.''

Sauti ya MUNGU ni ya muhimu sana kwako ndugu kama unataka kushinda vit ya kiroho.
MUNGU wetu hakawii kujibu Bali kwa wakati wake anatenda.
MUNGU wetu hakawii kuitimiza ahadi yake, Bali kwa wakati wake anatenda.
Wakati wake kutenda ni huu.
MUNGU wetu hakawii Bali kwa wakati wake anajibu.
2 Petro 3:9 "BWANA hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba."

Inawezekana unaonekana kama sio kitu kwa wanaokuzunguka, kwa sababu hawaoni majibu ya maombi yako.
Ndugu nakuomba endelea na maombi.
Inawezekana maadui zako wanadhani wamekuweza, lakini jibu lako kutoka kwa MUNGU litawamaliza na kuwaliza.
Endelea na maombi ndugu na shikilia utakatifu katika KRISTO daima.

Ndugu endelea na maombi.
Endelea kumwangalia Mwokozi wako YESU KRISTO na sio kuangalia wanadamu.

Songa mbele maana ushindi wako unaotokana n maombi yako na utakatifu upo tu na utafika.
Luka 18:1 ''  ......   imewapasa kumwomba MUNGU sikuzote, wala wasikate tamaa. ''


Kwa Leo mimi na wewe tuombe maombi haya chini.
omba mwenyewe maombi haya.


1. Likomboe Kanisa ili lipate mafanikio ya kiroho.
Zaburi 133:1 ''
Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.''

2. Zipige kimaombi roho za kipepo zinazovamia baraka yako unayoipata kama wewe ni mtoaji mwaminifu wa zaka na sadaka.
Malaki 3:11 ''
Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi.''

3. Omba kwa MUNGU kwamba kila mtu wa Kanisa awe mwekezaji kwenye kazi ya MUNGU.
Yaani ita wawekezaji kwenye kazi ya MUNGU.

 2 Kor 9:6-7 '' Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.  Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.''

4. Ita ushindi wa MUNGU katikati ya vita yako ya kiroho uliyopo.
Kutoka 14:14 ''
BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya. ''

5. Ombea miguu yako kiroho.  

Zaburi 56:6 ''Hukutanika, hujificha, huziangalia nyayo zangu, Kwa kuwa wameniotea nafsi yangu.''

Ukifungwa miguu kiroho maana yake unazuiliwa kiroho kufuata baraka yako ya kila namna.
 Ayubu 33:11 ''Hunitia miguu yangu katika mkatale, Na mapito yangu yote huyapeleleza''
=Ukifungwa miguu kiroho maana yake umewekewa mipaka kiroho na mawakala wa shetani ili usifanikiwe katika lolote.
Ikomboe miguu yako kwa damu ya YESU KRISTO ya agano la ushindi.


6. Ita ahadi za MUNGU kwako.
2 Kor 1:20 ''
Maana ahadi zote za MUNGU zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; MUNGU apate kutukuzwa kwa sisi.''

7. Mshukuru MUNGU.
 Zaburi 9:1-2  ''Nitamshukuru BWANA kwa moyo wangu wote; Nitayasimulia matendo yake yote ya ajabu. Nitafurahi na kukushangilia wewe; Nitaliimba jina lako wewe uliye ju''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

+255714252292(Hadi whatsapp).

+255786719090

mabula1986@gmail.com


Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments