![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU Kisha tuombe Maombi ya ushindi.
◾Leo tunajifunza jinsi ya kuombea ndoto tulizoota.
Ndoto za MUNGU huja kutimia kama ujumbe wake ni wa kutimia.
Habakuki 2:3 "Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia."
◼️MUNGU husema nasi kwa ndoto.
Ayubu 33:14-16 " Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,''
➡️Kwa ujumla Ndoto alizokuonyesha MUNGU katika KRISTO YESU Ziko katika makundi 4.
◼️Kundi la kwanza ni ndoto za MUNGU anazoonyesha Matendo yake au yale atakayotenda Baadae.
Mfano hai ni Ibrahimu kwa Ndoto aliambiwa atazaa uzao wake baadae utakuwa Mwingi kama Nyota za Mbinguni, wakati anaambiwa haya Ndotoni hakuwa na Mtoto hata mmoja, alipomwamini MUNGU kupitia Ndoto hiyo MUNGU akamuhesabia haki jambo hilo na likaja kutumia.
Mwanzo 15:1-6 " Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu KATIKA NJOZI, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. Nalo neno la BWANA likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki."
Mfano Mwingine Nebkadneza aliona kwa ndoto yatakayotokea Baadae.
Danieli 2:28 "lakini yuko MUNGU mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho. Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi;"
◼️Kundi la pili la Ndoto ni ndoto za MUNGU akikuonyesha umefungwa wapi, ndoto hizi utaona Nguvu za giza au maeneo ya kazi za shetani alizofanya shetani kwenye Maisha Yako.
Mfano unajiona unapigwa na watu, uko gerezani, uko kwenye shimo, umekamatwa, unaumwa na wanyama wakali n.k
Isaya 42:22 Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.
◾Kuna baadhi ya watu hudhani ndoto hizi sio za MUNGU na kumbe ni MUNGU anawajulisha kilichofanyika na adui ili tuombe tujitoe katika Mikono ya mawakala wa shetani.
Katika Ndoto hizi unamuona adui akifanya mambo mabaya lakini anayekuonyesha ni MUNGU ili umshinde adui huyo.
Mfano hai ni Mimi Peter Mabula Kuna kipindi kwa miezi kadhaa karibia Kila siku au wakati Mwingine Mara 3 hadi 5 kwa wiki naota Niko Kijijini nilikowahi kuishi, na ni wakati tu ambao napanga mipango yangu ya maendeleo ndio naota ndoto hizo.
ROHO MTAKATIFU akanionyesha kwamba Kuna madhabahu ya giza kule inafanya kazi kuzuia, Nyota imeshikiliwa kule n.k
Nilipoomba kuharibu madhabahu za giza kule, roho za mizimu na Kila aliyenishikilia kule zile ndoto zilikoma na ndipo mafanikio eneo hilo niliyaona.
◼️Kundi la tatu ni ndoto za MUNGU Zenye majibu Yako ya nini Cha kufanya ili ufanikiwe, ushindi au ili uwe fulani.
Mfano Abimeleki aliona Ndotoni kifo kwa sababu ya makosa yake ya kuchukua Mke wa Mtu, hapa alikuwa anapewa majibu kwamba akitaka asife aachane na Mke wa mtu.
Mwanzo 20:3 "Lakini MUNGU akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu."
◼️Kundi la Nne la Ndoto za MUNGU ni MUNGU kukuonyesha alichokifanya au anachofanya kukusaidia.
Zaburi 89:19 "Ndipo ulipowaambia watakatifu wako kwa njozi, Ukasema, nimempa aliye hodari msaada; Nimemtukuza aliyechaguliwa miongoni mwa watu."
Mfano unaona Mtumishi wa KRISTO mwaminifu akikuombea au akikushauri au akikuelekeza nini ufanye au akikuonya ili usiharibikiwe.
Mfano unaona Malaika akikusaidia au akikupa mbinu za ushind.
Mwanzo 31:11-12 " Na malaika wa MUNGU akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa.
Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda wanyama wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutendea Labani."
Mfano kuona Mtu au Viongozi wa serikali wakiwa upande wako, huo ni msaada wa MUNGU kwa njia hiyo.
➡️Jambo kubwa ukiota ndoto ni Maombi na aina gani ya Maombi uombe.
◾Jinsi ya kuombea ndoto uliyoota.
1. Husika na matukio ya ndotoni na mazingira ya ndotoni kuombea kulingana na ndoto husika.
➡️Yusufu aliona tukio la MUNGU kumwinua kuliko Ndugu zake.
Mwanzo 37:5-7 " Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu.
◼️Kwa ndoto kama hii Maombi ni kumshukuru MUNGU na kuomba Neema ya kufika hatua hiyo uliyoiona.
◼️Kama ni hila za adui haribu na kama ni jambo jema la ki MUNGU mshukuru MUNGU na zingatia ujumbe wa ndoto, hii ndio maana ya kuhusika na Matukio uliyoyaona.
2. Ujue Ujumbe wa ndani ya ndoto ili uombee huo ukifuta kusudi la giza huku ukilisimamisha kusudi la MUNGU.
Mwanzo 40:5 Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani.
◼️Mfano ujumbe wa Ndoto za Hawa wawili uliwataka kuchukua hatua hasa kwa aliyeona mabaya juu yake, yeye hakuomba akafa kweli kama ndoto yake ilivyokuwa.
Habari ya watu hawa na ndoto zao inaelezwa katika Mwanzoni 40:5-22 fungua Biblia Yako uisome.
3. Tafuta maandiko kwenye Biblia yanayoenda kinyume na mipango ya giza uliyoiona ili uombe ukitumia maandiko hayo kufuta ajenda zote za kipepo.
Zaburi 107:20-21 " Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu."
Kama ni mpango wa MUNGU uliouona ndotoni basi tafuta maandiko yanayothibitisha kisha ombea mambo ya ndoto yako kwa maandiko ili kulithibitisha jambo la ki MUNGU uliloliona.
4. Fanyia kazi kitu cha ki MUNGU ulichokiona Ndotoni.
Mwanzo 20:6-7 " MUNGU akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao."
◼️Mfano badilika tabia kama Ujumbe wa ndotoni unakutaka kubadilika tabia.
◼️Toa Sadaka au Zaka kama Ujumbe unakutaka hivyo.
◼️Anza kufungua biashara au tafuta kazi kama Ujumbe wa ndoto unakutaka hivyo.
◼️Vunja urafiki na baadhi ya watu wabaya kama Ujumbe wa ndoto umekuelekeza hivyo.
N.k
◼️Fanyia kazi maelekezo ya ndotoni ya MUNGU kwako.
5. Kama kuna jambo umeliona ndotoni na umeomba lakini bado huna amani, endelea na maombi mpaka uwe na amani ndio utakuwa umeshinda.
1 Wathesalonike 5:17 "ombeni bila kukoma;"
6. Wakati mwingine adui zako ndotoni huvaa sura za watu au wanyama au wadudu.
Mfano umeota kama andiko hili linavyosema.
Zaburi 38:19" Lakini adui zangu ni wazima wenye nguvu, Nao wanaonichukia bure wamekuwa wengi."
➡️Umeota adui zako Wanadamu au mapepo yaliyovaa sura za watu, umewaona Wana Nguvu umeona wakikutesa na kukuonea na ni wengi.
Wewe omba ukipambana ukisema mfano "Ewe wakala wa shetani unayefuatilia maisha yangu, huku nakuona ndotoni ukivaa sura ya Fulani au ya mnyama Fulani, sasa nakupiga kwa fimbo ya chuma kama Zaburi 2:9 inavyosema, naamuru njia yako ya kuja kwangu iwe giza na utelezi kama Zaburi 35 inavyosema, hutanifikia kamwe, hutaifikia Ndoa yangu, uchumba wangu, kazi yangu, biashara yangu, afya yangu katika Jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu nimeomba"
➡️huo ni mfano wa kuomba ukipambana na adui aliyevaa sura isiyo yake ndotoni.
7. Kama kuna vitu ndotoni umeona vimefanyika ardhini basi usisahau kimaombi kuhusika na ardhi.
◼️Mfano umeona madhabahu ya giza eneo Fulani au umeona uchawi ukifanyika katika Ardhi fulani, chukua hatua kimaombi katika Jina la YESU KRISTO.
Kumbukumbu la Torati 12:2-3 * Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo."
◼️Mfano Umeona vitu vinazikwa, umeona maadui wako ardhi fulani n.k
➡️Wewe haribu nguvu za Giza zilizofanyika ardhini, futa kumbuka mbaya kuhusu wewe iliyotunzwa ardhini n.k
8. Muhimu zaidi katika Maombi yako ya kuombea ndoto uliyoota ni wewe kuhusika na ROHO MTAKATIFU katika maombi hayo na husika na Neno la MUNGU katika Maombi hayo.
Yuda 1:20 "Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,"
◼️Kuna watu wanasumbuliwa sana na wachawi.
Kuwashinda hao mawakala wa shetani ni wewe kuhusika na YESU Mwokozi na ni wewe kuomba maombi katika jina la YESU KRISTO.
◼️Ziko aina nyingi za maombi na ROHO MTAKATIFU hutoa ufunuo wa kimaombi ili ujifunze na uombe.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments