| Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.  | 
Bwana YESU KRISTO atukuzwe Ndugu zangu.
Karibu katika kujifunza Neno la MUNGU.
Biblia inatutaka tuwe hodari katika MUNGU.
Waefeso 6:10 "Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika BWANA na katika uweza wa nguvu zake."
Najua kila Mkristo anatamani awe hodari katika MUNGU.
Natambua kabisa kila mtu anatamani mapepo yamuogope, wachawi wamkimbie , awe na kinywa chenye mamlaka dhidi ya nguvu za giza.
Na pia najua kabisa kila mtu anatamani awe na nguvu za MUNGU, awe na kibali kikubwa, awe na mafanikio ya kimwili na kiroho.
Najua kabisa kila mtu anatamani awe na macho ya rohoni yanayoona, awe na masikio ya rohoni yanayoisikia vyema sauti ya MUNGU, awe na kibali na mamlaka za kiroho zinazoleta ushindi.
Ni hakika katika KRISTO YESU Biblia inatutaka sana tuwe hodari katika MUNGU wetu kwa kutumia uweza wa nguvu zake.
Somo langu linasema kwamba namna au jinsi ya kuwa hodari katika MUNGU.
Je ufanyeje ili uweze kuwa hodari katika MUNGU?
1. Vaa silaha za MUNGU.
Waefeso 6:11 "Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani."
◼️Baada ya wewe kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako inakupasa sana kufanya mambo ya Kibiblia yanaweza kukufanya uwe hodari katika MUNGU na katika uweza wa nguvu zake.
Silaha za MUNGU zinaweza kukufanya uwe hodari katika MUNGU maana MUNGU hatakuwa kinyume na wewe.
Silaha hizi za MUNGU tunazivaa kwa kuziishi na sio kuzitaja tu.
Silaha hizi zimetajwa katika Waefeso 6:13-17, Naomba utazisoma ila hapa Mimi nakutajia tu.
Silaha za MUNGU ambazo unatakiwa kuzivaa kwa njia ya kuziishi ni hizi.
A. Kuwa mkweli daima.
B. Kuishi maisha ya hakika.
C. Kuwa na utayari siku zote wa kupeleka injili ya KRISTO.
D. Kuwa na Imani thabiti katika KRISTO YESU.
E. Uwe mtu wa kulipokea Neno la MUNGU daima.
2. Mpokee ROHO MTAKATIFU.
Yohana 14:26 " Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia."
◼️Ukimpokea ROHO MTAKATIFU hakika utapokea na yote yaayomhusu.
Utapokea nguvu, utapokea maelekezo ya kukusaidia, utapokea kibali kikuu kwa MUNGU n.k
3. Lifanyie kazi Neno la MUNGU.
Yakobo 1:22 "Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu."
4. Nyenyekea kwa MUNGU katika KRISTO YESU.
1 Petro 5:6 "Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa MUNGU ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;"
5. Ishi maisha ya kuongozwa na ROHO MTAKATIFU utashinda kila nguvu za kishetani.
1 Yohana 4:4 "Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye(ROHO MTAKATIFU) aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye(Shetani) aliye katika dunia."
6. Zitafute nguvu za MUNGU kwa maombi yanayoambatana na maisha matakatifu.
Waefeso 6:18 "kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika ROHO, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;"
◼️Maombi ni njia mojawapo kuu ya kukufanya uwe hodari katika MUNGU maana maombi yatakufanya uwe mshindi daima.
Maombi yapo ya aina mbili yaani maombi ya bila kufunga na kisha kuna maombi ya kufunga(Mathayo 17:21), haya nayo ni ya muhimu sana sana ili uwe mshindi mwenye nguvu daima.
Hivyo tafuta daima nguvu za MUNGU.
1 Nyakati 16:11 "Mtakeni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote."
7. Mtumikie Bwana YESU Mwokozi.
Danieli 11:32b " lakini watu wamjuao MUNGU wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu."
Ukimtumikia MUNGU kwa usahihi katika KRISTO YESU lazima uwe hodari.
1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."
◼️Nguvu za MUNGU kubwa sana huwa zinaambatana na Neno la MUNGU, hivyo unavyomtumikia Bwana YESU ujue nguvu za MUNGU lazima ziambatane na wewe.
8. Tumia Mamlaka nne(4) za kiroho tulizopewa na MUNGU sisi wateule wake katika KRISTO YESU.
Mamlaka hizo ni hizi;
A. Jina la YESU KRISTO(Yohana 14:13)
B. Damu ya YESU KRISTO(Ufunuo 12:11)
C. Nguvu za ROHO MTAKATIFU (Matendo 1:8)
D. Neno la MUNGU la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU (Zaburi 107:20)
Hakikisha unakuwa hodari katika YAHWEH MUNGU wa pekee.
Hakikisha unakuwa hodari katika Bwana YESU.
"Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
Comments