![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.
Neno ''Mafanikio'' lina maana matokeo mazuri ya jambo fulani.
Kuna aina 3 za Mafanikio.
1. Mafanikio ya ki MUNGU.
Mwanzo 14:19 "Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na MUNGU Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi."
Mafanikio ya ki MUNGU chanzo chake ni MUNGU wa Mbinguni.
Ni Mafanikio ambayo hayamtoi Mtu kwa YESU KRISTO Mwokozi.
Mwanzo 35:9 "MUNGU akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki."
Haya ni Mafanikio ambayo yanatokana na Mtu kufanya kazi njema halali huku akimuomba MUNGU ambariki na kweli anabarikiwa na MUNGU kupitia kazi njema anazofanya.
2. Mafanikio ya kidunia.
Mathayo 16:26 "Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?"
Mafanikio ya kidunia ni Mafanikio ambayo Mtu anafanya juhudi mbaya za kibinadamu ili afanikiwe, sehemu kubwa zaidi ya juhudi hizo ni dhambi kama utapeli, kuuza madawa ya kulevya, Mtu anaiba, kufanya kazi ambazo ni dhambi, kupokea rushwa, kuuza pombe, kutumia mwili kupata Mali n.k
Marko 8:36 "Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?"
Mafanikio haya Mtu anaweza kuyapata lakini Yana hasara kubwa kwake Baadae asipopata Neema ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.
3. Mafanikio ya kishetani.
Maandiko haya yanaonyesha shetani shetani anaweza kumgawia Mtu utajiri au Mafanikio ila tu kama Mtu huyo atamsujudia.
Mathayo 4:8-9 " Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia."
Bwana YESU kupitia hapa alifundisha kwamba Mtu mwenye Akili hatakiwi kumsujudia shetani kwa namna yeyote ile, hata kwa ajili ya Mali.
Lakini Leo wako watu kwa sababu ya tamaa ya mali na ufahari wa Duniani wamemsujudia shetani kwa kuingia naye mkataba.
Wengi sana wameingia mikataba na shetani na kutoa kafara wazazi wao au Watoto wao au Ndugu zao, ni hatari sana.
Kutafuta Mafanikio kwa shetani na mawakala zake ni kujiangamiza mwenyewe maana hata ukipata utajiri wenye masharti bado Kuna jehanamu.
Luka 9:25 "Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?"
Je wewe una mafanikio gani?
Kama una Mafanikio nje na MUNGU katika KRISTO YESU utapata faida gani ukiondoka Duniani?
Watu wengi hupata mafanikio au matokeo mazuri ya mambo wanayoyahitaji lakini chanzo cha mafanikio hayo sio MUNGU, Ni hatari sana.
Hata wewe ndugu najua una mafanikio mengi tu, je ulishawahi kujiuliza mafanikio yako chanzo chake ni nini?
Hakikisha unatafuta mafaniko ambayo chanzo chake ni MUNGU na sio dunia au nguvu za giza.
Mafanikio ya kidunia hutanguliwa zaidi na dhambi, hiyo haifai.
Mafanikio ya kishetani chanzo chake ni nguvu za giza, hiyo ni hatari sana na haitakiwi kuwapo katika watu wa MUNGU wanaoipenda mbingu.
1 Yohana 2:15-17 " Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele."
Moja ya kitu muhimu sana kinachotakiwa kuambatana na maisha yako siku zote ni kumcha MUNGU.
Mithali 1:7" Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, wapumbavu hudharau hekima na adabu."
Usipojifunza sasa kumcha MUNGU ujue maisha yako baadae yatakuwa na utata ndipo hapo wengine hujikuta wakitafuta Mali kwa kufanya dhambi au wengine kwenda kwa shetani ili wapate Mali.
Kumcha MUNGU ni jambo la muhimu sana.
Kumcha MUNGU kunaambatana na kujiepusha na kila uovu.
Mtu hupata maarifa anapomcha MUNGU maana kumcha MUNGU ndio chanzo cha maarifa sahihi.
Hakikisha unakuwa mtu bora, mteule wa KRISTO uliye safi rohoni na mwilini na Fanya kazi halali njema MUNGU atakubariki tu.
Kumcha MUNGU kutakufanya uwe msafi rohoni, uwe msafi wa tabia na uwe msafi wa mavazi.
Kumcha MUNGU huleta maarifa mengi mazuri sana.
Ndugu hakikisha unaishi maisha ya kumcha MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.
Lakini hata kama ni MUNGU Mwenyewe amekubariki ukawa tajiri bado Kuna angalizo.
1 Timotheo 6:17 "Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha."
Sasa wako watu wako katika mikataba ya kishetani inayowatesa sana.
Wako watu wako katika vifungo vya kishetani walivyoviingia wenyewe, hawavipendi ila wanaogopa kutoka katika vifungo hivyo kwa kuwaogopa wakuu wa giza maana walipokuwa wanaingia Walipewa masharti kwamba wakitoka watakufa.
Wako watu kwa kuogopa mashariti ya waganga wa kienyeji wameendelea kuwa watumwa wa nguvu za giza.
Wako watu kwa kuwaogopa majini waliowafunga vifungo, wameshindwa kujinasua katika kamba hizo za kuzimu.
Isaya 42:22 "Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha."
Ndugu unatakiwa utoke katika mikataba hiyo ya kishetani, unatakiwa ufunguliwe kutoka vifungo vya giza. Anayeweza kukufungua na kukuweka huru kisha asiwepo mkuu wa giza wa kukudhuru, ni YESU KRISTO Mwokozi.
Bwana YESU ni Mwokozi maana yake anakuokoa, anakufungua na kukulinda dhidi ya waliokuwa wamekufunga.
Yohana 10:28-30 " Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. BABA yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa BABA yangu. MIMI na BABA tu umoja."
Labda ngoja nikupe siri hii ambayo labda ulikuwa huijui.
Siri yenyewe ni hii kwa namna gani unaweza kutoka katika mikataba ya kishetani?
1. Chagua sasa Bwana YESU KRISTO awe kiongozi wako.
Bwana YESU anasema na wewe sasa kupitia Neno lake akisema "Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.-Mathayo 11:28"
2. Amua kuombewa kwa Jina la YESU KRISTO utakuwa huru kabisa.
Mathayo 21:22 "Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.'
3. Kuanzia Sasa jitenge mbali na nguvu za Giza na mawakala wa shetani kama Waganga n.k
Yakobo 4:7-8 " Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili."
4. Ishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU ili uwe huna kifungo tena cha kipepo kilichokufunga au kukufuatilia.
Yohana 8:36 "Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli."
Ndugu yangu, kanuni ni moja tu ukitaka kutoka katika mikataba ya kishetani kisha ubaki salama bila kufuatiliwa na mawakala wa shetani.
Kanuni ni wewe kumkimbilia Bwana YESU Mwokozi ili akuokoe, okoka ndugu, acha dhambi na anza sasa kuishi maisha matakatifu ya Wokovu.
Ni YESU tu anayeweza kukufungua mikataba ya kishetani yote iliyokufunga na kisha anakulinda kuanzia hapo.
Mambo yanayowafanya watu wengi wasitoke katika mikataba ya kishetani waliyoingia.
1. Kuchanganyikiwa baada ya kuingiziwa mapepo ndani yao.
2. Kuwa waoga kwa kumuogopa shetani wakati hana lolote.
3. Kufikiria kwamba milango ya giza iliyowafunga kwamba haiwezi kufunguliwa.
Ndugu, Ukitaka kufunguliwa vifungo vya giza na mikataba ya kishetani kisha ubaki salama siku zote za maisha yako inakupasa sana uokolewa na YESU KRISTO.
Ni kwa YESU tu ndio kwenye mikono salama baada ya kufunguliwa vifungo na mikataba ya giza.
Bwana YESU anasema "Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja.-Yohana 10:28-30.
YESU akikufungua ndugu na atakulinda hivyo usiogope kukimbilia Kanisani au kwenye mikutano ya injili kule anakohubiriwa YESU maana waliokutisha kwamba ukivunja mkataba watakuua, wakati huu ukiwa kwa YESU hakika MUNGU hatawaruhusu hata kukugusa.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments