| Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU. |
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.
Somo la leo linasema Kama umewahi kumsengenya mtu tubu na usirudie kusengenya watu.
✓✓Kusengenya ni nini?
◼️Kusengenya ni kumsema mtu kwa mabaya wakati hayupo.
Kusengenya ni kumteta mtu.
◼️Kuteta ni nini?
✓✓Kuteta ni kumsema mtu kwa ubaya bila ya mwenyewe kujua.
Je wewe hujawahi kumsengenya mtu?
Kama hujawahi kumsengenya mtu ujumbe huu haukuhusu ila kama umewahi kumsengenya mtu hata mmoja basi tubu na usirudie kusengenya watu.
Je ulihusika kumsengenya nani?
Je ni wazazi wako au ndugu zako?
Je uliwasengenya watumishi wa MUNGU au wafanya kazi wenzako?
Je uliwasengenya marafiki zako au watu wa Kanisani kwenu?
Je ulimsengenya nani?
MUNGU Baba anasema '' Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia. Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza; Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe. Walakini nitakukemea; Nitayapanga hayo mbele ya macho yako. Yafahamuni hayo, Ninyi mnaomsahau MUNGU, Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya. -Zaburi 50:20-22 ''
Biblia inasema kwamba unaweza ukapata madhara makubwa kwa kosa tu la kusengenya watu.
Najua katika jamii ya leo kila mtu yuko huru na uhuru huo wengine wanautumia vibaya na wengine wanautumia vibaya zaidi uhuru wao hata kuugusa utukufu wa MUNGU, Yaani wanawasema kwa mabaya watumishi wa MUNGU bila kosa lolote.
Katika jamii ya leo wapo hadi watu wanaweza kutengeneza picha au ku-edit picha za watumishi wa MUNGU na kuwazushia ili tu watumishi hao wadharaulike.
Leo unaweza ukakuta robo tatu ya wanakanisa wa mahali fulani kila siku kazi yao ni kumsengenya Mchungaji wao, ambaye hana kosa lolote.
Wako watu leo akionywa tu na watumishi anaanza usengenyaji wa hali ya juu sana dhidi ya watumishi hao.
Wako watu wakiona tu kuna mtu kafanikiwa kidogo katika jambo fulani basi kazi yao inakuwa kumsengenya na kumsema vibaya.
Wako watu wakisikia tu kuna mtu kabarikiwa baraka fulani basi kwa miezi kadhaa kazi yao itakuwa kumsengenya mtu huyo.
Hakuna faida hata moja katika kumsengenya mtu yeyoteb bali kuna hasara kubwa sana.
Masengenye huzalisha dhambi nyingi na masengenye humfnya mtu kuwa mbali na MUNGU.
Warumi 1:28-30 ''Na kama walivyokataa kuwa na MUNGU katika fahamu zao, MUNGU aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, WENYE KUSENGENYA, wenye kusingizia, wenye kumchukia MUNGU, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao,''
MUNGU hataki wewe ndugu uwe msengenyaji.
Bwana YESU hataki wewe mteule wake uwe mtu wa masengenyo.
Vyanzo vinavyopelekea mtu kumsengenya mwingine.
1. Wivu juu ya mtu huyo.
Yakobo 3:14-16 '' Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya.''
2. Mtu kutawaliwa na dhambi na hajajitenga na dhambi.
Isaya 59;1-2 ''Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. ''
Dhambi ni kikwazo kikubwa sana cha mafanikio ya watu wa MUNGU.
Shetani hupata uhalali wa kumtesa mtu baada ya dhambi, hivyo matokeo ya dhambi yanaweza kumfanya mtu kujaa tu masengenyo.
Biblia inatutaka tujitenge na ubaya wa kila namna ikiwemo na masengenyo.
1 Thesalonike 5;22 '' jitengeni na ubaya wa kila namna. ''
3. Ulegevu, uzembe na uvivu uliopelekea yeye kuwa chini.
Mithali 13;4 ''Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. ''
Biblia iko wazi sana kwamba mtu mvivu hutamani bila kupata.
Ndugu, inawezekana hao waliopata wao walifunga na kuomba bila kuchoka ndio mana wamepata, wewe je?
Inawezekana hao waliopata ni matokeo ya wao kutoa zaka, sadaka na dhabihu, wewe je?
Inawezekana hao waliisikiliza sauti ya ROHO MTAKATIFU hadi wakafanikiwa katika utumishi wao, wewe je?
Somo langu hili nazungumza na watu wa MUNGU waliookolewa na Bwana YESU ndio maana zizungumzii mafanikio ya kipepo ya watu wasio na YESU. Hapa nazungumza na Kanisa hai la Bwana YESU duniani hivyo wewe uliye Kanisa jifunze na itakusaidia.
Biblia inatushauri sisi Kanisa kwamba '' Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia BWANA; kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu;-Warumi 12:8-12 ''
Tukidumu katika ushauri wa Neno la MUNGU hata masengenyo hayatakuwepo.
4. Mtu kumilikiwa na nguvu za giza.
Isaya 42:22 '' Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha. ''
Wako watu ni wasengenyaji kwa sababu ya kumilikiwa na nguvu za giza.
Ndugu kama ni wewe basi tafuta kufunguliwa kwa maombi kupitia damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO.
Inawezekana unaowasengenya ndio wanaendelea kufanikiwa huku wewe unaendelea kudumaa kiroho hadi kiuchumi.
Ndugu tafuta kufunguliwa vifungo vyote vya giza.
5. Kutamani kitu kisha usipate, huku wengine kitu kama hicho hicho ulichotamani wamekipata.
Yakobo 4:2 '' Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!''
Kuna watu wanatamani vitu fulani na wanapokosa huku wengine wanapata ndipo wao huanza tu masengenyo tu.
Binti anaweza kutamani kufunga ndoa, hafuati kanuni za MUNGU za kuita baraka zake. Sasa kwa sababu yeye ni wa siku nyingi Kanisani anadhani kwamba atafunga ndoa kwanza yeye. Sasa anaweza akahamia binti kanisani pale na baada ya mwaka mmoja akafunga ndoa, ndipo mabinti wakongwe kazi yao walio wengi unaweza kukuta ni masengenyo.
Ndugu, Ukimuona mtu kafanikiwa wakati mwingine ni kwa namna alivyomsikiliza ROHO MTAKATIFU na kumtii.
Zaburi 32:8 '' Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.''
Sasa wewe umekalia kusikiliza watu huku mwenzako anamsikiliza ROHO wa MUNGU na kumtii ndio maana amefanikiwa kupata baraka ambayo na wewe unaitaka.
6. Moyo wako kuujaza mabaya na sio kujaza Neno la MUNGU.
Mathayo 12:34 ''Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. ''
Yaani Neno akisema Bwana YESU hilo ni kweli na ndio milele.
Sasa hapa anasema mtu huongea yaliyojaa moyoni mwake.
Sasa wewe moyoni kama umejaza wivu, husuda na majigambo basi kazi yako nyingine inaweza kuwa ni kusengenya tu watu, ni jambo basa sana.
Je moyoni mwako umejaza nini?
Je umejaza mabaya ndio maana kazi yako ni kuwasengenya watumishi waaminifu wa Bwana YESU?
Marko 7:21-23 ''Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.''
Bilia inakusaidia kwamba ili angalau uwe na muda wa kusema mema na sio mabaya basi lijaze moyoni Neno la KRISTO YESU.
Wakolosai 3:16 ''Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. ''
7. Uvivu wa maombi au kuomba vibaya na kupelekea kutokupata ulichotamani.
Mathayo 7:8 '' kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.''
Biblia inasema anayeomba kwa MUNGU hupewa alichoomba.
Inategemea tu na maelezo ya ROHO MTAKATIFU juu ya maombi yanayoleta majibu kwa mtu huyo.
Wengine huomba wakiambatanisha maombi yao na sadaka njema.
Wengine huomba maombi ya kufunga mara kadhaa na kwa kwa siku nyingi.
Wengine huomba kwa kutumia Neno la MUNGU, Wengine huomba kiufunuo n.k
Hivyo Biblia inaposema kila aombaye hupewa basi Omba sawasawa na matakwa ya MUNGU juu ya hitaji lako, matakwa ya MUNGU juu yako anayo ROHO MTAKATIFU hivyo mtii sana yeye.
Inawezekana wewe ni mvivu wa kuomba ndio maana hupati na kwa sababu wengine wanapata wewe unaanza kuwasengenya.
Inawezekana wewe unaomba kimazoea ndio maana hupati,na kwa sababu wengine wanapata wewe unaanza kuwasengenya.
Inawezekana wewe unaomba huku ukichanganya dhambi na wokovu ndio maana hupati na kwa sababu wengine wanapata wewe unaanza kuwasengenya.
Inawezekana wewe unaomba vizuri lakini una malengo mabaya kama ukipewa hivyo unavyoomba.
Yakobo 4:3 '' Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. ''
Kama kweli umeokoka basi hakikisha unaacha ya kale yote, yaani achana na matendo ya kipindi hujaokoka yakiwemo masengenyo.
Masengenyo ni ya wapagani na sio ya waenda mbinguni.
Wakolosai 3:8-9 '' Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; ''
8. Kutokuwa na tunda la ROHO MTAKATIFU liitwalo uvumilivu.
Wagalatia 5:22 '' Lakini tunda la ROHO ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,'',
ROHO MTAKATIFU huja kwako kipindi umempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.
Anapokuja ROHO MTAKATIFU kwako hukuletea matunda yake tisa ili uendelee kumpendeza MUNGU hata mahali ambapo utatakiwa kusubiri kidogo.
Moja ya matunda ya ROHO MTAKATIFU ni uvumilivu.
Maana yake nini?
Wakati mwingine unaweza ukaomba jambo lakini MUNGU asikupe kwa wakati huo kwa sababu kwa mujibu wa mbingu majira ya jambo hilo kwako sio wakati huo, hata kama unahitaji wakati huo.
Sasa kama una tunda la uvumivu utaendelea kuvumilia na kuomba bila kuwasema vibaya wanaofanikiwa kupata kitu kama ulichohitaji wewe.
Kumbuka tunapofanya maombi huwa hatumlazimishi MUNGU kutenda tunachotaka ila huwa tunaomba na kwa neema yake yeye hutupa katika wakati sahihi kwetu.
Uvumilivu wa ROHO MTAKATIFU ukiwa ndani yako wala hutaumia ukiona wengine mfano wamefunga ndoa na wewe bado, hutawasengenya maana hakuna faida hata moja katika kumsengenya mtu.
Ndugu, hakikisha unaishi na tunda la ROHO MTAKATIFU liitwalo uvumilivu.
Waebrania 6:11-12 ''Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho; ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu. ''
9. Hasira zinazokaa vifuani vya wapumbavu, zinazotokana na kukosa.
Mhubiri 7:9 '' Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.''
Kuna aina zaidi ya moja za hasira na katika aina hizo iko pia aina mojawapo ya hasira. Hasira hii Kibiblia inaitwa hasira ikaayo tu kifuani mwa mpumbavu.
Hii hukaa kwa watu wengi wakiwemo na wasengenyaji wanaosengenya mtu baada ya mtu huyo kupata kitu fulani na wao kukosa.
Anaweza mtu akarekodi nyimbo nzuri za injili lakini waimbaji wenzake wenye hasira za kundi hili kazi yao inaanza, nayo ni kumsengenya tu na kumsema vibaya, kumbe chanzo ni wao kukosa na yeye kupata.
Hasira za namna hii ni mbaya sana na hizo kukaa tu vifuani vya mapumbavu.
Ayubu 5:2 ''Kwani hasira humwua mtu mpumbavu, Nao wivu humwua mjinga.''
Mfano hao ni Sauli alipoanza kumuonea wivu na kumchukia Daudi kwa sababu tu Daudi amefanya vizuri kuliko yeye Sauli.
1 Samweli 18:9 ''Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.''
Baada ya hapo utaona Mara Sauli ameitisha kikao kumbe ni ili kujadili Daudi na kutafuta nafasi ya kumuua n.k
Biblia inatushauri vyema sana ikisema '' Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;-Weefeso 4:31''
Kama umewahi kumsengenya mtu tubu na usirudie kusengenya watu.
.'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp)
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
Comments