KAZI ZA MALAIKA WA MUNGU BAADA YA MAOMBI YAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU Mwokozi atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Kuna aina mbili za Malaika.
1. Kuna Malaika wa nuru yaani Malaika wa MUNGU.

2. Kuna Malaika wa giza yaani majini na kwa jina lingine wanaitwa majeshi ya pepo wabaya au maroho wa kuzimu.


Malaika wa Nuru wanafanya wanafanyia kazi Ufalme wa MUNGU uliyo chini ya YESU KRISTO, maana YESU KRISTO ndiye Mfalme wa ufalme wa MUNGU.

Malaika wa Giza yaani pepo wabaya, majini, mizimu na kila watenda kazi wa kishetani kutoka kuzimu wao huufanyia kazi ufalme wa shetani.

Sasa kwa watu walio upande wa shetani yaani watu wanaoufanyia kazi ufalme wa giza wanajua sana kuwatumia malaika wa giza katika kazi zao za kipepo.
Lakini katika ulimwengu wa roho wa nuru ambapo wateule wa KRISTO wote wapo, walio wengi hawajui jinsi ya kuwatumia Malaika wa MUNGU na wengi hawajui jinsi ya kushirikiana na Malaika wa MUNGU.
Kazi yangu Leo nazungumzia upande mmoja tu wa Malaika yaani Malaika wa nuru au kwa jina lingine malaika wa MUNGU.


Kuna makundi kadhaa ya Malaika wa MUNGU, lakini makundi makuu mawili ni haya.

1. Maserafi.
Isaya 6:1-2 " Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona BWANA ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama MASERAFI; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka."

Tunaona hapa Maserafi ni daraja la kwanza kabisa la Malaika, hawa wako maeneo kabisa ya kiti cha enzi cha MUNGU.


2. Makerubi.
Ezekieli 10:1 "Ndipo nikaangalia, na tazama, katika anga lililokuwa juu ya vichwa vya  MAKERUBI, kulionekana juu yao kana kwamba ni yakuti samawi, kuonekana kama mfano wa kiti cha enzi."

Makerubi ni Malaika wa cheo cha chini ya Maserafi.
Maana yake Maserafi ni Malaika wa cheo cha juu zaidi kisha wanafuata  Makerubi.
Kazi za Makerubi ni waimbaji wa kumsifu na kumwabudu MUNGU.
Kama tu ulikuwa hujui ni kwamba Shetani Kabla ya kuasi alikuwa Malaika aina ya kerubi.

Ezekieli 28:14  "Wewe ulikuwa KERUBI mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa
juu ya mlima mtakatifu wa MUNGU, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto."

Hivyo napenda pia kuchukua nafasi kuwafungua ufahamu watu wale waliokamatwa na dini za mpingaKristo hata wanadhani kwamba shetani alikuwa mkuu sana mbinguni, Mara wengine wanadanganya watu kwamba shetani alihusika na uumbaji, wengine wanadanganya kwamba shetani ameumba dunia baada ya MUNGU kuumba mbingu.
Dini nyingi za mashetani zinampamba sana shetani kwamba alikuwa Malaika mkuu mbinguni lakini ukweli wa Kibiblia ni kwamba shetani alikuwa Malaika aina ya kerubi, wala hakuwahi kufikia hata cheo cha serafi.

Malaika aina ya Kerubi ni wengi tu, hata baada ya Adamu na Eva kufukuzwa Edeni MUNGU alimuweka Malaika aina ya Kerubi kulinda Edeni.
Mwanzo 3:24 "Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka
MAKERUBI, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima."


Nimewahi kukutana na maswali ya watu wakiuliza kwamba Wenye uhai wanne na wazee 24 ni Malaika au ni akina nani?
Hata wewe inawezekana una swali kama hilo.
Majibu yangu ni kwamba hatujafika mbinguni bado hivyo siku tukifika huko ndipo tutajua kama kutakuwa na nafasi ya sisi kujua, ila Biblia imewaita tu Wenye uhai wanne, wakiwakilisha Injili 4 za YESU KRISTO na wazee 24. Hayo ndio majina yao Kibiblia hivyo hata Mimi nasema kwamba sijui kama ni Malaika ila ninachojua wanaitwa Wenye uhai 4 na wazee 24 japokuwa kwa kuangalia maandiko unaweza ukaona kwamba hawa  Wenye uhai 4 kwa sehemu wana sifa zinazokaribiana na Maserafi.


Malaika wa MUNGU wana kazi kubwa na nyingi kwa ajili ya wateule wa MUNGU.
Kwa sababu hili ni somo la kimaombi basi acha tuangalie kazi za Malaika ikiwa wewe umemuomba MUNGU.


1. Malaika huwazunguka wateule wa KRISTO, kuweka kituo kwao na kuwaokoa dhidi ya hila za shetani.
Zaburi 34:7 " Malaika wa BWANA hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa."

Sasa Kama umemuomba MUNGU  kwamba Malaika zake wakuokoe na hila mbaya dhidi yako na wafanye kituo kwako ujue ni hakika Malaika wa MUNGU watakuokoa.
Mfalme mmoja siku moja alikubali ulinzi wa MUNGU kupitia Malaika kwa watu wake.
Mfalme huyo alijua wateule wa MUNGU watakufa ndani ya tanuru la moto lakini MUNGU wa uzima alitenda muujiza kwa watu hao.
Mfalme huyo alisema hivi "Na ahimidiwe MUNGU wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma MALAIKA wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila MUNGU wao wenyewe.-Danieli 3:28"


Malaika pia  katika kukuokoa mteule wanaweza hata kuwapiga upofu maadui zako ili tu wewe usidhulike.
Mfano ni huu ambapo Malaika waliwapiga upofu maadui wa familia ya Lutu.
Mwanzo 19:11 "Kisha wakawapiga hao watu walioko mlangoni kwa upofu, wadogo kwa wakubwa, hata wakachoka kwa kuutafuta mlango."

Changamoto ya wateule wengi hawajui jinsi ya kuwatumia Malaika au jinsi ya kushirikiana na Malaika ili ushindi dhidi ya mawakala wa shetani upatikane.
Labda ngoja nikupe points chache za kukusaidia.
A. Usimuombe Malaika bali muombe MUNGU ndipo Malaika watakuja kukusaidia.
Ukiomba Malaika hawaji na utakuwa unaabudu miungu na sio MUNGU.


B. Malaika wanasikiliza maelekezo ya MUNGU na sio ya kwako, hivyo husika na MUNGU kwenye maombi ukipendekeza Malaika zake wakuokoe au wakutendee kile unachotamani.


C. Malaika wa MUNGU ni watakatifu hivyo ukitaka ushirikiane na Malaika wa MUNGU katika kuleta ushindi kwako basi hakikisha unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.


2. Malaika huwahudumia wateule wa KRISTO.

Waebrania 1:14 "Je! Hao wote(Malaika) si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?"

Katika Malaika kukuhudumia wewe mteule sio lazima uone sura ya Malaika.
Mfano siku moja nikiwa mwanafunzi wa sekondari Biharamulo nilikuwa sina pesa kabisa na nilitakiwa kulipa shuleni na wasiolipa pesa hiyo wangeadhibiwa hadharani na kudhalilishwa. Niliomba sana kisha yakabaki masaa machache tu ili wote tukutanike, na wasio na pesa hiyo waadhibiwe.
Nikiwa Bwenini baada ya kuomba nilijikuta najisemea kwamba ngoja nikatembee barabarani na yule wa kwanza kukutana njiani naye ningemuomba pesa ili tu nikatoa shuleni nisiabike maana yalikuwa yamebaki masaa machache shule nzima kuingia kwenye bwalo na ningeabika.
Nilitoka na kuanza kutembea barabarani. Kwa mbele nikaona mzee mmoja wa kama miaka 80 au 90 anatembea huku amepinda kidogo mgongo maana alikuwa ni mzee mkongwe sana. Nikajisemea moyoni kwamba yule sitaweza kumuomba pesa maana alikuwa mchafu, hana viatu na nguo zake zina viraka, huku ni mzee sana. Roho yangu iliuma maana nilikuwa nimejiapiza kwamba mtu wa kwanza kukutana naye ningemuomba hiyo pesa. Kwa hasira nilimpita Yule mzee bila kumsalimia maana niliona mzee huyo kanipotezea malengo yangu ya kupata pesa lakini nilipompita kama hatua kumi akaniita na anakinambia ''Njoo uchukue pesa'' nilishangaa sana kwamba anataka kunipa pesa, kisha akanipa kiwango kile kile nilichohitaji na akaendelea na safari yake. Nilibaki nashangaa pesa na kisha nilipogeuka kumwangalia sikumuona tena.
MUNGU anaweza kumtuma Malaika wake kwa njia kama hiyo na ukatoka kwenye tatizo lililokuwa linakukabili.

Malaika walimhudumia Bwana YESU alipokuwa katika mwili kama sisi tulivyo katika mwili, wakati wa kujaribiwa jangwani na shetani.
  Marko 1:13 ''
Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia. ''
Hata wewe kuhudumiwa na Malaika ni jambo linalowezekana.
Kwenye maombi yako Leo omba MUNGU kwamba Malaika zake wakuhudumie.

3. Malaika huitangulia safari yako yenye baraka za MUNGU na kuifanikisha.
Mwanzo 24:7  '' BWANA, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke tokea huko; ''
Katika maandiko haya tunaona maombi ya Ibrahimu kwamba MUNGU atamtuma Malaika ili kufanikisha Isaka mtoto wake kupata mke mwema.
Na ni kweli Kazi ya Malaika wa MUNGU ilionekana, ukisoma Hiyo Mwanzo 24 yote utaona kazi ya ajabu sana iliyofanywa na Malaika wa MUNGU hadi Rebeka akawa mke mwema wa Isaka. Mstari wa 12-16 wa hiyo Mwanzo 24 Biblia inasema '' Naye akasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu. Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu.
 Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake. Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda.'
Yaani wakati Eliazari anawaza moyoni mambo ambayo yalitakiwa kumthibitisha mke wa Isaka, Biblia inasema Kabla hajamaliza kunena moyoni mwake tayari Rebeka amefika hapo na anatimiza yote yaliyo katika moyo wa Eliazari. Aliyemleta hapo ni Malaika wa MUNGU kama maombi ya Ibarahimu yalivyokuwa. Kumbuka hiyo ilikuwa ni nchi ya mbali lakini Malaika wa MUNGU pia alimwelekeza Eliazari na watu aliokuwa nao kwenda kwenye hicho kisima ili kumpata Rebeka, yaani huo ni muujiza wa MUNGU tu na ilikuwa kazi ya Malaika wa MUNGU baada ya maombi ya Ibrahimu.
Yaani Mfano ni mimi Peter Mabula niko hapa Tanzania kisha niende kumtafuta anayetakiwa kuwa mke wa rafiki yangu, nikamtafute huyo Mwanamke Zimbabwe au Somalia na sijawahi kufika huko na huko sijui hata mji mmoja na sifahamiani na mtu hata mmoja, na cha ajabu yale niliyojisemea moyoni yanaenda kutimia bila kupungua neno, huo ni muujiza wa MUNGU tu, na kwa Isaka na Rebeka iliwezekana maana MUNGU alimtuma Malaika kufanikisha mpango huo mtakatifu.
Inawezekana kabisa unahaha mwenzi wako wa ndoa atatoka wapi, inawezekana Binti unaangalia vijana wa Kanisani kwako na huoni mwenye mpango wa kukuoa, inawezekana kijana unaangalia mabinti wa Kanisani kwenu na huna amani na hata mmoja hata utake kufunga naye ndoa. Unajiuliza mke/ mume wako atatoka wapi?
Ndugu, kama wewe ni muombaji na unajua jinsi ya kumuomba MUNGU ili Malaika zake wakufanikishe hakika Malaika wanaweza kufanya muujiza ambao hata hukuwahi kuwaza. 
Wapo watu leo ni mtu wa Mwanza lakini ameoana na mtu wa Tanga au Mtwara na hakuna ambaye angejua kama atafunga ndoa takatifu na mtu wa mbali hiyo, ndugu husika na maombi ukimuomba MUNGU kwamba Malaika zake wafanye kazi yao kwako kama Neno la MUNGU linavyoonyesha kwamba Malaika wanaweza kufanya kazi kwako uliye Mteule mwaminifu wa KRISTO YESU.
Malaika anaweza kukufanikisha upate kazi ambayo hata hukudhani kama ungeipata maana uliokuwa unashindana nao kupata kazi hiyo ni watu wa hadhi kuliko wewe, Malaika wa MUNGU anaweza akakutangulia Mahakamani na ukashangaa unashinda kesi uliyoonewa hata kama kila mtu alijua ungefungwa, Malaika wa MUNGU wanaweza wakakutangulia katika safari yako na kuifanikisha, Malaika wa MUNGU wanaweza wakakutangulia kwenye huduma yako ya injili, Malaika wa MUNGU wanaweza wakakutangulia kwenye kikao ambako ulijua unaenda kufukuzwa kazi, Malaika wanaweza kukutangulia katika Biashara yako na kung'oa tungurui walizokutegea maadui zako.
Malaika wa MUNGU wanaweza kukutangulia katika mitihani na kufuta kila uchawi uliowekwa ili ufeli, Malaika wa MUNGU wana kazi nyingi kwako Mteule wa KRISTO, hakikisha tu unajua kuwatumia Malaika kupitia maombi yako kwa MUNGU. Nimesema  usiwaombe Malaika bali muombe MUNGU, Usiwasujudie wala usiwe na kisanamu chochote cha Malaika au cha Mariamu au cha mtu yeyote kiibada. Ukifanya hivyo ndipo utatoa nafasi kwa Malaika wa MUNGU kukutangulia na kuifanikisha kazi njema inayokuhusu.

4. Malaika wa MUNGU ni walinzi kwetu wateule wa KRISTO.
Kutoka 23:20 '' Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.''
Baada ya maombi yako uliyoomba kwa MUNGU ili Malaika zake wakulinde, hakika Malaika wa MUNGU watakulinda.
Hata kama uko eneo ambalo limetawaliwa na nguvu za giza za kiwango cha juu sana, Malaika wa MUNGU akikulinda utakaa salama. Na wala Malaika wa MUNGU hawako mbali na wewe Mteule wa MUNGU, tatizo tu hujui jinsi ya kuwatumia Malaika wa MUNGU ili kukulinda.
Wewe Muombe MUNGU kwamba Malaika zake wakulinde na muda huo huo Malaika wa MUNGU watakuja kwako na kukulinda maana hakuna umbali kwenye ulimwengu wa roho.
Hakikisha tu unahusika na MUNGU anayeweza kuwatuma Malaika na sio wewe kuhusika na Malaika tu, ukifanya hivyo Malaika wa MUNGU hawafanyi kazi kwako. Ndugu, nakuomba sana husika na MUNGU, Mche MUNGU kupitia YESU KRISTO, Mtii ROHO MTAKATIFU na tembea kwenye Neno la MUNGU ndipo utakuwa umetoa nafasi nyingi za Malaika wa MUNGU kufanya mambo mengi mema yenye kusudi la MUNGU kwako.

Biblia iko wazi sana kwamba MUNGU hutuma Malaika zake kutulinda sisi wateule wake katika KRISTO YESU.
Zaburi 91:10-12 '' Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.''

5. Kukueleza Maelekezo ya MUNGU.
Waamuzi  2:4 '' Ikawa, hapo huyo malaika wa BWANA alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia.''
Biblia inaonyesha kwamba Malaika wa MUNGU aliyasema yale maelekezo ya MUNGU, Hata kwako unaweza kuomba kwa MUNGU kwa muda mrefu na ukashangaa Malaika anakuja na kukueleza yakupasayo.
Sio lazima umuone Malaika kwa sura ila unaweza kusikia sauti au unaweza kumuona kwa maono au kwa ndoto na ROHO MTAKATIFU akakupa amani kuufanyia kazi ujumbe huo wa Malaika maana ni maelekezo kutoka kwa MUNGU.
Katika Waamuzi 13 kuna Maelekezo ya Malaika wa MUNGU kwa familia ya Manoa maana japokuwa mke wa Manoa alikuwa Tasa lakini Malaika wa MUNGU alileta ushindi akisema kwamba Mwanamke huyo atapata uzao mtoto wa kiume, na Malaika aliendelea kutoa Maelekezo,  Waamuzi 13:13 Biblia inasema hivi ''Malaika wa MUNGU akamwambia Manoa, Katika hayo yote niliyomwambia huyo mwanamke na ajihadhari.''
Hiyo inaonyesha ya kwamba Malaika wa MUNGU anaweza kukupa maelekezo ya nini cha kutenda ili ufanikiwe katika mambo mema unayoyaendea.
Katika 1 Wafalme 19 tunamuona Malaika wa MUNGU akimwendea Eliya Nabii  na kumpa Maelekezo.
1 Wafalme 19:7 '' Malaika wa BWANA akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako.''
Hata wewe unaweza ukapewa Maelekezo ya MUNGU mengi tu lakini wengi huwa wanapuuzia, wengine huwa wanadharau na wengine huwa wanashupaza shingo hivyo wanakaribisha uharibifu.
Malaika wa MUNGU anaweza pia akavaa sura ya Mtumishi wa MUNGU na wewe ukadhani ni Mtumishi tu wa MUNGU anakupa maelekezo au anakufundisha Neno la MUNGU, anakuonya au anakuelekeza na kumbe ni Malaika wa MUNGU.
Hata watumishi wa MUNGU wakati mwingine wanaweza kuelekezwa na Malaika wa MUNGU ili tu kuwasaidia kiroho baadhi ya watu.
Kwangu imeshatokea mara kadhaa, Huwa ninakuwa na watu wengi sana wa kuwaombewa kwa simu baadhi ya siku ninapokuwa na nafasi.
Siku moja nilikuwa na ahadi za kuombea watu zaidi ya 30 kwa siku moja  na muda wa kuwahudumia watu hao wote ulikuwa ni saa moja na nusu tu maana nilikuwa busy sana, wote niliwapa muda mmoja kunipigia ili kuwaombea lakini muda ulipofika alipiga mtu mmoja niliyeongea naye saa nzima na kumuombea muda mrefu sana, mtu huyo alikuwa katika kufa na vita yake ilikuwa kubwa sana, kwa muda huo nilimfundisha, nikamuombea, nikamshauri na kumuelekeza na alifunguliwa siku hiyo  maana baadae alinipa ushuhuda wa ajabu sana. Ni mtu ambaye katika maelezo yake alijua hamalizi hata siku mbili akiwa hai lakini kwa sasa anamtumikia YESU KRISTO. Nini kilifanyika? Watu ambao wengine kimuujiza walizuiliwa kunipigia simu na siku hiyo nzima katika muda wa kuombea watu nilimuombea mtu mmoja tu. Watu wale wengine baada ya siku hiyo walianza kuniomba tu msamaha kwamba walikwama  kidogo ndio maana hawakupiga,  mimi nilijua hata wangepiga wasingenipata maana nilipata mzigo mzito wa kuombea mtu huyo aliyekuwa katika hatari mbaya. Huo ni muujiza wa MUNGU kwamba watu 30 wote wasipige simu wakati wengine kutoka kundi hilo waliandika meseji zaidi ya mbili kwamba huo muda watapiga, wengine walikuwa wamesema ''Nimetunza dakika ili tu kuongea na wewe Mtumishi Mabula uniombee'', sasa muujiza wa MUNGU uliwafanya waombewe siku nyingine.
Siku moja pia nilikuwa na ahadi za kuongea na watu wengi tu ili kuwaombea na kuwashauri, Mtu wa kwanza alipopiga simu alikuwa na msichana wake wa kazi na msichana huyo alikuwa ameolewa na jini, nilipoanza kumuombea alidondoka chini na na akaanza kupiga kelele huku akiwa na nguvu kuliko waliokuwepo pale, ilibidi majirani wajae pale maana ilikuwa ni hatari na majirani wote waliofika pale hakukuwa na Mkristo hata mmoja, na simu ilibidi iwekwe sauti kubwa na yule mwenye mapepo ilibidi nimuombee kwa njia hiyo. Majirani walijaa na niliomba muda mrefu huku simu ikisogezwa sikioni kisha akafunguliwa na nikaanza kuwafundisha Neno la MUNGU, karibia saa nzima iliisha na ajabu wale watu wengine waliotakiwa pia kupiga simu hawakupiga siku hiyo na kesho yake kila mmoja alisema alikwama kupiga simu, nilimshangaa MUNGU sana.
Ndugu zangu, Malaika wa MUNGU wana kazi kubwa sana na sisi wateule, na hutuelekeza katika mengi hata kama hatujui kama ni Malaika wa MUNGU wanaifanya kazi hiyo.

6. Kuwaua maadui za wateule.
2 Nyakati 32:21 '' Naye BWANA akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga.''
Pale ambapo kuna mawakala wa shetani wanalizuia kusudi la MUNGU, pale ambapo mawakala wa kuzimu ameshaonywa mara nyingi wakishupaza shingo, pale ambapo wachawi au waganga sasa wanashindana na kusudi la MUNGU kwako au kwa Kanisa au kwa kazi ya MUNGU inaweza kufika kipindi ambacho MUNGU anaweza akamtuma Malaika kwa ajili ya kuwaua kabisa hao mawakala wa shetani.
Malaika wa MUNGU anaweza kuja na kuwaangamiza kabisa mawakala wa kuzimu wanaokutesa wewe mteule wa KRISTO unayempendeza MUNGU.
Mimi nina shuhuda nyingi na siwezi kusema hapa shuhuda hizo zote.
Kuna Mchungaji mmoja ni rafiki yangu, yeye alikuwa anashindana na wachawi ana kwa ana ambao walitaka lisiwepo Kanisa la kiroho katika eneo hilo, Mchungaji huyo ilifika kipindi akaomba maombi magumu. Aliomba kwamba anatoa siku tatu kwa wachawi wale ama kuokoka, ama kuhama hilo eneo au ama kufa. Aliwaambia wale wachawi walidharau na kumcheka lakini baada ya siku 3 walikufa wote wawili kwa siku moja bila hata kuumwa wala kulazwa hospitalini.
Biblia inaposema usimwache Mchawi kuishi usidhani ilikosea kuandika, wako watu waaminifu kwa MUNGU wanaoweza kutembea katika maandiko kimaombi na hiyo ikapelekea wachawi hao kufa.
 Jambo muhimu tu kuzingatia ni kwamba usipigane vita kimwili bali pigana kiroho kwa njia moja tu yaani maombi, Ukitaka upigane kwa nguvumi au kwa silaha za kimwili utakufa wewe na sio huyo mchawi, pigana vita kiroho maana wewe ni mtu wa rohoni.
Wako watumishi walikuwa na vita na mawakala wa shetani na ilifika kipindi Malaika wa MUNGU akaja ili kuwaua watu hao maadui na watumishi hao wakaombwa na Malaika watoe uamuzi, waliposema wafe hakika walikufa, na waliposema tuwaache kwanza walibaki.
Inaweza ikafikia kipindi ukashangaa unapata ufunuo wa kuomba wakuu wa giza waliokutesa kwa muda mrefu wafe na wakafa kweli.
Malaika wa MUNGU wana kazi nyingi sana kwa Kanisa la MUNGU na kwa wateule wa KRISTO.

Malaika wa MUNGU baada ya maombi yako wanaweza kuleta mabaya sana kwa adui zako hata ukaanza kuwahurumia.
Zaburi 35:4-6  '' Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha chini. Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia.''

7. Kuleta mabaya kwa maadui za watu wa MUNGU.
Zaburi  78:49 '' Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya.''
Kuna kundi la Malaika lipelekao uovu kwa nguvu za giza,  hapo mteule lazima ushinde vita ya kiroho.
Inawezekana mawakala wa shetani wanakuletea mabaya kila mara, wamekufunga na unateseka sana. Ndugu kimaombi unaweza kumuomba MUNGU ili malaika zake wapeleke mabaya kwa wakuu hao wa giza na utashangaa watapatwa na mabaya mengi mno.
Hizo points 7 unaweza kuzitumia kimaombi ukimwambia MUNGU kwamba Malaika zake wafanya hakika utashinda vita yako ya kiroho.
Muhimu tu hakikisha kwanza unaishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU, hakikisha umeokoka, hakikisha unaongozwa na ROHO MTAKATIFU na hakikisha unajifunza sana Neno la MUNGU ili ujue kulitumia Neno la MUNGU kihalali, uwe mwaminifu katika utoaji n.k


Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

+255714252292(Hadi whatsapp).

+255786719090

mabula1986@gmail.com

Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments