![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu Tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Mtu Kuwaheshimu wazazi waliomzaa ni jambo la muhimu sana na la lazima sana.
Waefeso 6:2-3 " Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia."
➡️Kumbe Mtu kuishi miaka mingi Duniani inatokana na sababu nyingi, Moja ya sababu zinazoweza kumfanya Mtu aishi miaka mingi Duniani ni pamoja na Kuwaheshimu wazazi wake.
Wewe Mteule wa KRISTO YESU lijue na hili na lifuate.
◼️ Ndugu mheshimu Baba Yako aliyekuzaa.
◼️ Ndugu mheshimu Mama Yako aliyekuzaa.
Ukisoma Biblia unaona Biblia ikisema kwamba Watoto wanaotoka katika viuno vya Baba zao Mfano (Mwanzo 15:4) na wanaotoka katika matumbo ya Mama zao Mfano (Isaya 49:1)
◼️Waheshimu sana Wazazi wako waliokuzaa, usije ukakengeuka ukaacha Kuwaheshimu.
Mithali 23:22 "Msikilize baba yako aliyekuzaa, Wala usimdharau mama yako akiwa mzee."
➡️Biblia Kwa ukali inasema Mtu yeyote anayeweza kumtukana Mzazi wake kufa na afe.
Walawi 20:9 "Kwa maana kila mtu amlaaniye baba yake au mama yake hakika atauawa, amemlaani baba yake na mama yake; damu yake itakuwa juu yake."
➡️Kumbe Mtu anaweza kufuatiliwa na roho ya mauti kwa sababu haheshimu wazazi wake.
➡️Mtu anayemdharau Baba yake au Mama yake huyo ni mjinga.
Mimi binafsi tangu nikiwa na umri wa miaka 3 na nusu Sikuwahi kuishi na Baba yangu Mzazi wala Mama yangu Mzazi lakini Mama ni Mama tu na Baba ni Baba tu na anatakiwa kupewa heshima yake kama Mzazi.
Nikiwa na huo umuri wa miaka 3 Baba yangu alifariki na Mama akaondoka ambapo Mama nilikuja kumuona masaa machache tu miaka 10 baadae na baada ya hapo naye akafariki.
Lakini Baada ya Baba kufariki Kuna Ndugu Muhimu sana kwangu ambao walichukua nafasi ya Baba na Mama kunilea na hata Leo Niko hivi nilivyo kwa Neema ya MUNGU wa Mbinguni na Kwa malezi ya ndugu Muhimu ambao MUNGU aliwapa jukumu la kunilea, hao nao ni wa kuheshimiwa kama Wazazi.
1 Timotheo 5:17 "Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha."
◼️Kijana nakusihi sana mweshimu Baba Yako na Mama yako.
◼️Binti nakusihi sana mweshimu Baba Yako na Mama yako.
➡️Bila Baba Yako na Mama yako kuzaliwa hakika na wewe usingezaliwa.
Nasikia uchungu juu ya hili ila nawasihini sana ndugu zangu wote mheshimu Wazazi wenu.
Narudia tena ndugu yangu mweshimu Mama yako na Baba Yako.
➡️Binti usitake Baba Yako au Mama yako atoe machozi wakati huu wa uzee wake kwa ajili tu ya kiburi chako na dharau zako kwake, kumbuka kuna machozi mengine huwa hayafutiki kirahisi Bali hutengeneza laana.
Kama huna hatia kwa hakika mbele za MUNGU basi machozi hayo hata yakimwagika hayatakugusa. Lakini kama unamtukana Mama yako au Baba Yako kwa sababu tu wewe sasa uko mjini na una kazi nzuri wakati Mzazi wako yuko kijijini.
◼️Mzazi wako ni Mzazi wako tu na kwa huyo tu ndio maana wewe ulitokea duniani.
MUNGU alimwamwini Mzazi wako na akakuweka ndani yake, hivyo mweshimu Mzazi wako na muombee sana.
➡️Kumbuka Biblia inasema anayemlaani Mzazi wake hata akifa ni juu yake.
Kutoka 21:17 Yeye amwapizaye baba yake au mama yake, sharti atauawa.
◼️Kumbuka agizo la Kuwaheshimu wazazi wako halikutolewa na Wanadamu Bali MUNGU Mwenyewe.
Kumbu 5:16 "Waheshimu baba yako na mama yako; kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako."
➡️Ni eneo Moja tu ambalo hata ukitofautiana na Mzazi wako hutakuwa na hatia mbele za MUNGU.
◼️Eneo hilo ni Mzazi asiye na YESU KRISTO akitaka kutumia nafasi yake kama Mzazi kukuondoa kwa YESU, katika hilo hata ukimkatalia Mzazi wako hutakuwa na hatia kwa MUNGU na Wala miaka Yako haitapunguzwa.
Luka 12:51-53 " Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu."
➡️Eneo hilo linahusisha pia Mzazi kukufundisha tabia mbaya Mfano uchawi, kuabudu miungu au kuabudu sanamu au kukufundisha uongo ili umwache YESU hapo ukimkatalia Mzazi wako hata angetamka laana ya namna gani kama una YESU KRISTO ujue laani hiyo haitakupata ila yeye ndio atakuwa na tatizo mbele za MUNGU maana amekuhubiri Injili nyingine akitaka kukutoa kwa YESU.
Wagalatia 1:8 "Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe."
◼️Ila kwa ujumla tu Mzazi anahitaji kuheshimiwa na Watoto wake na ni jambo la baraka kwa Watoto husika.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments