![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la Maombi.
◾Kuna watu wanasumbuliwa sana na wachawi.
◼️Kuwashinda hao mawakala wa shetani ni wewe kuhusika na YESU Mwokozi na ni wewe kuomba Maombi katika jina la YESU KRISTO huku ukifuata maelekezo yake.
Yohana 14:13-15 " Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. Mkinipenda, mtazishika amri zangu.
◼️Ziko aina nyingi za Maombi na ROHO MTAKATIFU hutoa ufunuo wa kimaombi ili ujifunze na uombe.
➡️Mfano huu ambapo Yahazieli alijiliwa na ROHO MTAKATIFU juu ya namna ambavyo wangeshinda vita na kweli wakashinda.
2 Nyakati 20:14-15 " Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na ROHO YA BWANA, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya MUNGU."
➡️Watu wengi hawajui kwamba Neno la MUNGU ndio unabii wa moja kwa moja kwao.
Watu hawa hungoja kutabiriwa na watumishi, wakati hata wao wenyewe binafsi kwa kulisoma Neno la MUNGU wataona unabii kabisa unaowahusu, wakiamini na kuomba watafanikiwa sana sana na Neno la MUNGU lililo unabii kwao.
◼️Daudi wakati wa Vita yake na Goliath alijitabiria kwa Jina la MUNGU ambalo hilo Jina la MUNGU amejifunza kwenye Neno la MUNGU namna ambavyo amgeshinda.
1 Samweli 17:45-47 " Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, MUNGU wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko MUNGU katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi mikononi mwetu."
Ndio maana Daudi kwa kuijua Nguvu ya Neno la MUNGU anasema hivi katika Zaburi 33:4 kwamba "Kwa kuwa neno la BWANA lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu."
◼️Neno la MUNGU hufanya kazi yake kwa uaminifu, Wewe umelitumia Neno gani la MUNGU ili lifanye kazi yake kwa uaminifu ili Wewe ushinde vita ya kiroho?
Ndugu Hakikisha una Neno la MUNGU katika Maombi Yako.
➡️Tena Daudi huyu huyu anayejua thamani ya Neno la MUNGU anasema katika Zaburi 56:4 kwamba "Kwa msaada wa MUNGU nitalisifu neno lake. Nimemtumaini MUNGU, sitaogopa; Mwenye mwili atanitenda nini?"
◼️Daudi analisifu Neno la MUNGU Kwa sababu ameshinda mara nyingi vita kupitia Neno la MUNGU.
➡️Mfano unateswa na wachawi katika biashara yako kisha ukakutana na Neno la MUNGU wakati ukisoma Biblia mfano Isaya 54:17 inayosema "Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA."
◼️Kumbe silaha za Mashetani huwa zinaharibiwa kupitia Maombi uliyoyapata kupitia Maarifa ya Neno la MUNGU ulilojifunza.
Ndugu, uwe na muda Sasa wa kuomba kwa Imani kwa Neno la MUNGU.
◼️Kwa sababu wewe ni mteule wa KRISTO unayeishi maisha matakatifu unaweza tu ukajitamkia/Kujitabiria kwamba "Kwa jina la YESU KRISTO sasa naagiza kwamba wachawi hawatairoga biashara Yangu"
Unajua inakuwaje?
◼️Kama umetamka kwa imani huku ni kweli jina la YESU KRISTO liko kwako hakika jina la YESU litakutangulia kwenye Biashara yako ili kuzuia wachawi Kuiroga hiyo.
➡️Kwa sababu jina la YESU lina nguvu na mamlaka juu ya kila kazi za giza. Huoni sasa hapo unakuwa umejitabiria ushindi na ushindi huo unatimia?
Wewe unataka hadi Watumishi wakutabirie ndio utaamini kuwa umeshinda?
Ongeza imani ndugu maana katika KRISTO Kila ambaye hupewa alichoomba katika mapenzi ya MUNGU.
Mathayo 7:8" kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."
◼️Ukitaka ushinde Mfanye MUNGU kuwa MUNGU wako binafsi, na sio MUNGU wa Mchungaji wako.
Zaburi 5:2-3 " Uisikie sauti ya kilio changu, Ee Mfalme wangu na MUNGU wangu, Kwa maana Wewe ndiwe nikuombaye. BWANA, asubuhi utaisikia sauti yangu, Asubuhi nitakupangia dua yangu na kutazamia."
◼️Mfanye YESU KRISTO kuwa Mwokozi wako binafsi katika kila kitu.
Matendo 3:6-8 " Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la YESU KRISTO wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu MUNGU.
◼️Mfano ROHO MTAKATIFU kuwa kiongozi wako namba moja kwenye maisha yako maana Ukiwa na yeye unashinda na zaidi ya kushinda.
Matendo 6:10 "lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye."
◼️Ndugu jitabirie mwenyewe, sio kusubiria kutabiriwa.
➡️Usiwe wewe Biblia unaifungua Kanisani jumapili tu huku huna muda kuisoma Biblia mwenyewe na kuitafakari.
➡️Ukiwa Mtu wa kusomewa tu Biblia hakika utakuwa Mtu wa kutabiriwa tu huku hata unabii huo wanaokutabiria hautimii.
◼️Mfano unahitaji ulinzi wa MUNGU, jiombee mwenyewe ulinzi wa MUNGU huku ukijua kanuni zinazotumika ili MUNGU akulinde, alinde ndoa yako au familia yako.
Mfano umesoma Biblia na kukutana na Isaya 26:3 ambapo Biblia inasema " Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini."
➡️Katika andiko hilo nje na Maombi ya ulinzi unatakiwa ujue kanuni za MUNGU ili akulinde.
◾Kanuni za MUNGU ili akulinde ukimuomba ulinzi kulingana na Isaya 26:3 ni;
1. Kumtegemea MUNGU.
➡️Usipotegemea ulinzi wa MUNGU hakika MUNGU hatakulinda.
➡️Usipomtegemea MUNGU kwa sababu unaamini sana mafuta chumvi za upako ujue hatakulinda.
2.Kumtumaini MUNGU.
➡️Kumbe ili MUNGU akulinde ni lazima wewe mwenyewe umtegemee MUNGU na umtumaini MUNGU.
➡️Usipomtumaini MUNGU ujue umekosana na ulinzi katika maeneo yako unayohitaji ulinzi wa MUNGU.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments