MAOMBI YA KUFUTA NGUVU YA MADAWA ZA KICHAWI NA KIGANGA .

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU


Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi.
Biblia iko wazi kwamba Bwana YESU alikuja ili kuzivunja na kuzitowesha nguvu za giza zilizokuwa zinawatesa watu.
1 Yohana 3:8b ''Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. ''

Watu wengi sana waliwahi kwenda kwa waganga wa kienyeji na kunyweshwa madawa kisha baadae wanaanza kuteswa  na nguvu za giza kama majini n.k
Wako watu matatizo yao makubwa sana yalianzia siku wameota ndoto wananyweshwa madawa ya kichawi.
Wako watu waligusa madawa yaliyotegwa kichawi na ndio ikawa chanzo cha nguvu za giza kuwatesa.
Wako watu walitegewa madawa ya kichawi ili wadhulike.
Biblia inaonyeshwa kwamba wapo wachawi na waganga wa kienyeji ambao ni sehemu ya vyanzo vikuu vya vifungo vya kiroho kwa watu wengi.
Wako mawakala wa shetani wengi tu ambao kazi yao ni kuziwinda roho za baadhi ya watu na ili kuwatesa kwa kupitia madawa ya kichawi, hirizi n.k
 Ezekieli 13:18 ''useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe? ''

Wako watu wanateseka sana kwa sababu ya uchawi na uganga wa kienyeji.
Ngoja nikupe shuhuda hai zilizotokea nikiwa katika Kazi ya MUNGU ya Injili ya KRISTO.
Mama mmoja alikuja Kanisani ili tumuombee, alikuwa kipofu. Baada ya ibada nikamuuliza macho yake yalipofuka tangu akiwa mtoto akasema ''hapana, bali nilienda kwa mganga na huko nikanyweshwa damu ya mbuzi usiku wa manane, huku mganga akisema hiyo ndiyo dawa ya tatizo langu, baada ya kunywa damu ile nikashangaa naona giza na tangu siku hiyo mimi nikawa kipofu nisiyeona macho yote mawili, nikiwa pale kwa mganga yeye alidai kwamba tumekosea masharti hivyo akatuambia tuondoke pale, mimi na mdogo wangu tuliyeenda naye tukaondoka huku mdogo wangu akiniongoza njia maana macho yangu tangu siku hiyo hayakuona tena hadi leo''

Dada mmoja alikuwa akiumwa tumbo hadi anazimia  na maumivu hayo ya tumbo yalimtesa kwa muda mrefu. Siku moja akaniita baada ya ibada na kunieleza siri yake akisema kwamba Siku moja baba yake mzazi alimleta mganga nyumbani kwao na akawachanja chale kisha akampa kitu kidogo kama jino akimwambia akimeze, alikataa lakini baadae alishikwa kwa nguvu na kitu kile kiliposogezwa tu mdomoni kilienda chenyewe tumboni huku akikisikia na kikiwa cha baridi kama barafu. Tangu siku hiyo akilala tu usiku majini huwa yanakuja na kunyoosha mkono kuelekea tumboni mwa dada huyu na kile kidude kinatoka kupitia kitovuni na kinaenda kwenye mikono ya jini na jini anafanya ishara fulani kisha anakielekeza tena  tumboni mwa dada huyo na kinaingia hadi tumboni, maumivu anayoyapata ya tumbo ni kutokana na nguvu hizo za giza na dawa hiyo aliyoshweshwa. Namshukuru MUNGU tulimuombea akafunguliwa.

Mama mmoja yuko nje ya Tanzania siku moja aliniambia jambo la ajabu sana, alisema kwamba katika familia yao walizaliwa watoto 12, baada ya miaka mingi wakiwa watu wazima wazazi wao walijihusisha na waganga wa kienyeji lakini jambo hilo lilipelekea kila mwaka wale watoto wa tumbo moja 12 walianza kufa mmoja mmoja kila mwaka, Wazazi wao wote wawili walishafariki lakini nguvu zile za giza ziliendelea kuwatesa, yaani kwa miaka 8 mfululizo kila mwaka walizika mmoja,  wakabaki wanne. Mwaka 2015 ndipo yule dada alinipigia simu akisema nimuombee, namshukuru MUNGU maana nguvu zile za giza zilikoma kuwaua.

Mwaka juzi kuna kaka mmoja aliletwa kanisani ili tumuombee, alikuwa amevimba sana mguu na hadi hospitalini walimwambia arudi tu nyumbani maana vipimo havionyeshi ugonjwa. Alikuwa amevimba mguu mmoja isivyo kawaida, Mchungaji wangu  akamuuliza chanzo ni nini? Akasema siku moja yeye na rafiki zake walienda beach lakini walipokuwa wanatembea maeneo ya beach yeye alikanyaga kitu fulani kilichokuwa kimetegeshwa na mguu ukavimba dakika ile ile.

Ndugu zangu, wapo watu wanateswa sana na nguvu za madawa za kichawi walizojihusisha nazo.
Leo mwite Bwana YESU kwa maombi yako ili akuokoe.
Zaburi 55:16 '' Nami nitamwita Mungu, Na Bwana ataniokoa;''

Kuna watu madawa ya kichawi waliyohusika nayo ndiyo yaliwafanya wawe mawindo ya majini, kumbuka mapepo hayawezi kuingia kwa mtu kama hayakufunguliwa mlango na mtu huyo au na wazazi wa mtu huyo au watu wa karibu wa mtu huyo. kwenda kwa waganga ni sehemu mojawapo inayoweza kukufungulia mlango mpana sana wa kuteswa na nguvu za giza katika maisha yako.
Pigana kimaombi na makuhani wa giza, moja ya makuhani wa giza ni waganga wa kienyeji na wachawi na katika kufanya kazi zao hutumia maadawa ya kipepo ili kutesa watu wa MUNGU.
Watu wengi sana wamefungwa na madawa ya kichawi.
MUNGU hataki wewe ndugu ukamatwe na kuteswa na madawa ya kichawi.
Ezekieli 13:20 '' Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege. ''

 Watu wengi sana wameteswa na madawa ya kichawi.
Pesa inaweza ikapakwa madawa ili mtu mwingine akiishika pesa ile  na kuichanganya na pesa zake anase kwenye vifungo vya giza kama kufilisika, madeni n.k
Mama mmoja wapangaji wake walikuwa wakimpa pesa ya vyumba walivyokuwa wamepanga kwake, alikuwa na zaidi ya wapangani 5,  alikuwa anazichukua pesa zile na kuzichanganya  na madawa aliyopewa na mganga  ili waendelee kukaa pale. Watu wale walikuja kupata ufunuo wa maombi ya kuvunja na kuharibu roho za kishetani za kuwazuia kujenga baada ya miaka 7. Yaani mtu amepanga nyumba ile ile kwa miaka saba na ana mshahara zaidi ya milioni, kumbe walikuwa wameshikwa kichawi ili waendelee kubaki pale bila kujenga wakati uwezo wa kujenga walikuwa wao.
Ndugu, kuna mbinu nyingi wanaweza kutumia wakuu wa giza kupitia madawa na kama sio muombaji wanaweza kukunasa.
Kiti chako ofisini kinaweza kupakwa madawa ili usifanikiwe.
Kuna ndoto zingine huwa unaota hata usiwe tu unadharau. Inawezekana kila mara unaota umekalia kiti chako ofisini kumbe unajulishwa umefungwa kipepo kupitia kiti hicho maana kilipakwa madawa.
Eneo lako la biashara linaweza kunyunyuziwa dawa ili usifanikiwe, mimi nina shuhuda nyingi sana za watu walionishirikisha maombi wakiwa wanateswa na nguvu za madawa ya kichawi, siwezi tu kuandika hapa shuhuda nyingi maana ziko nyingi.
Kuna wakuu wa giza wanaweza kutega dawa njiani au njiapanda ili tu watu fulani wakamatwe na vifungo vya giza.
Ezekieli 21:21 '' Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini.''

Mchungaji mmoja aliletewa zawadi ya suti kutoka ulaya lakini suti ile ilikuwa imepakwa madawa ya kichawi na kuambatanishwa na maroho wa kuzimu.
Maroho wale walimtesa kila akivaa ile suti na hakujua hadi siku moja mchungaji mwenzake alipopata ufunuo juu ya suti hiyo ndipo wakaichoma moto huku wakiomba na mateso yale na vifungo vile vikakoma.
Shetani anatafuta mlango wa kuvamia maisha yako, anaweza akatumia madawa wakati mwingine na ukanasa kwenye vifungo vya giza.
Usikubali katika maisha yako kwenda kwa mganga wa kienyeji yeyote.
Usikubali katika maisha yako yote unalishwa  ndotoni vitu vya ajabu au madawa au vyakula na kisha usiombe maombi ya kuharibu nguvu za giza wanayoyapitisha mawakala wa shetani kupitia vyakula n.k
Jina la YESU KRISTO na damu ya YESU KRISTO ya agano ipo siku zote ili kukushindia ila pasipo maombi unaweza ukabaki na kifungo chako.
Baba mmoja baada ya kushikana mikono na mwanamke mmoja anayetumika kipepo alijikuta anaanza uhusiano wa kingono na mwanamke huyo ambaye ni wakala wa shetani na hiyo ilipelekea baba huyo kuikimbia familia yake hadi mtoto wake mmoja mdogo alikufa kwa sababu kulikosekana pesa ya kumpeleka hospitali. Yaani aliisaliti ndoa yake na kuikimbia na familia yake ikaanza kuingia katika mateso makali sana wakati baba yule alikuwa na kazi nzuri sana, yaani hadi mtoto wake anafariki huku yeye hajali lolote.
Ndugu, leo kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO futa kila nguvu za giza zilizoletwa na madawa ya kichawi.
Inawezekana unateseka na magonjwa kwa sababu ya madawa ya kichawi uliyotegeshewa.

Kwa jinsi gani inaweza kuwa, hadi madhara ya dawa za kichawi yakakupata.

1. Kwa wewe kuishika dawa hiyo ikiwa kuna mtego wa kipepo dhidi yako.

2. Kwa wewe   Kuinywa dawa hiyo ikiwa kuna mtego wa kipepo dhidi yako.

3. Kwa wewe  Kuikanyaga dawa hiyo ikiwa kuna mtego wa kipepo dhidi yako.

4. Kwa wewe  Kuigusa dawa hiyo ikiwa kuna mtego wa kipepo dhidi yako.

5.  Kwa wewe  kuvaa nguo au kitu  kilicho na dawa hizo  ikiwa kuna mtego wa kipepo dhidi yako.

6. Kwa wewe  Kupuliziwa kipepo  dawa hiyo ikiwa kuna mtego wa kipepo dhidi yako.

7. Kwa wewe Kulishwa dawa hiyo ukiwa umelala  ikiwa kuna mtego wa kipepo dhidi yako.

8. Kwa wewe Kulishwa ndotoni  dawa hiyo ikiwa kuna mtego wa kipepo dhidi yako.

 9. Kwa wewe kwenda kwa waganga wa kienyeji ili wakutibu, huko ni kutafuta vifungo vya kipepo, huko ni kutafuta kifo, ona mfano wa kiongozi huyu mkuu wa nchi aliyeamua kwenda kwa waganga na kupelekea kifo chake.
2 Nyakati 16:12-13 '' Akashikwa Asa na ugonjwa wa miguu katika mwaka wa thelathini na kenda wa kumiliki kwake; ugonjwa wake ukazidi sana; lakini hakumtafuta BWANA katika ugonjwa wake, bali waganga. Asa akalala na babaze, akafa katika mwaka wa arobaini na mmoja wa kumiliki kwake.   ''

Leo futa nguvu zote za madawa ya kiganga ulizowahi kunyweshwa.
Tumewahi kuombea watu wengi wanaoteswa na nguvu za giza na wengine kufunguliwa kwao ni pale walipozitapika  hizo dawa walizowahi kunyweshwa.
Katika dunia ya leo inatupasa sana kuishi maisha matakatifu katika KRISTO, inatupasa sana kumsikiliza ROHO MTAKATIFU, inatupasa sana kuombea kila tunachonunua au kula, vingine vina madawa ya kipepo yaliyobeba vifungo.
Ndugu, takasa kwa damu ya YESU KRISTO nguo zako, vyakula vyako na vitu unavyonunua.
Kuna watu leo wanateswa na majini mahaba na chanzo ni siku ile walipokwenda kwa waganga wa kienyeji, ni hatari sana.

Kwanini tujitenge na nguvu za giza na madawa ya kipepo?

1. Ili tukimwomba MUNGU atatusaidia maana hata yeye hataki tuteswe na uganga, uchawi wala madawa ya kichawi.
Muombe MUNGU katika KRISTO YESU na mapigo yatawaelekea mawakala wa shetani.
Isaya 47:9 '' lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kitimilifu, uchawi wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno. ''

 2. Kwa sababu kuna madhara kwako kama ukinaswa na nguvu za giza.
Walawi 19:26,28 ''Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi.   .....  Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA. ''

3. Kuhusika na uganga au uchawi ni kijifunga nira ya kishetani.
Sisi hatutakiwi kufungiwa nira moja na wasiomwamini YESU KRISTO, wakiwemo wachawi wote na waganga wa kienyeji wote.
2 Kor 6:14 ''Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? ''

4. Ili vifungo vya giza vinavyotokana na uganga na uchawi vituachie.
Isaya 10:27 ''Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.''


Maombi ya leo kulingana na somo hili.

1. Tubu kwa kilichosababisha wewe kukamatwa na kuteswa na madawa ya kichawi.

2. Futa agano la giza lililotengenezwa na madawa hayo ya kipepo.

3. Haribu madhabahu ya giza inayoleta   madawa ya kichawi kwako.

4. Takasa vitu vyako vyote unavyohisi viliwekewa madawa ya kichawi.

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa na somo hili mwakani nitalifafanua zaidi ndani ya kitabu.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni
MAOMBI YA KUFUTA NGUVU YA MADAWA YA KICHAWI NA KIGANGA.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda.



 MAOMBI YA KUFUTA NGUVU YA MADAWA YA KICHAWI NA KIGANGA.

Eee MUNGU Baba wa mbinguni, ni wema wako tu ndio maana mimi ninaishi.
Ninakushukuru MUNGU wangu maana umenilinda , sifa, heshima na utukufu  ni kwako tu wewe MUNGU Muumbaji wangu.
Niko mahali hapa BWANA ninaomba unisamehe dhambi zangu zote, makosa yangu yote na uovu wangu wote.
Nisamehe MUNGU wangu kuhusu madawa ya kipepo yeyote ambayo nilihusika nayo hata yakafungulia milango ya shetani kuvamia maisha yangu na kunitesa.
Eee MUNGU wa Israeli ninaomba unisamehe BWANA na unitakase sasa kwa damu ya YESU KRISTO.
Eee Bwana YESU Mwokozi ninaomba damu yako ya agano jipya initakase mwili wangu dhidi ya kila madawa ya kichawi niliyohusika, nitakase BWANA iwe niligusa, nilikunywa, nilinusa, nilishika, nilikanyaga au nililishwa ndotoni, ninaomba MUNGU wangu unitakase, katika jina la YESU KRISTO ninaomba mbele zako MUNGU wangu.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO na kwa damu ya YESU KRISTO ninafuta kila agano la kipepo lililofanyika kupitia madawa ya kwa mganga ili kunikamata maisha yangu.
Ninafuta kila agano la kichawi kupitia madawa ya kichawi lililofanywa kuhusu ndoa yangu, ninalifuta agano hilo kwa damu ya YESU KRISTO.
Ninafuta kila agano la kichawi kupitia madawa ya kichawi lililofanywa kuhusu afya  yangu au uchumba wangu, ninalifuta agano hilo kwa damu ya YESU KRISTO
Ninafuta kila agano la kichawi kupitia madawa ya kichawi lililofanywa kuhusu uchumi wangu au kazi  yangu, ninalifuta agano hilo kwa damu ya YESU KRISTO
 Ninafuta kila agano la kichawi kupitia madawa ya kichawi lililofanywa kuhusu uzao wangu au biashara  yangu, ninalifuta agano hilo kwa damu ya YESU KRISTO.
 Ninafuta kila agano la kichawi kupitia madawa ya kichawi lililofanywa kuhusu nguo zangu, vyakula nilivyokula au baraka yangu  yangu yeyote, ninalifuta agano hilo kwa damu ya YESU KRISTO.
 Sasa naharibu madhabahu za giza zote zilizoleta   madawa ya kichawi kwangu, naharibu madhabahu hizo na kuzivunja, Kwa jina la YESU KRISTO sasa zimevunjika na kuharibika hata hazitafanya kazi tena.
Imeandikwa  katika Kumb 7:5 kwamba ''lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. ''
Hivyo kwa jina la YESU KRISTO ninavunja madhabahu za kipepo zote za waganga wa kienyeji na za wachawi, naziharibu madhabahu hizo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Imeandikwa tena katika Kumb 12:2-3 kwamba ''Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo.''
Sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninaharibu madhabahu za kiganga na kichawi zote zilizo juu ya milima mirefu kama Neno la MUNGU linavyosema, nazivunja na kuzitowesha hizo kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninaharibu madhabahu za kiganga na kichawi zote zilizo juu ya milima  na vilima  kama Neno la MUNGU linavyosema, nazivunja madhabahu hizo na kuzitowesha hizo kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
 kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninaharibu madhabahu za kiganga na kichawi zote zilizo chini ya kila mti  kama Neno la MUNGU linavyosema, nazivunja madhabahu hizo  na kuzitowesha hizo kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
 Kila madhabahu ya kiganga na kichawi inayoleta magonjwa au mikosi au balaa, naiharibu madhabahu hiyo kwa jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu ya kiganga na kichawi inayoleta kuvunjika ndoa, naiharibu madhabahu hiyo kwa jina la YESU KRISTO.
 Kila madhabahu ya kiganga na kichawi inayoleta kufa kwa uchumba, naiharibu madhabahu hiyo kwa jina la YESU KRISTO.
 Kila madhabahu ya kiganga na kichawi inayoleta umasikini na kufeli, naiharibu madhabahu hiyo kwa jina la YESU KRISTO.
 Kila madhabahu ya kiganga na kichawi inayoleta kukosa kazi na kufilisika, naiharibu madhabahu hiyo kwa jina la YESU KRISTO.
 Kila madhabahu ya kiganga na kichawi inayoleta kitu chochote kwangu, hiyo madhabahu huko iliko naibomoa na kuvunja kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
 Sasa kwa damu ya YESU KRISTO ninatakasa vitu vyangu vyote, navitakasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Ninatakasa tumbo langu na kichwa changu, Ninatakasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Ninatakasa miguu yangu na mikono yangu, natakasa kiganja changu na nyayo za miguu yangu, Ninatakasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Ninatakasa mwili wangu wote nje na ndani,Ninatakasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Ninatakasa vyakula vyangu na vitu vyangu nilivyonunua vya kutumia,Ninatakasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Ninatakasa ofisi yangu na sehemu yangu ya biashara,Ninatakasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Ninatakasa familia yangu, ninamtakasa mwenzi wangu wa ndoa,Ninatakasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Ninawatakasa watoto wangu, Ninawatakasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Ninatakasa fedha zangu zote, Ninazitakasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Ninatakasa kila kitu changu, Ninakitakasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Asante MUNGU Baba maana umenishindia leo.
Ninakushukuru sana MUNGU wangu maana umenipa ushindi leo.
Ninakushukuru Bwana YESU maana Damu yako ya agano na jina lako lenye mamlaka kupita vyote vimenishindia.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi.
 Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 4 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho.

Nasubiri ushuhuda kutoka kwako Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsap).


Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments