KUOTA UNAFUKUZWA, UNAPAMBANA AU UNAPIGANA NA VIUMBE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU




Bwana YESU KRISTO asifiwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

◼️Ndoto ni taarifa ya rohoni inayoonyesha mambo yanayoendeleo kwenye ulimwengu wa roho kuhusu wewe.

Unaweza ukaota pia ndoto ikionyesha chanzo cha tatizo lako hivyo unajua jinsi ya kulishughulikia.
Mfano ni huu
Mwanzo 20:3 "Lakini MUNGU akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu."
 
✓✓Huyu alijulishwa juu ya chanzo cha tatizo lake, na madhara ambayo angeyapata yanayotokana na tatizo hilo.

✓✓Hata wewe unaweza kujulishwa kitu ndotoni.

✓✓Ndoto pia inaweza kuonyesha mambo yajayo kuhusu wewe hivyo kama ni mambo mabaya umepewa nafasi na MUNGU ili uyaharibu sasa ili yasitokee baadae.

✓✓Ndoto inaweza kukujulisha aina ya kifungo chako na wapi ilikuwa na nini kilitokea.

✓✓Ndoto inaweza kukupa maelekezo ya ki MUNGU ili utoke katika kifungo chako.

Mwanzo 20:6 "MUNGU akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse."

Sasa ukiona kila Mara ndotoni unapambana na wachawi au majini, au maadui waliovaa sura za watu,
Au mara kwa Mara unaota unakimbizwa na nyoka au wanyama wengine wakitaka kukudhuru, au unaota ukiwa katika hali ya kuonewa, au unaota watu wakikupangia mbaya inawezekana kuwa inahusika na mambo haya chini au baadhi ya mambo haya chini.
Jifunze mambo haya ambayo Mimi Peter Mabula nakuletea Leo Wewe rafiki yangu, fanyia kazi kimaombi na kivitendo pale inapohitaji vitendo vya kiroho.

◼️Ndoto za kuota  unapambana ndotoni zinakujulisha mojawapo ya haya chini.

1.  Ndoto hiyo inakujulisha kwamba uko katika eneo lililotawaliwa sana na nguvu za giza.
 
Kuna mganga wa kienyeji karibu na hapo au kuna mchawi maeneo hayo.

✓✓Dawa ni kuliombea eneo hilo lote na kuharibu kila kazi ya kishetani katika eneo hilo kwa Maombi katika Jina la YESU KRISTO, katika Maombi yako usisahau kuhusisha damu ya YESU KRISTO ili kuufuta utawala huo wa nguvu za giza katika eneo hilo.

Biblia Iko wazi sana kwamba tunashinda kwa damu ya YESU KRISTO.

Ufunuo 12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ......"

Hivyo omba katika Jina la YESU KRISTO ukiachilia damu ya YESU KRISTO.

Maombi mengine katika kipengele hicho ni 
✓✓Achilia mapigo ya MUNGU juu ya kila wakala wa shetani katika eneo hilo.

Zaburi 2:9 "Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi."
 
2.  Ndoto hiyo inaweza kujulisha kwamba kuna mawakala wa shetani wanakuwinda.
 
Anaweza kuwa ni adui wa siri ila ni ajenti wa kuzimu, mtu uliyekosana naye akakuendea kwa mganga. Mtu mwenye wivu juu ya kazi yako au biashara yako, ndoa yako n.k
Pambana na mpambe huyo wa shetani na hakikisha hafanyi kazi zake za kichawi na kiganga.

Yeremia 51:20-21 " Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;"

✓✓Omba mbele za MUNGU kwa malaika wa mbinguni wamuwinde yeye huyo wakala wa giza na kumtowesha.

Zaburi 35:4-7 " Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha chini. Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia. Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu."

3. Eneo hilo halina nuru ya KRISTO.

Yohana 1:5 " Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza."

YESU ni nuru ya ulimwengu na Neno lake hutoa nuru.
Wateule wake ni nuru ya ulimwengu hivyo mahali walipo wateule wengi tena waombaji ujue kuna kazi za shetani huondoka eneo hilo.
Mfano mdogo ni maeneo ambako makanisa ya kiroho ni machache waganga na majini ni wengi, hata mikoa isiyo na makanisa mengi majini ni mengi.
Sasa unapoota ndotoni vita ya kiroho kila Mara dhidi yako tambua kwamba watu wengi zaidi wa eneo hilo hawajaokoka, hakuna makanisa yenye waombaji eneo hilo au makanisa ni machache na hayana waombaji.

✓✓Ombea neema ya Wokovu kwa watu wa eneo hilo, omba MUNGU ainue waombaji katika eneo hilo.

Ezekieli 22:30 "Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, ......."

✓✓Ita kazi ya MUNGU eneo hilo kama mikutano ya injili na semina.
Usisahau wewe mwenyewe kuendelea na maombi ukinyamazisha nguvu za giza.

4. Ukiota ndoto hizo inaweza kuwa ni wewe umefungwa vifungo vya giza au kuna maagano ya kishetani yanakushikilia au yanashikilia watu wa hapo au eneo hilo.
 
Isaya 42:22 "Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha."

✓✓Okoka kama hujaokoka, ombewa na watumishi juu ya kuharibiwa Nguvu za giza zilizokushikilia.

✓✓Hakikisha YESU KRISTO anakuwa Bwana na Mwokozi wako na anza kumtii daima.

5. Ndoto hizi pia zinaweza kukujulisha kwamba una mahusiano ya karibu na watu wanaotumika kishetani ili wakuletee madhara. 
 
✓✓Vunja uhusiano na watu wabaya na anza kuishi maisha matakatifu katika YESU KRISTO.
Pambana kimaombi na usimpe siri zako kila mtu.
Zaburi 71:12-13" Ee MUNGU, usiwe mbali nami; Ee MUNGU wangu, fanya haraka kunisaidia. Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya."

6. Ndoto hizi pia zinaweza kukujulisha kwamba Wewe unafungulia milango ya shetani kukuonea.
 
Isaya 59:1-2 " Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."

Yaani inawezekana unatenda dhambi, wewe sio muombaji na hujaokoka, humtii MUNGU, huenendi kwa ROHO MTAKATIFU n.k Jifunze kumcha MUNGU, kuishi maisha matakatifu na kutembea kwenye kusudi lake.

Kumbu 28:1 "Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;"

7. Ndoto hizi pia zinaweza kukujulisha kwamba huzijui haki zako kiroho mbele za MUNGU.
 
Dawa ni hakikisha unakuwa mtu wa ibada, kujifunza sana Neno la MUNGU na kutafakari maandiko ili ujue haki zako, liishi Neno la KRISTO.

Hosea 4:6 " Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, .........."

Maarifa ni Neno la MUNGU.
Ili yawe maarifa mazuri basi Neno la MUNGU liishi na lifanyie kazi.

8. Ndoto hizi pia zinaweza kukujulisha kwamba una vitu vya kishetani na hujajitenga navyo.
 
Mwanzo 35:2 "Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu."

✓✓Hakikisha unaondoa miungu migeni yote.

✓✓Ondoa hirizi, ondoa mafuta au leso au maji ya upako ya kipepo uliyopewa n.k

✓✓Ondoa kila kitu cha kishetani.
Jitenge na vitu hivyo, vitupe au vichome moto huku ukiwa muombaji.

2 Wakorintho 6:17-18 " Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, asema BWANA Mwenyezi"

9. Ndoto hizi pia zinaweza kukujulisha kwamba hujui kuzitumia mamlaka za kiroho za kuwashindia wateule wa KRISTO.
 
Mathayo 18:18 "Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni."

Ziko mamlaka 4 za kiroho za kukupa ushindi dhidi ya kila nguvu za Giza, mamlaka hizo ni Jina la YESU KRISTO, Damu ya YESU KRISTO, Nguvu za ROHO MTAKATIFU na Neno la MUNGU la ufunuo akupao ROHO MTAKATIFU.

Mathayo 7:7-8 "Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."

10. Ndoto hizi pia zinaweza kukujulisha kwamba Badilisha Maombi.
 
Kama tu ulikuwa unaomba sala za kukaririshwa acha, kama ulikuwa unaomba bila kufunga anza kufunga, omba Maombi ya vita, Maombi ya ya kumsihi MUNGU n.k kulingana na ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.

Zaburi 32:8 "Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama."

11. Ndoto hizi pia zinaweza kukujulisha kwamba Ondoa madai ya shetani kwenye maisha yako na ondoa uhalali wa nguvu za giza kukuonea.

✓✓Dawa ni kumtii MUNGU katika KRISTO YESU na huku ukimpinga shetani siku zote.

Yakobo 4:7-8 " Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili."

Tubia dhambi ambayo hujaitubia, anza kuwa mtoaji wa zaka, sadaka na dhabihu.
Kama uliikimbia kazi ya MUNGU anza sasa kumtumikia katika KRISTO YESU.
Kimaombi jitenge na maroho ya kuzimu ya ukoo yanayokufuatilia, jitenge na mizimu, jitenge na machukizo yote ya kidunia n.k

12. Ndoto hizi pia zinaweza kukujulisha kwamba Weka imani kwa MUNGU katika KRISTO YESU.
 
1 Petro 5:8-9 " Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, ........"

Hakikisha unakuwa thabiti katika KRISTO YESU.

✓✓Usitegemee vitu kukulinda, usitegemee mafuta ya upako, maji ya upako, leso n.k kama ulinzi wako.

✓✓Pambana na madhabahu za Giza na hakikisha unazishinda kimaombi.

Kumb 12:3 "nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo."

✓✓✓Muhimu zaidi Mtii ROHO MTAKATIFU katika yote.
Warumi 8:14 "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU."

Tembea katika nguvu za MUNGU , omba ki ufunuo na katika jina la YESU KRISTO.
Utashinda.
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU KRISTO Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292( whatsapp).

Comments