ALIVYO MWANAFUNZI WA NENO LA MUNGU.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki zangu wote.
Karibuni Tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

➡️Neno la MUNGU la Biblia Takatifu ni la Muhimu sana na limebeba hatima ya Kila Mwanadamu.

Zaburi 12:6 "Maneno ya BWANA ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba."

◼️Je Wewe huhudhuria Ibada na kusikiliza Neno la MUNGU hapo Ibadani?
Kama jibu lako ni "Ndio" unafanya vyema sana na Wewe ni Mwanafunzi wa Neno la MUNGU.

Waebrania 10:25 "wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia."

◼️Je Wewe husikiliza Mahubiri Redioni, kwenye Tv au Mtandaoni?
Kama jibu lako ni Ndio unafanya vyema na Wewe ni Mwanafunzi wa Neno la MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.

➡️Ni lazima Neno la KRISTO lienee Kila mahali.

Matendo  12:24 "Neno la BWANA likazidi na kuenea."

◼️Je Wewe hujifunza Neno la MUNGU Kwa njia ya kulisoma Mtandaoni au kwenye vitabu vya Watumishi mbalimbali wa KRISTO?
Kama jibu ni Ndio unafanya vyema sana na Wewe ni Mwanafunzi wa Neno la MUNGU.

Isaya 40:8 "Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la MUNGU wetu litasimama milele."

Je Wewe hufungua Biblia na kuanza kuisoma ili ujifunze Neno la MUNGU, ujue kusudi la MUNGU juu Yako na Upate maarifa sahihi ya kiroho yatakayokusaidia katika safari Yako ya Maisha ya Wokovu Duniani?
Kama jibu ni Ndio basi Wewe ni Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU na hicho unachokifanya ni kitu kizuri mno.

Mithali 30:5 "Kila neno la MUNGU limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio."

◼️Sasa kama Wewe umejigundua ni Mwanafunzi wa Neno la MUNGU basi pia Wewe ni Mwanafunzi wa YESU KRISTO, Leo tunamuangalia Mwanafunzi wa Neno la MUNGU ambaye anatakiwa awe na sifa hizi 10 hapa chini, hakika unakuwa na sifa hizi.

Mwanafunzi wa Neno la MUNGU yukoje?

1. Anajifunza Neno la MUNGU.

2 Timotheo 3:16-17" Kila andiko, lenye pumzi ya MUNGU, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa MUNGU awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema."

➡️Kama wewe ni Mwanafunzi wa Neno la MUNGU Hakikisha unakuwa na muda wa kujifunza Kila mara au hata Kila siku Neno la MUNGU.

2. Analiweka moyoni Neno la MUNGU ili asitende dhambi

Zaburi 119:11 "Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi."

➡️Kama wewe ni Mwanafunzi wa Neno la MUNGU Hakikisha unaliweka moyoni ili ulikumbuke Ukitaka kutenda dhambi ili Sasa ukilikumbuka Neno la MUNGU unaloliheshimu hutatenda  hiyo dhambi.

3. Analifanyia kazi Neno la MUNGU alilojifunza

Yakobo 1:22" Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu."

➡️Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU haishii tu kujifunza Neno na kuliacha pale ila hujifunza Neno la MUNGU na kuanza kulifanyia kazi katika Maisha yake katika KRISTO YESU Mwokozi.

4. Analitumia Neno la MUNGU kwa uhalali

2 Timotheo 2:15 "Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na MUNGU, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli."

➡️Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU hulitumia Neno la MUNGU Kwa halali kama kusudi la MUNGU katika KRISTO YESU lilivyo.

◼️Kulitumia Neno la MUNGU kihalali ni kutokulipotoa Bali kulitumia kama lilivyo.

Leo wengine hupotoa Neno la MUNGU la Biblia Takatifu.

mfano Leo Kuna wajinga fulani husoma katika Biblia Mathayo 7:7 inayoanza kwa kusema " Ombeni nanyi mtapewa" Kisha Kijana mmoja mzinzi asiye na akili anaenda kumtongoza Binti akimwambia "Hata Biblia inasema Ombeni nanyi mtapewa hivyo kwa sababu nakuomba penzi naomba unipe"  
au Binti kwa tamaa zake za kipumbavu anajitongozesha kwa Kijana akisema " ukiomba nakupa hata maandiko yanasema Ombeni nanyi mtapewa"

➡️Hawa wanapotoa maandiko na ni hatari sana kwao wasipotubu.

Biblia inasema kwamba Mtu anayefanya yasiyompasa kwa kutumia Neno la MUNGU atapata mapigo ya MUNGU yaliyoandikwa katika Biblia, hivyo usiongeze Wala usipunguze Neno la MUNGU.

Ufunuo  22:18-19 " Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, MUNGU atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
 Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, MUNGU atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki."

➡️Ambaye hatumii Neno la MUNGU Kwa halali maana yake ama anaongeza au kupunguza au kupotoa Neno la MUNGU, ni dhambi.

➡️Leo Kuna watu husema "Biblia inasema jisaidie nitakusaidia" hakuna andiko hilo.

➡️Wengine husema "Maandiko yanasema Malaika mtoa roho anaitwa Israeli " 
Na hadi baadhi ya Wakristo utawasikia wakisema baada ya Mtu kufa Mfano kwa ajali, utasikia wakisema " kakutana na Israeli mtoa roho ndio maana amekufa"
Hakuna andiko hili  katika Biblia labda lipo tu kwenye vitabu vya Mashetani na sio kwenye Biblia Takatifu, hivyo Mtu yeyote anayejaribu kuongeza andiko la Biblia, kuisingizia Biblia au kupunguza ni Dhambi.

◼️Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU analitumia Neno la MUNGU Kwa halali tu.

5. Ana upendo safi kwa wanafunzi wenzake wa YESU KRISTO

Yohana 13:34 -35 "Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi."

◼️Neno la MUNGU huzaa upendo wa kweli wa ki MUNGU kwa watu wote, huwezi kuwa Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU Kisha Kuna watu unawachukia.

6. Ana ushirikiano na wanafunzi wenzake wa YESU KRISTO

Zaburi 133:1 "Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja."

◼️Watu wote waliompokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao wana ushirikiano wao kwa wao kama Kanisa la MUNGU.

Umoja huo na ushirikiano huo huletwa na Neno la MUNGU Kwa kulitii na kulifuata.

Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU lazima ana umoja na Wateule wa KRISTO wenzake.

7. Ni mwanafunzi wa YESU KRISTO.

Waefeso 2:8 "Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;"

◼️Mwanafunzi wa Neno la MUNGU mzuri lazima kwanza awe ameokolewa na Bwana YESU KRISTO.

➡️Huwezi kuwa Mwanafunzi wa Neno la MUNGU harafu unakataa Wokovu wa KRISTO.

◼️Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU ni Mwanafunzi wa YESU KRISTO pia.
Yaani ameokolewa na YESU KRISTO.
Hivyo Kuokoka ndio Mwanzo mzuri wa kuwa Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU.

Mwanafunzi wa kweli wa Neno la MUNGU lazima akubali kuokolewa na YESU KRISTO Mwokozi.

8. Anawafanya na wengine wote wawe wanafunzi wa YESU wanaojifunza Neno la MUNGU na kumtii Bwana Mwokozi.

Marko 16:15-16 " Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa."

◼️Kwa sababu Mwanafunzi wa Neno la MUNGU lazima pia awe Mwanafunzi wa YESU KRISTO, Mtu huyo hufuata agizo la Bwana YESU la Wanafunzi wake wawalete Watu kwake.

◼️Hivyo Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU huwaleta watu wengine kwa YESU, kama hujaanza kufanya hivyo Anza leo, waambie familia Yako, Ndugu zako, kazini kwako na watu wote walio Karibu Yako ili wampokee YESU KRISTO kama Mwokozi wao.

9. Ni mwanafunzi wa Neno la MUNGU asiyeshindana na wanafunzi wenzake wa Neno la MUNGU.

Wafilipi 2:14 "Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,"

◼️Neno la MUNGU linakataza mashindano baina ya Wateule wa KRISTO wao kwa wao.

◼️Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU hashindani na Watu.

10. Anamsikiliza ROHO MTAKATIFU aliye Mwalimu Mkuu wa kufundisha Neno la MUNGU.

Warumi 8:14 "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU."

◼️Kiini kikuu Cha kuwa Mwanafunzi wa Neno la MUNGU ni Kumsikiliza ROHO MTAKATIFU na kufuata anachotaka yeye.

➡️Ukishindwa Kumsikiliza ROHO MTAKATIFU Wewe hujawa Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU.

◼️Mwanafunzi mzuri wa Neno la MUNGU humsikiliza ROHO MTAKATIFU daima.

➡️Hata Neno la MUNGU kulielewa unamhitaji ROHO MTAKATIFU.
MUNGU akubariki Sana kama ukifanyika Mwanafunzi wa YESU KRISTO uliye mwanafunzi safi wa Neno la MUNGU.
Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments