NINI KIJANA AFANYE KATIKA MAISHA YA WOKOVU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Leo nataka nizungumze mambo kadhaa kuhusu vijana lakini hata asiye kijana ujumbe huu unamfaa kwa sababu kuna makundi mawili ya vijana, kuna vijana wa umri maana yake wako umri kati ya Miaka 13 hadi 45 na wapo pia vijana kiroho maana yake wamempokea YESU KRISTO siku za karibuni haijalishi wana miaka chini ya 45 au juu ya 45..
Biblia inasema katika Maombolezo 3:27 ''Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake. ''
Ni vyema kijana akaichukua nira yake wakati akiwa kijana.
Hiyo nira ni ipi?
Nira hiyo ni hii, Mathayo 11:29 ''Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;''
Nira inayozungumzwa na Nemo la MUNGU ni kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako kisha unaanza kumtumikia MUNGU.
Sasa nira hiyo ya kumpokea YESU KRISTO inathibitikaje?
Biblia iko wazi sana ikisema kwamba '' Lakini yeye aliyeungwa na Bwana(YESU KRISTO) ni roho moja naye.-1 Kor 6:17''

Sasa naamini umeelewa kwanini Biblia inakutaka kuichukua nira yako wakati wa ujana wako.
Mimi najua ujana wako ni sasa na wala hujachelewa kuichukua nira yako yaani kumpokea YESU na kuanza kumtumikia.
Wakati wa ujana ndio wakati wa maamuzi sahihi ya kuonyesha kijana huyo baadae atakuja kuwa nani.
Wengine wanachukua nira za ulevi na ukahaba na maisha yao baadae yanaharibiwa na pombe, ukahaba na magonjwa yaliyosababishwa na nira waliyoichukua wakati wa ujana wao.
Wengine wanachukua nira za ujambazi na kupenda mambo ya dunia wakati wa ujana wao na hivyo maisha yao baadae yanaharibiwa na nira hizo walizochukua wakati wa ujana wao,
Ndugu Biblia inakushauri kuichukua nira ya wokovu wakati wa ujana wao.

Ukiokoka wakati ukiwa kijana mdogo hakika utaepuka mabaya mengi baadae.
Wako baadhi ya watu ni vilema sasa kwa sababu walichukua nira za wizi na ujambazi na matokeo ya nira zao ndio sasa ni vilema, japokuwa sio vilema wote walikuwa majambazi.
Wako watu wana magonjwa ya zinaa yanawatesa kwa sababu tu walichukua nira za uzinzi na uasherati.
Wako watu leo wameshindwa kuolewa/kuoa kwa sababu walibeba nira za dhambi zilizotengeneza laana zilizowashikilia sasa.
Ndugu Biblia inamtaka kila mwanadamu kwamba aichukue nira ya Wokovu wa KRISTO angali akiwa kijana mdogo.
Ndugu kama umeshavuka eneo la ujana nakuomba fundisha watoto wako na watu wako wa karibu walio vijana ili waichukue nira ya KRISTO wakati wa ujana wao.
Kijana asipoichukua nira ya Wokovu wa KRISTO anaweza akajikuta anaichukua nira ya shetani na kujikuta amejaa tu kiburi kinachotokana na mapepo yaliyoingia ndani yake baada ya yeye kuichukua nira ya shetani.
Kijana anaweza kukosa adabu kwa sababu tu ameikataa nira ya Wokovu wa KRISTO.
1 Petro 5:5 '' Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu MUNGU huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.''

Kama kijana hana nira ya KRISTO ni ngumu kijana huyo kuwa mnyenyekevu, ni ngumu kuwaheshimu wazee.
Kijana kama hana YESU KRISTO ni ngumu sana kuwa na kiasi.
Tito 2:6 ''Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi;''
Ewe kijana, MUNGU ana neno na wewe, MUNGU anakutaka uichukue nira ya Wokovu wakati wa ujana wako.

Labda sasa nini ufanye kijana uliyeokoka katika wakati wako wa ujana?

1. Mtumikie MUNGU.

Mhubiri 12:1 ''Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.''
Kiroho kuna mambo mengi sana yenye faida njema baadae kama ukiamua kuambatana na MUNGU aliye hai tangu wakati wa ujana wako.
Mojawapo ni  kutengeneza hazina yako mbinguni, hazina yako unaitengeneza wewe mwenyewe tu na haiwezekani mtu mwingine kukutengenezea hazina yako. 
Hazina yako unaitengeneza kwa kuhusika na mambo haya manne kwa pamoja,  kuwaleta watu kwa YESU, Kwa kumtolea MUNGU zaka, dhabihu na sadaka nyingi, Kumwabudu MUNGU katika roho na kweli  na kwa kumtumikia MUNGU kwa juhudi na uaminifu.
Sasa usipoutumia ujana wako kutengeneza hazina yako ya mbinguni tambua kwamba hutaweza kwenda huko mbinguni kama hazina yako haipo.
Mathayo 6:20-21 '' bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.'' 

Ndugu, hazina yako ndio makazi yako ya mbinguni, hivyo kama hutatengeneza hazina yako wakati wa ujana wako ujue ukitaka kutengeneza hazina hiyo wakati wa uzee wako hutajenga jengo kubwa wala zuri la kuishi wewe baada ya kufa, haya mambo ni ya rohoni mno ila ni muhimu sana kwako.
Ndio Maana Biblia inakutaka mkumbuke Muumba wako katika kipindi cha ujana wako maana uzeeni mwako hutakuwa na nguvu kama za ujanani.
Ndugu hakikisha unatimiza mambo manne(4) niliyokuambia hapo juu.
Biblia iko wazi sana ikisema  ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.-1 Kor 15:58''

 2. Tumia nguvu zako kwa kuleta faida katika ufalme wa MUNGU.

Mithali  20:29a '' Fahari ya vijana ni nguvu zao,''
Iko wazi sana kwamba fahari ya kijana ni katika nguvu zake.
Fahari ni nini?
Fahari ni jambo au kitu cha sifa  cha  kujivunia kwa watu.
Fahari ni ukuu au utukufu hivyo kitu kikubwa cha kujivunia katika ujana wako ni nguvu za mwili, ndivyo Biblia inasema.
Yaani kama kuna kitu kijana anaweza kusijifu ukilinganisha na mzee ni nguvu, sina pia maana ya kwamba mzee hana cha kujisifu nje na nguvu.

Sasa nguvu zako kijana unazitumia katika nini?
Wapo vijana wanatumia nguvu zao kuibia watu au kuteka watu.
Wako vijana wanatumia nguvu zao za ujanani kufanya kila kazi za kishetani, hao wanautumia vibaya ufajari wao.

 Nguvu zako kijana unazitumia katika nini?
Ukiangalia kila harakati duniani ziwe za kisiasa, maandamano  au za kivyovyote utaona vijana ndio wanaotumikishwa zaidi kwa sababu tu wana nguvu.
Ndugu, mimi nakushauri tumia nguvu zako za ujana wako kuleta faida katika ufalme wa MUNGU.
Biblia inakupa muongozo mzuri hapa,  
1 Yohana 2:14-17 ''......... Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu. Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. ''

Tumia nguvu zako za wakati wa ujana wako kuipeleka mbele injili ya YESU KRISTO inayookoa.

3. Ishi maisha matakatifu.

1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''
Aliyekuita ni YESU KRISTO, yeye ni mtakatifu na anakutaka na wewe uishi maisha matakatifu siku zote za kuishi kwako.
Utakatifu ndilo vazi la waenda mbinguni, hakikisha unaishi maisha matakatifu katika YESU KRISTO.
Zaburi 34:14 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''

4. Shirikiana na Mchungaji wako katika mema yote.

Kumb 12:19 ''Jilinde nafsi yako usimwache Mlawi siku zote uishizo katika nchi yako. ''
Biblia inasema kwamba jilinde sana usije ukamuacha mlawi siku zote.
Mlawi ni nani?
Lawi ni kabila mojawapo kati ya makabila 12 ya Israeli, kabla hili lilichaguliwa na MUNGU ili watu wa kabila hili wote wawe makuhani, Kwa leo walawi ni wachungaji wote wa makanisa na watumishi wote wanaomtumikia YESU KRISTO na wamekuwa walimu wako, wanakufundisha Neno la MUNGU, wanakuombea, wanafunga kwa ajili yako, wanapoteza muda wao mwingi ili tu wewe ufunguliwe, upone, upokee baraka na uwe na ushindi.
Biblia inasema jilinde usije ukamsahau mlawi wako.

Sasa ufanye nini kwa ajili ya mlawi wako?
Anakupa vya rohoni hivyo sio vibaya na wewe ukimbariki vya mwilini yaani chakula cha kimwili na mahitaji ya kimwili.
Usikubali Mchungaji wako avae suruali zenye viraka wakati wewe una uwezo wa kumnunulia suruali mpya, usikubali Mchungaji wako alale na njaa kisa chakula hamna wakati wewe kwako unakula na kubakiza na kutupa.
Ndugu Biblia inasema jilinde usije ukamsahau mlawi wako, mlawi wako anaweza kubeba ushindi wako wa kiroho wa kila namna hivyo mtumie kwa faida yako ila pia mhudumie.
Kuna wachungaji kila siku amefunga ili kuombea Kanisa lakini watu wa Kanisani kazi zao ni kufanya kampeni watu wasitoe fungu la kumi na sadaka.
Mchungaji anaweza akawa asiwe na kazi, kazi yake ni kukuombea wewe na kumuuliza MUNGU kwa ajili yako ili ufanikiwe, kazi yako kama huijui naomba ujue leo kwamba unatakiwa kumhudumia vya mwilini mradi ni katika utakatifu tu.
Biblia kwa kukazia inasema kwamba '' Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote.-Wagalatia 6:6''
Mema yote ni pamoja na sadaka nzuri na vitu vingine ulivyo na uwezo navyo mradi ni katika utakatifu tu.
Kuna wachungaji wala hawakutaka kwamba wawe wachungaji ila MUNGU aliwaita na kuwaambia waache kazi zao ili wamtumikie, walitii ndio maana leo kazi yao ni kulichunga tu Kanisa, sasa wewe uliye Kanisa hakikisha unajitambua kwamba ni wajibu wako kumhudumia vitu vyakula na mavazi na vitu mbalimbali kwa kadri ya uwezo wako, hiyo ni muhimu sana na izingatie wakati wa ujana wako.
Kuna watu kutoa sadaka au zaka mpaka apate mabalaa kisha aombewe ndipo atatoa sadaka, ndugu wewe amua kuanzia leo kumhudumia mlawi uliyepewa na MUNGU, mhudumie siku zote kwa kadri ya uwezo wako, mhudumie hata wakati hauna kifungo wala tatizo.

5. Uwe kielelezo kwa mema na sio mabaya.

1 Timotheo 4:12 '' Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.''
 Kuwa kielelezo chema ina maana ya kwamba wewe uwe wa mfano mzuri katika mema.
Wakiuliziwa vijana wanaoishi maisha matakatifu na wewe uwemo.
Wakiuliziwa watu wasio wazinzi wala washerati na wewe uwemo.
Hakikisha unakuwa kielelezo katika mema yote.
1 Thesalonike 1:7 ''Hata mkawa kielelezo kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya.''
Hawa walikuwa kielelezo chema katika miji ya Makedonia na Akaya na wewe hakikisha unakuwa kielelezo chema katika mtaa wako, wilaya yako, mkoa wako na taifa lako.

'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''



Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

+255714252292(Hadi whatsapp).





Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments