| Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.  | 
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Natambua kabisa katika kila kanisa au kila jengo la ibada la Kanisa kuna viongozi walioteuliwa au kuchaguliwa ili tu kuwe na utaratibu mzuri na ili kazi ya MUNGU iende mbele.
Uongozi wa kiroho ni suala la kibiblia kabisa.
Hata Waisraeli walipokuwa wanatoka Misri ni Musa ndio alikuwa kiongozi wao, lakini kwa sababu ya majukumu kuwa mengi ni MUNGU alimwambia Musa juu ya kuchagua watu 70 kutoka kila kundi la watu ili tu wawe viongozi na kazi ya MUNGU iende mbele.
Hesabu 11:16-17 '' Kisha BWANA akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe. Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu hawa pamoja nawe, ili usiuchukue wewe peke yako.''
Hivyo kila Kanisa kuwa na viongozi wanaosaidiana na Mchungaji wao ni jambo jema la linahitajika sana.
Mchungaji hawezi kuwa kiongozi peke yake bali wanahitajika wa kumsaidia ndio maana Makanisani huwa kuna Katibu wa Kanisa, Mhasibu wa Kanisa, Wazee wa Kanisa, Mashemasi, wenyeviti na makatibu wa idara mbalimbali kanisani, viongozi wa uijilisti, walimu wa watoto n.k hiyo ni sawa kabisa kwa ajili ya kuifanya kazi ya MUNGU kusonga mbele.
Soma langu hili linamlenga kila aina ya kiongozi katika Kanisa la MUNGU duniani, awe ni Mchungaji, Askofu au yeyote hata kama anaongoza kikundi cha watu watatu.
Sasa kwa sababu viongozi wanahitaji sana kuwepo basi sifa zao pia nazo ni muhimu ili kazi ya MUNGU isonge mbele na ili Neno la MUNGU lisitukanwe.
Sifa za kiongozi sahihi kanisani.
1. Awe ameokoka na anaishi maisha matakatifu.
Huwezi ukawaongoza watu waliookoka wakati wewe hujaokoka, kwa Kanisani hakutakiwi kuwa hivyo. Hivyo Basi kiongozi mzuri Kanisani lazima awe amempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake na anaishi maisha matakatifu ya Wokovu.
1 Petro 1:15 ''bali kama yeye(YESU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''
Kila kiongozi anatakiwa kuwa ameokoka, na anaishi maisha matakatifu maana ni lazima watumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU kuishi maisha matakatifu.
Kwa hiyo kabla hatujaangalia lolote kuhusu anayefaa kuwa kiongozi Kanisani kwanza lazima tuangalie kama mtu huyo amempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake na lazima tuangalie kama mtu huyo anaishi maisha matakatifu.
2. Awe Mkweli na Mwaminifu.
Kiongozi sahihi ni yule anayesema ukweli daima.
Anaongea ukweli na anaiishi kweli ya MUNGU ambayo ni Neno la MUNGU.
Tangu zamani viongozi wa Kanisa la KRISTO walikuwa wakweli, hivyo hata sisi viongozi katika wakati wetu inatupasa kuwa wakweli daima.
Warumi 9:1 ''Nasema kweli katika KRISTO, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika ROHO MTAKATIFU,''
Katika kutimiza majukumu yake kama kiongozi wa kiroho anatakiwa kuwa mkweli daima.
Pia asiwe mkweli tu bali awe mkweli na mwaminifu.
Awe mwaminifu kwa MUNGU katika maisha yake ya kiroho.
3. Awe kiongozi bora.
Kiongozi bora ni yule anayefanya kazi yake kwa ubora.
Kiongozi bora hafanyi kazi ya MUNGU kwa kulipua bali anafanya kazi yake kwa ubora.
Ubora wa majukumu ya mtu katika uongozi wake Kanisani unaweza kuonyesha kabisa kwamba ana moja ya sifa nzuri za kiongozi sahihi.
2 Timotheo 2:15 ''Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na MUNGU, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli. ''
4. Anatimiza kusudi la MUNGU la yeye kuwa kiongozi.
Huyu anafanya kazi sahihi aliyopewa na MUNGU.
Warumi 8:28 ''Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote MUNGU hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. ''
5. Ajifunze kutokana na makosa na afahamu kutatua matatizo.
Hii haina tu maana ya kwamba afanye makosa kisha ajifunze kutokana na makosa hayo, bali katika kufanya kazi ya MUNGU ili hiyo kazi iwe nzuri zaidi basi kiongozi aboreshe kutoka kiwango cha kwanza kwenda kiwango bora zaidi, maana atafikia kiwango bora baada ya kukiona kiwango cha kwanza kuwa kina mapungufu fulani.
Lakini pia inawezekana amepewa nafasi ambayo mtangulizi wake alifanya makosa mengi, huyu kiongozi wa sasa anatakiwa kujifunza kutokana na makosa ya kwanza ili asiyarudie.
Inawezekana pia kama kiongozi akakosea katika kutimiza majukumu yake, hivyo inampasa kujifunza kutokana na makosa hayo ili asiyarudie.
Lakini pia kiongozi huyo lazima ajue kutatua matatizo yanayotokea.
Kwenye suala la kutatua matatizo ndiko utamjua kiongozi mzuri na kiongozi pia asiye mzuri.
Wailipi 4:8 '' Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.''
6. Aungane na walio chini yake.
Hakuna mtu aliye kisiwa kiasi kwamba hahitaji msaada wa wengine.
Huwezi kufanya kazi peke yako kwa sababu tu wewe ni kiongozi, bali tu vingo katika mwili mmoja hivyo ungana na wenzako walio chini yako ndipo kazi ya MUNGU itaenda mbele kwa usahihi.
1 Kor 12:12 '' Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na KRISTO. ''
7. Akubali lawama na akubali kukosolewa inapobidi.
Wakati mwingine kunaweza kutokea lawama kutokana na uongozi wako.
Kama ni lawama za kweli zikubali na rekebisha ili zisiwepo tena.
Kama ni lawama za uongo zikubali ila julisha kwamba hizo lawama hazikuhusu, pia kama zimesambaa hizo lawama za uongo zifute kimaombi kupitia jina la YESU KRISTO.
Wakati mwingine pia katika uongozi kuna kukosolewa.
Kiongozi mzuri ni ambaye hukubali kukosolewa pale ambapo ameenda isivyo.
Waebrania 3:13 '' Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.''
8. Awe anawasikiliza na wengine huku pia akitofautisha mambo yake mengine na uongozi.
Kiongozi sahihi wa kiroho ni lazima awe na tabia ya kumsikiliza kila mtu bila kubagua yeyote.
1 Kor 8:2 '' Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.''
Pia kama kiongozi katika kanisa ni lazima ujue kutofautisha mambo mengine yanayokuhusu ili asiuharibu uongozi wako.
Mfano ukikwaza na mke wako au mume wako usiwakwazikie hadi kundi unaloliongoza.
Msongo wako wa mawazo sio uvuruge hadi kazi ya MUNGU uliyopewa.
dhibiti msongo wako wa mawazo ili kazi ya MUNGU pabaki pale pale na iendelee mbele.
9. Awe mbunifu, na mtu wa malengo.
Ziko sifa nyingi za kiongozi sahihi wa kiroho, moja ya sifa hizo ni kiongozi huyo kuwa mbunifu na awe na malengo.
Kama kiongozi unatakiwa kuwa mbunifu ili kuifanya kazi ya MUNGU kukua, kupanuka na kuongezeka.
Mfano kama mlikuwa mnashuhudia tu basi kwa ubunifu mnatengeneza tracks za Neno la MUNGU ili katika kushuhudia mnagawa na vijitabu, hivyo watu watafunguliwa zaidi.
Lakini ubunifu wote ni lazima usiende kinyume na Neno la MUNGU.
Na ubunifu huo ni muhimu uongozwe na ROHO wa MUNGU.
Ni vyema sana pia kuwa kiongozi unayejiwekea malengo na kuyatimiza na unajitoa sio kwa kulazimishwa bali kwa upendo kwa MUNGU.
Waefeso 4:4 ''Mwili mmoja, na ROHO mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. ''
10. Awe anasimamia maamuzi na anajitambua mwenyewe.
Ili kiongozi aaminiwe kwa anaowaongoza basi kusimamia maamuzi ni silaha muhimu sana na kubwa ya kukufanya uaminike.
Ndio yako lazima iwe ndio na sio yako lazima iwe sio.
Ni Vyema kusimamaia maamuzi sahihi ili kazi ya MUNGU isonge mbele.
Mathayo 5:37 ''Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu. ''
Pia kiongozi wa kiroho lazima ajitambue kamba yeye ni kiongozi na anatakiwa afanyeje kama kiongozi.
Hakikisha unajua uwezo wako kiuongozi na upungufu wako kiuongozi, jifunze pia ili kuelewa majuku yako.
11. Yajue majukumu yako kama kiongozi wa kiroho na yatimize.
Kila kiongozi lazima ajue majukumu yake na ayatimize.
Kuna baadhi ya makanisa Mchungaji anafanya hadi kazi za shemasi, huko ni kutokujua majukumu.
Kuna Makanisa hadi wazee wa kanisa au mchungaji wanafanya kazi za viongozi wa kwaya, huko kunasababishwa na kutokujua majukumu.
Kuna migogoro mingi makanisani kwa sababu tu Mchungaji hajui majukumu yake, wazee wa Kanisa hawajui majukumu yao au wameyaacha au kwa sasa hawafanyi majukumu yao bali wanafanya majukumu ya Mchungaji na yeye yupo na anatimiza wajibu wake, hapo lazima mgongano utokee.
Ni muhimu sana kila kiongozi kuyajua majukumu yake na kuyatimiza.
Wagalatia 5:13 ''Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. ''
12. Tofautisha karama yako na uongozi.
Karama ni karama na uongozi ni uongozi.
Karama sio uongozi bali kuna karama inaweza pia ikafanywa na kiongozi na kila kitu kikakaa sawa.
Inawezekana wewe uko katika wadhifa wa juu Kanisani kwenu na huwa unatumika kuchagua viongozi walio chini yako. Sasa ni muhimu kujua kwamba sio kila mhubiri mzuri basi ni kiongozi mzuri.
Sio kila mwimbaji mzuri anafaa kuwa kiongozi mzuri.
Sio kila mtu muongeaji sana anafaa kuwa mzee wa Kanisa.
Kuna watu Kanisani wana karama nyingi na vipawa vingi lakini wasifae katika uongozi.
Kuna watu hawana karama lakini ni viongozi wazuri.
1 Kor 12:4-7 '' Basi pana tofauti za karama; bali ROHO ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana(YESU) ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.''
13. Uwe mvumilivu.
Kiongozi mzuri lazima pia awe na uvumilivu.
Wakati mwingine unaweza kupitia kusengenywa, kuandamwa, kutukanwa, kudhalilishwa n.k lakini uvumilivu kwa kiongozi unahitajika sana.
2 Kor 6:3-6 ''Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe; bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa MUNGU; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika shida; katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha, katika kufunga; katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika ROHO MTAKATIFU, katika upendo usio unafiki;''
14. Kukataa uovu na kufanya juhudi za kuuondoa uovu huo katika kundi lako.
Umepewa nafasi ya uongozi lakini pia uongozi wako unajumuisha na kuwasaidia watu ili wampendeze MUNGU mnayemtumikia.
Hujaitwa kuwa kiongozi unayewafanya watu wampendeze shetani bali wampendeze MUNGU katika KRISTO YESU.
Kazi muhimu pia kwa kiongozi sahihi Kanisani ni kukataa uovu, dhambi na makosa.
Usiwe kiongozi wa kuwakemea wanaokupinga tu bali kemea na waovu na kemea dhambi daima.
1 Thesalonike 5:20-22 '' msitweze unabii; jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna. ''
15. Amtii YESU KRISTO.
Kiongozi yeyote wa kiroho ni lazima awe chini a YESU KRISTO na amtii YESU KRISTO.
Kila kiongozi Kanisani anatakiwa kuwajibika kwa YESU KRISTO Mwokozi.
Usipomtii Bwana YESU katika jambo lolote hakika wewe unakosa sifa muhimu sana ya kuwa kiongozi sahihi.
Usipomtii Bwana YESU hakika wewe hufai kuwa kiongozi Kanisani.
Kumtii Bwana YESU ndiko pia kumtii MUNGU.
Kumtii Bwana YESU kunahusisha kuishi maisha matakatifu katika yeye, kuongozwa na ROHO MTAKATIFU na kulifanyia kazi Neno la MUNGU.
1 Petro 1:14-15 '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU
 akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI 
YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je,
 Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika 
Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima 
Wa Milele?
Majibu
 Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea
 Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
Comments