USIBAKI MCHANGA KIROHO MIAKA YOTE

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mtoto anapozaliwa wazazi wake hutarajia mtoto huyo kukua na kufikia hatua ya kuwa mtu mzima.
Vipi kama wazazi watazaa mtoto na kisha baada ya miaka mitano mtoto bado anahitaji tu maziwa ya mama na wakati huo bado hawezi hata kukaa mwenyewe, hawezi kusimama mwenyewe? Hakika itawachanganya sana wazazi hao.
Sasa kama ambavyo kuna watoto wa kimwili wapo pia watoto wa kiroho.
Kitu kimoja muhimu ambacho kinaweza kumfanya mtoto akue katika afya njema ni chakula bora.
Mtoto anakula chakula ili aishi na ili akue.
Mtu anayeokoka anatakiwa kula chakula cha kiroho safi kila Mara ili akue kiroho.
Kukua kiroho ni jambo la muhimu sana kwa kila mteule wa KRISTO.

Waefeso 4:14-15 " ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, KRISTO."

Kwanini ukue kiroho?

1. Ili usiwe tena mtoto mchanga kiroho.

2. Ili usichukuliwe na kila upepo wa elimu zilizo kinyume na YESU KRISTO Mwokozi.

3. Ili usifuate njia za udanganyifu.


Kutokukua kiroho kumewafanya baadhi ya watu kubaki wakidanganywa tu na wanaojiita watumishi na kumbe sio watu wa MUNGU. Mfano mmoja wapo wa kufahamu sana ni huu.
MUNGU zamani alisema na watu wake kupitia manabii.
Ujumbe ule wa Manabii ulitimia ule uliotakiwa kutimia, na ule ambao haujatimia ipo siku utatimia.
Mfano ni huu ambao MUNGU alisema kupitia nabii na Neno hilo likatimia.

Mathayo 8:17 "ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu."
Kwanini nimesema Neno hili?
Nataka ujue sasa kwamba kwa sasa MUNGU hasemi tena kupitia manabii bali anasema na sisi kupitia YESU KRISTO.

Inawezekana hujaelewa vyema ila ngoja tuone maandiko yanasema nini.
Waebrania 1:1-3 " MUNGU, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;"


Hivyo kwa sababu MUNGU kwa sasa anasema na sisi kupitia KRISTO YESU nataka ujue kwamba YESU KRISTO ameweka watumishi wake waaminifu na hao anasema nao na wao wanasema na sisi.
Bwana YESU anasema ''Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;-Mathayo 7:24''
 
Kama MUNGU anasema kupitia KRISTO basi huyo mleta ujumbe wa kweli wa MUNGU ni lazima awe anamtii YESU KRISTO.

Mtu aliyekua kiroho ndio tu anayeweza kupambanua mambo kama haya.
Ukiona mtu anampinga YESU hata kwa neno moja ujue mtu huyo hajapewa ujumbe na MUNGU.
Sasa wapo watu wanajiita watumishi na mafundisho yao yanampinga YESU KRISTO na wakati mwingine ni watumishi hao wamejiita Yesu na wengine wamejiita Mungu na kujikusanyia maelfu ya waumini, waumini hao ni kundi la wasiomjua MUNGU ama walimjua MUNGU kidogo sana ila hawakukua kiroho katika KRISTO ndio maana walitekwa na maajenti wa kuzimu.
Mathayo 24:24 ''Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.''

Sasa ukiona Mtumishi hahusiki tena na YESU Mwokozi, Mtumishi huyo hata kama akikwambia kwamba MUNGU amemsemesha usikubali maana MUNGU hasemi na walio nje ya KRISTO. Kumbuka walio ndani ya KRISTO ambao MUNGU husema nao ni wale waliookolewa na YESU KRISTO na wanamtii.
Watumishi wengi sasa wanajiepusha na YESU Mwokozi na bado wanasema kwamba MUNGU amewaambia, ukweli ni kwamba ukiwa kinyume na YESU KRISTO huwezi kupewa ujumbe na MUNGU kwa ajili ya watu wa MUNGU.
Siku za karibuni ni adimu sana kuona mtumishi anaongoza sala ya toba waamini wapya, lakini ni rahisi tu kumuona Mtumishi anatabiri au anadai MUNGU amemwambia.

Ndugu, Biblia imekuwekea mzani wa kumpima kila Mtumishi ili asikudanganye kwa tamaa zake.
Mzani mmoja wapo ni huu.
1 Yohana 4:1,3 " Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.
Na kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani."

Mtu anayeendelea kula chakula cha kiroho kinachomfanya akue kiroho anatakiwa kujipima katika hayo mambo matatu hapa chini, ndipo atajigundua kama amekua kiroho.

1. Je wewe sio mtoto mchanga kiroho?
Kama sio Mchanga kiroho basi umekuwa kiroho, ila usikubali kuruhusu kudumaa kiroho.

2. Je wewe huchukuliwi na kila upepo wa elimu zilizo kinyume na YESU KRISTO Mwokozi?
Kama huchukuliwi na wapingaKristo na unamtii ROHO MTAKATIFU huku ukilitumia Neno la MUNGU kwa uhalali hakika wewe sio Mchanga kiroho.

3. Je wewe  hufuati njia za udanganyifu?
Kama wewe hufuati njia za udanganyifu za kila namna basi wee sio mchanga kiroho.

Wafilipi 1:6 ''Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya KRISTO YESU;''

Je ndugu unakua kiroho au wewe siku zote umebaki mtoto mchanga kiroho.
Je unakua kiroho au umedumaa kiroho?
Ndugu, nakuomba fanya juhudi za kukua kiroho.


MAOMBI YA LEO.

1. Kama ROHO MTAKATIFU yuko ndani yako watangazie kufunguliwa kwao vifungo vya giza waliokuwa wamefungwa wote. Hata wewe kama ulikuwa unateswa na vifungo vya giza basi leo jitangazie kufunguliwa, kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Tangaza uhuru kwa waliokuwa mateka wa nguvu za giza, hata kama ni wewe ulikuwa mateka basi jitangazie uhuru kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Panapohitaji toba basi tubu na panapohitaji kuacha mabaya hakikisha unayaacha kuanzia leo.
Kwa maombi yako leo inaweza kuwa ni siku njema ya kutangaza kufunguliwa kwako na kwao unaowaombea.
Isaya 61:1 ''ROHO ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. ''


2. Fanyika silaha ya MUNGU katika KRISTO YESU ili uombe kuvunja kila kazi za kishetani ili isifanye kazi tena kwako.
Fanyika silaha za MUNGU ili kuwazimisha wachawi, majini na wakuu wa giza wote na kila majeshi ya pepo wabaya wote katika ulimwengu wa roho..
Yeremia 51:20-22 ''Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake; na kwa wewe nitawavunja-vunja mwanamume na mwanamke; na kwa wewe nitawavunja-vunja mzee na mtoto; na kwa wewe nitawavunja-vunja kijana mwanamume na kijana mwanamke; ''

 
3. Omba MUNGU akubariki kwa maana umemtegemea na kumtumainia.
Yeremia 17:7 ''Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye Bwana ni tumaini lake.''

Kumtegemea Bwana YESU na kumtumaini ni jambo la muhimu sana kwa kila mteule.
Kumtegemea MUNGU na kumtumaini ni jambo zuri sana maana hilo hutoa kibali cha MUNGU kukulinda.
Isaya 26:3-4 '' Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele.''


Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

+255714252292(Hadi whatsapp).



mabula1986@gmail.com


Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments