USIOGOPE KUFUATILIWA NA MAWAKALA WA SHETANI, WENGINE NI KWA KUANGAMIA KWAO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe sana ndugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Mama mmoja alinipigia simu siku moja akilia huku akisema kwanini nguvu za giza zinamfuatilia yeye tu?
Inawezekana na wewe una mawazo kama hayo, uko kwenye vita kubwa ya kiroho kwa muda mrefu. Mimi nikuambie hivi "Siku ukifunuliwa aina ya maombi unayotakiwa kuomba unaweza ukapeleka kilio ambacho hakijawahi kutokea Kwenye kambi ya adui zako wa kuzimu"

Usiogope kufuatiliwa na mawakala wa shetani, wengine wanakufuatilia ili maombi yako yawafanye kufa na kutoweka kabisa.
Sijui kama wewe muombaji unajitambua kama Neno la MUNGU linataka uwe unapokuwa unapigana vita vya kiroho na mawakala wa shetani.
Biblia inasema hivi.
Yeremia 51:20-21 " Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;"


Yaani wewe unaweza ukatumika na MUNGU kuwafuta wakuu wa giza katika eneo lako.
MUNGU kupitia wewe kwa maombi yao atamuua farasi na mpanda farasi yaani mchawi na tunguri zake, mfuga majini na majini yake, mkuu wa giza na zana zake za kipepo n.k
Usiogope kufuatiliwa na mawakala wa shetani, wengine wanakufuatilia ili maombi yako yawafanye kufa au kupata uharibifu mkubwa sana.
Anaweza kuwa ni mchawi aliyeroga wengi sana lakini wakati huu amekosea njia, anajaribu kukuroga wewe Mteule wa KRISTO na wewe unajua kuomba na kumsikiliza ROHO MTAKATIFU katika maombi, unaweza ukaomba maombi ya vita na ndio ukawa mwisho wa Mchawi yule aliyetesa wengi. Yaani aliwatesa wengi na alijiona hakuna wa kumshinda kumbe alisogezwa kwako ili Maombi yako yawafanye Malaika wa MUNGU kumwangamiza.
Ona mfano huu ambapo maombi ya watu wa MUNGU yalitengeneza kifo cha maadui zao.


2 Nyakati 32:21 '' Naye BWANA akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga.''


Mfalme wa Ashuru ni mfano wa mkuu wa Giza anayetuma. Majini kwako au uchawi kwako ili uteseke.
Maombi yako yanaweza kuwafanya wachawi wasiroge tena, maombi yako yanaweza kuwafanya wakuu wa giza wahamie mji mwingine na sio unakokaa wewe.
Shetani ni shetani tu hivyo usimhurumie kwenye maombi yako.
Aliyetumwa na kuzimu kuja kukutesa, kukufunga vifungo au kukuonea unaweza ukaomba kwa MUNGU na adui huyo anaweza kufa, Malaika wa MUNGU anaweza kumkatilia mbali kwa sababu ya Maombi yako.


Usiogope kufuatiliwa na mawakala wa shetani, wengine wanakufuatilia ili maombi yako yawafanye kufa na kutoweka kabisa.

Mfano hai mwingine ni huu.
Waliopanga Danieli afe kwa kuliwa na simba, wao wote ndio walikuja kufa kwa kuliwa na simba wale wale waliodhani atakufa Danieli.


Danieli 6:24 "Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danielii, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu."

Kwa hiyo anaweza akapata madhara aliyekupeleka kwa mganga, anaweza akapata madhara aliyekutumia majini au uchawi, unatakiwa tu uwe umeokolewa na YESU KRISTO, unaishi maisha matakatifu na huwa unaomba maombi katika jina la YESU KRISTO.
Watu hawa walipanga Danieli afe, walidhani Danieli atakufa ili wachukue nafasi yake ya kazi, walijua atakufa ili wajisifu kwa miungu yao lakini walisahau kwamba Danieli alikuwa anaingia kwenye maombi Mara tatu kwa siku.

Danieli 6:10 "Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za MUNGU wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo."

Hivyo wao ndio walikufa na sio Danieli.
Hivyo inawezekana kabisa mshirikina aleyekutumia roho ya mauti akafa yeye, wewe omba katika jina la YESU KRISTO.
Inawezekana kabisa mchawi anayeroga ndoa yako, uchumba wako, uchumi, biashara, afya yako, kazi yako au huduma yako, huyo wakala wa shetani mabaya aliyoyakusudia kwako yakampata yeye na sio wewe, wewe omba katika jina la YESU KRISTO.
Inawezekana kabisa wanaoroga uzao wako, wanaoroga kibali chako au wanaotumia nguvu za Giza za namna yeyote wao ndio watapigwa na kutoweshwa, wewe omba katika jina la YESU KRISTO.


Zaburi 40:14-15 " Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe!"


Mimi huwa nasema hivi " Wakala wa shetani ninayemuona ndotoni au kwenye maono au ninayemuona kwa ufunuo wa ROHO MTAKATIFU, huwa naona hivyo ili wakala huyo wa kuzimu apigwe na kutoweka. Haijalishi ni jini amevaa sura za wanyama au wadudu, haijalishi ni mkuu wa giza amevaa sura za watu n.k, huwa najua kwamba nimemuona mpambe huyo wa shetani ili niombe apondwe kwa jina la YESU KRISTO"

Usiogope kufuatiliwa na mawakala wa shetani, wengine wanakufuatilia ili maombi yako yawafanye kufa na kutoweka kabisa.
Kama tu ulikuwa hujui ni kwamba Wale waliowabeba akina Meshaki, Shedraki na Abednego ni wao ndio walikufa hata kabla hawajaweka watumishi wa MUNGU kwenye tanuri la moto.


Danieli 3:20-22 " Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi watu hao wakafungwa, hali wamevaa suruali zao, na kanzu zao, na joho zao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile tanuru ilikuwa ina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego."


Yaani waliowabeba watumishi wakafa kabla hata adhabu haijatekelezwa.
Hivyo majini waliotumwa kwako wanaweza wakateketea kabla hawajakugusa, kazi yako ni kuomba ukitumia jina la YESU KRISTO, ukitumia Damu ya
YESU KRISTO, ukitumia Nguvu za ROHO MTAKATIFU na ukitumia Neno la MUNGU la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.

Unajua kwanini YESU anaitwa Mwokozi?
Ni kwa sababu anaokoa.
Akina meshaki, shadraka na Abednego aliwaokoa na hawakupa madhara ya wakuu wa giza wa Babeli.
Usiogope ndugu bali omba na MUNGU hakika atawatowesha mawakala wa Giza waliokutesa.
MUNGU Baba anasema katika Isaya 41:10-13 kwamba " usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni MUNGU wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.
Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia."


Ipo siku utawatafuta na wala hutawaona waliokuwa wamekufunga kipepo, MUNGU atakuwa ameaangamiza kwa maombi yako.
Ipo siku utawatafuta wala hutawaona waliokuwa wanafanya mikakati ili ndoa yako ife.
Ipo siku utawatafuta wala hutawaona waliokuzuilia kipepo ili usifunge ndoa takatifu.
Ipo siku utawatafuta wala hutawaona waliokuwa wanakuletea magonjwa.
Ipo siku utawatafuta wala hutawaona waliokuwa wanakuzuilia uzao katika ndoa yako.
Ipo siku utawatafuta wala hutawaona waliopanga ufukuzwe kazi.
Ipo siku utawatafuta wala hutawaona walioua familia yako.
Ipo siku utawatafuta wala hutawaona walioroga ardhi yako ili usifanikiwe.
Ipo siku utawatafuta wala hutawaona waliokuwa wanakaa vikao vya kipepo ili uangamie.
Ipo siku utawatafuta wala hutawaonaaaaaaa, kazi yako ni maombi, utakatifu,utoaji na kulitiii Neno la MUNGU.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).


Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments