![]()  | 
| Na Mwl Peter Marco Mabula  Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi  | 
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Ijue nafasi yako kiroho na itumie nafasi hiyo kwa kusudi la MUNGU.
◼️Nafasi kiroho ni nini?
✓✓Nafasi ni mahali palipo patupu ambapo panaweza  kuwekwa kitu.
✓✓Nafasi   kiroho ni sehemu ya kiroho iliyo wazi ambayo wewe unawekwa na MUNGU ili ulitumikie kusudi lake.
Ziko nafasi nyingi watu hupewa na MUNGU lakini hawazitumii nafasi hizo kwa kusudi la MUNGU.
MUNGU anapokupa nafasi anataka uitumie nafasi hiyo kwa kusudi lake .
◼️ Unaweza ukaokoka wewe katika familia yako au ukoo wako ili tu utumike kuzimaliza ibada za sanamu au za mizimu zilizokuwa zimezoeleka katika familia yenu au ukoo wenu, tatizo watu wengi hawazijui nafasi zao kiroho.
◼️Unaweza wewe kuwa sehemu ya viongozi wa Kanisani ili tu utumike kuondoa udhalimu uliokuwepo hapo, wengi hawazijui nafasi zao kiroho.
◼️Unaweza kuwa mshirika Kanisani sehemu fulani na kumbe MUNGU amekupa nafasi hiyo  ili uwafanye Kanisa zima kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO Mwokozi.
MUNGU anaweza akapendezwa na wewe hivyo akakuokoa na ndani ya Wokovu huo akakupa nafasi fulani kiroho ili umtumikie, wengi hawazijui nafasi zao kiroho walizopewa na MUNGU.
2 Samweli 22:20 '' Akanitoa akanipeleka panapo nafasi; Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami.'' 
Inawezekana ulikuwa ni mtu aliyedharauliwa sana, inawezekana ulikuwa ni mtu aliyekataliwa au aliyekuwa si kitu lakini MUNGU amekubariki sasa na kukupa nafasi , hivyo itumie nafasi hiyo kwa kusudi la MUNGU.
Wapo baadhi ya watu baada ya MUNGU kuwapa nafasi  hawakujitambua na hivyo hawakutumikia kusudi la MUNGU, ni hatari sana.
Mfano hai ni Malikia Esta.
Esta 4:14 '' Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?''
Esta alikuwa amejisahau kabisa, hakujua kwamba ni MUNGU alimpa nafasi ya kuwa ikulu ili awe msaada kwa watu wa MUNGU waliokuwa wanaonewa.
Maneno ya Mordekai hapo juu ndio yalimfanya ajitambue na kuitumia nafasi yake kwa faida ya wateule wa MUNGU.
Je wewe umepewa nafasi gani na MUNGU?
Je unaitumia nafasi hiyo kwa faida ya ufalme wa MUNGU?
Wengine walipopata nafasi walizitumia ili kuidhoofisha kazi ya MUNGU na sio kuifanya ikue, ni hatari sana.
Esta hakujua kama nafasi ya umalikia aliyopewa ilikuwa imebeba kusudi la MUNGU kwa ajili ya faida ya watu wa MUNGU.
Inawezekana na wewe katika kazi yako  ya kuajiriwa kuna kusudi la MUNGU la msaada kwa watu wa MUNGU, Je unatambua hilo?
Inawezekana MUNGU akubariki katika biashara yako kumbe ni nafasi hiyo ya kiroho amekupa MUNGU ili uitegemeze kazi yake.
Inawezekana umesoma hadi Chuo kikuu na ukijikagua tangu unaanza chekechea ni wengi sana walikuwa na juhudi za kusoma kuliko Wewe lakini walifeli, shule ya msingi ni hivyo hivyo na sekondari ni hivyo hivyo lakini wewe ulifunguliwa mlango na MUNGU wa kufaulu kila mitihani na sasa una kazi nzuri, wewe ni bosi na una mshahara mkubwa, kumbe MUNGU alikupa neema ukafaulu masomo na kupata kazi  na kumbe ndani ya mambo hayo kuna nafasi MUNGU amekupa ili uitegemeze kazi yake, wengi sana huzidharau nafasi walizopewa na MUNGU kiroho, na madhara yanapokuja kutokea baadae  ndipo humgeukia MUNGU kwa machozi.
Nimewahi kuombea watu ambao MUNGU alikuwa amewainua sana sana ila hawakuzitumia nafasi zao kiroho kwa faida ya ufalme wa MUNGU.
Ndugu mmoja siku moja aliniambia kwamba anahitaji hata nusu kilo ya mchele ili ale na familia yake, na katika maongezi yale alisema kwamba aliwahi kupata kazi shirika moja ambapo mshahara ulikuwa milioni 4 kwa mwezi, akiwa na kazi hiyo hakuwahi kutoa fungu la kumi na aliona ni kawaida tu, mambo yalipogeuka ndipo fahamu zilimrudia.
Mtu mmoja siku moja aliniambia kwamba miaka michache nyuma alikuwa anabadilisha gari kama nguo, yaani alikuwa ananunua kila gari inayotoka ikiwa inatamba, katika miaka hiyo ya ufahari hakuwahi kutoa fungu la kumi wala hata muda wa ibada hakuwa nao, mambo yalipogeuka ndipo alijua kwamba kulikuwa na nafasi alipewa na MUNGU ila akaitumia vibaya na kupata hasara.
Ndugu, inawezekana ni wewe umepewa na Bwana YESU nafasi ya ajabu sana lakini umemdharau MUNGU wa Wokovu wako aliyekupa nafasi hiyo.
Kwa sasa unadhani wewe ni akili zako na juhudi zako ndizo zimekufanya kuwa juu sana kimaisha, ndugu kama ni MUNGU alikupa nafasi hakika ni hasara kwako kama huitumii nafasi hiyo kwa kusudi
Inawezekana wewe hapo Kanisani ulipo unatakiwa uitumie nafasi yako kiroho ili kurudisha msingi thabiti wa kiroho  wa Wokovu wa KRISTO uliokuwa umeharibiwa na watu wabaya.
Inawezekana wewe ni muombaji  na una mzigo mkubwa wa kuombea kazi ya MUNGU, kanisa,nchi, ukoo wako n.k
Je unaitumia nafasi hiyo kwa kusudi la MUNGU?
Watu wengi sana hawazijui nafasi zao ndio maana hawazitumii. Ndugu inakupasa kuijua nafasi yako kiroho na anza sasa kuitumia nafasi hiyo kwa kusudi la MUNGU.
Zaburi 119:45-47 ''Nami nitakwenda panapo nafasi, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako. Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu. Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda.''
Baadhi ya nafasi wanazopewa watu na MUNGU ili wazitumie kwa kusudi lake.
1. Nafasi ya kutubu na kutengeneza.
Waebrania 12:17 '' Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi.''
Esau hakuona nafasi ya kutubu ndio maana alikataliwa.
◼️Hakuna nafasi muhimu kama nafasi ya kutubu ambayo watu wengi hupewa.
Inawezekana ni wewe ndugu, yaani wewe ni mzinzi au mwizi n.k na MUNGU kila mara analituma Neno lake kama hivi leo kwamba utubu na kuacha dhambi hiyo, ndugu nafasi hiyo ya kutubu na kutengeneza ikipita unaweza kuja kuitafuta kwa machozi na hutaipata.
Wako watu wamepewa nafasi za kutubu, zikipita hizo nafasi ni hatari sana kwao, mfano hai ni Yezebeli ambapo Bwana YESU anasema juu yake kwamba  '' Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake. Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake; -Ufunuo 2:21-22 '' 
✓✓✓Kila siku MUNGU anatoa nafasi kwa kila mwenye dhambi Kumpokea YESU kama Mwokozi na kisha kutubu lakini sio wote hutii, na nafasi hiyo ikipita ni hatari ya milele.
Waebrania 3:8 '' Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha, Siku ya kujaribiwa katika jangwa,''
Ndugu, MUNGU anakutaka uokoke leo, usifanye moyo wako kuwa mgumu.
MUNGU anakutaka uache uzinzi na uasherati, usifanye moyo wako kuwa mgumu.
Bwana YESU anakutaka umpokee kama Mwokozi wako leo na uache dhambi zote, usifanye moyo wako kuwa mgumu.
Nafasi hiyo ikipita ni hatari kama umeikosa. 
2 Kor 6:2 (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa) 
2. Nafasi ya kumkaribia MUNGU.
Zakaria 3:7 ''BWANA wa majeshi asema hivi, Kama ukienda katika njia zangu, na kama ukishika maagizo yangu, ndipo utakapoihukumu nyumba yangu, nawe utazilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi ya kunikaribia kati yao wasimamao karibu.'' 
Wako wakristo wamepewa nafasi ya kumkaribia MUNGU lakini sio wote wamebaki kwenye nafasi hizo walizopewa na MUNGU.
Ndugu inawezekana ni wewe umepewa nafasi ya kumkaribia MUNGU, wewe ni Mtumishi, wewe ni Askofu au Mchungaji n.k
Je unaitumia nafasi hiyo adimu uliyopewa? je unaitumia kwa kusudi la MUNGU?
3. Nafasi ya kutengeneza boma.
Ezekieli 22:30 ''  Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu. ''
Hii ni nafasi ya kimajukumu ambayo mteule wa KRISTO anapewa na MUNGU, Je unaijua nafasi yako ya kutengeneza boma katika nchi yako au katika Kanisa.
Je unaijua boma unayotakiwa uitengeneze kwa kusudi la MUNGU?
✓Kutengeneza boma maana yake ni kutengeneza nyumba iliyokuwa imeharibika.
Inawezekana boma yako ni dhehebu lako au ukoo wako au mji wako  au familia yako au Kanisa lenu au jamii yako au kundi lenu au huduma yenu au wilaya yako au taifa lako au eneo lako au familia yako n.k
Je unaitumia nafasi hiyo kwa kusudi la MUNGU?
4. Nafasi za kuajiriwa serikalini au kwenye kampuni au kwenye mashirika.
Mithali 8:15-16 ''Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia. Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.''
Biblia inaonyesha kwamba watu hupata nafasi  kimadaraka kwa msaada wake, hupata madaraka kwa msaada wake.
Nafasi na madaraka apatazo mtu ndizo humfanya kutawala na Biblia inasema anatawala kwa msaada wa MUNGU.
Je nafasi ya namna hiyo uliyopewa serikalini au kwenye kampuni au shirika unaitumia nafasi hiyo kwa kusudi la MUNGU?
Nafasi hiyo ni cheo au madaraka au wadhifa uliopewa, je unaitumiaje nafasi hiyo?
Je cheo hivyo unakitumia kwa kusudi la MUNGU?
Je kuna faida hata moja Kanisa la MUNGU linapata kutokana na wewe kuwa katika nafasi uliyopo?
5. Nafasi za kihuduma.
Matendo 13:2 '' Basi hawa walipokuwa wakimfanyia BWANA ibada na kufunga, ROHO MTAKATIFU akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.''
Wako watu hupewa na ROHO MTAKATIFU nafasi za kihuduma ili wazitumie kwa  utukufu wa KRISTO katika kusudi la MUNGU.
Sio wote huzitumia nafasi zao kwa kusudi la MUNGU, hiyo ni hatari sana.
Baadhi ya vipengele vya nafasi za kihuduma ambazo watu hupewa.
a. Nafasi za kuhubiri kweli ya KRISTO inayowataka watu kutubu na kuacha dhambi zote.
Ezekieli 3:18 '' Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.''
b. Nafasi za kuwaonya wanaotaka kumwacha YESU Mwokozi.
Ezekieli 3:20 '' Tena mtu mwenye haki aiachapo haki yake, na kutenda uovu, nami nikiweka kikwazo mbele yake, atakufa; kwa sababu hukumwonya, atakufa katika uovu wake, wala matendo yake ya haki aliyoyatenda hayatakumbukwa; lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.''
c. Nafasi za kuwa walinzi wa kiroho.
Hawa ni waombaji  na wahamasishaji wa kiroho na wanaona rohoni na kuwasaidia watu kiroho.
Ezekieli 33:6 '' Bali mlinzi akiona upanga unakuja, kama hapigi tarumbeta, wala watu hawakuonywa, na upanga ukaja ukamwondoa mtu awaye yote miongoni mwao; ameondolewa huyo katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwa mlinzi huyo. ''
 Hizo ni baadhi tu ya nafasi za kihuduma na MUNGU anaweza kukupa, ndugu kama umepewa nafasi yeyote ya kihuduma basi itumie kwa kusudi la MUNGU.
◼️Itumie nafasi ya kihuduma uiliyopewa kumwinua YESU KRISTO na sio kujiinua wewe.
Mimi Katika utumishi wangu kwa KRISTO nimewahi hadi kukutana na watumishi zaidi ya watatu ambao  walinisema vibaya wakisema kwanini namtukuza sana YESU KRISTO kwenye masomo yangu hasa kila somo kwanini naanza na ''Bwana YESU atukuzwe'' 
Nilitamani kuwashangaa sana lakini Biblia iko wazi sana, mfano ni huu ROHO MTAKATIFU kazi yake mojawapo ni kumtukuza YESU KRISTO, na ni Bwana YESU Mwenyewe anasema  '' Yeye(ROHO MTAKATIFU) atanitukuza mimi(YESU KRISTO), kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba(MUNGU) ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.-Yohana 16:14''
Sasa kama wewe ni mtumishi na unasema una ROHO MTAKATIFU harafu humtukuzi Bwana YESU, je wewe ni mtumishi gani? maana ROHO MTAKATIFU humtukuza YESU KRISTO na hutufundisha na sisi watumishi wake kumtukuza YESU KRISTO Mwokozi wetu. Ninachoweza kusema kwako wewe uliyepewa huduma hakikisha unamtukuza YESU KRISTO na sio kutukuza dhehebu lako au kujitukuza wewe na huduma yako au kumtukuza Baba Yako wa kiroho au Mchungaji wako.
6. Nafasi ya kuwatia moyo watu waliokata tamaa kiroho
Isaya 35:3-6 '' Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea.  Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, MUNGU wenu atakuja na kisasi, na malipo ya MUNGU; atakuja na kuwaokoa ninyi.  Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa.  Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani.''
Mfano hai wa kuwatia moyo watu waliochoka na kukata tamaa ni huu.
Hesabu 13:30 '' Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka.''
Je unaitumia nafasi hiyo kwa kusudi la MUNGU?
Katika utumishi wangu kwa KRISTO Mimi Peter Mabula nimewahi kuwatia moyo watu waliokuwa katika kutaka kujiua kwa sababu ya kusalitiwa na hawakujiua na wengine sasa ni watumishi wa MUNGU, huo ni mfano wa kujifunza kwamba kama Mteule wa KRISTO wakati mwingine umepewa huduma ya kuwatia moyo watu na kuwaimarisha kiroho ili wasifie jangwani bali wafike Kaanani ya mbinguni.
Itumie vyema nafasi yako ya kiroho uliyopewa na ROHO MTAKATIFU katika masuala ya huduma.
7. Nafasi ya kulisikiliza Neno la MUNGU na kulifanyia kazi.
Mathayo 7:24 ''Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;''
Ziko nafasi nyingi sana MUNGU anaweza kukupa ili tu uitumie nafasi hiyo wa utukufu wake, Moja ya nafasi muhimu sana ni nafasi ya kulisikia Neno la MUNGU.
Mfano siku moja nikiwa sekondari kule Biharamulo niliumwa na tumbo nusura nife maana nilikuwa hata kutembea siwezi, na tumbo hilo lilianza ghafla tu siku ya jumapili asubuhi baada ya kula Biscuits. Hali ilikuwa mbaya sana na saa, karibia na jioni wanafunzi walikwenda uwanjani kwa ajili ya  michezo, nilibaki Bwenini naugulia maumivu ya tumbo ambayo sijawahi kuyapata tangu nizaliwe, lakini MUNGU akaniletea Neno lake la uponyaji.
Zaburi 107:20 '' Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. ''
Ningekuwa jirani na wewe hapo ulipo unaposoma Neno hilo ningekuambia ''Usilidharau kamwe Neno ambalo MUNGU anakuletea''
Nini kilitokea kwangu siku hiyo?
Ni kwamba ghafla nilichukua radio na kuweka station iitwayo  radio RFA ya Mwanza na nikakuta Mwalimu Mwakasege anafundisha redioni kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa moja jioni jumapili, siku hiyo  alikuwa karibu na kumaliza na alipomaliza kufundisha alianza kuombea na alisema alisema ''Wewe kama unanisikiliza na unaumwa shika mahali unapoumwa nami nitamuomba MUNGU anayeponya na atakuponya'' Na kweli nilishika tumboni kwa shida sana lakini MUNGU kwa sababu alilituma Neno lake basi Mtumishi alipokuwa anataja magonjwa mbalimbali basi na tumbo hakusahau, alipotaja ''maumivu ya tumbo kwa jina la YESU KRISTO wa Nazareti tokaaaaaaa'' nilisikia kama tumbo linaunguruma na mungurumo ule ulichukua sekunde kadhaa tu na ulipokoma ule mungurumo hakika YESU wa miujiza alikuwa ameniponya. Niliamka muda ule ule nikiwa nimepona kabisa wakati masaa machache kabla wanafunzi wenzangu walikuwa wamenizunguka wakishangaa nimepatwa na nini, inawezekana wengine walidhani sijui kama nitafika kesho. Lakini MUNGU ambaye hulituma Neno lake ili lituponye na kututoa katika maangamizo basi hakika siku hiyo alituma Neno la uponyaji na nikapona.
Vipi ningedharau?
Hakika hata mimi sijui maana maumivu yale yangeendelea usiku kucha sijui ningekuwa wapi?
Ndio maana ndugu nina ujasiri wa kukuambia kwamba MUNGU anapokupa nafasi ya kulisikia Neno lake zingatia sana.
Bwana YESU anapolituma Neno lake kwako hakikisha unazingatia sana sana sana, usidharau kamwe.
Inawezekana MUNGU amekuinua kiuchumi, je unaitumia nafasi hiyo kwa kusudi la MUNGU?
Ayubu 36:16 '' Naam, yeye angekuongoza utoke katika msiba Hata mahali penye nafasi, ambapo hapana msonge; Na kilichowekwa mezani pako kingejaa mafuta.''
 Baadhi ya madhara ya kupewa nafasi harafu usiitumie.
1. Uharibifu utawatokea uliotakiwa kuwaonya lakini hukuwaonya, pia itakuwa ni dhambi kwako.
Ezekieli 33:8 ''  Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. ''
2. MUNGU anaweza kukuondolea nafasi yako na kumpa mwingine huku wewe ukipata madhara.
Esta 4:14 '' Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp)
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments