![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
◼️Ukimpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako wewe unakuwa umefanyika mtoto wa MUNGU.
Yohana 1:12 "Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;"
➡️Ukiwa mtoto wa MUNGU unapata haki zote za kiroho kama Mtoto wa MUNGU.
➡️Haki za watoto wa MUNGU kutoka kwa Baba yao ziko nyingi sana ila mojawapo ni wewe kuwa na kinywa chenye Mamlaka.
Luka 21:15 "kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga."
Unaweza ukajiuliza mfano swali hili,
◼️Hatukemei mapepo kwa kutumia mikono au miguu, tunakemea mapepo kwa kutumia vivywa tu na mapepo yale yanawatoka watu huku yanalia kwa kipigo kisicho cha kawaida, lakini kipigo hicho kimefanywa tu na kinywa cha Mteule wa KRISTO, Huu ni muujiza wa MUNGU tu na unaopatikana katika KRISTO YESU pekee.
Hii ni mamlaka ya Wateule wa KRISTO tu.
Tatizo tu la baadhi ya watu wa MUNGU ni kujawa na uoga, imani haba, kutokuwa na Neno la MUNGU mioyoni mwao, kuwa mtu wa michanganyo, kutokuenenda katika ROHO MTAKATIFU N.k
◼️Ukijitambua hakika utakuwa na kinywa chenye mamlaka sana.
◼️Vinywa vyetu vina nguvu kuliko miguu na mikono, vinywa vyetu vina nguvu kuliko bunduki na mabomu, bunduki na mabomu haviwezi kuua mzimu au jini lakini vinywa vyetu vinaweza.
◼️Unaweza ukawa na bunduki nzuri lakini bado wachawi wakakukaba na kukufanya usilale usiku mzima, lakini ukiwa ni Mkristo mwenye kinywa chenye mamlaka hakika wachawi watakukimbia daima.
◼️Mteule wa MUNGU inakupasa sana kukitumia kinywa chako katika Maombi, kifanye kinywa chako kuwa na mamlaka ya kuzishinda silaha zote za shetani na mawakala zake.
Bwana YESU mwenyewe anamwahidi kila mteule wake aliyeokoka kwamba '' kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga.-Luka 21:15 ''
◼️Yaani MUNGU mwenyewe atatupa kinywa ambacho maadui wote hawataweza kushindana nacho, yaani tutakuwa na usemi wenye mamlaka ambayo utawashida maadui.
◼️Mteule wa MUNGU hakikisha uanatembea kwenye nguvu za ROHO MTAKATIFU na hakikisha una kinywa chenye mamlaka dhidi ya kila kazi za shetani ili kazi hizo zisifanikiwe popote.
✔️✔️Tuna mamlaka kubwa Mno katika KRISTO Mwokozi wetu.
◼️Tunaweza kufanya jambo na likafanikiwa haijalishi kulikuwa na wakuu wa giza wangapi kutuzuia.
Ayubu 22:28 ''Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako.''
◼️Kwa kinywa chako kwa Jina la YESU KRISTO unaweza kuuhamisha ugonjwa mbaya ukatoka ndani ya mwili wa Mtu na Mtu huyo kupona kabisa.
◼️Kwa kinywa chako kwa Jina la YESU KRISTO unaweza ukazuia ajali ambayo wachawi walikesha usiku mzima kwenye vikao vyao ili ajali hiyo itokee asubuhi, wewe kwa maombi kupitia jina la YESU KRISTO unatumia dakika tatu kuomba na jambo hilo halitatokea haijalishi ni majini 500 walitumwa kutekeleza ajali hiyo.
◼️Kwa kinywa chako unaweza kuupiga mzimu uliokaa katika ukoo wako kwa miaka 200, mzimu huo ukatoka na kurudi kuzimu huku watu wa Ukoo wako wakifunguliwa kutoka magonjwa au vifungo vinavyotokana na mizimu.
◼️Kinywa cha Mteule wa MUNGU kina nguvu sana kama Mteule huyo atajua jinsi ya kukitumia kinywa hicho.
➡️Hakikisha tu wewe Mteule wa KRISTO unajua kimaandiko na kiufahamu kuzitumia mamlaka za kiroho nne tulizopewa na MUNGU Baba ili kutupa kila ushindi tunaoutaka uliokuwa umezuiliwa na nguvu za giza.
◼️◼️Mamlaka zako Mteule ni Jina la YESU KRISTO, Damu ya YESU KRISTO, Nguvu za ROHO MTAKATIFU na Neno la MUNGU la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.
Mimi Peter Mabula Nimewahi kuona Miujiza mikubwa sana na ya ajabu sana ambayo MUNGU aliifanya kupitia vinywa vya Watumishi wake waaminifu.
◼️Hata wewe kuwa na kinywa chenye mamlaka ni jambo rahisi na linalowezekana maadamu tu uko na YESU KRISTO kama Mwokozi wako. Ukijitambua hakika neno lako lako la kimaombi litakuwa kama moto na wakuu wa giza unaoshindana nao kila mara watakuwa kama kuni tu na huo moto unaotoka katika kinywa chako kwa kutamka tu, huo moto utawala hao maadui na kuwatowesha.
Yeremia 5:14 ''Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala. ''
➡️Inawezekana wewe kweli umeokoka na unaishi Maisha Matakatifu lakini hujui ufanyeje ili uwe na kinywa chenye mamlaka.
➡️Inawezekana wewe upo upo tu, hujaokoka hata kama Kanisani huwa unahudhuria na unatamani sasa baada ya kujifunza somo hili uwe na wewe na kinywa chenye mamlaka.
ROHO MTAKATIFU siku moja aliniambia kwamba ameniita ili kuwa Mwalimu wa kufundisha Neno la MUNGU, tangu siku hiyo mimi nikajua kwamba huduma yangu mimi ni Mwalimu wa Neno la MUNGU.
Sasa kama Mwalimu sitakiwi kukuacha njiani ngoja nikuambie mambo ya kufanya ili uwe na kinywa chenye mamlaka, hakikisha tu unayazingatia mambo haya yote chini hadi mwisho wa somo hili.
UFANYE NINI ILI UWE MKRISTO MWENYE KINYWA CHENYE MAMLAKA?
Mambo 14 haya yazingatie
1. Mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako kisha ombewa maombi ya kuhamishwa kutoka ufalme wa giza na sasa ukawe katika ufalme wa YESU KRISTO.
Wakolosai 1:13 '' Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ''
2. Hakikisha Neno la MUNGU liko kwa wingi ndani yako.
Wakolosai 3:16 '' Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu. ''
✓✓Soma sana Biblia.
✓✓ROHO MTAKATIFU anapokupa Neno la Ufunuo litumie kimaombi.
Yeremia 1:9 '' Ndipo BWANA akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; BWANA akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; ''
3. Hakikisha unakuwa Mtu wa Imani thabiti katika KRISTO.
Waebarnia 11:1 ''Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. ''
4. Hakikisha unakuwa Mtu wa Maombi kila mara.
1 Thesalinike 5:17 '' ombeni bila kukoma; ''
5. Ishi maisha matakatifu siku zote ili umuone MUNGU akitenda Miujiza kupitia wewe.
Mathayo 5:8 '' Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona MUNGU.''
6. Usikitumie kinywa chako katika maovu au mambo ya kidunia yaliyo mabaya.
1 Thesalonike 5:22 '' jitengeni na ubaya wa kila namna. ''
7. Mruhusu ROHO MTAKATIFU akuongoze, akutumie na akufundishe vita ya kiroho.
Zaburi 32:8 '' Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.''
8. Mjue adui yako kwenye ulimwengu wa roho ili kinywa chako kimshinde maana utakuwa unamjua adui yako.
➡️Ufahamu wa rohoni utakufanya umjue Kila adui wa rohoni.
Wakolosai 1:9 ''Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni;''
◼️Maadui wa rohoni ni pamoja na hawa hapa chini, hawa inakupasa kuwashinda.
Waefeso 6:12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
9. Tambua nini cha kuongea katika kumtamkia wakala wa shetani unayepambana naye.
2 Kor 5:7 ''(Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona.) ''
10. Tumia Neno la MUNGU katika kutumia kinywa chako kumshinda adui.
◼️Neno ni upanga hivyo upanga huo ukitoka katika kinywa chako aliye upande wa shetani hawezi kuhimili.
Waebrania 4:12 '' Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. ''
✔️✔️Neno la MUNGU ni moto ulao na ni nyundo ambayo hakuwa ajenti wa kuzimu atapona ukimtamkia kimaombi kwa imani katika Jina la YESU KRISTO Mwokozi wetu.
Yeremia 23:29 ''Je! Neno langu si kama moto? Asema BWANA; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?''
11. Hakikisha YESU KRISTO anakuwa ni wako Binafsi.
Wagalatia 2:20 ''Nimesulibiwa pamoja na KRISTO; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali KRISTO yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa MUNGU, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.''
➡️Usiseme ''kwa jina la YESU wa Paulo'' kama hawa Ndugu hapa chini Bali Wewe Mfanye YESU awe wako binafsi na sio kuwa YESU wa watumishi wengine.
Matendo 19:13-16 '' Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana YESU juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa YESU, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, YESU namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa. ''
◾Wengine kwenye vinywa vyao wanamtaja YESU anayeonekana kwa Watumishi fulani wakati Watumishi hao wanaliishi kusudi la MUNGU lakini huyu yeye hajamfanya YESU KRISTO kuwa Mwokozi wake Binafsi.
◼️◼️Hakikisha YESU KRISTO ni Mwokozi wako binafsi na unamtii Binafsi na kutembea kwenye kusudi lake.
12. Omba kwa MUNGU kwamba maneno ya kinywa chako yapate kibali kwanza kwa MUNGU, ambaye ndiye chanzo cha ushindi wako.
Zaburi 19:14 '' Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.''
13. Mtumikie Bwana YESU kwa uaminifu ili mamlaka yake iambatane na wewe.
Marko 16:17-18 '' Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya. ''
14. Mjue MUNGU vyema na zijue Kanuni zake katika kila jambo.
Danieli 11:32B '' lakini watu wamjuao MUNGU wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu. ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714252292(whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments