![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai |
Mtu mmoja siku moja aliniuliza Mimi kuhusu nilifanya nini baada ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wangu.
Nilimjibu na sehemu ya majibu ni haya chini, naomba ujifunze kitu wewe unayempokea YESU na timiza kusudi la MUNGU la wito wako.
Mimi Peter Michael Mabula niliokoka mwaka December 2008 nikiwa Unguja Zanzibar.
Namshukuru MUNGU kwa neema yake, nimeshawahi kufafanua ilikuwaje hadi nikaokoka, nilisema jinsi nilivyosemeshwa kwa sauti huku nikiangalia bila kuona anayenisemesha lakini maneno yake yalikuwa ''Nenda Kanisani maana usipoenda utakufa''
Baadae nikakatazwa kwenda Makanisa matatu siku hiyo hiyo huku ile sauti ikisema ''Hao wanaenda kwenye makanisa yao na wewe nenda kwenye Kanisa lako''
Nakumbuka nilishasema mengi ila leo ngoja nikuambie kile nilifanya baada ya kuokoka.
1. Siku nampokea YESU kama Mwokozi nilifika Kanisani mapema sana na ndani ya Kanisa kulikuwa na kiongozi wa ibada tu pamoja na watu kama watano, tulikaa kwa muda kisha kiongozi wa ibada akasema muda wa ibada umefika hivyo akaanza kuimbisha wimbo wa kuabudu. Tuliimba na kisha akasema tufungue Tenzi namba 45, Wimbo huo unasema ''Mtazame huyo(YESU) aliyeangikwa juu ili upate kuishi''.
Mimi sikuwa naujua wimbo huo na ajabu na hata wengine wale watano hawakuwa na vitabu vya tenzi na walikuwa hawaujui wimbo hivyo kiongozi wa Ibada aliimba wimbo huo peke yake huku sisi tunaguna guna tu. Nilitamani watu wajae Kanisani muda huo ili wimbo uimbike vyema, niliwaza hadi kwamba nitakuwa nachelewa Kanisani ili kuepuka mitihani kama hiyo ya kuimba wimbo huku sina kitabu na sijui wimbo.
Nilijisikia vibaya sana na kisha nikajisemea moyoni kwamba baada ya Ibada nitaenda kununua kitabu cha tenzi na nitaanza kukariri tenzi za rohoni ili nikiwa Ibadani nisiwe mgeni wa Tenzi.
Ni kweli nilinunua kitabu cha Tenzi na nikafanikiwa kukariri nyimbo 61 kutoka ndani ya kitabu cha Tenzi za rohoni, nilichukua miezi kadhaa kukariri nyimbo hizo, hiyo ilinisaidia maana hadi leo kila niendako hata kama sina kitabu cha tenzi huwa naimba na wengine wenye vitabu maana nimekariri nyimbo nyingi.
◼️Hata wewe unaweza ukafuata kanuni yangu hiyo ili usiwe mgeni kila siku ibadani.
Wakolosai 3:16 '' Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu. ''
2. Nilipookoka nilikuwa sijui Biblia vyema.
Nilikuwa namshangaa Mchungaji anavyosema maandiko kiufasaha katika kufundisha.
Sikutaka kuwa mgeni wa maandiko hivyo niliamua kuanza kusoma Biblia yote neno kwa neno na nikaimaliza Biblia yote kuisoma baada ya miezi 8.
Kuisoma Biblia yote neno kwa Neno kulinisaidia sana na kunanisaidia sana hata leo katika huduma yangu.
Baada ya kama Mwaka mmoja na nusu nikaanza tena kuisoma Biblia yote neno kwa Neno, ndipo kipindi hiki niliamini kwamba Neno la MUNGU ni jipya kila leo.
Zaburi 12:6 ''Maneno ya BWANA ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba.''
◼️Nikatambua kwamba neno la MUNGU ni zaidi ya dhahabu safi.
Zaburi 119:127''Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako, Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi. ''
Nilipoisoma Biblia ilikuwa ni mpya kana kwamba sijawahi kuisoma kamwe.
Niliisoma tena yote.
Baada ya miaka kadhaa siku moja tena nikapata ufahamu wa kuisoma Biblia kwa jicho la ndoto yaani ili nijue maana za ndoto maana Biblia imeweka wazi maana zote ila watu wengi hawaelewi. Hata mimi katika kipengele hiki nilielewa kwa sehemu chache sana maana ROHO MTAKATIFU tu ndiye anayeweza kutusaidia kuyaelewa maandiko.
Siku moja nilimsikia Mwalimu Mwakasege anafundisha akisema kwamba ''Inampasa kila Mkristo angalau aisome Biblia nzima mara moja au zaidi katika siku za maisha yake'' Nilifurahi na nikatamani kuisoma Tena Biblia nzima.
Wakati huu nilipata ufunuo wa ajabu sana yaani kusoma kitabu cha Mwanzo tu nilipata masomo zaidi ya kumi ya kuwafundisha watu wa MUNGU, ni masomo muhimu sana, wakati huu nilianza kulielewa Neno la MUNGU kuliko Mwanzo.
◼️Ndugu hata wewe hakikisha unajifunza Neno la MUNGU na soma Biblia yote hata mara 7 ili uelewe na kuelewa zaidi.
◼️Kumbuka hakuna mwanadamu anayejua yote ila tunajua kwa sehemu tu kama ambavyo ROHO MTAKATIFU anatufunulia tunapojifunza, wote bado tu wanafunzi hivyo hakikisha unaisoma Biblia yote mara kwa mara.
◼️Ndugu kitendee kazi chakula cha mbinguni ambacho ni Neno la KRISTO.
Yohana 6:27 '' Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na BABA, yaani, MUNGU.''
◼️Neno la KRISTO ndilo Neno la MUNGU, ndio Biblia takatifu.
MUNGU akubariki kwa kujifunza kitu.
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(whatsapp).

Comments