![]()  | 
| Na Mwl Peter Mabula  Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi  | 
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.
◾Ndugu mmoja aliniuliza hivi
"hivi kuna tofauti gani kati ya agano la kale na agano jipya."
Nilimjibu rafiki yangu huyo ila nimeona nifafanue kidogo kama somo ili hata wewe ujifunze kitu.
✓✓Ni kweli kabisa kuna tofauti kati ya Agano la kale na agano jipya.
✓✓Agano ni mapatano.
◼️Na kuna mapatano makuu mawili ambayo MUNGU aliyafanya na wanadamu.
◼️Mapatano makuu ya kwanza ambayo MUNGU alifanya na wanadamu yanaitwa AGANO LA KALE.
Kutoka 24:7-8 " Kisha akakitwaa KITABU CHA AGANO akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii.
 Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, HII NDIYO DAMU YA AGANO alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote."
◼️Na Mapatano ya pili na ya mwisho yasiyo na ukomo yanaitwa AGANO JIPYA.
Luka 22:19-20 " Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki NI AGANO JIPYA KATIKA DAMU YANGU, inayomwagika kwa ajili yenu.]"
◼️Patano la kwanza au Agano la kale lilifanyika Madhabahu ni kupitia Musa likiwa na vitu vikuu viwili.
1. Kitabu cha Agano yaani Neno la MUNGU la wakati huo liitwalo Torati.
2. Sadaka ya agano.
Sadaka za wakati huo zilikuwa wanyama na damu ya wanyama wale ilitumika ili kulifanya liwepo hilo agano.
Damu ya wanyama ilikuwa kama muhuri au kitu kinacholithibitisha Agano na kulifanya liishi hilo Agano.
✓✓Agano la kwanza lilimaliza kazi yake Kalvari ili kupisha Agano jipya la milele.
✓✓Agano la kale lilihusisha sadaka ya wanyama, damu ya wanyama na kitabu cha agano kiitwacho torati, hivyo vyote vilikoma siku ile YESU KRISTO anatukamilishia Agano jipya pale Golgotha, ndio maana Biblia inasema ujio wa YESU KRISTO ndio mwisho wa sheria za Musa yaani mwisho wa torati kutumika.
Warumi 10:4 "Kwa maana KRISTO ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki."
✓✓Na Biblia inaendelea kusema kwamba kule MUNGU kutuletea AGANO JIPYA maana yake huo ndio mwisho wa agano la kale kutumika.
Waebrania 8:13 " Kwa kule kusema, AGANO JIPYA, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka."
◼️Sasa kuna vitu viwili nataka niviweke sawa hapa maana watu wengi sana wamekwama hapa, wengine wameanzisha madhehebu Fulani baada ya kukwama hapa.
✓✓Kwa watumiaji wa lugha ya kiingeleza kuna maneno haya "Covenant" na Testament " maneno haya yana maana tofauti kabisa.
◼️Ukisoma Kutoka 24:8 kwa Lugha ya kiingeleza wakati Musa analitaja Agano, hilo Agano linaitwa Covenant na ukisoma Biblia ya Kiingeleza majina ya Vitabu 39 vya Agano la kale vinaitwa Old Testament.
✓✓Lakini Neno linalotumika kule kwenye kutoka 24:8 kwa kiswahili linaitamkwa "Agano" na majina ya vitabu 39 vya Agano la kale vinaitwa Agano la kale.
✓✓Hivyo kuna Agano Covenant na kuna Agano testament.
◼️Baada ya kukueleza hayo sasa naomba utambue kwamba covenant ya Musa kwa sasa haifanyi kazi ila Testament ya vitabu 39 vya Agano la kale vyote vinafanya kazi hadi Leo.
✓✓Yaani tunaposema agano la kale halifanyi kazi leo hatuna maana ya Vitabu 39 vya Agano la kale kwamba havifanyi kazi Leo, bali vyote vinafanya kazi kwa jinsi ya KRISTO na kwa namna ya Injili ya Wokovu wa KRISTO YESU.
✓✓Ukisoma Torati sio kwa jinsi ya KRISTO huwezi kuwa Mkristo Bali utakuwa Falisayo au Sadukayo tu.
✓✓Ukiifanyia kazi Torati kwa jinsi ya Torati na sio kwa jinsi ya KRISTO ujue utakuwa ama mpingaKristo ama Falisayo.
Kama hujaelewa ngoja nikupe andiko hili likusaidie msimamo wa kidhehebu uliokushikilia rohoni mwako.
Waebrania 7:22 "basi kwa kadiri hii YESU amekuwa mdhamini wa AGANO LILILO BORA ZAIDI."
◼️Kumbe kuna AGANO BORA na AGANO BORA ZAIDI.
◼️Fanyia kazi AGANO BORA KWA KUTUMIA AGANO BORA ZAIDI.
✓✓Vitabu vya Agano la kale viitwavyo Old testament vimeitwa hivyo sio kwa sababu ni Agano la kale Bali kwa sababu viliandikwa tu kabla ya YESU KRISTO Mwokozi hajaja duniani kwa ajili ya Wokovu wetu.
Hivyo mtu akikuuliza kwanini nyie Wakristo mna Vitabu vya Agano la kale na agano jipya?
◼️Mwambie Vitabu vya Agano la kale vinaitwa hivyo kwa sababu viliandikwa Kabla ya Bwana wetu YESU KRISTO kutuletea Wokovu, na Vitabu vya Agano jipya vinaitwa hivyo kwa sababu viliandikwa baada ya Bwana YESU Mwokozi kutuletea Wokovu.
Akikuuliza mtu kwamba je tutumie Vitabu vya Agano la kale na Agano jipya?
◼️Mwambie tumia vyote kwa jinsi ya KRISTO maana wakati wetu ni wakati wa Wokovu wa YESU KRISTO kwa watu wote.
◼️Agano jipya tukitaka kulielezea maana yake tumwelezee YESU KRISTO na Wokovu wake kwa wanadamu wote.
Matendo  4:12 "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo."
◼️Agano jipya linawahitaji wanaomwabudu MUNGU katika roho na kweli.
Yohana 4:23 "Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu BABA katika roho na kweli. Kwa maana BABA awatafuta watu kama hao wamwabudu."
◼️Agano jipya linawahitaji watu wampokee ROHO MTAKATIFU na wakubali kuongozwa na yeye maisha yao yote.
Yohana 14:26 "Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia."
1. Agano jipya ni la milele hivyo hakuna Agano jingine la Wokovu kwa Wanadamu nje na Agano jipya kupitia damu ya YESU KRISTO.
Waebrania 13:20" Basi, MUNGU wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa DAMU YA AGANO LA MILELE, yeye Bwana wetu YESU,"
2. Agano jipya limefanyika kupitia kifo cha Bwana YESU ili kupitia damu yake tupate ondoleo la dhambi.
Mathayo 26:28 " kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi."
3. Wanaohitaji uzima wa milele wanampokea YESU kama Mwokozi yaani wanaokoka.
Warumi 10:9-11 " Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika."
4. Kama umeokolewa na YESU KRISTO hakikisha unaishi maisha matakatifu.
1 Petro 1:15 "bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"
Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana

Comments