KANUNI MUHIMU SANA ZA KUFANIKIWA KIROHO KUPITIA MAOMBI YAKO.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

✓✓Biblia iko wazi sana ikitutaka tuwe tunafanya maombi na tutapokea kutoka kwa MUNGU.

Mathayo 7:7-8 " Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."

◼️Moja ya kitu cha muhimu sana katika maisha ya Mkristo ni maombi.

✓✓Inawezekana wewe in muombaji, unafanya vyema sana ila jifunze Kanuni hizi za kiroho zinazokufanya ufanikiwe kupokea ulichoomba.

1. Utambue uhitaji wako kiroho.

Wafilipi 4:6 "Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na MUNGU."

✓✓Yajue mahitaji yako unayotaka kumwambia MUNGU akutendee.

Je unahitaji nini kiroho?
Hicho unachokihitaji anza kumshirikisha MUNGU katika KRISTO YESU kimaombi.

2. Tambua njia za ki MUNGU za kufuata ili kupokea jambo hilo ulilohitaji.

Njia hizo ziko mbili.

◼️Jifunze ndani ya Biblia.

Zaburi 33:4 "Kwa kuwa neno la BWANA lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu."

✓✓Je kama njia yako ya kupokea hitaji lako ni kutoa sadaka kama Mama wa Sarepta utakubali?

1 Wafalme 17:13-14 "Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao.Kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi."

✓✓Sadaka ya Mama huyu haikuwa tu Bora Sadaka Bali Sadaka inayouma.

✓✓Je kama unatakiwa uhubiri Injili ya KRISTO kwanza ndipo utapokea utakubali?

Marko 10:29-30 "YESU akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili,
 ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele."

✓✓Biblia inasema Mtu aliyeamua kuhubiri Injili ya KRISTO atapewa Nyumba, Watoto, mashamba n.k
Je kama hitaji lako upate Watoto na imeshindikana kwa njia ya kawaida uko tayari kumtumikia Bwana YESU KRISTO maana Ndani ya utumishi MUNGU anaweza kukupa Watoto.

Hii ni Mifano 2 kati ya mingi ya kujifunza ndani ya Biblia kwa ajili ya kupata ushindi kupitia Maombi Yako.

◼️ Muulize ROHO MTAKATIFU ili akusaidie katika udhaifu wako wa kujua.

Zaburi 32:8 "Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama."

✓✓Zitambue kanuni za ki MUNGU za kukufanya upokee ulichokiomba, kwa kujifunza ndani ya Biblia au kwa kumuuliza ROHO MTAKATIFU.

3. Uliza mapenzi ya MUNGU juu ya hicho unachokihitaji.

1 Yohana 5:14 " Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia."

✓✓Lazima kwanza kujua mapenzi ya MUNGU juu ya hicho unachohitaji.

✓✓Mapenzi ya MUNGU ni matakwa ya MUNGU yaani kile ambacho kiko kwenye mpango wake  juu yako.
Hili ni muhimu sana.

Ngoja nikupe mfano.

Kabla Mimi Peter Mabula sijamuoa Mke wangu Jemimah kulikuwa na binti nyumbani kwetu  Mwanza ambaye nilikuwa namkubali sana moyoni mwangu, sasa nilipoingia kuomba kwamba nipate mwenzi, nilitamani kumuoa yule Binti lakini kwenye ulimwengu wa roho nilijulishwa kwamba yule hatakuwa mke wangu. Sasa ningeng'ang'ania kuomba juu ya huyo wakati mapenzi ya MUNGU ni kwamba huyo hakuwa wangu basi ningeomba kwa kupoteza muda maana sio mapenzi ya MUNGU Mimi nifunge ndoa na Binti huyo.

Nilipotii na kuyafuata mapenzi ya MUNGU Binti yule alifunga Ndoa kabla yangu, yaani ni kama Mimi ndio nilikuwa namzuia kuolewa maana nilitamani sana awe Mke wangu na yeye alitaka sana iwe hivyo ila kumbe haikuwa mapenzi ya MUNGU.

✓✓Ni muhimu sana kuyatafuta mapenzi ya MUNGU kwanza kuhusu hicho unachokihitaji kwa MUNGU kwa maombi.

✓✓Je kama mapenzi ya MUNGU utoe sadaka nzuri utatoa?

◼️Hapo ndipo pagumu sana lakini ni mfano mmoja wapo wa mapenzi ya MUNGU kama ROHO MTAKATIFU atakuelekeza hivyo.

4. Kifungue kwa maombi hicho unachokihitaji ili kiachiliwe kwenye ulimwengu wa roho na kiwe tayari kuja kwako.

◼️Mamlaka ulishapewa na Bwana YESU KRISTO siku ulipompokea kama Mwokozi wako.

Mathayo 16:19 "Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni."

✓✓Mfano Maombi Yako upate cheo kipya kazini, kifungue hicho cheo kwenye ulimwengu wa roho Kisha omba kukipata.

✓✓Mfano ombi lako upone ugonjwa, jitenge na huo ugonjwa kwenye ulimwengu wa roho, Kisha omba kupona.

✓✓Mfano ombi lako ni kuzaa kwenye Ndoa Yako, mfungue Mtoto wako katika ulimwengu wa roho Kisha omba MUNGU akupe Neema ya kuzaa utazaa.

5. Anza kumiliki kimaombi hicho ulichohitaji.

✓✓Una nguvu ya kumiliki na kutawala na kutiisha kwenye ulimwengu wa roho, MUNGU alishakupa nguvu hizo tangu siku uliyozaliwa Mara ya pili baada ya kuokolewa na Bwana YESU KRISTO.

Mwanzo 1:28 " MUNGU akawabarikia, MUNGU akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi."

◼️Kwa Imani katika Jina la YESU KRISTO Anza kumiliki kitu hicho unachohitaji kilicho katika mapenzi ya MUNGU.

✓✓Kumbuka Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yajayo ila kwa Sasa hayaonekani katika mwili.

Waebrania 11:1 "Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana."

✓✓Kumbuka ukiomba jambo katika mapenzi ya MUNGU huku ukiamini utalipata uwe na uhakika utalipata.

Mathayo 21:22 "Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea."


6. Jitenge mbali na dhambi zote maana dhambi huzuia maombi.

Yohana 9:31 "Twajua ya kuwa MUNGU hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha MUNGU, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo."

✓✓Kataa dhambi, iache dhambi, ikimbie dhambi na usifanye dhambi Tena.

7. Yajua majira ya kupokea kwako, kaa kwenye eneo la kupokelea hitaji hilo na kaa kwenye kusudi la MUNGU ili upokee.

Mhubiri 3:1 "Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu."

✓✓Majira wakati Mwingine yanaambatana na kiu ya ndani, mfano yaani unatamani Kuoa au Kuolewa kumbe ni Majira Yako kiroho kuingia kwenye Ndoa.

✓✓Majira wakati Mwingine yanaambatana na Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU unafunuliwa Kwa ndoto au Maono ukihubiri au Ukifanya Maombi kumbe ni Majira Yako ya kupokea.
Hii ni Mifano 2 kati ya mingi sana ikionyesha majira Yako yamefika.
Zingatia  na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili, Ushauri, Whatsapp n.k)
Ubarikiwe sana.

Comments