KILA MWENYE PUMZI YA UHAI NA AMSIFU MUNGU.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU aliye hai. 

◼️Neno la MUNGU linatupa agizo zuri wanadamu kwamba kila mwenye pumzi na amsifu MUNGU.

Zaburi 150:6 '' Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA. Haleluya.''

Ukisoma andiko hilo katika tafasiri ya BHN Neno la MUNGU linasema ''Kila kiumbe hai kimsifu Mwenyezi MUNGU''

◼️Kumbe kila mtu aliye hai inampasa kumsifu MUNGU wa mbinguni.

Ndugu, kuwa hai  tu ni jambo kubwa sana na ni kwa upendo wa MUNGU tu ndio maana uko hai.

✓✓Kumbuka uhai huwa unaondoka mara moja tu bila kurudi hivyo wakati uhai wako uko ndani ya mwili wako inakupasa sana kumsifu MUNGU aliyekuumba.

◼️Kumsifu MUNGU ni nini?

✓✓Kumsifu MUNGU ni kuelezea wasifu wa MUNGU unayemsifu.

✓✓Kumsifu MUNGU ni kumshukuru, kumwinua juu, kufanya shangwe kwa ajili yake na kujishuja chini yake kwa unyenyekevu.

✓✓Kumsifu MUNGU ni kuonyesha kwamba ni yeye peke yake anastahili heshima kuu na utukufu wote.
 
Kumbuka wanasayansi wamejaribu kila kitu lakini ni kitu kimoja wameshindwa na wataendelea kushindwa milele, kitu hicho walichoshindwa ni kutengeneza nafsi hai.

◼️Ndugu, wewe kuwa na nafsi hai ni kwa sababu tu ya JEHOVAH MUNGU aliye hai.

Hakuna mwanadamu anayeweza kuitengeneza nafsi hai kamwe.

◼️Ni MUNGU tu ndiye amekufanya kuwa nafsi hai.

Mwanzo 2:7 '' BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.''

Kuna kila sababu ya kumsifu MUNGU kwa kila mwanadamu duniani maana hakuna Mwanadamu alizaliwa kwa mapenzi/matakwa  ya Mwanaume na Mwanamke waliokutana kimwili.

Mwanaume na Mwanamke wanaweza kukutana kimwili na kutunga mimba lakini anayeiweka pumzi ya uhai ndani ya huyo mtoto tumboni ni MUNGU, mfano hai tunaweza kuona Biblia inavyosema katika Yeremia 1:5 ''  Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. ''

 ◼️Kumbe kila mwanadamu aliumbwa na MUNGU ndani ya tumbo, yaani roho iliwekwa na MUNGU ndani ya mimba iliyotungwa, na mtu ni roho anayeishi katika mwili hivyo MUNGU anaposema kabla sijakuuumba katika tumbo la Mama yako maana yake kabla hajaiweka roho yako ndani ya mwili baada ya mimba kutungwa.

◼️Kumbe Biblia inaposema kwamba kila mwenye pumzi amsifu MUNGU ina maana muhimu sana maana hakuna mtu aliyejiumba bali wote tuliumbwa na MUNGU.

➡️Ndugu, hauko duniani kwa sababu  ya Baba yako na Mama yako bali upo duniani  kwa kusudi la MUNGU na ni MUNGU ndiye aliyekupa uhai, hivyo kumsifu MUNGU lifanye kuwa jambo la lazima kwako.

Zaburi 145:3 ''BWANA ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana, Wala ukuu wake hautambulikani. ''

Jambo baya sana na la ajabu sana ni kwamba kuna watu hawamjui MUNGU aliyewaumba, watu hao  husifu majini, husifu masanamu, humsifu shetani, huko ni kutokujitambua.

Ndugu, wa kusifiwa ni MUNGU Muumbaji tu.

Wako pia akina mungu, hawa ni feki hata kama wanadai wameumba mbingu na dunia na dini nyingi zilizo kinyume na KRISTO zinadai kwamba hao akina mungu ndio walioumba mbingu na dunia, sio kweli milele maana aliyeumba mbingu na dunia ni MUNGU wa mbinguni anayeabudiwa pekee katika KRISTO YESU kwa njia ya ROHO MTAKATIFU.

◼️Ndugu, MUNGU wa kweli ni mmoja tu ni JEHOVAH au kwa jina lingine anaitwa YAHWEH, jina lingine anaitwa MUNGU Baba au NIKO AMBAYE NIKO.

◼️Ndani ya MUNGU kuna YESU KRISTO na ROHO MTAKATIFU
Hivyo ukitaka kumsifu MUNGU halisi basi msifu katika KRISTO YESU kwa njia ya ROHO MTAKATIFU.

Zaburi 48:1 '' BWANA ndiye aliye mkuu, Na mwenye kusifiwa sana. Katika mji wa MUNGU wetu, Katika mlima wake mtakatifu.''

   Njia za kumsifu MUNGU.

1. Kumwimbia nyimbo za kumsifu.

Zaburi 33:2-3 ''  Mshukuruni BWANA kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.  Mwimbieni wimbo mpya, Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.''

Wapo waimbaji wengi hudai wanaimba nyimbo za kumsifu MUNGU lakini ukisikiliza ujumbe wa nyimbo zao au pambio unagundua kabisa hizo sio nyimbo za kumsifu MUNGU.

◼️Ndugu, kama ni kipindi cha kumsifu MUNGU kwa nyimbo na ni wewe unaimbisha hakikisha unaimba wimbo wa kumsifu MUNGU na sio vinginevyo.

2. Kumsifu MUNGU kwa kucheza ukimtukuza moyoni mwako.

Zaburi 150:4 '' Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na filimbi;''

Hii unaweza kuiona kwa mtu ambaye ametendewa muujiza na Bwana YESU utamuona anacheza kwa furaha, au anapiga makofu au anatikisika kwa furaha  na moyoni mwake anamtukuza MUNGU na kumshukuru sana sana. 

Sio kila mtu anayecheza anamsifu MUNGU, hivyo unapomsifu MUNGU kwa kucheza hakikisha unacheza kuwa furaha ya neema ya MUNGU, kama unapiga makofu basi kwa furaha njema, kama unatikisa mguu basi kwa kumtukuza MUNGU.

◼️Kumbuka Biblia inatutaka tufanye yote katika Bwana YESU na sio katika shetani.

Wakolosai 3:17 '' Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye. '' 
 
Sasa ukiona mtu anacheza kidunia ujue huyo hamsifu MUNGU, ukiona mtu anaiga staili za kidunia katika kumsifu MUNGU ujue huyo hamsifu MUNGU.

Shetani naye kawakamata waimbaji wengi sana wa Kanisani kiasi kwamba hata wakiona staili za kuzimu na wao watazitumia.

◼️Lazima ionekane tofauti ya wanaomsifu MUNGU na wanaomsifu shetani, uwe makini sana katika kipengele hiki cha kumsifu MUNGU ili mwili wako usiutumie vibaya hata ukavuruga utaratibu mzuri uwapasao wateule wa KRISTO katika kumsifu MUNGU..
 
3. Kumsifu MUNGU kwa njia  ya maombi.

Wakolosai 4:2 '' Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; ''

Maana yake katika maombi yako lazima kuwe pia na muda wa kumsifu MUNGU kwa kutamka kwa maneno na shukrani kwa MUNGU inayompa MUNGU sifa na heshima. 

◼️Unapomshukuru kwa ajili ya jambo fulani ujue unamsifu pia na kumpa utukufu.

4. Kumsifu MUNGU kwa kutaja shuhuda zinazompa utukufu.

 Kutoka 12:26-27 ''Kisha itakuwa, hapo watoto wenu watakapowauliza, N'nini maana yake utumishi huu kwenu?
 Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya pasaka ya BWANA, kwa kuwa alipita juu ya nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa nyumba zetu. Hao watu wakainama vichwa na kusujudia.''

Huu ni mfano hai ambapo Waisraeli waliambiwa watawaambia watoto wao jinsi ambavyo MUNGU aliwapiga wamisri na kuwapa ushindi wao Waisraeli.

 ◼️Unapoyataja matendo ya MUNGU ujue hiyo ni njia mojawapo ya kumsifu MUNGU na kumtukuza na ushuhuda unaweza hata kuwainua na wengine.

✓✓Unaweza hata katika maombi yako kutumia muda mrefu zaidi ukitaja matendo aliyoyatenda MUNGU katika KRISTO na unamsifu MUNGU kwa mambo hayo aliyotenda.

Unaweza kutumia muda wako unapoongea na watu kushuhudia alichotenda MUNGU na kwa njia hiyo unamsifu MUNGU aliyekutendea.

Tafuta hata mambo aliyoyatenda kwako au kwa watu wengine au kwa watu wa ndani ya Biblia na taja katika maombi yako ukimsifu MUNGU.

Zaburi 105:1 '' Haleluya. Mshukuruni BWANA,liitieni jina ,Wajulisheni watu matendo yake. ''

 5. Kumsifu MUNGU kwa kulisifu jina la YESU KRISTO Mwokozi.

Wafilipi 2:9-11 ''  Kwa hiyo tena MUNGU alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la YESU kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO ni Bwana, kwa utukufu wa MUNGU Baba.'' 

◼️Jina la YESU KRISTO ndilo jina kuu kuliko majina yote.

◼️ Maombi yetu ni katika Jina la YESU KRISTO, masha yetu na kila kitu chetu inatupasa kufanya katika jina la YESU KRISTO(Wakolosai 3:17)

◼️Njia mojawapo ya kumsifu MUNGU ni kulitaja jina la YESU KRISTO kama kiini cha ushindi wetu, maana ndivyo ilivyo.

◼️Unapotukuza jina la YESU KRISTO ujue unamtukuza MUNGU aliyeziumba mbingu na nchi.

Zaburi 113:1-2 ''Haleluya. Enyi watumishi wa BWANA, sifuni, Lisifuni jina la BWANA.  Jina la BWANA lihimidiwe Tangu leo na hata milele.'' 

➡️Msifu MUNGU kwa kumpa utukufu moyoni mwako.

➡️Msifu MUNGU kwa kumpa heshima katika kila eneo la maisha yako.

◼️Mtukuze MUNGU kila uliko iwe ni mbele za watu au kazini kwako au kwenye huduma zako za kiroho.

◼️◼️Japokuwa MUNGU anastahili kusifiwa na kila mwanadamu lakini yeye MUNGU anawafurahia walio wanyoofu wa moyo wanapomsifu.

Zaburi 33:1 '' Mpigieni BWANA vigelegele, enyi wenye haki, Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.''

MUNGU pia anawafurahia wenye haki na waliojitoa moyoni ili kumsifu kwa unyoofu wa moyo, hao ataonekana kwao.

◼️Hivyo ndugu unapokumbuka kumsifu MUNGU hakikisha wewe ni mnyoofu wa moyo,unaishi maisha matakatifu, umejitenga mbali na dhambi, umeokoka na YESU KRISTO ndiye Mwokozi wako.

Usiende kumsifu MUNGU huku umetoka kuzini au kuiba n.k

Usimsifu MUNGU huku umetoka kutenda dhambi, hiyo ni mbaya sana.

Usiende kumwimbia MUNGU nyimbo za sifa huku unaishi maisha ya dhambi, mbele za MUNGU wanahitajika wanyoofu wa moyo ili hao wamsifu MUNGU na kumtukuza.

Usikubali kumsifu MUNGU kwa kumwimbia ibadani tu lakini ukifika nyumbani unaanza kumwimbia shetani, wewe utakuwa hujitambui.

MUNGU anawahitaji wanyoofu wa moyo ili wamsifu, hivyo siku zote hakikisha unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.
Msifu MUNGU kwa kumtaja jina lake.

Kuna waimbaji wa nyimbo za injili lakini katika albamu zao za nyimbo hawajawahi kumtaja YESU KRISTO ambaye ndiye  mwenye injili.

Yaani mwimbaji anaimba nyimbo 5 au 7 au 10 bila kumtaja YESU KRISTO Mwokozi na hata kama akimtaja YESU kwenye nyimbo zake ni katika mifano dhaifu tu, huko ni kutokujitambua na kutotambua maana ya kumtukuza MUNGU na kumsifu.

◼️Kama wewe unamwimbia MUNGU sifa basi mpe MUNGU nafasi ya kwanza katika uimbaji wako.

◼️Kama wewe ni mwimbaji wa nyimbo za injili basi mpe YESU KRISTO nafasi ya kwanza na kwa njia utampa MUNGU utukufu stahiki.

   Matokeo ya kumsifu MUNGU.

1. Nguvu za MUNGU zitashuka ili kukupa ushindi.

Zaburi 50:23 '' Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa MUNGU. ''

2. MUNGU atashuka na kukutendea muujiza.

Matendo 16:23-26 ''Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba MUNGU na KUMWIMBIA NYIMBO ZA KUMSIFU, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.''

3. Kumsifu MUNGU huwafanya maadui zako kupigwa au  kukimbia.

2 Nyakati 20:22-24 '' Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe. Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka.''

 ◼️Ni muhimu sana kila mwenye pumzi ya uhai kumsifu MUNGU aliyeziumba mbingu na nchi.

✓✓Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana YESU KRISTO.
◼️
Kila mwenye Pumzi na amsifu MUNGU katika ROHO MTAKATIFU.

Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments