![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Je MUNGU alipokuagiza kitu ulitii?
◼️Je MUNGU alipokuita uliitika na kufuata maelekezo yake?
◼️Je MUNGU aliposema " acha hiki" uliacha?
✓✓Moja ya vitu vikubwa sana ambavyo vinawakosesha watu wengi ni watu hao kutokuzingatia maagizo ya MUNGU anayoyatoa ROHO MTAKATIFU kupitia watumishi wake waaminifu.
◾Ngoja tujifunze kwa mfano huu.
Nchi ya Misri siku moja ilipata Neema mbele za MUNGU maana MUNGU alisema nao kupitia Mtumishi wake Musa na waliotii hawakupata madhara ila wasiotii wengi walikufa na wengine walipata madhara.
MUNGU alisema Neno hili "
Tazama, kesho wakati kama huu, nitanyesha mvua ya mawe nzito sana, ambayo mfano wake haujakuwa huko Misri tangu siku ile ilipoanza kuwa hata hivi sasa. Basi sasa tuma wahimize waingie ndani wanyama wako na hayo yote uliyo nayo mashambani; kwani kila mtu na kila mnyama apatikanaye mashambani, wasioletwa nyumbani, hiyo mvua ya mawe itanyesha juu yao, nao watakufa.-Kutoka 9:18-19"
✓✓Neno hili alilisema MUNGU kupitia Musa ili kuwasaidia Wamisri, lakini wengine walitii maelekezo ya MUNGU na wengine hawakutii maelekezo ya MUNGU Mwenyezi.
Biblia inaendelea kusema katika Kutoka 9:20-21 kwamba "Yeye aliyelicha neno la BWANA miongoni mwa watumishi wa Farao aliwakimbiza watumishi wake na wanyama wake waingie nyumbani; na yeye asiyelitia moyoni neno la BWANA akawaacha watumishi wake na wanyama wake mashambani."
✓✓Biblia inasema kwamba mtu aliyeitii sauti ya MUNGU alifanya kama MUNGU alivyoelekeza, na Mtu aliyedharau aliendelea na shughuli zake kama kawaida lakini kama alikuwa nje ya nyumba alikufa, na wale ambao waliwaacha wanyama wao nje au watoto wao nje, au wafanyakazi wao nje, hao wanyama na wanadamu wote walikufa.
Biblia inasema,
Kutoka 9:22-25 " BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, ili iwe mvua ya mawe katika nchi yote ya Misri, juu ya wanadamu na juu ya wanyama, na juu ya mboga zote za mashamba, katika nchi yote ya Misri. Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; na BWANA akaleta ngurumo na mvua ya mawe, na moto ukashuka juu ya nchi; BWANA akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi yote ya Misri. Basi palikuwa na mvua ya mawe, na moto uliochanganyikana na ile mvua ya mawe, nzito sana, ambayo mfano wake haukuwapo katika nchi yote ya Misri tangu ilipoanza kuwa taifa. Na ile mvua ya mawe ikapiga kila kilichokuwako mashambani, binadamu na mnyama, katika nchi yote ya Misri; hiyo mvua ya mawe ikapiga kila mmea wa mashambani, na kuuvunja kila mti wa mashamba."
✓✓Biblia inasema kila kilichokuwa shambani iwe ni mwanadamu au mnyama wa kufugwa au chochote kilivunjika na vingine vilikufa.
✓✓Wale tu raia wa Misri walioitii sauti ya MUNGU ndio walipona.
✓✓Ilinyesha mvua ya mawe na mvua ile iliambatana na moto mkali hivyo kiumbe hai ambaye ingemnyeshea asingepona, hivyo watu wengi na wanyama walikufa, lakini MUNGU alikuwa ameshawaambia ila wengine walitii na wengine hawakutii na hivyo wakapata madhara makubwa sana.
✓✓Hata wewe ndugu, MUNGU katika KRISTO YESU anaweza akasema na wewe juu ya chochote ni kazi yako kutii maana usipotii utapata hasara.
✓✓Maelekezo ya MUNGU yapo ya namna nyingi tu ila muhimu zingatia tu maelekezo hayo.
◼️Ndugu katika maisha yako yote hakikisha unakuwa mtu wa kumtii MUNGU kupitia YESU KRISTO.
✓✓Biblia inakutaka usifanye moyo wako mgumu kwenye kutii maagizo ya MUNGU.
Waebrania 3:15 "hapo inenwapo, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha."
✓✓Inawezekana wewe umeitwa na MUNGU ili umtumikie katika kazi ya Injili ya KRISTO lakini umedharau, hiyo ni hatari sana.
◼️Hata baraka zako zingine zinaweza kuzuiliwa kwa sababu tu hujatii agizo la MUNGU.
✓✓Wakati mwingine MUNGU anaweza kukupa jukumu na kumbe ndani ya jambo hilo na baraka yako imewekwa, hivyo ukidharau kufanya hicho alichokuagiza MUNGU basi hata baraka hiyo hutaipata.
◼️Ndugu, Bwana YESU akikuita hakikisha unatii na kuzingatia sana maana hiyo ni kwa faida yako.
◼️MUNGU anapokupa agizo zingatia sana maana ni kwa faida yako na ni kwa ushindi wako.
◼️MUNGU akikukataza chochote hakikisha unaacha baraka sana.
✓✓Inawezekana uko katika wakati mgumu na wewe ni Mkristo mcha MUNGU na sauti ya MUNGU inakujia ikikutaka uendelee mbele, ndugu hakikisha unaendelea mbele maana kuna ushindi wako.
✓✓Wengine waliambiwa waendelee mbele wao wakaamua kuingia dhambini hivyo wakapishana na MUNGU na wakapishana na baraka za MUNGU.
✓✓Wengine waliona wamechelewa kupata wenzi wa ndoa hivyo wakaamua kuzini na kwa njia hiyo wakamkosa MUNGU na wakakosa baraka zao sahihi.
✓✓Wengine walipitia mazingira magumu, Neno la MUNGU likawajia kusema wavumilie lakini wao waliamua kwenda kwa waganga wa kienyeji hivyo kumkosa MUNGU na wakaongeza matatizo na vifungo.
◼️Ndugu, kutokutii maagizo ya MUNGU kunaweza kukuletea hasara kubwa sana.
Biblia inajulisha hivyo ikisema,
Kumbu 28:15-19 " Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata. Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani. Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia. Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo,"
Maana yake nini?
✓✓Yaani mtu anaweza akaipuuzia sauti ya MUNGU ya maagizo na mtu huyo kupata madhara makubwa sana.
◼️Maandiko hapo juu yanasema kwamba mtu anaweza kudharau maagizo ya MUNGU kwake na mtu huyo kupata laana, na laana hiyo itaambatana naye kokote atakakokwenda, iwe ni mjini au vijijini, iwe ni mashambani au kwenye biashara au kwenye kazi, ni hatari sana kupuuza maagizo ya MUNGU kwako.
✓✓Biblia inasema kinaweza kulaaniwa chanzo cha uchumi cha mtu kwa sababu tu hakutii maagizo ya Bwana YESU KRISTO.
✓✓Biblia inasema hata uzao yaani watoto wanaweza kutembea kwenye laana kwa sababu ya mzazi wao aliyekataa kumtii MUNGU na akachagua kutii mawakala wa shetani.
◼️Ndugu, wewe MUNGU amekupa agizo gani?
◼️Je ROHO MTAKATIFU amekuelekeza nini?
Ukitii hakika utapata faida kubwa sana.
MUNGU anaweza kusema na wewe kwa njia zifuatazo.
1. ROHO MTAKATIFU kukufunulia rohoni mwako.
2. MUNGU kusema na wewe kupitia Malaika.
3. MUNGU kusema na wewe kupitia watumishi wake waaminifu katika KRISTO YESU.
4. MUNGU kusema na wewe kupitia andiko la Biblia.
5. MUNGU kusema na wewe kupitia mazingira uliyopo.
✓✓Yaani mazingira tu yanakujulisha nini ufanye kitu cha ki MUNGU.
6. MUNGU kusema na wewe kupitia mahubiri ya Neno lake.
7. MUNGU kusema na wewe kwa ndoto au maono.
✓✓Ndugu, nakuomba tu ifanyie kazi sauti ya MUNGU anayosema na wewe ili tu usipate hasara.
Kumbu 28:1" Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;"
◼️Je MUNGU amesema na wewe nini?
◼️Je umesema na wewe kuhusu utoaji?
◼️Je amesema na wewe kuhusu utumishi.
◼️Je amesema na wewe kuhusu nini?
Ndugu mmoja aliambiwa na MUNGU anunue kiwanja cha Kanisa na kujenga Kanisa japokuwa yeye sio Mchungaji na haabudu hapo.
Mtu mmoja akiambiwa amtumikie Bwana YESU hivyo akaacha ufahari mkubwa na heshimu kubwa aliyokuwa anaipata, akaamua kwenda kumtumikia MUNGU.
Mtu mmoja aliikimbia kazi ya MUNGU ili aajiliwe na kupata pesa, kilichotokea baadae ni kila akipata kazi anafukuzwa.
✓✓Ndugu, tii sana maelekezo ya MUNGU kwako.
◼️Inawezekana kuna kazi ya MUNGU mahali imelala kwa sababu wewe umegoma kufuata maelekezo ya ROHO MTAKATIFU rohoni mwako, ndugu ni hatari kwako.
✓✓Maana unaweza ukajikuta kwenye madhara makubwa na hujui chanzo ni nini, kumbe chanzo ni wewe kutikuzingatia maagizo ya MUNGU kwako.
' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''
Zingatia na MUNGU atakubariki sana.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe sana

Comments